Hivi rushwa bado ni adui wa haki?

Na Gureni Lukwaro

Kabla ya kuanzishwa kwa somo la uraia kwenye mtaala wa elimu ya msingi kulikuwa na somo la Siasa. Kwa wale tuliosoma somo hilo tunaweza kukumbuka, pamoja na mambo mengine, tuliwasoma maadui wakubwa watatu wa maendeleo yaani umaskini, maradhi na ujinga.

Tulifundishwa kuwapinga maadui hawa kwa nguvu zote maana maendeleo yetu, ya nchi yetu na ya watu wetu  yanategemea sana ushindi wetu dhidi ya maadui hawa.

Lakini zaidi ya maadui hao watatu, tulifundishwa kuhusu adui mwingine, adui rushwa. Katika hilo tulifundishwa kuwa rushwa, siyo tu ni adui wa maendeleo, lakini pia ni adui wa haki. Kwa hiyo katika maadui hao wanne, tulifundishwa kuwa rushwa ni adui mkubwa zaidi ambaye tulitakiwa tupigane naye kwa nguvu zaidi ili kutetea haki yetu na kujiletea maendeleo sisi na nchi yetu ya Tanzania.

Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa shujaa mahiri wa kupambana na adui huyu wa haki kwa maneno na kwa vitendo. Hili linadhihishwa na mojawapo ya hotuba zake ya mnamo Mei 17, 1960 ambapo alinukuliwa kujadili maadui watatu wa umaskini, maradhi na ujinga na kisha adui wanne, rushwa.

“Nataka kuongezea kwamba kuna adui mwingine ambaye ni lazima tumuongeze kwenye orodha ya maadui hawa wa umaskini, maradhi na ujinga…Kuna ufisadi. Sasa mheshimiwa, nadhani ufisadi unapaswa kushughulikiwa bila huruma kabisa kwa sababu binafsi naamini kwamba ufisadi na rushwa ni maadui wakubwa zaidi wa ustawi wa watu wakati wa amani zaidi ya vita. Binafsi naamini kwamba ufisadi katika nchi yoyote unapaswa kushughulikiwa karibu sawa na uhaini unavyoshughulikiwa. Kama watu hawawezi kuwa na imani na serikali yao, kama watu wanahisi kwamba haki yaweza kununuliwa, unawaachia tumaini gani watu hao? Jambo pekee wanaloweza kufanya ni kuchukua silaha na kuiondoa serikali ya kijinga iliyopo madarakani. Hawana tumaini jingine…”

Lakini ukiangalia mwenendo wa nchi yetu ulivyo kwa sasa, huna budi kujiuliza kama rushwa bado ni adui wa haki ambaye tuliaswa kupambana naye bila huruma kabisa kama ambavyo tunapambana na uhaini.

Ingawa serikali imeunda taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa lakini ufanisi wa taasisi hiyo katika kupambana na adui huyu mkubwa wa haki una walakini. Nchi imekumbwa na kashfa nyingi za rushwa tena rushwa kubwa kubwa lakini katika chunguzi zake, taasisi hiyo imeshindwa kupata ushahidi wa kufikisha mahakamani watuhumiwa wa kashfa. Taasisi imeishia kushtaki watuhumiwa wadogowadogo na pale shinikizo lilipozidi kufikisha mahakamani maofisa waandamizi wachache wa serikali ambao si watajwa katika tuhuma hizo ili kuonyesha tu kwamba wanao uwezo wa kukamata maofisa wa ngazi za juu wa serikali hasa wale wasiohusishwa na kashfa za ufisadi.

Uchunguzi wa taasisi ya kupambana na rushwa kuhusu kashfa ya ufisadi katika uzabuni wa mradi wa kufua umeme wa Richmond ulionyesha kutokuwepo tatizo lolote katika zabuni hiyo.

Lakini kamati teule ya Bunge ilipofanya uchunguzi wake ikabaini kasoro nyingi katika mradi huo. Taarifa ya kamati hiyo Bungeni ilifunua matatizo mengi yaliyopelekea Waziri Mkuu na mawaziri wengine watatu kujiuzulu nyadhifa zao. Sasa iweje taasisi ambayo ndiyo chombo kilichopewa dhamana ya kupambana na rushwa na yenye wataalamu na nyenzo zaidi ya kamati teule ya Bunge ishindwe kuona kasoro ambazo zilikuwa wazi kabisa kwa kamati teule ya Bunge? Ushahidi wa kamati teule ya Bunge ulikuwa dhahiri kiasi gani taasisi hiyo ya serikali ilivyo kiini macho katika mapambano dhidi ya rushwa na hivyo kuwa chombo cha kufuja kodi za watanzania bila tija.

Hivi karibuni tumesikia kwamba kampuni ya BAE system inayotengeneza vifaa vya anga ya Uingereza imeridhia kulipa Paundi za Uingereza milioni 29.5 kama mrejesho wa ziada ya fedha iliyotokana na manunuzi ya rada yaliyoghubikwa na ufisadi. Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya hapa nyumbani juu ya kashfa hiyo pia ulionyesha kutokuwepo kwa tatizo lolote la ufisadi katika mchakato mzima wa ununuzi wa Rada hiyo.

Lakini uchunguzi uliofanyika Uingereza ulibaini kasoro nyingi ambazo zingeweza kupelekea kampuni hiyo ya Uingereza kushtakiwa na kuadhibiwa. Lakini kwa kuogopa mashtaka na adhabu ambayo wangeweza kupewa, kampuni ya BAE waliamua kufikia suluhisho nje ya mahakama kwa kulipa faini ya Paundi za Uingezeza nusu milioni huko Uingezeza na kuifidia Tanzania kiwango tajwa hapo juu ili kuepuka kushtakiwa.

Swali linakuja tena, iweje mapambano yetu dhidi ya rushwa yasione kasoro yoyote katika mchakato wa ununuzi wa rada na uchunguzi wa wenzetu uone ushahidi na kasoro nyingi zilizoiogopesha kampuni hiyo ya Uingereza hadi kukubali kuzirejesha fedha za ziada walizoitoza Tanzania katika manunuzi ya rada hiyo ili kuepuka mashtaka ambayo yangeweza kupelekea adhabu kubwa dhidi yao? Hivi, rushwa bado ni adui wa haki? Kama bado ni adui wa haki, je tunafanya maendeleo yoyote katika kupambana dhidi yake?.Je, tunaishinda rushwa au rushwa inatushinda katika mapambano tunayoyafanya?

Zaidi ya hapo, siku za hivi karibuni tumesikia baadhi ya watu wakisifia nia ya chama tawala  yakujisafisha na rushwa kwa kujivua gamba. Kulingana na azma hiyo ya chama, si lazima ihakikishwe kwamba viongozi wa juu wa chama wamehusika na rushwa, chama kilinuia kuwawajibisha hata wale wanaotajwa tajwa na kuhusishwa na kashfa za rushwa. Na katika hili, ni vyema kumpongeza  aliyekua mbunge wa Igunga, Mheshimiwa Rostam Aziz kwa kuona haja ya kujivua gamba baada ya kutajwa kwenye kashfa hizi za rushwa.

Lakini kama kweli chama tawala na serikali yake kimenuia kupambana na rushwa pamoja na wala rushwa, basi hawapaswi kuishia kujivua gamba bali kitendo cha hao wanaotuhumiwa kujiuzulu kinamaanisha ukweli wa wao kuhusika na rushwa na hivyo wanapaswa kufikishwa mahakamani.

Azma ya chama tawala na serikali yake ya kujivua gamba inaonekana kuwa utapeli na hadaa kwa watanzania kama invyodhihirishwa na sakata la hivi karibuni la  katibu mkuu wa wizara ya Nishati na Madini David Jairo la kuchangisha  taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zaidi ya shilingi bilioni moja ili ziweze kutumiaka kuwahonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.

Ingawa Mheshimiwa Waziri Mkuu alionekana makini kabisa katika maelezo yake ya kuondoa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni, na muelekeo wake wa kile ambacho angemshauri Mheshimiwa Raisi, lakini hatua dhidi ya Jairo zilichelewa kuchukuliwa na hata zilipochukuliwa hazikuwa zile zilizopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyu. Watanzania wengi walitazamia Jairo si tuu kuwajibishwa kwa kufukuzwa kazi na  pia kushtakiwa, lakini badala yake alipewa likizo tena yenye malipo.

Tunakubali kwamba watu wote wanatakiwa kuhesabiwa hawana hatia hado pale watakapothibitishwa kuwa na hatia. Lakini mlolongo wa matukio yanayohusisha kashfa ya rushwa na azma ya watawala wetu kujivua magamba, si yale tu yaliyothibitishwa kuhusika na ufisadi, bali hata yale yanayotajwa tajwa kuhusika, ilipelekea wengi kuamini kwamba hatua kali zaidi zingechukuliwa dhidi ya Jairo.

Ukiangalia kwa undani zaidi unajiuliza ilikuwaje kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini isione mapungufu yoyote na bajeti ya wizara hiyo na kuiruhusu kupelekwa bungeni na mapungufu mengi hadi pale ilipokwamishwa na wabunge? Je inawezekana mkakati wa Jairo ulianzia kwa kamati hii kuishawishi kupitisha bajeti isiyo na tija kwa taifa? Inashangaza kuona kamati iliyopewa dhamana ya kuchuja mikakati mibovu ya serikali kutokuona kasoro yoyote huku waandaaji wa mikakati hiyo iliyomo kwenye bajeti kuona kasoro nyingi hadi kupelekea kuanzaa njia mbadala, ya rushwa, ya kuwezesha bajeti yao kupitishwa bungeni.

Wakati uchunguzi wa hili kama ulivyoahidiwa na serikali ukiendelea ni vyema viongozi wetu kujihoji na kufanya tathmini kama kwa mtazamo wao bado rushwa ni adui wa haki? Na kama jibu ni ndiyo, basi waonyeshe kwa vitendo jitihada zao za kupambana na adui huyu wa haki kama ambavyo Hayati Mwalimu Nyerere aliainisha au hata zaidi kama wanataka kurejesha imani ya wananchi kwa serikali na kwa chama tawala.

Gureni Lukwaro ni mwanajukwaa la mtandaoni la Wanazuoni wa Tanzania. Anapatikana kupitia: gureni (at) yahoo (dot) com

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend