Unajua kipaji chako?

Utambuzi wa vipaji hula fikra.

Vijana wengi tumeshapitia au tunapitia kwenye kipindi kigumu sana maishani. Nina uhakika wengi wetu tumeshawahi kukosa usingizi wakati tupo kitandani na kubaki tu kuangalia dari na kujiuliza maswali mengi sana; nitafanya nini maishani? Mustakabali wa maisha yangu ni upi? Nitakuwa wapi baada ya miaka miwili, mitano au hata kumi?

Bahati mbaya Watanzania hatuna hulka ya kujadili mambo kama haya kwa uwazi tukiwa na ndugu, jamaa na marafiki zetu. Na matokeo yake (tunaonekana kama) hatujifunzi kutoka kwa wenzetu — hili suala ndilo linalonipa misongo kwenye mijadala mbalimbali. Kwahiyo, ni matumaini yangu kuwa nasaha zilizopo kwenye makala hii zitabadilisha fikra za angalau kijana mmoja na kutambua kuwa maisha yake ya baadae yako kwenye viganja vyake! Kwa maneno mengine, wewe msomaji ndio mwenye uwezo mkubwa wa kuamua maisha yako huko mbeleni yaweje.

Je, unajua una kipawa, kipaji au talanta ipi? Baada ya kumaliza elimu ya sekondari au chuo kikuu, ulikuwa au unajua unataka ufanye nini; uwe mtu wa aina gani kwenye jamii?

Kama unashindwa kujibu hayo maswali haraka na kwa ufasaha, usiogope na wala usitetereke. Hauko mwenyewe, kijana. Wengi tumeshapitia na tunaendelea kupitia kwenye kipindi ambacho fikra zetu zinakuwa zimejawa na mawazo ya utata. Lakini utakubaliana nami kuwa wenzetu ambao tayari wanajua wana vipaji fulani na kuvifanyia kazi, maisha yao huonekana marahisi machoni mwa wengi.

Amini usiamini, majibu ya maswali mengi hupatikana hapa — kwenye tovuti ya Bongo Celebrity. Jeff na timu yake wamekuwa wanajitahidi kutuletea mahojiano murua ya watu maarufu wanaofanya vizuri Bongo kwenye nyanja mbalimbali, ili mimi na wewe tujifunze mawili matatu kutoka kwao na kutumia ‘maujanja’ kwenye maisha yetu; kukuza vipaji vyetu na kuviendeleza.

Jifunze kutoka kwa waliofanikiwa

Kwa mfano, Profesa Jay akihojiwa huwa anatoa nasaha nyingi sana ambazo binafsi naamini zinatakiwa kuhamasisha kila kijana anayezisikia kwa namna moja au nyingine. Cha kusikitisha wengi wetu tutakumbuka tu ni lini Mzee wa Mitulinga atatoa album mpya. Basi.

Mmoja wa waliofanikiwa.

Sielewi kwanini tunafumbia macho ukweli kuwa Jay huwa anatembea na karatasi na kalamu karibia muda wote, na akiona kitu ambacho anadhani kitakaa vizuri kwenye mashairi yake huwa anakiandika papo kwa papo. Muda mwingine hata akiwa na marafiki zake. Kama bado hujanielewa, Jay ni mwandishi mzuri sana na huwa anaandika mashairi muda wote! Na suala la kipaji chake kukua, kupevuka na kukomaa linajidhihirisha kila kukicha. Kasikikilize wimbo unaoitwa Chuzi limekubali wa Hard Blasters Crew, halafu linganisha na mashairi yaliyojaa busara kwenye wimbo Machozi, Jasho na Damu aliouimba takribani miaka miwili baadae.

Ninachojaribu kukuasa kijana mwenzangu ni kama ifuatavyo: Fungua macho ukiwa kwenye pita-pita na mihangaiko yako; ukiona kichuguu kizuri angalia kwa makini na jifunze jinsi kinavyojengwa na siafu, badala ya kukisifia tu na kuendelea na safari.

Tambua una vipaji

Safari ya kutambua una kipaji au vipaji gani, kuvikuza na kuvifanyia kazi inaweza ikawa ngumu au rahisi kutegemeana na mazingira na mazingara uliyokulia na uliyomo. Huo ni mjadala mrefu sana ila sitaki kuzama huko, kwasababu naamini vitu ambavyo vinampa mtu motisha vina nguvu zaidi.

Kama nilivyosema hapo awali, usikubali mtu mwingine akuamulie maisha yako ya baadae yaweje kwasababu tu amekuzidi umri au ana mamlaka fulani. Aghalabu kauli zenye mamlaka zinaweza kukufunga mawazo yako na kukusukuma kufanya jambo ambalo labda sio ile kitu roho inapenda. Pia, usifuate mkumbo; jaribu kufikiria mustakabali wako binafsi kwanza.

Kwa mantiki hiyo, ni jukumu lako kugundua una vipawa gani. Sidhani kama kuna njia rahisi ya kukwambia, “Aisee, bwa’ mdogo una kipaji (fulani)! Kifanyie kazi.” Njia pekee itakayokuwezesha kufaulu huo mtihani ni kujaribu kufanya na kufuatilia mambo mbalimbali — iwe kwa kusoma vitabu vya taaluma au magazeti, kuongea na kubadilisha mawazo na watu n.k. Huwezi kung’amua kuwa wewe ni mchezaji mzuri wa mpira kwa kukaa kijiweni, wakati u mvivu wa hata kupiga danadana tu.

Wewe imba, mimi nitadonoa nyuzi za gitaa.

Jiulize, ingekuwa vipi kama Man Dojo na Domo Kaya wangekaa tu vijiweni Arusha na kutothubutu kujaribu kupiga gitaa na kuimba?

Usiogope kukosolewa

Changamoto kubwa mwanzoni ni kuondokana na hofu ya kufanya makosa au kuogopa kukosolewa. Ni kawaida kila  binadamu kuogopa, ila kinachotufautisha ni jinsi tunavyokivuka hiki kihunzi. Unadhani sikujawa na hofu hata chembe nilipopewa fursa ya kuandika hii makala na kuanika mawazo yangu hadharani? Kilichonipoza ni ile motisha ya kutumia kasoro zozote zitakazojitokeza na kuhakikisha naandika makala nzuri zaidi nitakapopewa fursa nyingine.

Lengo langu kubwa ni kuanzisha mjadala mzuri, kwasababu ninaamini kuna Watanzania wengine wengi wenye uzoefu na mawazo mazuri zaidi yangu, na nina kiu na njaa ya kujifunza kutoka kwao!

Ukiacha kipaji, huyu ana 'kismati' cha kupendwa kutokana na tabia yake.

Hadithi nzuri kuhusu kujua jinsi ya kutumia vema ukosolewaji inatoka kwa Sir Juma Nature. Sir Nature alitoka kwa njia ya kushirikishwa kwenye nyimbo kama Mtani Jirani, Mtulize na Maskini Jeuri. Mimi ni mmojawapo wa mashabiki wake wakubwa na nilivutiwa sana na kisa alichokiimba kwenye wimbo Mtani Jirani. Ila Juma wa kipindi kile ni tofauti na yule Juma aliyetikisa na Hili Gemu, Kighetto-ghetto (remix), Jinsi Kijana na nyimbo nyingine lukuki.

Juma alikuwa anatumia lugha ‘ngumu’ iliyokuwa inaeleweka kwa vijana wa Kurasini, Keko, Temeke, Tandika, Mtoni na Mbagala. Nakumbuka P-Funk, Bonny Luv, Sebastian Maganga na wengine wengi walimkosoa na kumshauri ‘alainishe’ mashairi yake. Kijana hakuzira wala kunywea, akaufanyia kazi ushauri.

Jiamini na amini unachofanya

Rock City sasa inaitwa Rap City.

Labda hii ndio nguzo kubwa kuliko zote. Sijui kama inajengwa kwa mambo niliyoyajadili kwa kifupi hapo juu, au ndio msingi unaohimili niliyoyataja. Kama wewe hujiamini na wala huamini kuwa unachofanya ni kizuri na kina manufaa kwa jamii, unategemea wanaokuzunguka wakuamini?

Hakika kauli za kutia moyo kutoka kwa wazazi, ndugu, marafiki na watu ulio nao karibu zinaweza kukusaidia. Ila huwa napenda kusisitiza zaidi ile motisha mtu binafsi aliyonayo.

Huyu Fid Q kipenzi cha wengi, safari yake haikuanzia na wimbo Mwanza au FidQ.com. Kijana ilibidi atoke Mwanza kwa hela ndogo aliyokuwa nayo hadi Dar ili aje kufanya alichoamini ni kipaji chake. Unaweza ukadhani  alikuwa anacheza karata tatu au kamari, kwasababu lolote lile lingeweza kutokea kwenye safari yake na labda tusingepata kumsikia hata mara moja.

Bahati mbaya (kwa wapinzani wake) na nzuri (kwa mashabiki wake), alipewa nafasi ya kughani kwenye wimbo mmoja unaoitwa Ukweli na Uwazi uliopo kwenye album ya Wachuja Nafaka. Fid Q akatoka rasmi. Ukisikiliza nyimbo zake mbili za kwanza, utaafiki kuwa alikuwa anajiamini na anaamini alichokuwa anafanya.

Sio kazi na dawa, bali ni kazi na kazi

Ingawa sipendi kurusha mawe ya lawama, nitajiona mwenye hatia kama nisiposema haya yafuatayo kwa wale ma-DJ na waandishi wa habari wanaopata fursa ya kuwahoji watu waliofanikiwa kwenye fani mbalimbali.

Waandishi hamna budi kuuliza maswali yatakayozaa majibu yenye manufaa.

Wachache wenu mmesahau kuwa kazi mliyokuwa nayo ni dhamana. Mna zana zote za kubadilisha fikra za watu wanaosikiliza vipindi vyenu. Mimi siridhiki mnapotaja tu wimbo au kitabu fulani cha mhusika kitatoka lini na mambo mengine kama hayo kwa dakika thelathini!

Mnasahau kuwa kazi mnazoletewa ni matunda yanayotokana na juhudi, jasho na uwajibikaji wa wahusika. Kwanini mnashindwa kusisitiza kazi nzuri hutokana na watu kujituma? Vipi, mbona mnashindwa kutuambia zile shows nzuri za Waunaume Halisi au TMK zinatokana na vijana kufanya mazoezi kila siku?

Ukiongea na watu waliofanikiwa utagundua kuwa, ukiacha vipaji walivyonavyo, ni wavumilivu na wanajituma. Kwahiyo, kijana mwenzangu, ukishagundua kipaji chako, huna budi kukilea, kukitunza na kukilinda kama mboni za macho yako. Na muhimu zaidi ni kukifanyia kazi kila siku; hakika hiyo ndio njia pekee itakayokuletea matunda.

Ukiangalia kulia, kushoto, mbele na nyuma utaona ‘vita baridi’ kati ya kizazi cha vijana wa sasa na wa zamani. Bahati mbaya vijana wa sasa (wanaonekana) wamepoteza matumaini na wamebakia kulaumu, ilihali wanaweza kuamka, kugundua vipaji vipaji vyao, kujenga moyo wa kujiamini na kufanya kazi ili kuleta mabadiliko.

Kila mkoa unatakiwa kuwa na vijana kama hawa!
Kila mkoa unatakiwa kuwa na vijana kama hawa!

Nchi inahitaji kina Modesta, Zitto na January kwenye kila mkoa; viongozi wapya wanahitajika. Magazeti yanahitaji waandishi wanaoweza kuakisi mawazo yetu. Jenerali Ulimwengu akistahafu, hatuna budi kuliziba pengo lake kwa kuwa tutaendelea kuhitaji makala zitakazotufanya tufikirie. Wahandisi na wanasheria wanahitajika na wataendelea kuhitajika.

Kijana, huu ni waraka kwako: Tambua na tumia kipaji chako ipasavyo — usijidharau.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 7 Comments

7
  1. Fantastic article SN:
    Absolutely priceless

    Jifunze kutoka kwa waliofanikiwa

    Hapa kwa wabongo tunakazi kidogo, maana kuna upungufu ma role models kwa vijana, aidha kutokana na viongozi wa ngazi za juu nchini kujihusisha na ufisadi, ujambazi na rushwa, hatuwasaidii vijana na watoto wetu kwa hili, maana kuna hulka TZ kwamba ku punch kimaisha lazima ukwapue, upige bomu au uwe na mahela sana, Na ndio maana kwa sasa, kuna msisitizo hapa nyumbani kuwa tunataka kuwaona wakina modesta, wakina January na akina SN wakihamasisha watoto na vijana wetu. Hata wasanii vijana waliobobea kama kina AY, Prof Jay n.k. Na sababu wao wako kwenye public eyes, wanalo jukumu bila kupenda kujiepusha na mambo ya ajabu, najua inakua tabu kweli kweli lakini ndio dunia yetu ilivyo kwa sasa kutokana public na media scrutiny. Tunaomba nyie mliobahatika kusoma na kuwa kazi zenu, muelimishe umma na kuwasisitizia kuwa kila mtu anaweza kuwa na maisha mazuri tu kwa kusoma au kwa kufuata nyayo za waliofanikiwa kimaisha kihalali! Upande wangu nilibahatika kuwa na kaka aliekuwa akipenda kubukua mno, pamoja na kwamba uwezo wangu kimasomo ulikua mdogo, nilijikongoja mpaka nilipoishia leo. Kasheshe kama watoto na vijana watafuata nyayo za mtu mtukutu na mbabaishaji, hapo kazi ipo!

    Tambua una vipaji

    Kuna kawaida ya wazazi TZ kuwakatisha tamaa watoto na vijana wapendao usanii wa kuimba, kuchora na kuigiza, kwa mantiki kwamba hawataweza kujimudu kimaisha hapo kwa baadae, sio kweli kutokana na mifano tulionayo kwa sasa TZ, wazazi, makaka na madada, tujitahidi kuwapa moyo na misaada ya hali na mali kwa watoto na vijana wetu, hasa baada ya kuhakikisha wanapata elimu ya kujua kusoma, kuandika na hesabu. Mwenzenu ningeweza hata kuchezea timu ya taifa (nawafunga kamba hapa!) kama wazazi wasingeniponda na kusema soka haina malipo. Inawezekana walikua sawa maana enzi hizo soka ilikua haina sponsors wala kuthaminiwa. Ila nina struggle kujua watoto wangu wana vipaji vya aina gani mpaka leo, uzuri ni bado wadogo, kasheshe niliambiwa juzi juzi na watoto wangu wa kike wa miaka tisa na kumi na tatu, eti wanataka kuwa “dancers”! Wazee nilifanya kosa la kuhamaki na kuwakumbusha kuwa mie na mama yao hatujafunga safari ya maili kadhaa kuja nchi za watu ili watoto wetu wawe “dancers”. Did I overeact? I think so, but what would you have done?

    Usiogope kukosolewa

    Mpaka leo napata tabu nikikosolewa, ila kidogo nina ahueni, kidogo huwa navuta pumzi na kuesabu mpaka kumi, na kutafakari yaliosemwa au kuandikwa, na kuchanganua. Najaribu kuwahimiza hata watoto wangu kuhusu hili swala, kama kweli wananisikiliza! Sababu ni tabu mno SN kukosolewa, hasa baada ya kuweka nguvu zako zote kwenye jambo fulani halafu unakuja kuambiwa eti hapo mkuu ni zero! Ila Kama tukiweza kukubali kukosolewa basi, kusonga mbele kimaendeleo ni rahisi zaidi kuliko kutokukubali.

    Jiamini na amini unachofanya

    Na kamsemo kangu kuwa, confidence without arrogancy is so welcoming to many people, pamoja yote ni lazima mtu ujiamini na ukumbuke kuwa utakosolewa kutokana jambo lako, iwe unafanya presentation, mtihani au kuchangia jambo. Bila kuwa na imani unachokifanya duniani basi unakua kama hujui baadae utataka kazi yako iwe ipi, kazi ni kazi, usanii, ualimu, soka, udaktari, ufundi na n.k. Uzuri ni kwanza kujua unataka kufanya nini, halafu unaweka nguvu zako zote kuelekea huko, usikate tamaa upatapo misukosuko, hiyo ni kawaida ya maisha.

    Sio kazi na dawa, bali ni kazi na kazi

    SN kwangu mie ni kazi na kupumzika kwa njia nizijuazo! Lakini huwa najikumbusha kuwa pamoja na kufuraia kufanya jambo fulani, bado kuna kazi zaidi mbele, sitaki kubweteka na kusema eti ndio nimefika kwa swala hili au lile, akili zetu na uwezo wetu ni mkubwa mno, labda kinachotufanya tusifike mbali zaidi inakua sa ingine ni vifo, kuumwa au kupoteza mwelekeo. Ila ni kweli kwa sasa wa TZ inabidi tuige mifano ya kupenda kufanya kazi, aidha za kuajiriwa au kujiari, mdingi wangu alikua na kawaida ya kunikumbusha kuwa niwe nahakikisha siku haipiti hivi hivi bila kufanya jambo fulani aidha nyumbani niishipo, kazini au shuleni.
    Haya yote tukiyawakilisha kwa watoto na vijana, basi maendeleo kwa wa TZ yataongezeka.

  2. Nionavyo, naona umeamua kuandika makala nyingine! Shukrani kwa kutupa mtazamo wako kama mzazi.

    Kwanza, nadhani ni vizuri tukifahamishana kuwa hii makala ni mchango wa wetu kwa tovuti ya Bongo Celebrity. Ni matumaini yetu ujumbe utafika kwa kutumia maudhui ya watu maarufu waliofanikiwa Tanzania, hasa watu wanaofuatiliwa na vijana wengi.

    Pili, Nionavyo, sio busara kuweka jina la mwandishi kwenye sentensi moja na kina Modesta na January!… You might get banned!

    Sasa, ukiacha yale mambo ambayo tunayasikia kila siku kutoka kwa niliowataja, nadhani kuna mambo ya kujifunza kutoka kwao — kama nilivyoelezea hapo juu. Lakini, kwa mtazamo wangu, nadhani wakianikwa hadharani hawaulizwi maswali sahihi yatakayozaa majibu yenye manufaa kwa watu ambao hata hawapendi muziki.

    Bahati mbaya, wale ‘role models’ ambao wengi wetu tungependa wawe kwenye majarida ya vijana kila siku, hawaonekani. Binafsi nadhani wapo wengi tu. Je, wanajificha? Au jamii yetu inawapa kisogo? Pop culture? Nini kifanyike?

    Mimi nawashauri watu ambao ni wanasiasa vijana, wahamasishaji, wanasayansi, walimu n.k. wajitokeze na wafanye yote wanayoweza kuelimisha wadogo zetu. Mimi nina role models lukuki — no. 1 ni Ben Carson (mama yangu alinunulia vitabu vyake)! Halafu kina William Kamkwamba ndio wanafuata (na Paul Scholes).

    Ukija kwenye mambo ya kukosoana, hapo kuna mtihani mkubwa. Kwanza, mara nyingi watu wanapokosoa (soma: Watanzania), hawatoi mawazo mbadala; kukuza kile ulichonacho au kukupa mtazamo tofauti. Mwishowe mtu ananywea na matokeo yake mtu anakuwa hajiamini.

    Na kuhusu “kazi na kazi”, nilikuwa naweka msisitizo kwenye ule moyo wa kujituma. Hakuna mtu anayefanikiwa bila kufanya kazi kwa juhudi! Hata geniuses push themselves to the limits…

  3. SN:

    Sawasawa, si unajua tena mkuu, I don’t do small! Sikawii kuiba kesi ya mtu na kuigeuza iwe yangu!
    Anyway, haya ndio maisha, kuiga mifano mizuri kwa waliokutangulia, bila kusahau kufumba na kujifanya kutokuyaona yale ya kubabaisha.

    Asante mkuu.

  4. Mimi nitatilia mkazo role-models. Tunao wa kutosha katika fani kama za muziki na sanaa, na vijana wanapata kuwaona/sikia kupitia TV/Redio. Wafanyabiashara mashuhuri je (industrialists kwa mfano)? Au wale wahandisi/architecturers wetu; je, wanafahamika na vijana wetu wa shule?

    Ningependa kuona shule zetu zikijaribu kuinua muamko wa kukuza vipaji kwa njia kama ya kuwaalika waliobobea katika fani fulani kutembelea shule na kuandaa mazungumzo na wanafunzi.

    Sidhani kama kwenye TV au Redio kijana ataweza kusikia kuhusu ni aina gani ya kipaji kinahitajika ili uwe mtu kama Ole Moiyoi:

    http://www.guardian.co.uk/science/2003/nov/13/scienceinterviews.research

    1. Hii ya Ole Moi-Yoi ni kali sana!

      Inaonekana tunaanza kutupia lawama vyombo vya habari. Labda watu wenye mafanikio kwenye fani nyingine za kitaaluma (zaidi) hawajitokezi, na kuwasukuma watu wa vyombo vya habari kuanzisha vipindi vya kuhamasisha wadogo zetu? Nikifikiria haraka haraka tu, ninafahamu zaidi ya vijana 20 (wa rika langu) ambao wanaweza kufanya haya mambo…

      Hata hapa tu, nimewaomba watu lukuki wanaofanya vizuri kwenye mambo kibao (hasa sayansi) kuja hapa na kusaidiana kufanya kitu cha maana; kuwahamasisha wenzetu (i.e. uplifting them) na kupeana taarifa muhimu… Lakini wapi! Hata kutoa mchango wako tu kwa kuandika maoni yako kwa kirefu ni mwanzo mzuri. Halafu baada ya miaka 20, wakiwa na watoto wao, watakuja kuvilalamikia vyombo vya habari kwa kutowapa nafasi watu ‘wanaowataka’.

      Mi’ kusema ukweli nimechoka kulalamika. Wengi hapa tunajua suluhisho la haya matatizo au mambo yanayoonekana kwenda mrama — ni kufanya tu unachoweza. Mmenipa wazo, nitahifadhi hizi makala sehemu halafu nitawaonesha watoto wangu huko baadae! Ingawa najua kulea mtoto na kuwapa muongozo vijana ni kazi nzito sana, sio vema kukata tamaa kabisa bila hata kujaribu.

      @ Nionavyo, kuhusu huyo aliyesema anatakuwa “dancer”, ungemwambia, “Hiyo ni hobby mwanangu. Hutaki kuwa kama Obama?”

  5. hahahah, hiyo ya kuwa dancer imenichekesha, manake hata mimi nilijaribu kujiweka kwenye nafasi yako, na kujipima kuona, je ingekuwa ni mimi ningesemaje..kazi ipo hapo. Nadhani SN ametoa jibu zuri, si la kutahamaki, wala la hasira lakini ujumbe umefikia mtoto bila kumfanya ajisikie amekaripiwa au kuvunjwa moyo na wazo lake.

    Suala la wana sayansi bongo ni kitu ambacho kipo kinasikitisha kwa namna nyingi sana. Kuna kipindi nilipata kuona watafiti wakienda kijijini kuonana na wanasayansi wa kitanzania. Nia ya huu umpango au utafiti, ulikuwa unalenga kutafuta wanasayansi wa nchini ambao wamevumbua teknolojia rahisi na ambazo zinaendana na mazingira yetu. Hivyo basi teknolojia yao hiyo, iweze kusaidia watu wenye kipato cha chini na hasa wale wa kijijini.

    Kitu kimoja walichokiangalia ni suala la, ni jinsi gani teknolojia zao zinawza kusaidia kulinda mazingira. Basi bwana, watafiti hao wakaenda kukutana na babu mmoja, (nimesahau kijiji gani) ambae alikuwa amevumbua jiko la kutumia miyonzi. Najua hili sio jambo geni siku hizi lakini mimi nazungumzia zamani kidogo, hivyo teknolojia hii ndio kwanza imevumbuliwa vumbuliwa.

    Mzee yule kweli alikuwa na kipaji na mawazo endelevu. Lakini sasa juhudi za watafiti hao, ambao baadhi yao walikuwa wanasayansi, nadhani zilikuja kugonga mwaba na urasimu wa Serikali na mfumo wake. Basi, nadhani kile kilicho vumbuliwa hakipewa maanani, na yule mwanasayansi hakuchukuliwa kwa umakini, hivyo kila kitu kikaishia hivyo hivyo tu.

    Kuna ujinga na kasumba, kama hii ya kuongea kiingereza ndio kuwa na akili, ndio hivyo hivyo kwenye mambo mengine. Kama ulichofumbua sio cha nje, au siyo kama vitu vya nje, basi hakina maana. Sasa kama hilo jiko, nadhani watu waliliangalia wakaona na teknolojia rahisi hivyo haina maana. Bila kujua kuwa, jiko hilo linaweza saidia watu wengi, na kupunguza ukataji wa miti. Huu ni mfano mmoja tu, kuna wavumbuzi wengi waliovumbua vitu ambavyo ni rahisi lakini zinakwendana na maisha ya mtanzania wa kawaida, hasa kule kijijini. Lakini ndio hivyo tena, hawapewi umakini na wala hawatambuliwi. Tanzania nadhani ni katika nchi pekee ambayo usemi wa mcheza kwao hutunzwa, una maana tofauti, bali ni cheza kwao hupewa kisogo, hushangaliwa tu, na hata kuonwa kama kituko. Hivyo mimi kwa kiasi fulani naelewa kwanini kuna baadhi ya watu wamekata tamaa

  6. @SN.
    Sikutegemea kama utakua mshabiki wa ManU, hapo baba umechemsha! Mie napendelea the Gunners, na kipenzi changu kilikua Viera, kwa sasa sina ila kale ka Wilshere kananiacha hoyi.

    @Bahati.
    Nakwambia mama yao ilikua kasheshe, alicheka mpaka akatoa machozi, huku mie siamini kama niliwasikia vyema au la! Ndio maisha lakini.

Leave a Reply to Bahati M Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend