Mbwa wa Pavlov III

Awali ya yote, napenda kuanza kwa kuwaomba msamaha Watanzania wote nchini na wengine wanaoishi kwenye kona mbalimbali za dunia. Matatizo na changamoto zinazoendelea kutusonga Watanzania, hasa wale wa tabaka la chini kabisa, zilipaswa kuanza kukoma takribani miaka 15 iliyopita.

Jumapili moja jioni, mwaka 1996, nilikuwa natazama kipindi cha ‘Africa Journal,’ pamoja na watu wa makamo, kilichokuwa kinarushwa na ITV kwa lugha ya Kiswahili. Kama desturi, kipindi kilianza kwa kujadili changamoto za kiuchumi zinazoikumba nchi ya Ghana, ingawa ardhi yake ilikuwa inasifika kwa kuzalisha madini ya dhahabu dunia nzima. Sehemu ya pili ya kipindi ikazama Afrika Kusini; kuangalia jinsi wanavyokabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii baada ya kuondokana na utawala na sera za kibaguzi (wa rangi).

Muda wote huu nadhani ni mimi pekee niliyekuwa nafuatilia kwa makini kinachoendelea. Wazee walikuwa wakitupia jicho runinga mara moja-moja huku wakiendelea kupiga soga na kupata moja baridi moja moto. Sasa, sehemu ya tatu ya kipindi ikaenda Zimbabwe. Na kilichokuwa kinaripotiwa ni mlipuko wa migawaha ya wasenge kwenye mji wa Harare.

Ghafla, ukimya ukachukua ukumbi. Mmoja wa wazee nusu apaliwe na bia! Nikadhani labda kwa sababu ITV wamekiuka maadili ya uandishi wa habari kwa kuruhusu “tusi” kwenda hewani. Nikajisemea kimoyo-moyo, “Mzee Mengi lazima atatimua kazi watu kesho!” Ripota kutoka Zimbabwe akaendelea kujadili na kutamka neno ‘wasenge’ kama vile ni neno la kawaida tu, wakati huo wazee niliokuwa nao wakiendelea kuikodolea macho runinga kwa umakini wa hali ya juu.

Nikaona isiwe nongwa, nikabadilisha kituo cha televisheni. “Paaaah!” Konzi likatua kwenye utosi wa kichwa changu. “Hebu rudisha ITV we’ mtoto,” mwingine akaongezea. Hapo ndipo nikaanza kuelewa unyeti wa jambo lililokuwa linaloripotiwa, kwa sababu hata baada ya kipindi kumalizika nilisikia wazee wakiendelea kujadili walichosikia kutoka Zimbabwe.

Bahati mbaya au nzuri, lile tukio nikaliacha na likayeyuka kwenye mawazo yangu — hili ndio kosa langu hasa.

Baada ya miezi kadhaa, nikakumbushwa lile tukio na mhubiri mmoja ambaye alikuwa anatumia kisa cha Sodoma na Gomora kuonya waumini wa kanisa kuachana na dhambi; akitumia mfano wa dhambi ya ufiraji. Ndio, ni kisa kutoka kwenye Agano la Kale (Mwanzo 18-19), na wengi tumesoma kuhusu ghadhabu ya Mungu. Abrahamu akabakia kumuuliza Mungu maswali, “Itakuwaje kama kutakuwa na watu 50 ndani ya Sodoma ambao sio wadhambi, utaiteketeza Sodoma?” Abrahamu akapunguza idadi hadi akafika 10. “Je, utaiteketeza Sodoma kama kukiwa na watu 10 ambao sio “wadhambi”?”

Malaika wawili wakatumwa kwenda kuiteketeza Sodoma na Gomora, ambapo Lutu, ndugu yake na Abrahamu, alikuwa anaishi na familia yake. Lutu akawakaribisha kwenye nyumba yake. Majirani wakapata habari kwamba Lutu amepata ugeni wa wanaume wawili, na habari zikasambaa mji mzima. Wakazi wa Sodoma na Gomora wakaizunguka nyumba ya Lutu, wakimuamuru Lutu awatoe nje wageni wake ili waweze ‘kuwajua’.

Lutu, akijua wageni wake ni watumishi wa Mungu, akakataa. Badala yake akawaambia yupo tayari kuwapa mabinti zake wawili, mabikira, na wawafanye wanachotaka! Wakazi wa Sodoma wakang’ang’ania kuwa wanawataka wale wageni tu, na kama asipofanya hivyo basi watamfanyia Lutu kitu kibaya.

Lutu akakataa kufuata matakwa yao. Watu wakaanza kuvunja mlango ili waingie kwenye nyumba ya Lutu. Malaika wakaingilia kati na kuwapofusha wale watu.

Ingawa tunafahamu nini kilitokea baadaye, itakuwa sio vibaya ukajikumbushia kisa kizima, mwenyewe, kwa muda wako, na kujenga mtazamo au maoni yako binafsi.

Kisha jiulize, dhambi ‘pekee’ iliyokuwa inafanywa na wakazi wa Sodoma ni ufiraji tu? Pia, mbele ya macho ya Mungu, dhambi zina uzito tofauti au dhambi zote ni sawa? Kama dhambi zote ni sawa, basi kuwahukumu mashoga na kufanya ushoga hakuna tofauti? Ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na vitendo vya ushoga vipo sambamba; yaani ni sawa katika kukiuka maadili?

Au mambo ya uongozi bora na kulitumikia Taifa kwa uadilifu sio sehemu ya maadili yanayojadiliwa kwenye Katiba ya Tanzania?

Hakuna haja ya kurudia kile kilichosemwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Camron, wiki iliyopita. Ila nimejifunza kitu kimoja muhimu mno baada ya kushuhudia jinsi Watanzania kwa ujumla — kasoro Rais — walivyounganika na kutoa sauti moja kupinga yaliyosemwa na Waziri Mkuu.

Kumbe ukitaka kupata umakini — masikio, macho na fikra zao — wakati unatoa dukuduku lako kuhusu maendeleo au changamoto kwenye nchi yetu huna budi kutaja tu mashoga na wasagaji kwenye risala yako. Mwaka 1996 niliona wazee walivyong’aka baada ya kusikia ‘wasenge’ kutoka kwenye runinga. Nilishindwa kuelewa mara moja kilichotokea pale, ila sasa hivi nimepata picha kamili!

Naanza kama ifuatavyo nikiamini wasomaji wataniunga mkono; kama mifano tu…

Shirika la Umeme limeshindwa kabisa kutatua tatizo la umeme nchini, mpaka tunabaki kuhoji kama bado tuna Wizara ya Nishati na Madini. Natambua kuwa kuna juhudi za viongozi wenye mamlaka zinaendelea. Lakini, tunawaomba kwenye tafiti zao basi wajaribu kuangalia na ule ‘upande wa pili’. Huwezi jua, labda kuna wafanyakazi kadhaa ambao ndio chanzo.

Sekta ya elimu Tanzania haina mbele wala nyuma, na ukiacha vijana wa sasa, inaonekana itahatarisha sana ‘vizazi vijavyo’. Wahusika hapa itabidi waangaliwe kwa makini, kwa sababu labda hawataki hata kuona ‘vizazi vijavyo’!

Ni dhahiri kwamba vitendo vya ufisadi vinaendelea na vinazidi kuongezeka kila kukicha. Hawa mafisadi wanaiba sana ili iweje? Labda wanatumia vijisenti kutembelea mara kwa mara nchi ambazo ‘tabia zao’ zinaruhusiwa?

Kama bado hujapata kile ambacho makala hii ilikusudia, natambua kuwa kila mtu ana mawazo na msimamo wake. Viongozi nao wana misimamo na mitazamo yao. Lakini, maadili yanatuhusu wote — maadili ya jamii husika hayapo kwa ajili ya kunyooshea kidole tabaka au kundi fulani tu, kwa kuwa huu utakuwa ni unafiki.

Pia, kwa kumalizia tu, nina mawaidha kwa watu ambao wana maoni au mitazamo kuhusu changamoto na mwelekeo wa nchi yetu  kwa ujumla. Nadhani Kijerumani labda ni lugha pekee ambayo hutofautisha aina za maoni au mitazamo. Kwanza, kuna Meinungen — maoni ambayo hubadilika kutegemea na hisia na mazingara ya mhusika. Pili, kuna Ansichten — haya hutolewa na mtu baada ya kufikiriwa kwa makini na kwa muda mrefu; hayabadiliki kwa urahisi.

Nazungumzia maoni ya viongozi na watu wenye mamlaka, na maoni ya watu juu ya viongozi na watu wenye mamlaka.* Tujiulize, Tanzania ingekuwa wapi kawa viongozi wangekuwa wakali kama kwenye hizi siku tano zilizopita?

Makala Zilizopita:

*Maoni kuhusu mashoga kwenye jamii nayo yanaruhusiwa na yanakaribishwa, ingawa makala inawalenga zaidi viongozi wa nchi yetu ili kujaribu kuwekeza kwenye maendeleo endelevu.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 6 Comments

6
  1. Siri ya mwana mazingaombwe mzuri ni kuku distract wakati anafanya mazingaombwe yake, ndo maana inaitwa kiini macho. Nia yangu kusema hivyo ni kuidhinisha kwamba, viongozi wa Tanzania wameshindwa kazi, sasa kutokana na hali ya uchumi, elimu, manzigira na kijamii kua mbaya, wanajaribu kutafuta ishu ambayo inawasahaulisha wananchi kuhusu mambo yanayowagusa kila siku na badala yake wang’ang’anie suala kama la ushoga. Kila siku mi nasikia kuhusu hizi mila na desturi/maadili ya mtanzania, lakini hii ni nchi yenye makabila lukuki na dini kadhaa, sasa ni muhimu kufata maadili au sheria? maana sheria inatakiwa kulinda kila mwananchi awe shoga au sio na tunapobagua watu flani kwasababu ya “dhambi” zao hiyo dhambi ya ubaguzi itatufikia wote, kama baba wa taifa alivyowahi kunena hapo nyuma.

    PS- umenikumbusha mbali ya hiyo episode ya Africa Journal, niliicheki na washua na ikaangua bonge moja la mjadala sebuleni.

  2. Shukrani SN – I’ve noticed that with an increase in people’s ability to connect to the Internet, people – leaders especially – seem to think that when they are on the grid, they can chill without speaking.

    But I would think that this medium – let’s call it new media – assumes all actors to engage in some kind of debate, discussion, etc. because that’s the real networking benefit of this infrastructure. So why be on it if you ain’t got things to say OR are not willing to hear what is being said to you?

  3. AK, I understand where you’re coming from. We have seen leaders refusing to say anything, if at all, when the going gets tough, meaning we have only a handful who are tough enough to get going. It’s only a few leaders who seem to know how to use the tools we have got at the moment.

    As Faraja says, most of them seem to be very good at discussing and offering their opinions when the matters at hand are not of interest of the nation as a whole. Hakuna matatizo ya mashoga Tanzania (ila wapo, kama nchi yoyote ile duniani). Nadhani hapa watu wamedandia treni kwa mbele na wameziacha hisia zao kuwaongoza.

    Ile kauli ya Cameron haiwahusu Watanzania tu*… alikuwa anazungumzia mambo ambayo yameripotiwa hivi karibuni kutoka Uganda, Zambia, n.k. Kuna mwanaharakati mmoja wa mashoga aliuwawa, na serikali ya Uganda inatamka wazi kuhusu vita yao dhidi ya mashoga.

    Bongo tuna sehemu kama kwa Macheni pale, lakini sijawahisi kusikia shoga kauwawa kwa kupigwa nondo vichochoroni, au polisi wameenda sehemu na kuwaweka mashoga chini ya ulinzi, kuwapeleka mahakamani na kuwapa kifungo cha miaka 30. Nisahihisheni kama nimekosea. Katiba na sheria ya nchi yetu inasemaje kuhusu hilo?

    Au kuchapisha magazeti yakiwa na majina, makazi na picha za mashoga? Hii imeshawahi kutokea Tanzania?

    Hivi tunaangalia kama watu ni mashoga kabla hawajaruhusiwa kupiga kura au kuajiriwa? Haya ndio mambo ya kuangaliwa.

    Sitaki wala sisubiri kauli ya Rais kwenye hili suala! Atuambie kwa urefu na mapana, umeme uko wapi? Dowans ipo vipi? Elimu mbona bado hali ni tete? Uchumi mbona unayumba?

    Watanzania wamecharuka wiki hii. Nadhani nguvu na jitihada zao zinapaswa kuelekezwa kwa viongozi ambao hawafanyi kazi zao kwa uadilifu badala ya mashoga.

    *Ila hilo suala la kuzalilishwa, inabidi tujiangalie. Tunavuliwa nguo mbele ya kadamnasi kwa sababu tu tunategemea misaada yao. Labda tuanze kufikiria kuendesha nchi zetu kwa chochote tulichonacho. Ndio maana kuna wakati naelewa hoja za Uncle Bob.

  4. SN
    Asante kwa kutoa hoja nzuri mno, ambayo nina uhakika itajadiliwa hapa vijanafm kwa ufasaha.
    Nimependa pale @Maarifa aliponena kwa macheni, mashoga huwa wanakusanyika na kustarehe kwa wakati wao, mie nitaongezea na kudai, familia nyingi tu Dar es Salaam (hasa zenye uwezo), zimekumbwa na hili swala la watoto wao wa kiume kujihusisha na ushoga. Uzuri ni kama alivyosema @Maarifa, wala hutasikia mashoga wamekusanywa na kusekwa jela, au kutendewa vitendo vyovyote vya kinyama! Je inawezekana sie wabongo tuko “tolerant?” Inawezekana. Nilipokuwa mtoto nakumbuka mie na wenzangu tulikuwa na kawaida ya kuwashangaa mashoga, na hata wengine kudiriki kuwazomea (kitu ambacho nakumbuka dhahiri sikuchangia kabisa).
    Sheria zetu za nchi ambazo zinafanana na za nchi zingine zilizo kwenye jumuia ya “Commonwealth”, zinapinga kuutambua ushoga, wa akina “Cameron” walishabadili, inawezekana wakaona kuna fursa ya kutushawishi kutunga sheria za kulinda haki za mashoga, itakuwa kazi mno kwetu kukubaliana na shria hizi, maana nakumbuka kule uswazi, wazazi walikuwa wanadiriki kusema ni “heri mtoto awe jambazi kuliko shoga!” Je watanzania tutaendelea kuukana ushoga hadharani, wakati ukweli tunajua upo kwenye baadhi ya mitaa yetu, na hata kwenye baadhi ya familia zetu?
    Ni kama @SN ulivyouliza hapo juu, je ushoga ni dhambi kubwa sana kuliko zote duniani? Kuna baadhi ya websites na vitabu vya historia, vinadai ushoga ulikuwepo toka zamani tu, http://bit.ly/5tRQpv. Labda watanzania itabidi tukae chini kuangalia kama nasi tutaweza kuunda sheria ya either kuwalinda hawa ndugu zetu, watanzania wenzetu ambao ni mashoga, au kuukataa kabisa na kuweka sheria kuwa ni kosa kuwa shoga. Either way, tunahitaji kufanya haya maamuzi.

  5. Iwapo dhambi zote ni sawa sielewi kwa nini tunapigia kelele mno ushoga wakati tunaancha uzinzi unafanywa jahara?

    Nadhani hiyo notion kuwa dhambi zote ni sawa ndio hasa inayowafanya watu wasione tatizo la kufisidi nchi na kuzembea wajibu na majukumu yao. Na labda pia hii ndio sababu hasa Watanzania hatujali sana kile wanachokitenda viongozi. Dhambi zote sawa; yeye anafanya ufisadi, mimi nasema uongo, yule anatenda uzinzi. Kwa Mungu sote kapu moja

    Ni muda wa kukaa chini na kufikiri tena tunataka kuongozwa kwa fikra zipi? Za dini au dunia?

  6. “Liwalo na liwe… Mungu anawaona.” Au, “Ni mapenzi ya Mungu.”

    Hii misimamo ya kidini inachanganya sometimes!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend