Uchaguzi 2010: Vyombo na vyanzo vya habari

Uchaguzi 2010: Vyombo na vyanzo vya habari

Leo hii Msajili wa Vyama akitangaza chama kipya cha siasa kinachoundwa na kabila fulani moja tu Tanzania, wengi tutashtuka, kisha wachache wataanza kuhoji. Kama hiyo haitoshi, wachache sana wataweza kuliangalia suala zima kwa ‘jicho la tatu’, kulichambua na hata kujaribu kutabiri mwelekeo wa nchi iwapo makabila mengine yatafuata mkumbo na kuunda vyama vyao.

Ngoja kwanza. Kama aya iliyopita imekufanya uanze kujiuliza maswali mengi, basi jua fika kuwa hilo ndilo lengo hasa la hii tovuti; kuwakutanisha watu — hasa vijana — na kubadilishana mawazo, kwa maana hatuamini mtu au kundi la watu fulani linajua kila kitu.

Tanzania, kama jamii nyingine yoyote ulimwenguni, ina mazuri na mapungufu yake. Hivyo itakuwa jambo la busara kuangalia nini kilitokea kwa majirani zetu ili kujifunza mawili matatu. Hii itatusaidia kuzuia maafa yoyote yanayoweza kutokea huko mbele.

Kama unadhani jamii yetu ni “takatifu” na haiwezi kukumbwa na majanga yaliyowakumba majirani zetu, nakusihi ujaribu kupembua mambo kwa kina ili uujue ukweli.

Kabla ya kuzama kwenye mjadala wa matumizi ya vyombo na vyanzo vya habari kwenye mchakato mzima wa Uchaguzi, itakuwa vema ukisoma makala ifuatayo ili tuweze kuelewana vizuri: Spreading the word of hate (Kenya). (Usiwe mvivu kwasababu tu makala ni ‘ndefu’; uzito wa haya mambo huhitaji mijadala ya kina!)

Taarifa au kampeni?

Kampeni zilianza kwa mwamko wa aina yake, ambao nadhani haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Tanzania. Lakini, kwa mtazamo wangu, kulikuwa kuna walakini jinsi matukio mbalimbali yalivyokuwa yakiripotiwa.

Baada ya kuwa mtu mzima na kupevuka kifikra nimeondokana na ile dhana ya “kuamini” kila taarifa ninayopokea. Nafikiria mambo mara mbili-mbili na kuhakiki kwa kutafuta taarifa zaidi (au nyingine) kwenye vyanzo vingine vya habari.

Ingawa nilikuwa ughaibuni, nilikuwa nina shauku kubwa mno ya kutaka kujua na kupata picha halisi ya mambo yanayojiri kwenye majimbo mbalimbali. Kuna wakati nilikuwa natembelea tovuti na blogs zaidi ya kumi kwa siku ili kupata picha halisi.

Labda unajiuliza, nini kilinisukuma kutembelea vyanzo vingi vya habari? Si kupoteza muda tu?

Baada ya vyama mbalimbali kuzindua kampeni zao, watu wengi, hasa wa vyama vya upinzani, walilalamika kutotendewa haki kwenye taarifa za habari. Na baadhi ya watu hawakusita kuanzisha vyombo ambavyo vilikuwa vinafuatilia kila chama kinapewa muda gani kwenye taarifa za habari.

Ingawa suala la muda ni muhimu, mimi niliamua kufuatilia jinsi matukio yalivyokuwa yakiripotiwa. Kimantiki ni kama ilivyokuwa inafanyika hapa. Kwa mtazamo wangu, kitu ambacho niliona na kinapaswa kuangaliwa kwa ‘jicho la tatu’ ni ile hali ya “utengano” (namaanisha polarization) wa maoni na mawazo ya watu, na hata matumizi ya lugha kwenye habari na mijadala mbalimbali. Kibaya zaidi, maoni ya wasomaji wengi yalikuwa hayana hoja, kitu ambacho kinakufanya ujiulize maswali mengi.

Siku chache kabla na wakati wa Uchaguzi

Bahati nzuri nilirudi nyumbani, Dar es Salaam, wiki moja kabla ya Uchaguzi na kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Hali halisi ilikuwa sio tofauti sana na ile picha niliyokuwa nayo. Kumbuka ya kuwa nilikuwa ninatembelea vyanzo lukuki vya habari; kinyume na kwenda kwa Michuzi au Jamii Forums tu na kuridhika na nilichoona pale.

Hali ilikuwa shwari, ila mwamko wa vijana ulikuwa ni wa kipekee sana! Kila kijiwe, kila sehemu, kila mtu alikuwa anazungumzia Uchaguzi. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba baadhi yao walikuwa wana hoja, tofauti kabisa na makelele niliyokuwa nayaona kwenye blogs.

Siku yenyewe ya Uchaguzi ilikuwa na matukio mengi. Sasa, hapo ndipo ile “jinsi” ya kuripoti mambo ilipochukua kiti cha mbele kabisa kwenye hafla. Maneno “kasoro ndogo ndogo” yalikuwa yamejaa kwenye vinywa vya wana-habari wengi sana. Ila wachache mno walikuwa na kiburi cha kukemea hizo “kasoro ndogo ndogo.”

Vinyonga

Nitakuwa sijatenda haki kama nisipogusia vitendo vya wana-habari na waandishi wa TBC 1. Vituo mbalimbali vya runinga vilianza kutanganza matokeo ya awali, yakiwemo ya Urais, kutoka kwenye kata mbalimbali. Na tarehe 1 Novemba, wakati naangalia TBC, nilidhani naangalia kituo tofauti cha habari! Kwa mara ya kwanza walialika mgeni ambaye alikuwa anakosoa mwenendo mbaya wa uongozi, na kueleza labda hiyo ndio ilichangia kambi ya upinzani kuelekea kupata viti vingi Bungeni.

Nikashindwa kujizuia kuhoji: je, ule mjadala ungekuwepo kama upinzani usingeelekea kushinda majimbo kadhaa? Walikuwa wapi kabla ya Uchaguzi?

Pia, kama ulikuwa makini, utagundua kulikuwa na mabadiliko ya mwenendo wa blogs fulani maarufu kwenye utoaji taarifa. Yaani, ghafla kulikuwa na taarifa kutoka kambi ya upinzani!

Chanzo cha matokeo na taarifa za matukio

Sijui kama ilikuwa ni busara au la kusitisha zoezi la utangazwaji wa kura za Urais kutoka kwenye kata mbalimbali. Ila nina uhakika unapata picha tete kama matokeo ya awali yangetofautiana kabisa na yale ya Tume ya Uchaguzi.

Bahati mbaya au nzuri, wote tukaishia kwenda Jamii Forums ili kupata taarifa za matokeo na matukio mbalimbali haraka zaidi. Bahati mbaya,  mambo yalikuwa kishabiki zaidi na nilisikitishwa na kitendo cha viongozi kuacha watu waandike chochote kile wanachotaka; kiwe na lugha za kukashifu, kusifia, kukosoa, kuelemishana au hata kutoa taarifa tu.

Labda unaweza ukanipinga kwa kusema hiyo ndio ‘demokrasia’ ya kweli, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni na mawazo yake.

Kumbuka, hivi vyombo vya habari vinakuja na dhamana, hasa pale watu wengi wanapovitegemea kupata taarifa nyeti. Visipotumiwa ipasavyo ndio hapo tunashuhudia majukwaa muhimu yakigeuzwa kuwa vyombo vya propaganda; na kushindwa kutupa picha halisi.

Lakini kulikuwa na watu wachache ambao hawakuchoka kuulizia “data” au “namba” kila mtu alipoleta taarifa. Jiulize, hao ni sehemu gani ya jamii yetu? Watu wangapi hupenda kuhakiki taarifa au habari fulani?

Mwishowe, kwasababu wengi wetu hatuwezi kufikiri wenyewe na kuuliza maswali ya msingi, tunaishia kwenda kwenye vyombo ambavyo vinaakisi mawazo yetu tu. Hatupendi kusikia mawazo mbadala ambayo hayatufurahishi. Yaani, kwa maneno mengine, tunapenda kwenda sehemu ambazo zina watu wenye mawazo kama yetu tu.

Hebu fikiria, tuwe na majukwaa mawili ambayo yana wachangiaji wenye fikra na mawazo (namaanisha porojo) yanayokinzana kabisa. Kila kundi litaamini wanachojadili kila siku kwa dhati. Itakuwaje hawa watu wa makundi husika wakikutanishwa mitaani?

Naamini Uchaguzi wa mwaka 2015 utakuwa una mwamko zaidi. Na kama hatutarekebisha kasoro zilizojitokeza — hususan jinsi ya kuripoti — basi tutaishia pabaya.

Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.