Waafrika tuna asili moja?

Na VR



Kwa muda mrefu nimekuwa nikiumia roho mno kwa jinsi watu kutoka Afrika tunavyolundikwa kwenye kundi moja kiasilia. Kukiwa na tatizo utasikia, waache hao, ni tabia ya Waafrika hio, hawatakoma. Bara/nchi yao imelaaniwa.

Ukweli ni kwamba bara letu lina watu wenye asili na tofauti nyingi mno kimaumbile, kiutamaduni na hata ukiingia kwenye chembe chembe za DNA. Ukiangalia bara la Ulaya, Wajerumani wamepakana na Wafaransa, lakini watu hawa hawapendi kabisa kufananishwa. Ukienda Amerika ya Kusini, ni mwiko kumuita mtu anayetoka Colombia Mbrazili.

Utafiti unaonesha kwamba idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika wana maumbile mengi na tofauti kuliko watu katika mabara mengine — hasa ukiangalia chembe chembe L1, L2 na L3 mtDNA (Krings et al, 1999).

Wanahistoria waliojaribu kutafuta jinsi ya kuelezea asili ya Mwafrika, walifanikiwa kusambaza mawazo yao pande zote za dunia. Mengi ya mawazo hayo yawezekana yalikuwa ya kudhani tu au imani. Inasemekana kuwa asili ya Mbantu ni misitu ya Kongo. Ingawa yawezekana ikawa ni kweli, nina hofu ikawa ni imani ya wenyeji wa pale waliodhani kuwa wako katikati ya dunia. Na mtafiti aliyefika pale hakuweza kupata mawazo ya staarabu, makundi au falme nyingine zilizokuwa mbali na eneo utafiti huo ulipofanyika.

Kwahiyo elimu iliyopatikana hapo haikuwa ya kutosha au tuseme ilikuwa hafifu. Ingawa mtafiti huyo alilifahamu hilo, aliamua kufanya hitimisho kuwa Wabantu wote walitokea eneo lile. Ninaweza nikahisi kuwa, Kibantu asili kama ilivyokuwa Kilatini na sasa Kiingereza, ilikuwa lugha ya wasomi wa kale hapa Afrika. Sasa, idadi ya watu wenye asili tofauti ilivyokuwa inaongezeka, lugha nayo ilikua na kubadilika taratibu ingawa iliendelea kuwa na asili yake miaka nenda rudi. Hitimisho hili halina uhakiki kuwa asili ya Wabantu na hasa watu wa kusini mwa jangwa la Sahara wawe na asili ya misitu ya Kongo. Cha kushangaza, chembe L0 mtDNA inayosemekana kuwa mzazi wa L1, L2 na L3 mtDNA, inahisiwa kuwa na chanzo chake Afrika Mashariki.

Kwanini Waafrika tukubali kuwekwa kwenye kundi moja kiasilia? Je, uanzishwaji wa Umoja wa Afrika unaangalia tofauti kubwa zilizopo za utamaduni na asili kati ya makundi mbalimbali hapa Afrika kwa nia ya kuboresha sera za muungano huo? Makala hii itaendelea na uchambuzi wa kina zaidi kuhusu hili jambo.

Picha/ramani inapatikana hapa.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend