Five Questions with SaRaha

Five Questions with SaRaha

Sara Lundström aka SaRaha (linatamkwa kama “furaha”) ni msanii anayefanya kazi zake kwenye studio za Usanii Production. SaRaha analeta sauti ya kipekee kabisa katika tasnia ya Bongo Flava. Baadhi yenu mnaweza mkawa hamjawahi kumsikia, lakini ucheshi wa mashairi yake utakufanya utake kujua zaidi juu ya msanii huyu!

Baada ya kusikiliza wimbo wake “Tanesco,” nilipatwa na hamu ya kujua zaidi, na ndipo hapo safari ya kumtafuta dada SaRaha ilipoanza. Lafudhi yake itakuacha ukijiuliza, SaRaha ni nani, na anatoka wapi?

SaRaha hakusita kulonga na Vijana FM, kutupa undani kidogo wa yeye ni nani kama msanii, Saraha, na kama Sara Lundström. Karibu kusikia misimamo ya msanii huyu na mitazamo yake ya kimaisha kupitia muziki…

1. SaRaha ni nani hasa? Fani hii ya muziki ulianza lini na ni nini kilikuvutia? Kiswahili chako ni kizuri, umekuwa ukiimba kwa Kiswahili kwa muda mrefu?  Katika uandishi wa mashairi, kuna changamoto zozote unazozipata, ukizingatia unajua Kiingereza na Kiswidi.   

SaRaha ni msanii na mwimbaji wa Bongo Flava. Nilizaliwa Sweden, lakini wazazi wangu wamekuwa wakifanya kazi hapa Tanzania kwa miaka mingi, na hivyo kwa muda mrefu niliishi Tabora na Nzega. Nimekuwa nikiimba maisha yangu yote, nilianza kupiga gitaa (guitar) na kuandika nyimbo nilipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu.

Mwaka 2001-2003 niliishi Harare, Zimbabwe, na nilikuwa nikipiga gitaa kwenye bendi moja ya huko, iliyokuwa inaitwa SIJ. Niliporudi Sweden, niliendelea kufanya kazi na bendi mbalimbali, na kwa miaka sita nilipiga live shows za muziki wa Pop na Reggae.

Sasa nimerudi (Tanzania) pamoja na mume wangu, producer Fundi Samweli, kufanya kazi zangu za kimuziki hapa Tanzania. Kiswahili changu nilikisahau niliporudi Sweden, lakini kwa sasa ninajitahidi kujifunza tena. Kuimba kwa Kiswahili sio kazi kubwa sababu bado ninazo flow zake.

2. “Tanesco” ulikuwa wimbo wa kwanza kuusikia kutoka kwako. Wazo la kutunga ule wimbo ulilipateje?  Pia, nimependa vocals zako kwenye wimbo “Fei” wa Fid Q, pamoja na wimbo “Kidogo” ulioshirikishwa na Magese. Unaandika mashairi yako mwenyewe?  Maana’ke umegusia matatizo ya msingi katika jamii kwenye wimbo “Kidogo”…

Ndiyo, wimbo wa “Tanesco” ulikuwa ni single yangu ya kwanza ya Kiswahili. Wazo lilikuja usiku mmoja nilipokuwa studio nikirekodi. Umeme ulikatika, kwa hiyo nikakaa gizani pamoja na gitaa langu, na nikapata wazo!

Nilifurahi kufanya wimbo ule (Fei) pamoja na Fid Q. Anazumgumza mambo muhimu, ninaheshimu sana kazi zake… Tulifanya show pamoja kwenye Zanzibar International Film Festival mwaka huu.

Kidogo” niliufanya pamoja na Magese… ni wimbo mzuri, style mpya na beat kali! Sasa hivi nasubiri releases za collaborations nilizofanya pamoja na wasanii wengine wa Tanzania. Pia, nimetoa wimbo mpya hivi karibuni, unaitwa “Kama Malaika.”

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

3. Wanasema muziki ni lugha ya dunia nzima, kwanini uliamua nyimbo zako ziwe na maudhui na mandhari ya Kitanzania, zaidi ya kutumia tu lugha ya Kiswahili? Na nini hasa kilikuvutia na kukusukuma kufanya kile unachofanya?

Niliporudi Tanzania 2006 kutembelea, nilitamani kurudi kuishi hapa. Pia nilisikiliza Bongo Flava, na nikaipenda saaana! Nilitaka kufanya kitu kipya, kwa hiyo nilipanga pamoja na Fundi Samweli nifanye Bongo Flava, na lazima niimbe kwa Kiswahili. Kiswahili ni lugha safi, ni lugha ya ushairi.

Nimeshafanya styles tofauti; Pop, Reggae, Dub, Acoustic music, na sasa hivi nina fanya Bongo Flava tu. Style yangu ya kuimba imekuwa influenced na wasanii wengi. Nimesikiliza sana waimbaji wa kike wa zamani na wapya kutoka Ulaya, kama Melanie Safka, Tori Amos, Björk, Amy Winehouse na Lily Allen. Sasa hivi najifunza style ya Tanzania, hivyo nasikiliza melodies na styles za bongo flava, lakini sitaki kuacha character ya sauti yangu na kuiga wengine. Nataka nikiimba watu wajue: huyu ni SaRaha!

4. Safari yako mpaka usani studio ilianzia wapi? Nimeona umefanya collabo kadhaa, je uko mbioni kutengeneza album? Kama msanii aliyeanzia muziki nchi nyingine, ni changamoto gani unapata au unazoziona hapa Tanzania katika fani ya muziki, na kwa wanamuziki wa Tanzania? Pia ni wanamuziki gani wa Tanzania ambao wanakuvutia, na kwanini?

Changamoto yangu ni lugha. Kuandika lyrics kwa Kiswahili inachukua muda, na ni kazi kubwa kuliko lugha yangu ya Kiswidi, au Kiingereza. Pia ni changamoto kufuata East African styles, melodies na flow kwani ni tofauti na muziki niliokuwa nafanya. Lakini vitu kama hivyo sio vibaya. Ukiweza kuzipita hizo changamoto basi vitu vizuri vitakuja! Nafanya Bongo Flava kwasababu naipenda, inakaa moyoni mwangu, lakini nitaingiza mawazo mapya kwa sababu background yangu ni tofauti kuliko wasanii wengi wa Tanzania.

Kwa wasanii wengi maisha ni magumu. Kuwa msanii ni kazi kubwa, na ni ngumu kupata fedha ya kutosha. Kwasababu ya piracy, hawawezi kupata malipo kupitia mauzo ya albums zao, na hata zikipigwa [kwenye vituo vya] radio hawapati fedha. Live shows tu zinabaki. Muziki ni muhimu sana, tunahitaji sana mabadiliko ya industry ya muziki.

5. Kama kijana na mwanamuziki, ambaye mashairi ya nyimbo zako yana mwamko wa masuala ya kijamii, unadhani muziki na wanamuziki wana nafasi gani katika jamii, hasa kwa hapa Tanzania, ukizingatia kuna maandamano ya ‘Occupy Wallstreet’ yanayosambaa dunia nzima? Tofauti ambazo umeziona kati ya vijana wa Tanzania na nchi nyingine, kama Sweden ni zipi?

Ninaamini, muziki unaweza kuleta mabadiliko katika jamii, siasa na katika maisha ya watu binafsi. Muziki unawapa watu nafasi ya kuzungumza mambo muhimu na kubadilishana mawazo mbalimbali. Pia, huwapa watu sauti. Kuna wasanii wa Kitanzania ambao huzungumzia matatizo ya kijamii, kwa mfano Fid Q, Nakaaya, Nako 2 Nako, Joh Makini, kutaja wachache tu, ambao sauti zao ni muhimu.

Vijana hukumbana na changamoto popote walipo duniani. Kuona matatizo na ukosefu wa usawa duniani inakasirisha sana, lakini hasira hizo zinaweza kubadilika na kuwa ndio chanzo cha mabadiliko. Pia, ni muhimu vijana washiriki katika mabadiliko hayo, kwa kurekebisha matatizo ya jamii. Hali ya kiuchumi ya Tanzania ni tofauti sana, na mfumo wa elimu ni duni. Ni vigumu sana kwa vijana kuendesha maisha yao. Rushwa pia, huongeza matatizo katika nyanja mbalimbali za kijamii, na ni kitu kugumu sana kukishinda.

Vijana wote duniani wanahangaika kujua nafasi yao katika jamii ni ipi, kwa mfano, wawe nani, wafuate kanuni gani, na vipi waishi maisha yao. Mifumo iliyopo, inawatenga na kuwabagua watu wengi, na kuwanyima sauti kama wanawake, walemavu, watu masikini, n.k. Tukija kwenye masuala kama haya, muziki ndio unaweza kutumika.

Vijana FM inapenda kutoa shukurani za dhati kwa msanii SaRaha kwa kukubali kufanya mahojiano mafupi na sisi. Tunakutakia kila la kheri katika maandalizi ya album mpya, kwani mwanzo ni mzuri. Tunafurahi kuona Bongo Flava inapata sauti tofauti.

Kama ndio mara yako ya kwanza kumsikia msanii SaRaha, basi kaa chonjo kwa habari zaidi kutoka kwake na nyimbo zake mpya. Lakini kwa sasa, endelea kuburudika na single yake mpya “Kama Malaika”:

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Tovuti muhimu za SaRaha:

Bahati was born and raised in Tanzania, and then moved to California to pursue his college education. He graduated in 2008 with a Bachelor’s Degree in Political Science and a minor in Sociology. Bahati expects to be doing his Masters in African Studies in the near future. He is currently working on starting a t-shirt business and a possible publication of some of his writings. One thing that Bahati cannot live without is music, specifically Hip Hop & Bongoflava which he argues are both the voice of the youth today, and is excited to look into how Bongoflava can be a source of further entrepreneurship among the youth in Tanzania. Bahati believes that Bongoflava can help to reduce poverty in Tanzania, as can a more collective effort among key players.

0 Comments

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Human verification:

Please type the characters of this captcha image in the input box

*