Tupeleke macho yetu Mara!

Niliambiwa kuwa fimbo ya mbali haiuwi nyoka! Lakini nakumbuka kuwa niliandika insha kadhaa kubatilisha baadhi ya methali na nahau zetu ambazo kwa namna moja au nyingine haziwezi kutusaidia kwenye baadhi ya mazingira na mazingara.

Najua unaanza kujiuliza maswali kuwa ninajaribu kusema nini haswa leo hii. Usiache kusoma…

Nimeingia ‘mzigoni’ leo asubuhi mapema, kama kawaida kwa kuanza kuangalia habari kutoka nilipokulia – Tanzania. Bahati mbaya siku imeanza kwa habari zinazosikitisha. Na sisiti kueneza habari zenyewe kama zilivyo; bila ya kuficha chochote kwa kutumia nahau, methali ua maneno mengine matamu.


Mei 24, 2009, Chambi Chachage alitoa taarifa kupitia blog ya Udadisi kuhusu vitendo vya Barrick Gold Mine vya kumwaga takataka za sumu kwenye mto Tighithe, Mara. Athari za takataka hizo kwa afya za watumiaji wa mto Tighithe zilianza kuonekana.

Jana, Machi 16, 2010, Chacha Benedict Wambura wa Foundation HELP alitupa picha halisi ya afya za waathirika kwa kutumia blog ya Udadisi tena. Idadi ya waathirika inazidi kuongezeka na mpaka wakati naandika hii nakala nilikuwa sijapata msamiati sahihi ambao unaweza kuelezea hali ya afya zao.

Kinachotia hasira zaidi ni ukimya wa Serikali yetu na watu wengine husika (uongozi wa Barrick Gold Mine)! Jamani, hawajui haya yanayojiri huko mto Tighithe? Au wamekuwa na roho ngumu kiasi kwamba vitu kama hivi haviwashtui? Hawajali?

Nimeshawahi kusoma visa kama hivi, ambapo urasimu na uchunguzi wa kuhakikisha kuwa takataka kutoka kwenye migodi ndio chanzo cha matatizo kama haya tunayoyaona huchukua miaka. Bahati mbaya wakati muafaka unapatikana vijiji karibu na Tarime vitakuwa vimesha’angamizwa; na hakuna fidia yoyote – kwa watoto na ndugu zao – itakayoweza kuwarudishia maisha yao!

Jamani, viongozi wetu chonde chonde, jamani! Kwenye usahili wa mgodi huu hamkuangalia vitu muhimu kama utupaji wa takataka za sumu? Au, hata hamkutaka kujua ni aina gani ya takataka zitatoka kwenye mgodi huu? Hela mnazopata ndizo zinawafumba macho?

Vijana wenzangu itabidi tufanye chochote tunachoweza kuokoa jahazi – popote tulipo! Fimbo yangu iko mbali, lakini mtandao utanisaidia kumchapa huyu nyoka.

Edit: Ripoti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyotolewa Juni 4, 2009 inaishia hivi:

………………………………………………..
Recommendations:
– Local village residents around the mine should be educated on the environmental impacts caused by vandalism and theft of liners…
– There should be timely reporting of various incidents by the mine to the licencing authority.
– It is proposed that liners be covered with compacted thick materials as deterrent to vandalism and theft.
– Mine management should work on ways to ensure that such environmental incidents do not occur in the future.
………………………………………………..

Vipi, mbona suala la afya za waathirika limefumbiwa macho? Watapata fidia za aina yoyote ile?

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend