Hotuba ya Mfungwa

Na Vitali Maembe| Chanjo — 2010

Ndugu waheshimiwa na wote msioheshimiwa,

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kuniweka hai na kunitia nguvu.

Hii ni hotuba ya kwanza kabisa ya Mfungwa Mswahili kwa watu wote. Naiandika huku nikiomba Mungu iwafikie ikiwa hivi hivi nilivyoiandika, lakini sijui kama itawafikia wakati mwili wangu utakuwa bado umeambatana na roho yangu.

Ndugu zangu, jela inatuumiza!

Mimi ni mfungwa, kuwa mfungwa haimaanishi kuwa ni mtu mwovu, bali ni mtu aliyeonwa na sheria. Hapa nilipo ni mahala muhimu sana, ni mahala pa kujenga. Ingawa wengi hutoka wakiwa wamebomoka na kuharibika kabisa, wamepoteza afya ya roho, akili na mwili.

Jela inawaumiza wanetu, jela inawaumiza wazazi na wapenzi wetu ingawa hawapo kifungoni. Jela inaiumiza nchi yetu.

Ndugu zangu kuna umri wa kufundishana adabu lakini kwa nafasi hii niliyoipata wacha niitumie kwa kazi hii ingawa umri wenu umeenda!

Nafanya hivi makusudi kwa kujua kabisa kwani hata Waswahili wamenionya kuwa samaki mkunje angali mbichi, akishakauka utamvunja bure upate lawama.

Ndugu Waheshimiwa, jiheshimuni, waheshimuni na wengine ili muheshimike kihalali!

Nanyi msioheshimiwa, muwaheshimu wenzenu na mamlaka zilizowekwa, jiheshimuni pia ndipo mdai heshima.

Naomba nieleweke nimesema kuwa nimesema kuheshimu, sio kuogopa wala kuabudu.

Nitaongea kwa mipaka ingawa leo nimepewa uhuru wa kuongea. Waswahili wamenionya kuwa Uhuru usio na mipaka ni utumwa. Haki ya nani sijaona lugha tajiri kama hii.

Ndugu zangu;

Nilikuwa nasubiri kutolewa huku kwa msamaha wa rais nije kuongea nanyi ana kwa ana lakini bahati haijawa yangu labda mwakani.

Jamaa zangu chonde nawaomba mseme na roho zenu, Mungu ajaalie tuonane nyumbani tukiwa hai wote, tujenge taifa lililo jema.

Maisha ya jela ni magumu na ya hatari, lakini kuna wakati tunapata nafuu, hasa pale wanapoletwa wakubwa huku ndani, mlo unabadilika na dawa za mbu zinapulizwa, uji sukari kibao na maji safi kama kawaida, lakini tatizo hawakai sana… Hata hivyo msemo wa Kiswahili huwa hauachi kutimia, “Mgeni njoo mwenyeji apone”. Ndugu zangu, kama nitajaaliwa kutoka  tutaonana nyumbani, ila sina matumaini sana maana wenye nguvu wameshaanza kunipiga kwa siri, kama roho yangu ikiachanishwa na mwili, basi msisahau kuwaambia watoto wa leo kuwa Tanzania mpya ipo, Tanzania mpya bora ipo, ila wajikaze na waishike vizuri adabu yao.

Muheshimiwa mwongozaji;

Sikia sauti ya kilio cha Mswahili tokea kwenye sakafu ya moyo wake.

Sikiliza bwana mkubwa, tutazame, nyuso zetu Watanzania hazijui kudanganya, zinazungumza hali waziwazi tena kwa lugha nyepesi kabisa!

Kuna kitu tumefanyiwa hapa! Sijui ni kwa ubaya au kwa wema, lakini ukweli ni huu. Mmekamata vyombo vya habari, mmetukamata makoo, mnavipa ruhusa baadhi ya vyombo vya habari kuua maadili na utamaduni wetu! Mmeharibu mfumo wa elimu, halafu mnatutishia dini. Mnafikiri hatujui Mungu anataka nini?

Mnatutishia madaraka mnatufanya hatuijui Siasa safi ikoje?

Nakumbuka nilipokuwa shule ya vidudu, sio chekechea, tulipofundishwa, mwalimu akiingia darasani monita anasema ‘Heshma’! Wote tunasimama na kusema, “Ili tuendelee twahitaji vitu vinne: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Sisi vijana wa CCM tupo tayari kujenga taifa… Shkaaaa mooo mwaaalimu!”

Wakati huo ukisema nasema kweli tupu na chama kinilinde, chama kinakulinda kweli. Kipindi hicho vituo vya polisi haba, mtuhumiwa akipatikana kwanza anafungiwa kwenye ofisi ya chama, unasikia watu wanasema ‘kapelekwa zoni’.

Ulaaniwe kujua, kujua si kwema, maana ningekuwa mjinga nisingepata shida akilini na moyoni kama hivi. Nimeishia darasa la nne tu nateseka hivi. Je, ninge…

Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… Tofauti ipo.

Tunategemea elimu ndio ituokoe, lakini elimu yenyewe, mitaala hailingani na maisha ya kweli! Kila kitu mnakitia siasa, mnakifanya biashara.

Utajiri wa nchi yetu ndio chanzo cha mateso kwetu. Hatufurahii maisha ndani ya nchi nzuri tuliyoachiwa na baba zetu.

Hivi, ni lini mtatupa fursa ya kuishi maisha yetu?

Ni lini tutafurahia uhuru wa nchi yetu? Tangu nchi inapata uhuru mpaka leo nchi inafikia nusu karne, inahitaji uhuru mpya, bado pua zetu hazijahisi hata kwa mbali harufu nzuri ya maendeleo.

Mnatuonesha kuwa njia rahisi ya mtu kuendelea ni kuwa mhalifu, sasa mnafikiri tutapungua huku jela?

Halafu, niliona mambo yanaharibika nikaomba kusaidia mapambano dhidi ya rushwa, nikaambiwa si kazi yangu, niliumia sana.

Halafu na wewe muweka kanda, nani kakupa kibali cha kazi hiyo wakati hujui unachofanya? Mnaona hii nchi ya kishkaji sio? Hujakatazwa kupiga muziki wa Waswahili redioni, lakini nikikuletea, “Ooh nisamehe kaka, maneno ya nyimbo zako hayatawafurahisha waheshimiwa.” Huu sio wakati wa kufurahishana huku nchi inaangamia, unaleta usomi wako wa kishamba bwana! Wamekwambia hawataki kusikia sauti ya kweli ya Mswahili? Acha kujipendekeza wewe! Unajua kazi ya muziki wewe? Au unafikiri kazi ya muziki ni kujaza ukumbi wa disko na kuvutia watu kwenye kampeni? Ukome kujipendekeza, kama hujui hata wao waheshimiwa wana haki ya kuburudika, kujifunza na kusikia sauti za ukweli. Usiwanyime haki yao ya kupata taarifa, elimu na burudani.

Viongozi wangu wapendwa;

Mliniziba mdomo Watanzania wenzangu wasinisikie kwa kuwa siendani na matakwa yenu. Mkaweka uadui kati yangu na wenzangu.

Mkawapa nafasi wanamuziki wanafiki ili wawafichie uovu wenu, nyimbo za matusi zinaimbwa wazi wazi nanyi mnazichukulia poa tu.

Eti maendeleo, Chuo cha Sanaa Bagamoyo kinakufa mnajifanya hamuoni. Chuo Kikuu Dar es Salaam kinazalisha matakataka mnachekacheka tu! Subirini kidogo muone matokeo ya bomu mnalolitengeneza.

Mnaandaa mitaala ya elimu ya kuwajaza ujinga watu, mtu amehitimu lakini bado yuko uchi akilini.

Heri mimi sikusoma kabisa. Ila najua kuhesabu hela.

Wenye makucha makubwa wanatutesa, wanajificha nyuma ya siasa, biashara, na dini, watushambulia wanyonge bila huruma.

Halafu na nyinyi waumini, mimi ndio nimewatoa maana kabisa kwa unafiki wenu! Na kwenye nyumba zenu za ibada mnifukuze kabisa mkitaka! Mungu atanipokea na kuwaaibisha wanafiki wakubwa nyie… Mtu anasimama kashika Katiba na kitabu cha Mungu wenu — anaapa kwa jina la Mungu halafu anaenda kinyume na kiapo chake, kisha nyie mnamkenulia meno tu, mnajua maana ya kiapo nyie? Sawa, Katiba imepitwa na wakati, Biblia na Msahafu je? Mnashindwa kusimama kwa ajili ya jina la Mwenyezi Mungu, mtasimama kwa ajili ya nani?

Nitasahau kusema yote lakini hili nitalisema kabla sijafa: Tanzania inataka Katiba ya Kitanzania — Katiba ambayo sio ya kikoloni, katiba ya zama hizi, ambayo hata tukiongozwa na bora kiongozi itamfanya aonekane ni kiongozi bora.

Katiba itakayotuongoza kwenye maendeleo ya kweli, kumuheshimu Muumba aliyeamua kuusimamisha Mlima Kilimanjaro Tanzania, akaiweka Ngorongoro na kutuzawadia bahari, akatupa ZiwaTanganyika, Nyasa, Rukwa, akajaza utajiri ardhini. Katiba itayoruhusu tume huru ya Uchaguzi, na pia taasisi huru ya kuzuia rushwa.

Nendeni mtoni mkaoshe akili na roho zenu ubinafsi umewachafua. Nasema mimi Mfungwa Mswahili. Mimi si yule msaliti anayesubiri nauli wakati aendapo ameshafika! Wala sina ujamaa naye, mie sitangazi ujomba ili nibebwe.

Msinichanganye, kwanza nina mwiko wa kuchanganyika na watu wanaoupenda sana uhai wao kuliko kuishi kwao.

Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… Tofauti ipo.

Siogopi maumivu mliyoniandalia, mimi ni marehemu niliyerudishwa kwa ajili ya Mswahili aliaye shidani. Mtu hafi mara mbili bwana.

Ndimi bwana, kaulize Bagamoyo, mimi pilipili, mimi dawa chungu, mimi nansimba, nene mwaromaini, nenu musilya nene nyimbwa zintaliwe, nene wakwe chomba chomba cha lushombo wakwe ntalenga nyama ulalenga na ya mulawa.

Nimetumwa naye mwenye uwezo wa kuumba na kuumbua, anasema kwamba huu ndio wakati pekee ambao sauti na kalamu zetu zinaweza kuiokoa nchi yetu kabla jua la amani hii halijachwea.

Ndugu wanafiki wafanyabiashara wa muziki, maadui wa utamaduni wetu wabinafsi na waabudu pesa wote;

Msijisumbue kunitishia umasikini, mkafikiri mtanibadilisha, mimi vita yangu sio ya utajiri na mali, sikuja na mizigo wala sihitaji mizigo katika kuondoka kwangu — nilikuja uchi kutoka tumboni mwa mamaangu nitarudi uchi katika tumbo la nchi.

Heshima ya nchi hii ya baba’angu itarudi, kwa vyovyote na kwa gharama yoyote, kikiharibika kitu Baba’angu atarekebisha, na sitakufa tena niwaache wanangu na njaa. Mimi sio masikini na kila Mtanzania aliyezaliwa baada yangu si mtoto wa masikini. Na njaa itamuheshimu, nene tundu kumusenga, wachisenga malezi nukumila ntaleka.

Tofauti ipo! Tofauti kati ya utawala bora na uongozi bora… Tofauti ipo.

Na wote mliotuibia;

Imekuwa vema hatukufundishwa kushika silaha, na Muumba atunusuru na hilo. Lakini ole wao watoto na wajukuu zenu, sijui wataoga wapi hata shombo na vumba la uozo wenu liishe. Maana wanakuja watoto wetu hodari, wala nyuki, nyoka waumao usiku.

Mungu wangu, ulikwisha ibariki Tanzania. Mungu ulishaibariki Afrika. Mungu usituondelee Baraka hii. Sina haki ya kupewa kila nitakachoomba, lakini kwa neema zako naamini utanijaalia kwa ajili ya Tanzania yako.

Tofauti ipo! Tofauti kati ya baraka na laana… Tofauti ipo.

Watie aibu maadui wa mtumishi wako. Amlaanie uliyembariki, laana yake imrudie.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend