Mifumo ya elimu Tanzania

Mdahalo kuhusu mfumo wa elimu ya Tanzania umekuwa ni mjadala wa muda mrefu sasa. Hapo mwanzo, enzi za Mwalimu Nyerere, matarajio na malengo ya mfumo wa elimu ulikuwa kwanza kupinga ujinga. Hivyo basi, lengo lilikuwa kuhakikisha kila Mtanzania anajua kusoma na kuandika ili kuweza kujitegemea; “education for self reliance.”

Leo hii, tunaweza kuwa na mdahalo wa kujadili mfumo wa elimu katika kipindi cha Mwalimu kama ulifanikiwa au la. Vyovyote vile tukakavyokubaliana katika mwisho wa mdahalo huo, matokeo hayataathiri ukweli — kuwa tulijua kwa dhati malengo na matarjio ya mfumo huo yalikuwa ni nini. Lakini dunia ya enzi zile sio dunia yetu ya leo, hivyo malengo na matarajio hayawezi kuwa sawa, au sio?

Dunia imebadilika sana, tangu enzi za Nyerere mpaka hivi leo, mabadiliko haya yakichangiwa vilivyo na utandawazi. Dunia imekuwa kama kijiji kimoja, huku ushindani ukiongezeka kwa kasi kubwa. Malengo na matarajio ya mfumo wa elimu ya Mwalimu Nyerere leo hii yangekuwa hayakidhi mahitaji ya soko la dunia. Kwani, kujua kusoma na kuandika pekee hakuwezi kukufikisha mbali maishani, ingawa ni kitu muhimu.

Hivyo, tulianza na mfumo uliohakikisha unatokomeza ujinga. Huo ndio ulikuwa msingi ambao ulijengwa na Serikali ya awamu ya kwanza. Kazi ya awamu zilizofuata zilikuwa ni kujenga kuta, kuweka madirisha, kuwezeka paa, na mambo mengine muhimu yanayohitajika katika ujenzi wa nyumba bora. Nyumba hiyo leo inafananaje? Tujiulize. Kwa maneno mengine, ninaweza kuuliza, malengo na matarajio ya mfumo wa elimu katika awamu zilizofuata umekuwa ni nini? Je, mifumo ya elimu iliyofuata ilikuwa na malengo ya kuchochea ongezeko la shule binafsi, na kuongeza idadi ya wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nje au ni kuboresha elimu ya Tanzania iwe ya ushindani kama enzi zile?

Mimi leo bado sielewi vizuri matarajio na malengo ya mifumo ya elimu iliyofuata baada ya mfumo wa Mwalimu Nyerere imekuwa ni nini hasa. Ninadiriki kusema hilo, kwani malengo na matarajio ya single book system ya Tanzania bado ni tata. Kama matarajio hayo ni kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mitihani, basi tumepiga hatua kadhaa nyuma, ndio maana nadhani itakuwa muhimu tukimsikiliza huyu binti katika video hii. Nadhani wasiwasi, maswali na mawazo yake hayapo tofauti sana na yetu, punde suala la mfumo wa elimu ya Tanzania linapowekwa mezani kujadiliwa.

Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete hatahudhuria mdahalo wa wagombea urais mwaka huu, hivyo hatuwezi kumuuliza maswali hayo. Lakini ningelipenda sana kujua Nyerere angekuwa na lipi la kusema kuhusu mifumo ya elimu uliyomfuata.

Previous ArticleNext Article
Bahati was born and raised in Tanzania, and then moved to California to pursue his college education. He graduated in 2008 with a Bachelor’s Degree in Political Science and a minor in Sociology. Bahati expects to be doing his Masters in African Studies in the near future. He is currently working on starting a t-shirt business and a possible publication of some of his writings. One thing that Bahati cannot live without is music, specifically Hip Hop & Bongoflava which he argues are both the voice of the youth today, and is excited to look into how Bongoflava can be a source of further entrepreneurship among the youth in Tanzania. Bahati believes that Bongoflava can help to reduce poverty in Tanzania, as can a more collective effort among key players.

This post has 19 Comments

19
  1. Habari nzuri,

    Pamoja na yote, Tanzania nafikiri tungekuwa na mfumo kama wa Uganda ama Kenya. Maana mwanafunzi anayemaliza elimu yake nchi Uganda ama kenya ana uwezo wa kuchanganua mambo mengi na ana uelewa mkubwa sana “Exposure”.

  2. Sidhani kama kuna mkakati mahsusi kuhusu suala hili nchini mwetu. Tumekuwa tukigaagaa tu. Serikali imezoea kubadilibadili ‘mipango’ miaka nenda rudi. Idhaniwayo ni mipango, mara nyingi ni ahadi hewa tu. Mfano: kuahidi kila mwanafunzi nchini kuwa na computer kabla ya 2015.

    Tatizo la access to education nadhani taratibu tunaanza kulisuluhisha. Karne hii mfumo wa elimu uzingatie hasa quality of education. Ningependa kuona kila shule iwe na maktaba iliyosheheni vitabu vya kutosha, na sio kuwa na maktaba gofu! Jambo hili tunaweza kulitatua sisi wenyewe tulio huku nje – nunua vitabu na vitume katika shule ya msingi kijijini kwenu. Au kama una resources zaidi, kuwa na kitu kama ‘mobile library’ ni jambo zuri. Library hii iwe inazunguka kijiji baada ya kijiji ikiazima vitabu kwa wanafunzi na watu wazima na kufanya ufuatiliaji wa maazimo.

    Mitihani

    Ninadhani itabidi tufute kabisa biashara ya mitihani ya taifa ya Form 4 na Form 6. Ningependa kuona mtihani mkubwa uwe baada ya kumaliza kidato cha pili. Nia ya mtihani huu uwe ni wa kuchuja wale wanaotaka kuendelea na miaka minne iliyobaki ya elimu ya sekondari ili wasioweza kabisa waongozwe kwenye shule maalum za ufundi, au sanaa – ili wa’explore vipaji vyao huko. Shule hizi ziwe legitimate na sio mwanafunzi anaenda huko akijiona kama ‘failure’ bali mwanafunzi aende huko akijisifia sifa kuwa anaenda kupokea elimu mbadala yenye manufaa fulani katika sekta maalum.

    Kwa wale wanaobaki mtihani utakaofuata uwe baada ya kidato cha nne ila, mtihani huu sio wa kuchuja wanafunzi (kama tuonavyo sasa ukipata Div 0 ndio basi tena) bali mtihani huu uwe maalum kwa waliofudhu kidato cha pili na kuwawezesha wanafunzi kujipima uwezo wao. Mtihani huu uwe maalum kwao ili waweze kuamua kama watataka kuendelea na miaka miwili iliyobaki ya sekondari (final cut-off point).

    Baada ya hapo mitihani itakayofuata iwe mitihani ya kitaifa ya mihula, ambayo kila mmojawake uhesabike sawasawa na mingine itakayofuata katika mihula ya mbele kwa kipindi cha miaka miwili (Form 5 na Form 6). Kuna semester mbili kwa mwaka, kwahiyo, mwanafunzi akiwa kidato cha 5 atakuwa na mitihani miwili kwa kila somo (Paper I and Paper II), na akiwa kidato cha 6 ataendelea kutihaniwa katika ‘series’ hiyo ya somo, Paper III na Paper IV. Mitihani yote hii minne kwa somo (each count for 25%) ihesabike baada ya kumaliza Form 6 na kutoa daraja la mwanafunzi. Mtaala huu utasaidia kumtayarisha mwanafunzi kwa elimu ya juu, na hivyo kutomfanya mwanafunzi kufikiria mtihani mmoja wa Form 6, unaofanywa kwa wiki mbili tu lakini unaoamua mustakabali wa maisha yake yote. In addition one can have another assessment in form of a project which has do be conducted during the course of the 2 years. For science students it can be on a particular scientific practical experiment – unique in nature – whose report will be examined, whereas, for humanities or social science students they can perform an extended written work on a particular research problem and submitted to a central office.

    Matayarisho kwa ajili ya mitaala hii inabidi ianze mapema. Kwanza, walimu waongezwe mshahara. Ualimu iwe ajira inayohitaji angalau B.Sc au BA kwa shule ya msingi (vyuo vya ualimu vitoe shahada hizi) na kuendelea kwa shule za sekondari. Wanafunzi wahimizwe kujihusisha darasani kwa kuuliza maswali na umuhimu wa mijadala ya darasani.

    Nimegusia machache tu hapa, ila ni mengi ambayo ningependa kuyaona katika mfumo wetu wa elimu. Arrgh, sitamaliza, ngoja nijimuvuzishe TED.

  3. @Patrick, asante kwa mchango wako. Umenifanya niwe ‘curious” ulivyozungumzia mifumo ya Kenya na Uganda na jinsi inavyoandaa wanafunzi. Mitaala/ mifumo yao ina utofauti gani na tuliyonayo Tanzania, na nini wanacho humo kinacho wanafanya wawe ‘successful’ kutuzidi..

    @Joji, mzee si mchezo, kweli wewe inabidi tuanze kukuita mdau wa elimu. Nakumbuka kuna kipindi waziri wa elimu Mh Mungai alichezea chezea mfumo akaharibu kila kitu. Alivyochukua wizara hiyo Mh. Sitta, akarudisha kama mambo yalivyo zamani, ikiwa pamoja na umiseta nadhani, au michezo mashuleni. Nadhani huu ni mfano mzuri wa sisi kutokuwa makini na mfumo wetu wa elimu, kwani kuna try & errors nyingi.

    Ulivyogusia maktaba nikakumbuka hii clip ya CNN. Nadhani mpango kama wa huyo jamaa ni mpango ambao ungesaidia sana vijijini. Kama Tanzania tunaweza kupata nguo za mitumba kwa bei chee kutoka nje, kwanini tusianzishe ‘book drive’, tuwe nampango wa kununua vitabu mitumba kutoka nje. Vitabu hivyo vinaweza kutumiwa huko vijijini au sehemu nyingine. Lakini najua, kununua vitabu vya mtumba kutoka nje, havitakuwa kwa lugha ya kiswahili, hivyo hilo laweza kuwa tatizo namba moja.

    Kuhusu uwezo wa walimu naungana na wewe kabisa. Nadhani kuna umuhimu wa kutahini walimu vilivyo na kuhakikisha wana elimu na uwezo unaoridhisha kufundisha.

  4. Kwanini Watanzania huwa tunamu-idolize Nyerere kwenye kila kitu? Ni jambo la kusikitisha sana. Ingawa Nyerere alijitahidi kufuta malengo ya wakoloni kwa kupeleka watu shule, nasikitika kuwa hakuna la maana zaidi lililofanyika ku-revolutionize system ya elimu yetu ili iweze kutusaidia baada ya miaka 50 ya uhuru. Blueprints za miaka hio zingeweza sana kutoa direction ya elimu yetu.

    @Joji, nimefurahia discussion yako ila ninadhani inachambua zaidi system ya elimu ya Uingereza ambayo pia ina mapungufu mengi yanayolalamikiwa hata na Waingereza wenyewe. Kusema kweli IB system ingesaidia sana kama ingekuwa kama sehemu ya mitaala ya nchi yetu.

    @ Bahati M, nimependa idea ya book drive, itafanya watanzania wengi wapende kujisomea na hili litainua kiwango cha ufahamu kwa community yote.

  5. @Anon, hata mimi nasikitika mpaka leo tunamu-idolize Nyerere kiasi hichi. Nasema hivi nikiwa na maana hii, Nyerere alifanya mengi ya msingi, kama ninavyo zungumzia, swala la kuwa alijenga msingi. Mimi nasikitika kutokana na kuwa mpaka leo hatujapata mtu ambae ameweza kufuata nyayo zake na kufanya mengi mazuri katika nyanja ya uadilifu na itikadi ya uongozi. Hiyo ni challenge kwetu vijana, kwani katika kizazi chetu na sisi tutahitaji mtu kama Nyerere ambae ni wa kizazi cha wazazi wetu.

    Nimefurahishwa na mchango wako, kwani umenifanye niwe na hamu ya kujua mapungufu ya mfumo wa elimu ya Uingereza aliyo izungunzia ndugu Joji. Mimi binafsi sijui mfumo wa Uingereza vizuri, zaidi ya mtihani wao wa IGCSE.

    Kidogo niko familiar na IB system, lakini out of curiosity, kwanini unadhani mfumo wa IB utatusaidia Tanzania?

  6. Mfumo wa elimu Tanzania umegeuka mradi wa mchicha au sukuma wiki! Inasikitisha kiasi cha kulia na kusaga meno – lakini huu sio wakati wa kulia na kusaga meno.

    Mwaka 1995:

    Hapa ndipo palifanyika mabadikilo lukuki katika sera ya elimu nchini, na kwa kweli ukiisoma sera yenyewe [bofya], utafurahi na kushangaa.

    Utafurahi kuona kwamba watu walioifikiria na kuiandika kweli walijitahidi kufikiri mahitaji ya Mtanzania kielimu kwa wakati huo. Walitilia maanani mabadiliko yaliyokuwa yametokea duniani.

    Na kama umesoma shule ya msingi, sekondari au chuo (katika kipindi cha 1995 mpaka sasa) UTASHANGAA maana sera hiyo kwako itakuwa ngeni mithili ya viumbe wa sayari ya Zebaki (hakuna viumbe waishio Zebaki!). Ni machache sana ambao utayaona humo, ambayo utakuwa umewahi kuyaona katika kukurukakara zako za kielimu!

    Tatizo:

    Ufanisi au nguvu ya mfumo fulani, inapimwa kwa kipengele chake ambacho dhaifu kuliko vyote (Waswahili wenzangu nisaidieni hapa; ninajaribu kusema, “a system is only as efficient/string as its weakest/least efficient component.“).

    Elimu pia, kama mifumo mingine, una vipengele mbalimbali ambavyo vinategemeana ili kuhakikisha unatimiza malengo kusudiwa kwa ufanisi. Hivyo basi, ikiwa kipengele cha sera kinaonekana kuwa decent, kwa kiasi fulani, na hali halisi ya elimu mashuleni na vyuoni inaonekana kuwa duni (kuna shule lukuki hazina darasa hata moja, wanafunzi wanakaa kwenye udongo, na zingine zina mwalimu mmoja anafundisha Inglishi mpaka Jografia na Hesabe n.k. yeye mwenyewe. Sisemi kwamba hawezi lakini haitakiwi kuwa hivyo!) basi kutakuwa na tatizo katika kipengele fulani. Hapa ndio ule mradi wa mchicha na sukuma wiki unapokuja!

    Implementation ya sera ya elimu imegeuzwa mradi wa mboga za fastafasta. Unapanda leo, unamwagiliamwagilia na maji ya mtaroni, wiki mbili unavuna, unauza, unapanda tena mbegu nyingine! Baada ya miaka minne, bado unalima kabustani kalekale na hakuna maendeleo yoyote!

    Wizara ya Elimu ndiyo imekuwa na majukumu ya kutafsiri sera ya elimu kuwa vitendo. Ninaposema vitendo ninamaanisha kuanzia miongozo mbalimbali ya wadau mbalimbali wa elimu kama vile, walimu, wanafunzi, wamiliki wa shule, wasimamiaji wa shughuli za elimu, wakaguzi n.k. Na pia kuhakikisha miongozo hiyo inafuatiliwa kwa makini na kutendewa kazi. Hili halifanyiki. Lingekuwa linafanyika tusingekuwa na shule zisizokuwa na madawati leo hii, au mwalimu mmoja shule nzima!

    Kuna Haja ya Badiliko la kimtazamo:

    Ndugu Joji umeibua suala ambalo ni muhimu sana, hususani kuhusiana na vyuo, shule za vipaji (sio Ilboru, Mzumbe, Kibaha, Kilakala, Msalato n.k.) namaanisha vipaji vya sanaa, ufundi n.k. Vyombo hivi vya elimu kwa sasa vinaonekana kama mahali ambapo mtu akifeli darasa la saba, form four au form six, basi ndio anaenda huko! Hili ni kosa la jinai tena nathubutu kusema kuwa ni dhambi! Mtazamo uliopo kwa wengi ni elimu ya msingi — O-level — A-Level — Chuo kikuu! Ikitokea ukashindwa mahali flani huko katikati basi angalia vyuo vya ufundi na sanaa! Hapa ndio tunaua vipaji, na kushindwa kuwapeleka wajenzi kwenye miti!

    Mtu mwenye kipaji cha uigizaji, kuimba n.k. sio lazima akasome HGL, au HKL (halafu aishie kushindwa mtihani sababu alikuwa anaumwa malaria wiki mbili za mtihani)! Kwanza akienda kwenye hiyo shule yenye A-level, uwezekano wa kukuta rasilimali pamoja na support zitakazokuza kipaji chake ni mdogo mnoooo, wakati angeweza kwenda Bagamoyo chuo cha sanaa, akakutana na manguli wa kuimba na kuigiza, wakampika vilivyo akabobea, na akimaliza diploma yake, aapply chuo kikuu akitaka na kuendeleza libeneke!

    Kuna Haja ya Kubadili Mfumo wa Management ya Elimu:

    Sera ya Elimu ya mwaka 1995, ilikuwa based on theme ya liberalization (najiuliza hapa kama hakukuwa na pressure kutoka kwa donors wa misaada..kina IMF na WB na wengineo). Basi theme hiyo ikatumika kuparaganyua (Hivi hili neno ni la kiswahili au? Mie nimezoea kikwetu..Ila I mean kuusambaratisha) mfumo mzima wa management of educational institution.

    Decentralization and liberalization ni jambo zuri sana kwani linawapa wadau mbalimbali uhuru wa kuanzisha shule na kuchangia katika maendeleo ya taifa. Pia in theory, inaipa jamii nguvu na uwezo wa kushika hatamu katika sekta ya elimu ambayo ni muhimili muhimu sana katika maendeleo. Binafsi ninafikiri decentralization and liberalization ni jambo zuri likipangwa vizuri na likifuatiliwa vizuri.

    Ila sasa, mradi wetu wa mchicha na sukuma wiki ukaanza. Ghafla shule inabidi zijimeneji zenyewe, na pia jamii inapewa jukumu la kusimamia shule. Hapa kilichotokea ni kwamba kila shule ilitakiwa kuunda bodi, jumuiya ya wazazi (kuna shule nyingine nafikiri bado hazina hii kitu au kama ipo haitumiwi ipasavyo!). Pia kukawa na menejimenti katika ngazi ya kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa. Ila sasa mchicha wenyewe ulikuwa hivi. Hakukuwa na mwongozo wowote wa jinsi gani jamii (communities) au wanafunzi watai-hold menejimenti acountable.

    Labda nikuulize tu swali la kizushi wewe uliyeko shule Bongo sasa hivi! Hivi unajua serikali inaipa shule yako kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yenu wanafunzi? Umeshawahi kuiona bajeti ya shule? Achana na ile kwamba mwalimu mkuu amesema kwamba Serikali inatupa shilingi milioni tano tu au sijui shing’ ngapi… Je, umewahi kuona ripoti ya mkaguzi wa mahesabu ya shule yako? Kama hujawahi kuona, unafikiri utaulizaje maswali ya msingi kama huoni madawati shuleni kwenu, au huoni vitabu au huoni madarasa? Au umezoea tu kwamba “sisi ni masikini, shule haina hela, Serikali haina hela kwahiyo nitakomaa tu hivihivi nitoke?”

    Miaka michache pale Ilboru, kulitokea migomo na wanafunzi wakatokea kupata ripoti ya mwaka ya fedha nafikiri (sijui waliipataje). Si wakakuta imeandikwa kuwa wanafunzi wanakula samaki na machopochopo kibao ambayo hawajawahi kuyaona. Wakati wao wamezoea ugali, maharage, kande na KITEI mara moja kwa wiki?

    Suala la uwazi, transparency ni la LAZIMA na nafikiri itungwe sheria kuwa mambo kama bajeti ya shule na kiasi cha fedha ambacho serikali inatoa kwa ajili ya shule/chuo yawekwe bayana kwa walimu, wazazi wanafunzi n.k. Tena ichapishwe kwenye magazeti kabisa!

    Mwisho kabisa ili ku-prove point kwamba kuna tatizo kati ya sera na implementation. Kama umewahi kufanya mtihani wa form 4 au form 6: Hivi unajua 50% ni internal assesment (ripoti zako za muhula) na 50% ni mtihani wa mwisho? Unabisha nini? Hujui sera ndio inasema hivyo? Hahahaha… najua unajiuliza sasa utajuaje kama ni kweli? Ndio hapo, hatujui kama ni kweli au ni chai tunauziwa lakini inabidi haya mambo yawekwe bayana. There is a need for transparency!

    Imetosha kwa leo. Wacha niendeleeze useremala hapa… nachonga dawati!

    [Edited: Kutokana na umuhimu wa mambo uliyoweka bayana, SL, ilinibidi niweke na nipange mawazo yako vizuri ili kila mtu asome na kuelewa kwa urahisi. Shukrani sana kwa mchango wako! — Mhariri]

  7. @ SL; Ndugu kwa kweli nimeukubali uchambuzi wako. Nadhani itabidi niicheki hiyo ripoti ya mabadiliko yaliyo fanyika kipindi hicho. Lakini nini mtazamo wako wa mfumo wa elimu tangia aingie Kikwete? Pamoja naelewa kuwa kabda Serikali imekuwa haiko makini kwenye sekta ya elimu, lakini suala la kuwa, bajeti ya taifa ni finyu sana, hivyo haiwezi kutimiza hahitaji makubwa ya wizara zake, kama hiyo ya elimu, au hilo si kweli ki vile.

    Je, unadhani kuna njia mbadala ya namna ambavyo tunaweza kutumia hilo hilo fungu finyu la wizara ya elimu, tukawa wabunifu na kufanya mabadiliko ya muhimu yenye mafanikio mazuri, japo yanaweza kuwa sio ya kasi mpya na nguvu mpya?

  8. Lakini nini mtazamo wako wa mfumo wa elimu tangia aingie Kikwete?

    Mimi nafikiri alipoingia Kikwete kulitokea mabadiliko machache katika mfumo wa Elimu. Mabadiliko hayo ni kama Uongozi (Nafasi ya Mungai ikachukuliwa na Mama Sitta). Kulikuwa na umuhimu mkubwa sana wa kufanya hivi ukizingatia jinsi wizara hii ilivyokuwa ikiongozwa pamoja na maamuzi yasiyoongozwa na utafiti hapo awali (Kuondolewa kwa michezo na mashindano ya michezo, kuunganishwa kwa somo la fizikia na kemia sekondari na mabadiliko mbalimbali ya mitaala yasiyokuwa na msingi wala malengo bayana n.k.).

    Pia nafikiri wizara imekuwa ikitengewa fedha nyingi zaidi katika bajeti, japo ukilinganisha na ongezeko la bei na jinsi hali ya maisha ilivyo, ongezeko hilo kiukweli linakuwa dogo kuliko linavyoonekana.

    Pamoja na mabadiliko haya na mengineyo, kumekuwa na matatizo sugu ambayo bado yanahitaji ufumbuzi wa haraka sana ili kunusuru mstakabali wa taifa letu hasahasa ukizingatia tunaelekea kwenye huu umoja wa Afrika Mashariki n.k. Moja ya matatizo ambayo nafikiri laima yatatuliwe kitaaluma ni suala la idadi ya walimu mashuleni.

    Kumekuwa na mfumuko mkubwa wa ongezeko la mashule pamoja na wanafunzi. Hili ni jambo ni baraka ila tusipoangalia linaweza kugeuka kuwa laana kubwa kwa elimu yetu. Serikali imekuwa ikifanya mambo kwa ku-react badala ya ku-plan ahead of time. Kutokana na mabadiliko ya sera ya 1995, ongezeko la wanafunzi ni jambo ambalo lilitabirika na lilitegemewa. Lakini mipango ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi hawa kwa kuhakikisha kutakuwa na resources za kuwawezesha kujifunza haikufanywa. Mwisho wake tukaona watu wanapigwa kozi za miezi mitatu na kupangiwa mashule mbalimbali.

    Mimi naamini Nchi yetu haina tatizo la upungufu wa walimu, ila tatizo ni geographical distribution ya hawa walimu, na pia namna ya kuwa-retain baada ya kupata training. Mwalimu akipigwa kozi ya miezi mitatu halafu akapangiwa kwenda kufundisha vijijini huko ambako inabidi apande basi, landrova, mkokoteni, punda, atembeee weee halafu ndio afike kwenye shule isiyokuwa na majengo wala nyumba ya mwalimu, halafu mshahara wake ni sh 160,000, ambao hatalipwa na akienda kudai atababaishwa miaka mitatu hivi; unategemea ataenda huko au ataangalia shughuli mbadala ya kumtoa kimaisha kama vile kufundishwa twisheni jijini dar, ambapo atatengeneza hiyo 160,000 akiwa na wanafunzi 62 wanaolipa buku tano kwa mwezi?

    Ninachosema hapo juu ni kwamba walimu kama wanadamu na watu wengine, pia wanapima mambo jinsi ambavyo watu wengine wanapima. Lazima waangalie opportunity cost ndio maana unakuta shule zilizoko karibu na huduma mbalimbali za jamii kama hospitali, usafiri au karibu na mji zinakuwa na walimu wengi kuliko ambazo ziko mbali na huduma hizi.

    Hivyo basi, kupiga watu kozi za miezi mitatu au sita au hata mwaka, itaongeza idadi ya watu wanao-qualify kuwa walimu lakini haitatatua tatizo la geographical distribution, upungufu au ukosefu wa incentives (economic etc) za kuwafanya walimu waende sehemu mbalimbali huko vijijini.

    Bottom Line: Utatuzi/Ufumbuzi wa matatizo kama haya bado unahitaji kufanyika.

    “…lakini suala la kuwa, bajeti ya taifa ni finyu sana, hivyo haiwezi kutimiza hahitaji makubwa ya wizara zake, kama hiyo ya elimu, au hilo si kweli ki vile…”

    Hapa umesema kweli kabisa. Ukweli ni kwamba bajeti ni finyu na kutimiza malengo kama ambavyo wengi tungetaka inakuwa kazi ngumu sana. Lakini mimi bado ninaona kuwa hata hiki kidogo tulichonacho, hatukitumii sawasawa, au hatujaweka mkakati madhubuti na wenye makusudi ya kutuondoa kwenye matatizo sugu tuliyonayo. Kwa kifupi, we are not serious.

    Labda niulize swali dogo tu na hii ni kutokana na kutokujua kwangu. Hivi wabunge wanalipa kodi ya mapato? Wakienda kwenye vile vikao, wakalipwa zile 160,000 kwa siku, zinakuwa zimekatwa kodi ya mapato au hapana? Sasa pima jibu la hilo swali na kitendo cha kwamba mwalimu anayelipwa 160,000 kwa mwezi anakatwa kodi ya mapato! Mimi ningekuwa na uwezo ningeondoa kodi ya mapato kwa walimu, iwe kama incentive kwao kuwa na moyo na ari ya kufanya kazi!

    Lingine katika kushindwa kutumia hata fedha kidogo zilizopo kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali imejitahidi na kuunda Mamlaka ya Elimu Tanzania, ambayo nafikiri ni chombo kinachohusika na ukusanyaji pamoja na distribution ya funds kwaajili ya elimu (they are in charge of the Tanzania Education Fund). Unaweza kupata information zaidi hapa [bofya].

    Huu ni mwanzo mzuri. Bado ninajiuliza, pamoja na kuwa na chombo kama hichi, ni kwanini kuna wanafunzi bado wanakalia mawe wakati wakijifunza? Hii ni karne ya 21! Ni aibu, ya kuvuliwa nguo zote mbele ya kadamnasi, kwa serikali yetu kuwa na wanafunzi wanaosomea chini ya mti kwasababu hakuna darasa, au hakuna dawati!

    Kwa leo niishie hapa!

  9. Kwasababu mambo yalikuwa mengi mzigoni, niliamua kukaa pembeni na kufuatilia haya “mahojiano”!

    SL, shukrani kwa kutuletea vielelezo muhimu kwenye huu mjadala (Maoni yako ya awali nadhani yanapaswa kutumiwa kuwakumbusha wahusika kazi wanayotakiwa kufanya. Nitalifanyia kazi hilo!). Hii sasa inatuwezesha kutambua wapi hasa ni chanzo cha matatizo kwenye mfumo wetu wa elimu.

    Umenikumbusha ile programu ya zima moto kwenye miaka ya tisini: Serikali/Wizara ya Elimu ilipotangaza kuwa kila mwalimu wa shule ya msingi anatakiwa kuwa na angalau elimu ya kidato cha sita. Kilichotokea ni walimu kupelekwa kwenye vyuo kwa kozi za miezi mitatu tu.

    Naona nitoe dukuduku langu (ambalo baadhi nadhani mnalijua). Naomba samahani kwa kupindisha mwelekeo wa mjadala…

    Tatizo ambalo mimi linanisumbua, ni ile mtu aliyehitimu elimu ya juu (kidato cha sita au chuo kikuu) anaposhindwa kunyambua mambo; ile kufikiria tu na kuja na mawazo yake mwenyewe. Wakati mwingine kinachotakiwa ni kuweka mawazo tofauti pamoja na kuja na hoja… Lakini, wanafunzi wengi wa kawaida kusema ukweli hawaliwezi hilo.

    Nimekuwa nafuatilia mijadala mingi tu mitandaoni, lakini nadhani labda kwetu tu ndio sehemu pekee ambapo mtu anayefanya “comprehension” ya mwelekeo wa kitu fulani anaitwa “genius”! (Sio dongo kwa mtu yoyote yule, nasisitiza jamani.)

    Pili, jinsi walimu wetu wanavyopatikana. Na binafsi nadhani kama hili lisipopatiwa ufumbuzi, tutaendelea kulalamika na kuwa midahalo kama hii milele.

    Kama mnavyojua, wengi huenda kwenye vyuo vya ualimu sio kwa hiari (baada ya kushindwa “kuunganisha” na kwenda chuo kikuu). Bahati mbaya jamii yetu haithamini walimu, na matokeo yake tunakuwa na walimu ambao labda wanashindwa kuwapa changamoto sahihi wanafunzi. Bahati mbaya matokeo ya misingi mibovu kwenye elimu ya shule za msingi na sekondari hujitokeza baadae (hasa kwenye yale masomo ambayo yanahitaji kujifunza na kuendeleza ubunifu — sizungumzii sayansi na hesabu tu; kuna mambo ya uandishi, utunzi wa riwaya, tamthilia n.k. Hivi Bongo tuna somo la Creative Writing? Au tuna walimu ambao wanaweza kuchochea mambo niliyoyataja hapo awali?)

    Nia yangu sio kuwalaumu walimu. Binafsi, nimebahatika kuwa na walimu wazuri tokea msingi (wachache) mpaka sekondari na sina budi kuwashukuru kwasababu walisaidia kufanya maisha yangu chuoni kuwa marahisi. Ila, nikiangalia upande wa pili wa shilingi, wenzangu wa Tosamaganga walikuwa na walimu wazuri?

    Kwenye matembezi yangu facebook huwa naona vipaji (kwa jicho langu la tatu) nikisoma “notes”. Bongo kuna vipaji – ucheshi, kugusa mioyo ya watu; watu wana ubunifu ndani ya vichwa vyao lakini they can’t channel that… Kuna kasoro ndogondogo za uandishi, lakini naamini kama hawa wangepewa mwongozo makini, labda tungekuwa tunasoma makala zao kwenye magazeti sasa hivi.

    Kwa kumalizia tu, nadhani itakuwa vizuri tukijaribu kuacha kulalamika na kuanza kutafuta suluhisho. Wale ambao wanadhani wanaweza kusaidia kwa namba fulani, itabidi waitikie mwito. Hii kazi haitafanywa na mtu mwingine yoyote yule, bali ni jukumu letu; mimi au wewe.

    Kwahiyo, tusaidiane. Iwe kwa kwenda mashuleni (ukipata muda) kuzungumza na wanafunzi kwa kifupi au hata kufundisha mara moja moja. Kitu kama hicho kinaweza kuwa kidogo sana kwako, lakini hujui yatakayotokea…

    Ulizia walimu wa Kiswahili hujisikiaje pale mmoja (TU!) wa wanafunzi wao anapoishia kuwa mwandishi mahiri! Just play your part…

    Kabla watu hawajaanza kuosha vinywa, mi’ nimeshapanga kutembelea chuo kikuu kila nikipata muda kumwaga ‘utirio’. Nikisema lazima kieleweke, I really do mean that!!!

    Fikiria, kama wewe unadhani ukienda kuzungumza sehemu fulani na kumwaga ‘maujanja’ unaweza ukabadili fikra za mtu mmoja.. Na huyo mmoja akaenda kijiweni na kubadili fikra za masela wake kijiweni. Sasa, itakuwaje pale vijana 1000 tu wakiamua kufanya kitu kama hiki; kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu?

  10. Dah si mchezo,

    hivi ushirikiano kati ya wataalamu binafsi wa elimu, taasisi zinazo jishughulisha na maswala ya elimu (ex; HakiElimu) na Serikali ukoje?. Manake nakumbuka kipindi cha mkapa, HakiElimu walipata shida sana.

    Labda pia swala la kuchagua mawaziri liwe swala la kutiliwa maanani sana, hasa kwenye wizara nyeti kama wizara ya elimu. Mimi sijui ni vielelezo gani vilivyofanya akina Mungai, Kapuya, Maghembe, na wengineo kupewa dhamana ya kushika wizara ya elimu. Hili pia ni kwa wizara nyingine. Nina wasiwasi kuwa labda kuna muda mwingine watu wanachaguliwa kutokana na titles zao, kama Prof. Kapuya bila kuangalia uwezo wake katika matendo.

    Kitu ambacho bado na shaka wakuu hawaja kichukulia manani, ni kuwa wizara na wizara ya elimu ina hitaji kupata waziri ambae ni mbunifu sana. Ngoja nichungulie sera ya elimu ya Chadema, alafu tutaendelea

  11. Kadri miaka inavyokwenda hali ni mbaya afadhali ya jana.Serikali imeshindwa kuwekeza katika elimu na badala yake imewaachia watu binafsi ambao wanasifiwa kwa kutoa elimu bora huku shule za serikali zikiendelea na mtindo ule ule wa bora elimu.

  12. ndugu zangu watanzania, katika suala la elimu mimi ninafikiri serikali iwe makini kwani sasa tunakoelekea ni kubaya. Mabadiliko ya muhutasari kila kukicha, vitabu havipatikani mfano hadi sasa vitabu vya darasa la saba havijapatikana ili hali hili ni darasa la mtihani wa taifa tunakwenda wapi?

  13. Elimu yetu haiwezi kubadililka kwa sababu imekaa kisiasa zaidi. Leo hii hadi mtoto wa sekondari anafikiri anafeli kwa sababu ya serikali iliyopo madarakani. Kwa hali hii hatuwezi kufika na kutimiza malengo ya elimu kama tunavyodhania.

  14. Tanzania lazima ibadilike hasa katika mfumo wa elimu. Kujenga tu shule, kudahili wanafunzi wengi na kuwaacha bila walimu wa kutosha na wenye uwezo ni jambo la kusikitisha kwa sababu ni la kisiasa. Kutokuwa na sera bora za elimu katika nchi yetu bado si jambo la busara sana kwa sababu elimu yetu haitakuwa na malengo thabiti kulingana ma mahitaji ya jamii yetu.
    suala la matokeo mabovu ya wanafunzi hasa kidato cha nne wakati mwingine ni kwa sababu elimu yetu imeshikwa na wanasiasa na si wataalamu. Leo hii wasomi wanaendeshwa na wanasiasa, hii inanifanya nishangae san hata huu wanaouita mgomo wa madaktari nchini kuhusishwa na siasa. kweli sasa tumefika nyakati za mwisho kabisa wakati ambao watu wa daraja la chini waswahili wanasema inakula kwao.
    Hivi ni nini mchango wa wasomi wanazuoni wa vyuo vikuu nchin? kama hata wao bado wanafikiri siasa ni sehemu kubwa ya maisha yao? watu wa vyuo vikuu ni lazima tufike mahali tuone siasa haina nafasi tena hasa pale tunapoona wananchi wanaumia na kwa kutumia taaluma zetu tunaweza kuwasaidia, tuwe wazalendo ingawa ni kweli “is not fair”.

  15. Mimi nafikiri kuwa ili sekta ya elimu nchini iweze kusonga mbele kwa kasi na mafanikio mambo yafuatayo hayana budi kutekelezwa:- kwanza kabisa unahitajika mfumo mpya wa elimu ambao utakuwa na malengo madhubuti kwa mtanzania wasasa na wa baadae(ndani ya miaka 50).mfumo huo uzingatie kumjenga mtanzania katika hali ya kujitegemea, kujiamini na kuwa na uwezo wa kutumia maliasili zinazomzungula katika kujiendelaza kimaisha hata kama ataishia kidato cha nne. Ninamaanisha kuwa kila hatua ambayo mwanafunzi atapiga kitaaluma iwe inaweza kumpa ajira binafsi. Sasa hivi mwanafunzi wa kidato cha nne akifiwa na wazazi wake na akashindwa kujiendeleza kimasomo ataishia kuosha magari kwa kuwa vile alivyokuwa akifundishwa havikumpa uwezo wa kujigemea. Pili,sera zote zitakazokuwa katika mfumo huo ziwekewe mwongozo ambao utaonesha taratibu za utekelezaji wake. Kisha sera hizo miongozo yake iwekwe bayana kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kama vile magazeti,redio,televisheni n.k. Mambo haya yatasaidia kufanya utekelezaji uwe hali ya juu. Nous besoin faire quelque chose dans l’education systeme`. Merci et aurevoir.

  16. hivi hii inakuwaje tanzania, tafadhali soma hii alafu uone tunaenda wapi kielimu.

    “JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

    WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

    UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU

    UTANGULIZI

    Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.

    Muundo wa Kwanza ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges) zifuatazo
    hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.

    Muundo wa Pili ni wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 – 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.

    Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea (private candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.

    Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.

    VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA KIDATO CHA SITA KWA MWAKA 2014

    Baada ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na muachano wake:

    a) Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.

    b) Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii

    (i) makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili. Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).

    (ii) Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi hili.

    (iii) Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama Filikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.

    c) Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo zitakatumika

    (i) Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),

    (ii) Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),

    (iii) Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),

    (iv) Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);

    (v) Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),

    (vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na

    (vii) Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).

    Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.

    d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.

    e) Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.

    f) CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama 10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.

    g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia Mitihani, CA zao zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali. Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.

    h) Kwa vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013.

    i) Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.

    j) Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.

    Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:

    Jedwali Na 1

    MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU

    ALAMA UWIGO WA ALAMA IDADI YA ALAMA TAFSIRI
    A 75 – 100 26 Ufauli Uliojipambanua
    B+ 60 – 74 15 Ufaulu bora sana
    B 50- 59 10 Ufaulu mzuri sana
    C 40 – 49 10 Ufaulu mzuri
    D 30 – 39 10 Ufaulu Hafifu
    E 20 – 29 10 Ufaulu hafifu sana
    F 0 – 19 20 Ufaulu usioridhisha
    Kwa aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.

    Jedwali Na 2

    MUUNDO WA MADARAJA

    MUUNDO WA ZAMANI MUUNDO MPYA MAELEZO
    POINTI DARAJA POINTI DARAJA
    7-17 1 7-17 I Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana
    18-21 II 18-24 II Kundi la ufaulu mzuri sana
    22-25 III 25-31 III Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani
    26-33 IV 32-47 IV Kundi ufaulu hafifu
    34-35 0 48-49 V Kundi la ufaulu usioridhisha
    Wataalamu wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.

    Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu.

    HITIMISHO

    Mabadiliko haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN). Ushirikiano wa wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio katika sekta ya elimu.

    Imetolewa na,

    KATIBU MKUU
    WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI”

    sasa kwa hali hii tunakwenda wapi jamani? hivi tunandoto za kufanya mapinduzi ya viwanda na biashara kwa mfumo huu mbovu wa elimu tulionao na unaozidi kuhalibiwa kila kukicha?

  17. Relevance ya elimu na sera zake ziko wapi?
    Je, mwanafunzi wa darasa la saba anaweza kufanya nini iwapo atafaulu au atafeli ikiwa ameshindwa kuendelea na shule ya sekondari?
    Mimi nadhani wizara pamoja na wadau wa elimu wasijikite sana kwenye ufaulu wa mwanafunzi, cha msingi mwanafunzi akihitimu awe na uwezo wa kutumia rasilimali zinazomzunguka ipasavyo………..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend