Uchambuzi: Fid Q – Propaganda (III)

na Bahati Mabala na Steven Nyabero

Mtunzi alianza kwa kugusia mahusiano ya sanaa na jamii, lakini baadae akazama zaidi kwenye “vita”: wanaokula ili waishi dhidi ya wanaoishi ili wale. Uchambuzi unaendelea kwa kujadili ubeti wa pili: Fid Q Propaganda – Lyrics.

Ile safari yetu ya Kigoma hadi Zambia kwa nia ya kufurahisha macho tu imekufa katikati ya ubeti wa kwanza. Dira ya mtunzi inatuelekeza kwenda Kongo ya Patrice Lumumba. Je, mtunzi anafungamana na Wabelgiji au harakati za Lumumba na wafuasi wake?

Kuna dhana miongoni mwa mashabiki wa muziki kwamba Fid Q/Fareed Kubanda hafuatilii au hapendi kuongelea siasa kwenye tungo zake. Kama ilivyojadiliwa kwenye aya za awali, neno ‘propaganda’ huhusishwa na michakato ya kisiasa zaidi. Ukiacha hayo, bila shaka uchambuzi wa ubeti wa kwanza umefungua fikra zako, na labda sasa hivi unaafiki mtunzi alikuwa anaegemea kwenye siasa zaidi, hasa mwishoni mwa ubeti wa kwanza.

Ubeti wa pili unaanza kama ubeti wa kwanza. Mtunzi — kama msanii — anazungumzia mambo yanayomkuta akiwa mitaani nyakati za usiku; wakati macho yetu hayaoni vizuri. Akiwa kwenye shughuli zake, ‘polisi wanamkamata’. Wanajua wanachokifanya kwasababu huwa wanasema, ‘Fid Q uko chini ya ulinzi kwa kosa la uzururaji’. Je, hawa polisi ni sehemu ya hadhira ambayo humsikiliza wakati anatumbuiza? Halafu baadae ‘wanamuotea’ kwenye vichochoro akielekea nyumbani?

Kisa cha bughudha zote hizi ni nini? Wanataka kumpiga pingu “ukweli”? Hapana, wanataka ‘kitu kidogo’. Cha kushangaza ni kuwa hata hawajifichi ‘wanapotoa ishara kama wanavuta uradi wa tasbih‘. Kuomba rushwa kwao ni desturi; ni sehemu ya maisha na imekuwa kama dini tu.

Mtunzi afanye nini? Ingawa inamuuma, anaangalia upuuzi wote huu kwa jicho la kifalsafa. Polisi kumbughudhi na kuomba rushwa tu ni ‘jambo baya’ ambalo ‘halimdhuru kimwili’. (Wengine hupewa mkong’oto!) Ni kama vile ‘jema lisilo na faida yoyote ile’.

Anachotaka na anachojali zaidi ni ‘kuendelea kusikika kila sehemu anavyotoa mawaidha’, akiamini ipo siku nasaha zake zitaangukia kwenye masikio ambayo yana dhamira ya kuwatatua “matatizo” kwenye jamii. Kama akifa ‘ataacha pengo’, kwa kuwa yeye ni mmoja wa wachache sana ambao wanaweza kubadili mawazo na mitazamo ya watu juu ya maisha. Kama hiyo haitoshi, mawaidha yake yanaweza kufanya watu wafanye mambo ambayo hawakuwahi kufikiria kuwa ipo siku watakuja kuyafanya. Yaani, ‘hata wakulima wanaweza kujikuta wanameza mbegu’.

Jamii ambazo zimeendelea zina uwiano sahihi wa watu wenye vipaji, fikra na mitazamo mbalimbali. Jamii yetu ina uwiano sahihi? Je, wangapi huchukulia wimbo ‘Propaganda’ kama ni harakati za kujikomboa? Kama ambavyo mwanamapinduzi  ‘Chegu’ (Ernesto “Che” Guevara) angefanya?

Hivi vina ni kama liberation struggle machoni mwa 'Chegu'.

Au tunachukulia hii kazi ya fasihi kama burudani tu; kwa kuangalia mambo juu juu kama ilivyo desturi yetu?

Anasadiki ukiwa ‘mkali kama jamaa aliyetengeneza midundo inayosindikiza mawaidha yake, Marco Chali, watu watakuja kukuelewa tu.’  Lakini, kwa upande mwingine, bahati mbaya jamii yetu imejaa ‘wajinga ambao hutumia muda mwingi kujadili watu’. ‘Wivu ndio kitu ambacho kinawadumaza na kuwaua kifikra’.

Jamii inaambiwa, ‘rafiki sio urafiki usipochanganywa na kazi’. Kinyume na dhana ambayo wengi wetu tunayo, mtunzi huamini urafiki wa kweli lazima uhusishe juhudi za kuleta maendeleo. Haoni umuhimu wa marafiki ambao hawashirikiani kwenye harakati za kujikwamua kimaisha. Ila, kama wengi tunavyojua, urafiki uliochanganywa na kazi huambatana na majaribu; hapo ndipo utajua upi ni urafiki wa kweli. Urafiki unafananishwa na mlango, ambao ili uitwe mlango lazima ujaribiwe kwa ‘kufungwa au kuachwa wazi’.

Wale ambao wameusikiliza huu wimbo mara nyingi, wakaangalia ni sehemu gani fanani anatumia lugha kali, wapi anapaza sauti, basi mistari hii ya mwisho inayofuata inaweza ikachukuliwa kama inatoka kwenye kinywa cha mtu mwenye “msimamo mkali”. Yote aliyokuwa anayoongelea yanampa ghadhabu na anashindwa kujizuia kuiambia hadhira kuwa ‘haipaswi kumuamini muongo hata kama akiongea ukweli’! Ni wazi kuwa amechoshwa na “matatizo” ambao wanatudanganya kila kukicha.

Lakini, si hata saa ya ukutani isiyo na betri inasema ukweli mara mbili kwa siku? Kwanini anakuwa mkali hivi?

Angalia sehemu ambazo kuna fukuto sasa hivi: minong’ono ya chini chini ambayo huchukuliwa kama vichuguu huweza kujiunga na kutengeneza mlima! Ndio kinachotokea kwa mtunzi…

Vichuguu vinaweza vikazaa mlima.

Anaamua kukemea baadhi ya tabia za wale “matatizo” wanaoishi ili wale, ‘dhambi kutumia dini kama njia ya kututapeli!’ Ananyoosha kidole kwa wanaoishi ili wale, ambao wana mamlaka zaidi kwenye jamii, na kutuambia, ‘wale “matatizo” wanajiingizia kipato kwa kivuli cha misaada’.

Hasira zinampanda na anashindwa kujizuia kupaza sauti, anatuambia ‘hawatufundishi kuwa viongozi’ ili tuwe mstari wa mbele ‘kufuata na kutekeleza chochote kile kinachotoka kwenye vinywa vyao’. Hawatufundishi kufikiria, kujenga hoja na kuamua kufanya mambo kwa matakwa na manufaa yetu sisi tunaokula ili tuishi. Lakini mara nyingi tunapowachunguza viongozi wetu ndipo ‘utata na siri zinapovuja’ na kugundua kuwa hawana nia njema nasi.

Tukishagundua hayo yote, je, tunachukua hatua zozote kuwatatua hao “matatizo”? La hasha. Hapana. Hiyo ndio ‘tabia yetu ambayo imetujenga’ na matokeo yake “matatizo” hujirudia-rudia. Kama “ukweli” alivyofanya kwenye ubeti wa kwanza, hawalaumu watu wenye mamlaka au viongozi tu. “Ukweli” hafungamani na upande mmoja. Anawaambia wanaoishi ili wale ambao hulalamika kila kukicha kuwa ‘wana nguvu ya kuendesha maisha yao kama wakitaka’.

Kwa hiyo, ‘kama wanatamani asali basi wajiandae kukwepa nyuki’. Kwa maneno mengine, ugoigoi hauiwezi kukuletea kile unachotamani; ni lazima kuwajibika. Fanani anaamua kwenda hatua moja mbele na kuwaambia wale wanaokula ili waishi kuwa wao ‘wana mawe tu mikononi mwao’. Lakini, upande wa pili huko, ‘wanaoishi ili wale wana bunduki’! Kwa mantiki hiyo, harakati za kujikomboa zinahitaji juhudi za ziada, ambazo fanani amezijadili kwa kirefu kwenye ushairi wake.

Hakuishia hapo. Mtunzi kaingalia jamii yetu kwa muda mrefu na anaamini ameilewa vizuri kiasi kwamba anaweza kutabiri kitakachotokea baada ya kuwasilisha ushairi wake.

Anadhani mambo yote aliyosema yatachukuliwa kama ‘uchunguzi wa kisayansi ambao haukufanikiwa’, kwa sababu hadhira itashindwa kuelewa nini anachojaribu kusema. Hadhira “itashangaa” tu ikiona ‘ng’ombe akila nyasi tu halafu anatoa maziwa’. Yaani, haitasumbuka kutafiti na kujifunza nini hutokea kwenye mfumo wa umeng’enyaji wa chakula, chakula kilichomeng’emywa hufanywa nini kwenye utumbo mdogo na kuishia kwenye mfumo wa damu n.k. Wengi wetu tutaangalia kilichoingia ni kijani na kinachotoka ni cheupe. Au kilichoingia ni yabisi na kinachotoka ni kimiminika. Basi.

Huyu kiumbe vipi, anakula nyasi halafu anatoa maziwa?

Mtunzi amewasilisha anachoamini kuwa ni “ukweli” kwa hadhira ambayo anadhani inafuatilia vitu ambavyo vinaendelea kwenye jamii — aidha kwa kusoma magazeti au kupitia vyombo vingine vya habari. Alichosema Fareed ni upande wa pili tu wa sarafu ambao aghalabu hufichwa na “wahusika”.

Kwa mantiki hiyo basi, kama umeelewa maana sahihi ya neno propaganda, je, mtu ambaye anasikia baadhi ya mambo yaliyojadiliwa kwenye beti kwa mara ya kwanza kabisa, huu ushairi kwake utakuwa ni propaganda?

Zinazohusiana na hii makala:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 21 Comments

21
  1. Ebwana jamaa anatikasha kiukweli ryme zinasamba kiubora kama cheguevara na ndoto za communism kutoka kwa marlx haisambaa kama hewa chafu inatoka viwandani. nageuka mtoa nasaa nasema its our time kumshukuru mama aliye 2zaa na kufanya watokee waandishi wa vitabu na mashairi hapa duniani pacngekuwepo tamaa isiundwa tripo aliance na tripple entente mwambieni fid vp kuhusu ma underground wenye michano ya hali ya juu anawasaidiaje

  2. Kila mtu anaweza kuandika mashairi ila tukatofautiana kwenye uwezo wa kufikiri naamini Fid Q ana uwezo mkubwa wa kufikiri na kuchambua mambo

  3. Ni hivi! Unahitaji kusikiliza mara mbili mbili mashairi ya huyu jamaa ili upate clear photo ya anachokisema! Other wise unaweza shtuka umetukanwa na haujagundua kama kichwa yako ni ya panzi…cku zote nimekuwa nasikiza mashairi ya fid tokea nyimbo za awali na kila cku naokota kitu! Pengine labda kwa kutumia metophorz nyingi inamnyima wigo wa mashabiki jinga(wavivu wa kufikiri) wale wanataka mpaka wasimulie kitu kama hadithi ndipo waelewe!..angalia kwa mfano UKISIKIA PAA! Ubeti wa fid unamfanya aonekane kama ndio mwenye nyimbo!..jamaa si tu ni tajiri wa vina na mistari bali pia ana eagle eye

  4. Huyu jamaa Fid Q, sasa ameadvance saana huyu ninaweza kumpa jina la Mwanazuoni!! Hv ni mwana hphop gani anaweza chambua nyimbo na ikawa na maana na dhana nzito kama NGOSHA anavyo fanya? Na wanatumia vigezo gani kutoa tunzo za kill award??? Wangekuwa ni wa2 makini kila mwaka Fid ungekuwa unajinyakulia tunzo, but mwaka huu sidhani kama Watakuchakachua tena!! naamini utachukua…..Hongera saana na naomba uchambuzi wa ngoma ya Profesional.

  5. nimekubaliana na huchambuzi wako na pia kaka FID Q kweli kweli anawaza mbali sana na pia mi ningependa awe anaimba nyimbo za kisiasa na kuwasema hao wanaokula rushwa na bila kusahau awe na msimo na asiwe anaogopa kwa kuwa yeye ni mwana mapinduzi alisi awe wazi kwa kuimba nyimbo za kisiasa maana hujumbe hutafika haraka zaidi

  6. Nikifa siachi skendo na uhakika nitaacha peNgo kwa hivi vina hata wakulima hujikuta wanameza mbegu……This Nigga is hot men…Malcom X part 1 lool BIg UP brother

  7. ki ukweli huyu ni mwanaharakati fulani anaependa kuangala mambo kwa ndani zaidi.si rahisi kumwelewa usipochunguza semi zake

  8. Willy, hututakii mema weye! Tuendelee kuchambua nyimbo nyingine za Fid Q?… Hili ni zoezi rasmi kama tulivyosema; nia hasa ni kuwaamsha wadau wa muziki kuwa wawe makini kusikiliza tungo nzuri. Kuna baadhi ya nyimbo ambazo ukisikiliza mara moja basi jua fika utatoka KAPA.

    Bahati mbaya nyimbo kama hizi huwekwa kapuni kwasababu ma-DJ wanaamini wasikilizaji hatupendi nyimbo “ngumu”. Ubunifu wa msanii huonekana pale tu ambapo ana kiitikio kizuri kinachoimbika*. Au zile hadithi ambazo ukisikiliza wimbo mara tatu tu basi unachoka.

    Tunachowaomba ni kuzipa nafasi tungo kama hizi (ingawa ‘Propaganda’ inabamba sasa hivi, amini usiamini nyimbo nyingine huwekwa kapuni). Na kwa upande wengine, wasanii wetu wasituletee nyimbo ambazo ni kama “bigi jii”; wawe makini zaidi kwenye uandishi.

    Nadhani jamaa labda ni mtu pekee ambaye watu wamemgomea asitoe album nyingine sasa hivi… That says a lot!

    *Mojawapo ya nyimbo zilizosimama ni “Mwanamalundi” ambao hauna kiitikio. My fav. nadhani ni “Nilipotoka” na “Unaua gemu”… ambao unabamba sana kwenye speaker kubwa!

  9. Hawatufunzi tuwe viongozi bali viongozi wa kuwafuata, utata huja tunapoanza kuwa chunguza. ebwana huyu jamaa kweli ni the last king of hip hop bila utata. fid anatisha but mwambieni anaprogram gani na wale watu wanao chukua rap+reality = hip hop, coz kuna watu wanapiga hili game kwa nia. one day alikuwa clouds akasema kuwa wa kwanza mungu 2. maisha 3. hip hop … ukifuata nyendo zangu lazima utaonekana kichwa its me mgumu swila ninaye fuata nyendo zake so one day atakuja kusikia falsafa zangu tchaoo

  10. huu ni mwanzo, kinachofuata ni ku-push agenda ya tungo kama hizi zianze kutumiwa madarasani, kwani kama tunaweza kutumia mashairi ya shaaban robert kwenye madarasa ya kiswahili na mengine ya fasihi, kwanini tusitumie tungo kama hizi kusaidia kuelimisha vijana.

    Nadhani tumezidi kukalia hazina, hivi leo tutoke hapa mpaka sijui wapi kuchukua kazi za fasihi za nchi nyingine kufundishia wakati tunazokazi zetu nzuri tena sana, kazi ambazo zinaakisi jamii yetu, kitu ambacho wanafunzi wengi wanaweza ku-relate to kirahisi. Nadhani kuna haja sana na mfumo wa elimu na walimu wenyewe kuwa creative

  11. Mpango mzima br fid q unatikisa ktk king wa ryhme A .mashariki na kati. ni wewe ambaye utaka dunia kwa mashairi mazito, km mpumbavu asiye weza kufikiri hawezi jua br fid q anaongea nini. Kikubwa kaka we ni mkali. watimbie side za university uwape ma-vocubulary. tchaoo.

  12. Whats up wachangia mada wote na people 4ro vijana fm. inabidi tujue umuhimu wa ngosha katika hip hop world. swila nasema hv usipige kelele kama haujui umuhimu wa moshi, kuna watu wanatoa sera ambazo hazina maoni, mwambieni ngosha atutajie nguzo 5 za hip hop, pia mwambie kuna mtu bado anaoga akitakata atatoka. ndoto ni kufanyia tongwe. underground ninayehitaji msaada wake! its me mr 0717703276.

  13. Jose, Mwanamalundi anapita hapa mara moja moja (umeme wa Tanesco ukiruhusu). Nadhani atakujibu/atakusaidia…

    Tunakutakia kila la kheri mkuu!

  14. Oya man sn unaongea na jose mimi au nipo wrong kama ni mim bac shukrani kwa maombi ni kweli nahitaji kutoka kiugumu zaidi coz walio mengi hawana mashairi ila biashara zao zinategemea radha zao ambazo zinafanana na midomo ya chupa haina noma mzaz ila kwa kweli ngosha yuko juu anatakiwa akae mbingu ya fikra mzazi Sn ucjari i want ze world to know truth about hip hop.raaaaaa!

  15. Jamaa anajitahidi kuwarudisha na kuwatoa tongotongo wale wote ambao bado wamelala. Fuatilia “Tunaogopana kwa sababu hatujuani, hatujuani sababu hatupendani…………. Tuendelee na Uchambuzi III

  16. Mambo wachangiaji!

    “i back again from house of hihop/ yes na make rain nafungua shampeni/ ninavyo wa drop kwenye rhyme some times wanatuma watu wanisake/ na gani nishawajua nishawatambua nawatupa kapuni/ unauchokoza muziki wa gangstar uta-gain more pain/ unanitishia kushika ukuta nitakuchapa na ukuni”

    ni yule swila ambaye ni noma zaidi – topic yangu leo ni kwamba ngosha yeye labda anaweza akawa anategemewa ndo mfalme wa rhyme la msingi amtafute yule mtoto wa tip top amueleze kwamba sio ishu sana yeye kusema hakuna mtoto atakayekuja kuchana kama yeye. kama hilo hawalioni sasa natoboa kwamba dogo hana rhyme isipokuwa anauza tu style ni hayo tu. pia nauja nijue sababu za kusema kuwa “media zinatangaza kuwa wayne ndo king wa hip hop ila ukweli hana strong rhyme” na vidude-dude kibao tu. kisha nikamsikia kwenye interview akisema kuwa dogo janja ni mkali ina maana makosa ya dogo hakuyaona au ndo… kiukweli bro ni mkali ila formula ya maisha ya watu ndo yatamfanya marashi ya kanike mnuko kama perfume za kichina. its me swila ninaye tema mawe any time!

  17. nimekua nikiusikiza wimbo huu kwa muda mrefù,nikautafakari kirahisi sana. lakini huu uchambuzi wa vijana fm umenifanya nigundue katika album ya propaganda kuna kila jibu la swali katika maisha. sasa itabidi niandike lyrics ya wimbo mmoja mmoja niutafakari.

  18. baya lisilokudhuru ni jema lisilo na faida… Ngosha nashindwa kuelewa unapoandika mistari huwa unawaza nini. mistari ni high sio eye level, you are so hot m’baba. wapo wanaoumiza vichwa but fid scratches… propaganda haigusiki kirahisi mazee. huff n puff the lyrics swagger don…

  19. Line zake zipo deep..kila alichoandika kina maana zaid ya moja..alikua anastahl tuzo bt celewi kwa nin..bt ni moja ya hotest song dunian…keep it up fareed

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend