Five Questions with Fid Q

Five Questions with Fid Q

Nimekulia Keko Juu, wilaya ya Temeke. Safari za kwenda Uwanja wa Ndani wa Taifa au ‘Fegi’ (Chang’ombe Sigara — TCC) kucheki mechi za kikapu ilikuwa desturi. Kama hakuna mechi, basi utanikuta kwenye mechi za mchangani mitaa ya Kurasini, Keko au Chang’ombe.

Wakati nipo darasa la tano, vijana ambao nilikuwa nawaona kwenye mitaa yetu, Gangstas With Matatizo (GWM), walikuwa wanatikisa na wimbo ‘Yamenikuta’ (ft. 2 Proud). Kwa hiyo, labda utaelewa kwanini naithamini sana Hip Hop.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000… Juma Nature aliamua kuwashirikisha “GWM” na wasanii wengine, na kuunda kundi la Wachuja Nafaka. Bila shaka utakuwa unakumbuka ule wimbo ‘Mzee wa Busara’.

Fid Hop: Sasa hivi tunaelewa kwanini Mwanza imegeuka kuwa "Rap City".

Baada ya albamu yao kutoka, mzee nikajipinda, nikabana hela ya matumizi shuleni na kununua kaseti ya Wachuja Nafaka. Ili tu niweze kusikiliza “malaria inapanda weeeeeeh, inapungua; inapanda weeeeeeh inapungua” muda wowote nitakaotaka!

Nadhani ile shilingi 700 niliyotumia kununua ile kaseti ilinipa zawadi ambayo sidhani kama kuna zawadi nyingine yoyote ile ambayo shilingi 700 nyingine itanipa. Kwenye wimbo ‘Ukweli na Uwazi’ kulikuwa na mistari ya msanii mpya kutoka Mwanza! Nikabaki kurudia kuusikiliza huo wimbo, hasa ubeti wa Fid Q.

Binafsi, mtu akitaja Fid Q tu, basi ile mistari yake (yenye metaphors) inayokufanya ufikirie inaanza kuchukua ukumbi kwenye fikra. Bila shaka Fid Q hatufundishi kuongoza kumfuata; bali anatufundisha kuongoza.

Wakati nyimbo na albamu yake nzito ya ‘Propaganda’ ikiwa inagombewa mitaani, tuliona hatuna budi kumtafuta na kumuuliza maswali matano.

Alianza hivi:

Kwanza kabisa ningependa kuwapongeza kwa juhudi za kimakusudi kuhakikisha ukweli unatengana na uongo for a better tomorrow!

Baada ya pongezi, ningependa kuwashukuru kwa kunipa nafasi hii ya mahojiano na nyinyi ambao ni wanajamii wenzangu; ambao kwa pamoja tukiungana, basi nina uhakika hakuna kitakachoshindikana chini ya jua.

Baada ya pongezi na shukrani zangu toka kwenye uvungu wa moyo wangu, ningependa kuyajibu maswali yenu ya msingi.

1. Umetoka wapi, uko wapi na unakwenda wapi? Uko mwenyewe kwenye hiyo safari?

Kusema ukweli, nilikotoka ni mbali sana! Tangu enzi za ku-rap ni uhuni, mpaka hii leo, miaka ambayo baadhi yetu tumepewa vyeo vya ubalozi wa jamii. Kwa sababu tu ya kuitumia sanaa hii ya muziki wa Hip Hop — kama kioo cha kuutazamia ukweli, na pia kama nyundo ya kuukazia.

Ufanisi huu wa kazi umepelekea wadau mbalimbali kutupa vipaumbele katika shughuli mbalimbali za kijamii, kama uelimishaji mashuleni juu ya suala zima la maambukizi ya virusi vya Ukimwi, jinsi ya kupiga vita malaria n.k. Yote haya yameletwa na kitu kimoja kinachoitwa nguvu ya msanii na sanaa yake.

Hakika nathubutu kutamka kwa ulimi ya kwamba, japokuwa jamii yetu iko ‘off balance’ katika nyanja mbalimbali, bado inaonesha kuwa na imani sana na wasanii wake. Na hiki ndio kitu ambacho kiliwafanya mpaka wanasiasa “kuwatumia” wasanii katika kuendesha kampeni zao kwenye kipindi cha uchaguzi. Ili kupata idadi kubwa ya wahudhuriaji watakaosikiliza sera zao; kwahiyo kumbe yule muhuni wa zamani amekuwa mheshimiwa wa sasa…

2. Mzee wa Kitaaolojia, nimesikiliza Propaganda zako kwa kina. Hivi, ulikuwa na lengo gani hasa?


Kabla ya kuandika Propaganda au kufikiria kuiita albamu jina hilo, nilikua nina mpango wa kuiita ‘Darwinz Naitmea’. Hata hivyo, huo mpango ulipotea ghafla baada ya kufanya mdahalo wa siku mbili na baadhi ya maprofesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao mpaka tunarudi mitamboni waliniacha na maswali mazito ambayo ni:

Je, humu ndani ya hii ‘Darwinz Naitmea’, wewe kama mwanaharakati ulikuwa unataka kumlaumu Hubert Sauper kwa kukutusi au unataka kuichukulia hii documentary yake kama changamoto?

Darwin's Naitmea: "Sitaki kukubali kama kuna kitu nilikuwa nakihofia."

Bila shaka, wale ambao wameiona hii documentary watakubaliana nami nitakaposema: hii documentary ina mengi ndani yake. Nikimaanisha, kilichoongelewa ni zaidi ya ile kashfa ya wakazi wenzangu wa Mwanza kulishwa mapanki, pamoja na wimbi kubwa la watoto wa mitaani au hata suala la maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Naam, kuna mengi mule ndani kiasi kwamba hata kama ningechukulia ‘amenitusi’ ni sawa na mimi ku-sell out. Na ule mtazamo wa kupata changamoto ulikuwa mkubwa sana kwangu, na mara nyingi ilikuwa inanifanya niote ndoto za michoro ya joka kubwa tena lenye miguu! Sitaki kukubali kama kuna kitu nilikuwa nakihofia, isipokuwa niliona itanigharimu muda mwingi sana ili kukamilisha utafiti wangu na tayari mashabiki walikua wamesha’anza kulalamika kuhusiana na ukimya wangu.

Wazo la Propaganda likanidondokea mithili ya theluji toka mbinguni; nami nikawawashia mshumaa Wabongo wenzangu ili tuache kulilaani giza.

3. Kama mmoja wa mashabiki wako wakubwa, nimeshuhudia kipaji na uwezo wako wa kufikiri kwa kina ukikua kwa kasi ya ajabu. Ni utu uzima tu au kuna juhudi nyingine?

Nilichagua sanaa tangu nikiwa mdogo, kwasababu niliamini ubongo wangu una zawadi, ambayo nikiipiga msasa wa vitabu, [basi] itakuwa ni ya kipekee na ya kuvutia zaidi kama sitokuwa mchoyo; kiasi cha kuwagawia wenzangu wanaonisikiliza kwa kupitia mlango wa fikra mbadala.

Hapa naongelea Hip Hop! Hivyo basi: I am Hip Hop… and I do this under the name of God.

4. Chimbuko la Hip Hop lilitokana na mazingira na mazingara ya taabu, hivyo kuchochea uanaharakati. Je, unadhani Bongo Hip Hop imekuwa ikifanya hivyo? Au nyumbani imekuwa na jukumu tofauti kidogo, hasa ukizingatia na tuliyoyaona katika mchakato wa Uchaguzi?

Nasikitika kukutaarifu kwamba Bongo bado hawajajua kutofautisha kati ya “rapper” na “mwana-Hip Hop”. Na bado hawajajua kuwa: Rap + Reality = Hip Hop!

Kwa hiyo wengi wao hawaangalii kile walichokiandika kabla hawajaanza kughani. Wala hawazingatii misingi na katiba nzima ya Hip Hop; na bado wanapewa heshima kama wana-Bongo Hip Hop.

Ku-rap hata Mao Santiago wa Machozi Band ana-rap. Lakini, je, hicho ndio kitamfanya aitwe mwana-Hip Hop? Hapana!

Mi’ binafsi nimeshangazwa na mwamko wa Wabongo safari hii kwa kuielewa Propaganda mapema, kiasi cha kuiita album bora ya Mwaka 2010. Nasema nimeshangazwa kwasababu mapokezi ya Propaganda yamekuwa ni makubwa kuliko hata yale ya awali kwenye ile albamu yangu ya kwanza ‘Vina mwanzo, kati na mwisho’.

Hata hivyo, sitaki kushangaa sana kwasababu tofauti ya ‘Vina mwanzo’ na ‘Propa’ ni kama ifuatavyo: ‘Vina’ aliisuka Majani pale Bongo Records; ambamo ndani yake nilitoa hits kama ‘August 13’, ‘Chagua moja’, ‘Mwanza-Mwanza’, ‘Kadi na Ua Rose’ n.k. Na Propa niliisuka mwenyewe… kuanzia beats mpaka song titles, contents, nani wa  kumshirikisha na vitu kama hivyo.

Tofauti iliyopo: Ile ya kwanza nilikua chini ya Majani. Hii ya pili nilionesha ukuaji wangu kimuziki kwa kuchangia machozi, damu, jasho na moyo wangu wote katika kuhakikisha napata kitu sahihi kabisa!

Hiyo ndio maana halisi ya kuwajibika na sanaa kama msanii. Na unapoamua kuwa MC, ni lazima uwe kama balozi ambaye amewekeza maisha yake yote kwenye Hip Hop. Vinginevyo utafanya map#&%@zeze waendelee kuamini wabana pua wanaweza kuwashika hata ya zaidi ya ma-hardcore.

5. Ule mradi wako wa utafiti wa nafasi ya Hip Hop katika jamii, hasa Afrika, unaendeleaje? Nini hasa dhamira yako?

Dhamira yangu ni kuhakikisha sanaa na muziki wa Hip Hop Tanzania kwa ujumla unatumika kuelimisha, ukiachilia mbali burudani iliyomo ndani yake. Nimekuwa nikisisitiza suala la elimu mara kwa mara kwasababu elimu ndio kitu pekee kitakachotukomboa sisi Waafrika tuishio ndani ya hizi nchi zenye umasikini wa kupindukia, ndani ya hili bara lenye giza. Nchi ambazo hata uchumi wake haupo kwa ajili ya maslahi ya watu wengi. Na mbaya zaidi, zina wasomi wachache sana, ambao nao bado wanaashiria kama [vile] walishawahi kuuogopa umande kipindi fulani.

Sababu hizo chache za msingi zilinipelekea kupata mtazamo mpya wa matumizi ya sanaa yangu na nguvu nilizonazo, kama msanii; kwa kuliamsha Taifa [sehemu] lilipo, huku nikijaribu kuliandaa Taifa lijalo kwa kupitia elimu ndani ya burudani inayoletwa na muziki wangu kwa ujumla.

Hivyo basi nilipokabidhiwa Certificate of Educational Art and Culture pale Bell Air, nilishukuru Mungu na pia niliwaahidi wadau wa State Department ya kwamba sitotamba kwa kukabidhiwa cheti nchini Marekani. Isopokuwa, nitazingatia kipi nitafanya baada ya kuwa na hiyo certificate… Mpaka sasa hivi nina projects zaidi ya tatu ambazo natarajia kuanza Machi mwaka huu, ikiwemo pamoja na kuingiza somo la ‘KitaaOLOJIA’ vyuoni!

Maneno mazito kutoka kwa Fareed Kubanda. Bila shaka nasaha zake zimevaa huu ushairi kutoka kwenye wimbo ‘Propaganda’: Tunachukiana kwasababu tunaogopana; tunaogopana kwasababu hatujajuana; hatujuani kwasababu tunatengana; dunia ni nzuri, walimwengu hawana maana.

Nasubiri nipate wajukuu ili nije kuwahadithia kuhusu albamu ya Propaganda. Ambao hamjaisikiliza mjue nyie ni tatizo ambalo litakuja kutatuka!

Timu nzima ya Vijana FM inamshukuru kwa muda wake, na tunachukua nafasi hii kumtakia kila la heri kwenye harakati zake kimuziki na kuamsha Taifa letu kwa ujumla.

Sikiliza baadhi ya nyimbo zake kwenye playlist ya Michael “Mx” Mlingwa:

Quantcast


Makala zinazohusiana na haya mahojiano:

Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.