Wakati ni upi, ujanani au uzeeni?

Na Michael Dalali

Mara kwa mara, msukumo mkubwa huwapata baadhi ya vijana wanaoonesha uwezo wa hali ya juu katika utendaji wa kazi zao, hasa upande wa nyota na karama ya uongozi (na uzalendo). Msukumo wa kutoka kwenye utumishi wao na kuingia katika utumishi wa umma; kushika nyadhifa za kisiasa, mathalani udiwani, ubunge na hata urais. Upi ni muda muafaka kuchukua njia hiyo?

Wasiwasi wa mlolongo wa kimaisha na mwenendo wa baadhi ya wanasiasa baada ya kuanza siasa mapema ni baadhi ya vyanzo vya changamoto.

Wapo baadhi ya wanasiasa ambao walijitosa kwenye siasa wakiwa na umri mdogo, na walipofika umri wa machweo wakajikuta wamechuja, wapo nje ya utumishi. Mbaya zaidi, baadhi yao wapo katika hali ngumu ya maisha. (Ingawa hali zao za sasa haziondoi kazi nzuri na ya thamani waliyoifanya.)

Tusisahau kuwa kuna baadhi ya wanasiasa pia walishiriki katika utumishi na wakadumu, na baadhi, hata kama walikuja kuachana na utumishi wa kisiasa baadae, hawakutetereka kimaisha. Wamemudu kutunza mwenendo imara wa kisiasa, kiuchumi na muonekano bora katika jamii. Hili ni kundi la kuangaliwa kwa makini — kama mwangaza kwa vijana ambao bado wanahoji.

“Nikiingia kwenye siasa sasa na kushinda, je,  nikishindwa kwenye uchaguzi ujao, nitaishije?” “Ameianza siasa mapema mno, angesubiri  na kufanya kazi kwanza nje ya siasa…” Hizi ni baadhi tu ya kauli ambazo hutoka katika pande mbili, yaani upande wa vijana wanaojihoji na wito wao katika kuanza utumishi wa kisiasa kwa umma, na upande mwingine ni kundi la wananchi na mtazamo wao kwa vijana wanasiasa.

Lakini tunapaswa kutosahau kwamba viongozi tunaowachagua kutuwakilisha hawaingii kwenye nyadhifa za kudumu. Leo anatuwakilisha huyu, kesho si vibaya akatuwakilisha yule. Hakuna ubaya endapo kijana makini akapatiwa fursa ya kuongoza, yeye kwa utashi wake akashiriki bega kwa bega na wananchi wengine kujenga nchi, huku akijua baada ya kipindi fulani — mathalani mihula miwili — ni vyema akapisha na kumpa kijiti mwingine. Inapaswa kujenga mtazamo huu ndani ya mioyo na fikra. Hauoti tu kama uyoga.

Ndipo hapo baadhi, katika kilio cha mabadiliko ya katiba, huja na hoja ya uwepo wa haja ya ukomo katika nyadhifa za utumishi wa kisiasa, kama udiwani na ubunge. Lisiwe tu jambo la utashi, jambo la msimamo wa mtu, bali sasa tuliweke pia katika vitabu vya sheria.

Samba Mapangala aliasa juu ya kufanya jambo wakati mhusika ana uwezo: “Vunja mifupa wakati meno ipo!”

Kuna mikiki-mikiki fulani katika hekaheka za siasa ambayo hakika wanasiasa vijana wanaweza wakaifanya pasipokuhisi kama wanaumia. Kwani damu inachemka, ndio muda wenyewe hasa wa hekaheka. Katika mikiki-mikiki hiyo, hata kama wanasiasa wazee wangalitamani kujitosa, kuna vitu mbalimbali ambavyo haviwapi fursa, kwa mfano afya, n.k. Na hapo ndipo wanawaachia vijana, huku wao wakiwa nyuma kama wachora ramani na washauri.

Si tu ujana, bali ukiwa kijana mwenye ufahamu mpana (au msomi), utashi wa kujifunza, msikivu, mnyenyekevu, ari ya kujituma, mchapa kazi hodari na mengine mengi, ni tunu kubwa kuwekeza nguvu na mwamko wa awali katika utumishi wa Taifa changa ambalo bado lina matatizo lukuki.

Natambua dhahiri uongozi si ujana tu; ni mkusanyiko wa mengi ikiwemo uwezo, kipaji  na uadilifu — haya yote yanahitajika na ni muhimu sana kwa mtu yeyote anayetaka kuongoza wengine.

Lakini tusisahau kuwa fursa ambazo huja kwa wakati. Na wakati huo ukishapita, fursa hiyo nayo inaweza kuyeyuka. Hivyo, wakati nyota bado i angavu, kijana anapaswa asonge mbele na kulitumikia Taifa na wananchi wake.

Tunatambua hatuijui kesho yetu, maana uhai anao Mungu na siri ya kesho aijuaye ni Yeye. Tunapaswa kutenda lile ambalo tuna uwezo nalo katika kipindi ambacho tunajaliwa na Mungu.

Uingiapo katika utumishi wa umma, bado inaendelea kuwa fursa ya kujua na kupanga maisha baada ya utumishi. Hivyo, hata kama utumishi utakoma baada ya muhula mmoja (miaka mitano), mhusika anapaswa kujua arejee katika utendaji wake wa awali au kuyachukua maisha mapya ambayo atakuwa amejipangia.

Si vibaya jamii ikajenga mtazamo chanya wa kuwapokea watu ambao wametoka katika utumishi wa kisiasa (hususan kutoka katika vyama vya upinzani) — kuweza kuwapokea na kuishi nao kama wananchi wa kawaida. Kuweza kuwapa fursa tena ya kuishi maisha kama raia ambao si watumishi tena. Nao pia wanapaswa kujijenga hivyo!

Isiwe vigumu kwa kampuni au taasisi kutoa fursa kumwajiri mhusika endapo anakidhi viwango na vigezo wanavyovihitaji, na si kumuengua kwa sababu za haiba yake.

Tuendelee kujadili — upi ni wakati muafaka wa kutumikia wana wa nchi! Ujanani au uzeeni?

Makala na kurasa nyingine:

Michael Dalali anapatikana kwa njia ya barua pepe:  michael (at) michaeldalali (dot) com.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 2 Comments

2
  1. Sura chache zinazoonekana kwenye Bunge, siasa kwa ujumla na sekta nyingine zinaweza zikawa zinatuhadaa. Vijana bado hawana mwamko wa wao wenyewe kufanya kile wanachopaswa kufanya (proactive) ili kushika hatamu ya maisha yao na kizazi kitakachofuata.

    Ni kosa lao? Ni mfumo wetu?

    Je, jamii yetu inaandaa watu kuwa na fikra za uongozi (sio lazima kwenye siasa tu)? Tunaruhusu au tunawafundisha watoto wetu kuhoji au kuuliza maswali majumbani mwetu? Kama jibu ni hapana, tutegemee nini wanapokuwa watu wazima?

    Naelewa kitu ambacho mwandishi anajaribu kusema; lakini kuna maswali ya msingi ambayo yanapaswa kujibiwa.

    Labda ni mtazamo tofauti, lakini mtu akiangalia tu jamii yetu anapata jawabu. Mara ngapi unaona vijana kwenye runinga wakijadili mustakabali wa nchi yetu kwa ujumla (achana na muziki na michezo). Iwe kwenye siasa, teknolojia, sayansi, biashara… Wakitupa wananchi mitazamo mipya, ambayo vijana haswa ndio wanapaswa kuwa nao.

    Ndio damu inaweza ikawa inachemka, lakini kama haipandi kichwani, what’s the use?

    Kuna chama au umoja wa vijana unaotambulika kama taasisi rasmi Tanzania? Tukiamua kupendekeza vifungu fulani kwenye Katiba Mpya, vijana gani watapewa jukumu la kujadili na kuwasilisha mawazo yetu (bila kujali wanatoka vyama gani)?

    Je, vijana sasa hivi wana uwezo? Kama jibu ni ndio, nafasi zipo au wanaheshimiwa?

    Kwa sababu tunachoshuhudia sasa hivi ni vijana “kutumiwa” kwenye mapambano kwa niaba ya wazee…

  2. Maarifa,

    Nashukuru sana kwa mchango wako.

    Nina machache, katika aya yako ya kwanza. Nadhani sura chache za vijana walio katika siasa na waliweza kuthubutu kushika nyadhifa mbalimbali hata nje ya ulingo wa siasa mathalani katika mashirika binafsi na asasi za kiraia si hadaa, bali ndiyo chachu halisi na tunu kuwa vijana wanauwezo wa kushika nyadhifa hizo na kutenda. Nakubali si vijana wote, bali wale wenye uwezo, visheni na fikra angavu.

    Umehoji sahihi juu ya “mifumo” kama i sahihi na kama kweli kwa upana kuna mifumo sahihi ya kuandaa viongozi imara (si tu wale katika siasa). Binafsi nadhani mifumo i dhaifu, (kama ipo). Lakini pia si yakutosha.

    Nimependa sana usemi wako; “ndiyo damu inaweza kuwa inachemka lakini je inapanda kichwani?”

    Chombo za kuwaunganisha vijana kitaifa, hiyo ni dana dana ya muda mrefu sana inakwepwa Tanzania kutokea.Miaka sasa imeshasonga.

    Kijana yeyote anayetumiwa, hatufai!Anapaswa kuwa kijana imara mwenye uwezo na mtazamo huru na kusimama yeye kama yeye na si kuwa kibaraka au kutumiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend