Uchambuzi: Fid Q – Propaganda (I)

Uchambuzi: Fid Q – Propaganda (I)

na Bahati Mabala na Steven Nyabero

Sikiliza wimbo kwa makini. Pia unaweza ukasoma kile Fid Q anachosema: Fid Q Propaganda – Lyrics.

Propaganda ni aina ya mawasiliano ambayo lengo lake hasa ni kubadilisha au kufanya watu kwenye jamii kuwa na itikadi, msimamo au mtazamo fulani kuhusu jambo husika. Lakini, kwenye aina hii ya mawasiliano, vitu au mambo kadhaa tu “huchaguliwa” na mtoa propaganda na kuwasilishwa kwa hadhira; kinyume na kuwapa watu taarifa na hoja sahihi — kikamilifu — na kuwaacha wafanye maamuzi yao wenyewe.

Kwa kutumia mfano na lugha nyepesi: Wewe unajua kuwa binti fulani mtaani ana virusi vya Ukimwi, na labda aliambukizwa wakati anafanya biashara ya ngono ili kukidhi mahitaji yake na mtoto wake. Kwa sababu wewe unataka jamii inayomzunguka imnyanyapae yule binti, basi, kama mtoa propaganda, utawaambia watu, “Yule changu ana ngoma.” Utaficha ukweli kwa makusudi kuwa kuna uwezekano alipata Ukimwi kwa njia nyingine, na wala hautagusia vitu vilivyomsukuma yule binti awe changudoa.

Propaganda hutumiwa sana wakati wa "vita".

Propaganda, ambazo huhusishwa na siasa zaidi, mara nyingi hudhamiria kuamsha hisia za watu. Hivyo kutoupa nafasi ujengaji wa hoja. Matokeo yake wapokeaji propaganda hushindwa kufanya maamuzi sahihi, au kwa matakwa yao kama wangepewa au wangejenga hoja sahihi kikamilifu. Vita ya Kwanza ya Dunia ni mfano mzuri wa jinsi propaganda zinavyotumiwa na wanasiasa na watu wenye mamlaka kwenye jamii.

Nyimbo kama ‘Juhudi za Wasiojiweza’, ‘Nyota ya Mchezo’, ‘Hey Lord’, ‘Mwanamalundi’, ‘Tema Noleji’, ‘Utaua Gemu’, ‘Nilipotoka’ na ‘Propaganda’ — zinazopatikana kwenye albamu ‘Propaganda’ — zinakupa picha kamili ya uanaharakati wa Fareed Kubanda kama msanii wa Hip Hop na raia wa Tanzania. Kwa wale wavivu kusikiliza tungo kwa makini, kufikiria wenyewe na kujenga hoja, kwa kifupi, albamu ‘Propaganda’ ni juhudi za dhati kabisa kutenganisha ukweli na uongo. Kwenye Bongo Hip Hop na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Na wimbo ‘Propaganda’ hubeba mantiki thabiti ya albamu nzima, hasa nyimbo zilizotajwa awali. Tungo zinabeba na kuwasilisha ukweli kuhusu sanaa ya muziki, siasa na maisha kwa ujumla, ili hadhira iweze kupambanua kama walichokuwa wakiamini kabla ni uongo — yaani, propaganda tu (kwa mtazamo wa Fid Q).

Wimbo ‘Propaganda’ unaanza kwa midundo yenye utulivu ambao unamlazimisha msikilizaji kusikiliza kile ambacho Fid Q anaghani. Wengi watakubali kuwa Fid Q anaghani vizuri na sambamba na midundo iliyoundwa na Marco Chali.

Badala ya kuanza kwa kughani ubeti wa kwanza moja kwa moja, Fid Q anaamua kuweka msingi wa ushairi wake kwenye kiitikio:

"Yule ni Last King of Scotland, sio Idi Amin wa Uganda."

Mambo anayosema na kuhoji kwenye mistari minne ya kwanza tu yanaamsha fikra. Ukifiria kwa makini utagundua kuwa anaanza na propaganda, “Polisi wanasapoti gangsta rap; ‘Ili uhalifu uongezeke'”,  kisha inafuatiwa na kitu ambacho anajipa fursa ya kuhoji, “Wabana pua kuimba mapenzi; ‘Je, ifatafanya Ukimwi usepe?'”. Kwa hiyo, mstari wa pili sio propaganda. Ila anahoji jinsi jamii yetu inavyozipa kipaumbele nyimbo za watu ambao hawana vipaji vya kweli na zinazochochea anasa, huku tukitegemea matokeo tofauti kabisa. Je, unadhani watoto na vijana wakiendelea kusikiliza mambo ya anasa na nyimbo zisizo na nasaha za kujilinda na magonjwa ya zinaa, tutegemee janga kama la Ukimwi kutoweka? Hamfungi mawazo msikilizaji, bali anahoji.

Lakini msikilizaji anaweza akadhani anayosema kwenye mstari wa kwanza labda yana ukweli — uhalifu mwingi humaanisha kazi nyingi kwa polisi! Kwanza, Tanzania hakuna “gangsta rap”. Pili, baadhi ya Wamarekani ndio walianzisha hizo propaganda ili kuchafua muziki wa Hip Hop, ambao mara nyingi huusishwa na uhalifu (matumizi wa madawa ya kulevya, mauaji kwa kutumia silaha, vitendo vya ngono na anasa kwa ujumla); kinyume na kuchukulia kinachoimbwa na wasanii kama ukweli wa mambo yanayotokea kwenye mitaa yao. Kama umekuwa unafuatilia mauaji ya halaiki mashuleni nchini Marekani, mara kwa mara vyombo vya habari vimekuwa vikisema watuhumiwa walikuwa wanasikiliza nyimbo za wasanii wa Hip Hop. “Gangsta rap”. Hivyo, bila shaka kinachoimbwa kwenye tungo za wasanii husika kimechangia mauaji ya halaiki.

Kama ilivyojadiliwa mwanzoni, mtoa propaganda hudhamiria kukufunga kimawazo kwa kutokupa nafasi ya kuhoji. Kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu. Watu wengine huweza kuita tabia hii determinism, kwasababu wanashindwa au hawataki kuzipa nafasi hoja mbadala.

Anarudi tena kwenye propaganda: “Media zinapromoti beef; ‘Wanadai zinakuza muziki.'” Kawaulize hao ma-DJ kama wanawajua wasanii wowote ambao ni ushahidi thabiti kwamba viwango vyao vya kuandika tungo bora, ubunifu, uwasilishaji wa kazi zao n.k. viliongezeka baada ya kuingia kwenye malumbano na wasanii wengine.  Ukiacha ushabiki na umbea wa malumbano, kuna lolote la maana? Kwanini hatuwabani wahusika wanapotupa upuuzi kama huu?… Ni kama tunameza chochote kile ma-DJ wanachotuambia. Hiyo ndio jamii yetu.

Baada ya hapo, anaamua kuhoji kitu kingine kwenye sanaa ya muziki Tanzania: “Wadau wana wasanii wabovu; ‘Nyie wakali mtatoka vipi?'” Ndio, ni swali gumu kwa wasanii wenye vipaji, kwani hawapewi kipaumbele na walioshika usukani wa gari moshi la muziki. Kama hili halitoshi, wanajamii nao wanaamini chochote kile kinachotoka kwenye midomo ya wadau wa muziki! Halafu, kama tunavyowapa vipaumbele “wabana pua”, tunategemea matokeo tofauti — Ukimwi usepe na sanaa ikue — kwani kila siku tunalalamika muziki wa Tanzania unakufa kifo cha mende.

Baada ya kusema na kuhoji hayo yote, hasa kuhusu sanaa, anakwambia, “Hizi ni propaganda.” Usiyatilie maanani aliyosema na haupewi nafasi ya kuuliza maswali na kujenga hoja zako binafsi. Wakoloni wetu wa mwisho wanaita hii kitu sarcasm. Anatucheka.

Wasanii wabunifu wa Hip Hop hupata sifa na kuheshimika kutokana na punch-lines. Tafsiri nyepesi inaweza ikawa ni [kama] mistari inayojumuisha aliyosema kwenye mistari kadhaa iliyopita kwa kutumia fumbo au kucheza na maneno na kuweka msisitizo. Kwa maneno mengine, anakupa vidokezo vya mambo aliyokuwa anazungumzia.

Na Fid Q anatumia punch-line ifuatayo: “Utaibiwa ukicheza blanda; ‘Yule ni Last King of Scotland, sio Idi Amin wa Uganda!'”

"The Last King of Scotland"

Hapa unahitaji hisabati na utundu. “Utakuwa umefanya makosa (makubwa sana) kama ukidhani Last King of Scotland ni Idi Amin wa Uganda!”

Kuna Idi Amin mmoja tu wa ukweli.

[The] Last King of Scotland ni filamu iliyoandikwa na Giles Foden. Ni hadithi ya kutunga. Alichofanya mwandishi wa filamu hii ni kutumia wasifu wa mhusika wa kubuni — Dr. Nicholas Garrigan — kujenga wasifu wa Idi Amin Dada. Kilichofanyika ni “kuchagua” matukio machache tu kutoka kwenye historia ya Uganda/Idi Amin na kuyapachika kwenye filamu.

Ukiacha hayo, kuna uongo wa hapa na pale. Kwa mfano, mke wa Amin, Kay Amin alipewa mimba na Dr. Garrigan. Lakini, ukweli ni kuwa Bi. Kay alipewa mimba na ‘mpenzi’ wake, Dr. Mbalu Mukasa. Pia, kadri filamu inavyoendelea, mambo yanayotokea kwenye filamu yanazidi “kutengana” na mambo halisi yaliyotokea kwenye historia ya Uganda.

Haya, tafuta kikokotozi na visoda kama umesahau kuhesabu…

Mstari wa kwanza na wa tatu kwenye kiitikio ni Last King of Scotland! Propaganda.

Mstari wa pili na wa nne (ambayo inahoji na kuruhusu ukweli kujulikana) ni Idi Amin wa Uganda! Na usishangae ukikutana na Waganda wanaomchukulia Idi Amin kama mzalendo.

Bado unaamini Last King of Scotland ni Idi Amin Dada?

Sehemu ya pili, ambayo itachambua ubeti wa pili, wiki ijayo!

Makala nyingine:

Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.