Uchambuzi: Fid Q – Propaganda (II)

na Bahati Mabala na Steven Nyabero

Baada ya kujadili maana ya neno “propaganda” na kiitikio, uchambuzi unaendelea kwa kujadili ubeti wa kwanza: Fid Q Propaganda – Lyrics.

Wakati tunaumiza vichwa kutafakari kama [The] Last King of Scotland ni Idi Amin au la, Fid Q anatutosa kwenye Ziwa Tanganyika la ushairi. Uelewa wa mambo anayozungumzia hutegemea ujuzi wa muogeleaji. Unaweza ukapanga safari yako kuanzia Kigoma kwenda Zambia kwa lengo la kutalii tu, lakini katikati ya safari dira yako ikakupeleka Kongo ya Patrice Lumumba. Ndio, Kongo iliyokuwa koloni la Wabelgiji!

Patrice Lumumba

Ukiacha sentensi ya mwisho ya kiitikio, mistari mingine yote imetaja propaganda au kuhoji mambo yanayojiri kwenye uhusiano wa sanaa na jamii. Kwa hiyo hutakosea ukidhani yanayojadiliwa kwenye ubeti wa kwanza ni mahusiano ya sanaa na jamii pia.

Kweli. Kama msanii, ‘inauma sana unapoona kazi yako maridadi ikizimwa ili kumpa nafasi mwingine ambaye kazi yake sio nzuri’. Kama hiyo haitoshi, ‘wanampa promo’. Lakini cha kufedhehesha ni kuwa ‘wakati mkitumbuiza kwenye jukwaa moja, hadhira inakukubali wewe zaidi’! Hivyo basi, anawaambia “wahusika” ambao wanaendeleza huu upuuzi unaoua sanaa, hata kama hawataki au kukubali, ‘anawachukulia kama tatizo, na tatizo linaweza kutatuka’.

Propaganda v. Ukweli: "Wanampa promo, lakini kwenye show nammeza!"

Fid Q anaweka msisitizo hasa kwa hao “matatizo” ambao anaamini lazima watatuke. Yeye ni jiwe lililorushwa gizani; hauwezi kujua kama litaangukia kwenye vichwa vya watu au la! Anawalenga watu fulani. Jiwe linapowaangukia wanapiga kelele, lakini kwasababu wapo gizani wanadhani hatawagundua. Wakiwa kwenye mwanga wanaficha nundu na vidonda vyao, lakini yeye amekwishawafahamu kwasababu alizisikia sauti zao ambazo anazijua tayari.

Cha kushangaza, hao “matatizo” wanaendelea na upuuzi wao. Hawakomi. Anawaambia, ‘kuendelea na upuuzi ni kama kumuiga tembo kunya’. Mwisho wao utakuwa mbaya, anaonya.

Anaendelea kuwauliza, ‘hivi mnaendeshwa na tamaa za matumbo yenu’? Na kama kuna ambao bado wanapuuza anayosema, labda wana ile dhana ya kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kupata usingizi, anawaonya, ‘tobo dogo linaloruhusu maji kuingia kidogo-kidogo linaweza kuzamisha meli’.

Ghafla, Fid Q anaanza kujadili kitu tofauti kabisa — shimo kubwa kati ya walio kwenye tabaka la juu na la chini; matajiri na masikini; wanyonyaji na wanyonywaji; wenye mamlaka na wasio na mamlaka kwenye jamii. Kama vile Fid Q anageuka kuwa Fareed Kubanda.

"Uswazi tunaomba mvua zinyeshe ili tutapishe vyoo." Nadhani sasa hivi unajua kwanini kipindupindu hulipuka wakati wa mvua.

Fareed anaona mazingira na mazingara hatari kwenye jamii. ‘Mabwana afya wanajilimbikizia mali’ lakini upande wa pili wa sarafu ‘watu wanaomba mvua inyeshe ili watu watapishe vyoo’! Wakati wanaoishi ili wale wanaota vitambi, wanaokula ili waishi hawana hata sehemu ya kutupa kile kidogo kichafu kutoka kwenye miili yao; Uswazi wanafungulia vinyesi, kuna wakati kinachotoka huko huishia kwenye matumbo ya wengine na kipindupindu hulipuka!

Hapa msikilizaji inabidi ajiulize maswali: Bado Fid Q anajadili mahusiano ya sanaa na jamii tu? Au Fareed Kubanda kaamua kuongelea anayoyaona kwenye jamii? Je, anazungumzia siasa? Maisha kwa ujumla?  Kuna uhusiano wowote kati ya hayo yote? Kuna mafumbo mengine zaidi?

Fasihi huipa hadhira uhuru wa kutafsiri kazi ya fanani kwa kujenga hoja kutumia vitu na mambo yaliyowasilishwa. Fanani huwa na kusudi lake, lakini mara nyingi hadhira huweza kupata zaidi ya kile kilichokusudiwa. Ni tatizo zuri kwenye kuchambua kazi ya fasihi, kwani inaonesha ubunifu wa msanii kuamsha fikra mbalimbali tofauti.

Badala ya kung’ang’ania kujiuliza kama fanani ana upeo wa kujadili mambo kwa kina au la, ni bora kuuchukulia ushairi wa ‘Propaganda’ kama kazi ya fasihi. Tusiridhike na uhuru wa mikono na miguu yetu tu, bali tukumbuke kufungua minyororo iliyofunga fikra zetu pia (‘Mwanamalundi’ Ubeti wa Pili).

Unadhani ni jambo la busara kujadili mstari ‘Yule ni Last King of Scotland, sio Idi Amin wa Uganda’ kwa juu juu tu? Kwa kutumia kigezo cha Forest Whitaker alikuwa anaigiza tu? Tutakuwa tumeitendea haki hii kazi ya fasihi? Kama jibu ni hapana na uliamua kufungua fikra zako kuangalia jinsi ile filamu ilivyoandikwa n.k., basi tuzame ndani zaidi.

Kama tulivyojadili kwenye utangulizi, neno propaganda huhusishwa zaidi na michakato ya kisiasa, na hasa wakati wa vita; iwe kwa kutumia maneno tu au silaha. Kwa hiyo hatuna budi kuangalia utunzi wa Fareed kwa kutumia kurunzi la kisiasa zaidi.

Ni sahihi kulinganisha hao “matatizo” na viongozi wabovu, au watu wenye mamlaka kwenye jamii, ambao wanaoishi ili wale?

Tundu dogo la "ukweli" linaweza kuzamisha meli ya "propaganda".

Kuna kitu kingine kinaweza kufanyika. Sahau mambo ya fanani na chukulia kinachowasilishwa ni “ukweli”, utapata picha nyingine. Yaani, chukulia kama “ukweli” ndio anawasilisha huu ushairi. “Ukweli” anaamini “propaganda” anapewa promo. Lakini akiwekwa pamoja na “propaganda”, atammeza tu! Kwa maneno mengine, ukweli, hata uwe mdogo vipi, taratibu utazamisha meli ya propaganda. Anaonya, lakini “propaganda” hakomi.

“Ukweli”, kama ilivyo kawaida yake, hapendelei. Hafungamani na upande wa wanaokula ili waishi tu; nao wanapaswa kujiangalia kwa makini.

Wanaokula ili waishi wanaambiwa, ‘mkipiga kura haraka-haraka, bila kuchanganua mchele na pumba, mjue hivyo ndivyo mnavyozalisha wanaoishi ili kula’. ‘Mchakato wa kuchagua viongozi ni kama ndoa; mkiingia kichwa-kichwa mstaishia kupeana talaka’. Inaonekana “ukweli” ameona ndoa kama hizi nyingi tu, hivyo anawaasa wanaokula ili waishi, ‘maneno matamu ya wanaoishi ili wale wakati wanawatongoza yasiwalaghai’ kwasababu ‘harufu mbaya kutoka kwenye vinywa vyao vitawafanya msiwe na ukaribu’.

Kisha anawapa moyo na nasaha wanaokula ili waishi, ‘ukipewa usisahau, na ukitoa basi toa bila kukumbuka’. Hii yote katika kusaidiana kwenye harakati za kujikimu kimaisha. Pia, anawapoza, ‘usihofie kupitwa na wenzako na wanaoishi ili kula’. Kitu muhimu ni kuhakikisha ‘muda haukuachi’; yaliyopita si ndwele. Jaribu kuamini ‘labda kesho itafika ikiwa na matatizo machache zaidi kulinganisha na leo’. Kwa sababu matatizo yanaweza kutatuka, kama ukifuata ushauri wake.

Mwishoni mwa ubeti wa kwanza Fareed Kubanda anarudi huku akighani polepole, na kwa utulivu wa hali ya juu, kutupa falsafa yake ambayo inajaribu kuelezea chanzo cha migongano, migogoro na mifarakano kwenye jamii:

Dunia ni nzuri, walimwengu hawana maana.

Je, wanaoishi ili wale na/au wanaokula ili waishi hawajuani kwasababu wametengana? Hawajuani kwasababu wanaogopana? Wanaogopana kwasababu wanachukiana?

Uchambuzi wa ubeti wa pili, ambao unajadili jinsi ya kuwatatua hao “matatizo”, utafuata…

Makala nyingine:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 6 Comments

6
  1. asanteni sana wana vijana FM kwa udadavuaji wa tenzi hizi za fasihi toka kwa Ngosha the Don mwana wa Kubanda. kweli ukimakinika kwa usikivu pembeni mwa mkulima redio, unapata taswira na tafsiri nyingi za stanza zilizotumika ndani ya mashairi yake. Inahitaji uelewa mkubwa ukitaka kwenda ndani zaidi kama mlivyochambua, pia inahitaji uwelewa wa kati kama unataka kutumia maneno yale kama fimbo, halafu mwingine atahitaji uelewa wa juujuu kusikila misemo na vichekesho ndani ya mashairi ya nyimbo hii..ni ukweli jamaa huwa hakosi kujumuisha pande zote hizo ili kujiweka karibu na hadhira yake.

    Naam nimeketi juu ya busati na ki-laptop changu nasubiri vitu.

    FK.

  2. dah kwanzi mko juu sana vijana fm nawapa Big up zza kutosha endeleeni hvo hvo wazee…Fid we mkali sana unalenga kwenye uhalisia unafanya k2 ambacho kiko kwa manufaa ya wa2 wako wanayokuzunguka uko juu sana broda afu unajua unachokifanya dats why unafanya wonders kika unapo drop hots baaab sana nam kip it up….BlESSED…..

  3. Hongereni sana vijana fm,mimi binafsi hizo nyimbo zote za fid zinanigusa kila cku,lakin propaganda imegusa kwing na pia naamin alioona mwanzo kua”kutafanyika uchakachuaji kwny tuzo za kili”kw7bu fid anaamin yy ni zaid ya wasanii wote wa hip hop afrika masharik na kati,kumnyima tuzo sawa na kumzalilisha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend