Heshima haina umri

Na Dezidery Kajuna

Ni asubuhi ya saa tano, natoka ndani ya nyumba ninayoishi katika mtaa huu wa Prästgatan hapa nchini Uswidi tayari kwa ajili ya kwenda shule, maarufu kwa jina la SFI (Svenskundervisning för Invandrare) — kwa lugha ya Kiswahili ikiwa na maana ya Elimu ya Lugha ya Kiswidi kwa Wahamihaji au Wageni. Ni shule mahususi kabisa kwa ajili ya wale wanaopenda kujifunza Kiswidi ili iwe rahisi kwao kuwasiliana na wenyeji.

Sababu kubwa ya wageni kujifunza lugha hii ni muhimu, kwani lugha itumikayo katika nchi hii ni Kiswidi kila utakapokwenda. Ni tofauti na nchi kama Uingereza, Marekani na Australia ambako lugha muhimu ni Kiingereza. Ulazimu huu unarandana na hali ilivyo Ujerumani na nchi nyingine ambako lazima usome lugha yao kwa mawasiliano ya kawaida katika jamii zao. Jambo zuri ni kuwa katika nchi hizi, ofisi zote za serikali pamoja na vyuo vyote vinatumia lugha ya Kiingereza kwa ajili ya wageni, na lugha yao kwa ajili ya wenyeji.

Serikali ya Uswidi, kupitia halmashauri zake, zinatoa fursa ya bure kwa watu wote, bila kujali kama wewe ni mkimbizi, mhamiaji haramu au ni mgeni wa kawaida, kama vile mwanafunzi au mtalii, kujifunza Kiswidi. Makundi hayo yote yana haki ya kupata fursa ya kusoma Kiswidi bure bila kutoa senti mfukoni. Cha muhimu ni kuwa na namba ya uraia, hili ni jambo geni sana Tanzania, na sidhani kama tutaweza kufikia hatua hii ndani ya miaka ishirini.

Ukungu ni mwingi, theluji ikiwa imepukutika sana, na nimevaa viatu, si kama hivyo navyotumia nikiwa natoka kwa Mama Mtey (mwenye nyumba) hapo Ubungo kwenda mjini, hasa Posta ya Zamani kutafuta kazi katika maofisi. Kipindi cha baridi na hasa kipindi cha theluji inakulazimu kuvaa viatu maalumu kwa ajili ya kuweza kutembea salama kwenye theluji au barafu ili usianguke na wala miguu isigande.

Wakati huo huo umevaa makoti mazito kwani baridi hili si mchezo, kama haukupata mlo wa kutosha lazima tumbo lilalamike. Katika mtaa huu kila unayekutana naye anahema huku akitoa ‘moshi’ mdomomi, si kwamba wanavuta sigara, la hasha! Ndilo baridi lilivyo mwili unakuwa umepigwa baridi kiasi cha kufanya mvuke utoke kinywani.

Najikongoja taratibu, nabonyeza kitufe chekundu ili taa za barabarani zisimamishe magari nami nivuke na kwenda zangu shuleni. Nakatiza uwanja, bila shaka nimefika shuleni. Wanafunzi wachache wapo nje wanavuta sigara, huku ni kawaida sana kutokana na hali ya hewa.

Nalazimika kusafisha viatu vyangu kwanza kabla ya kuingia ndani maana barafu limeganda kwenye viatu vyangu mithili ya matope ya soko la Tandale. Ndani ya jengo la shule, kabla ya kuingia darasani, napita sehemu yenye komputa nyingi mahususi kwa ajili ya wanafunzi, ghafla nasikia mtu anaita, “Eric! Eric! Eric!”

Nageuka, naona mtu wa makamo akiwa amesimama karibu na kompyuta akiwa na begi kubwa kama msafiri, nami namsogelea nisikilize anasemaje. Wakati anaita ‘Eric’, alikuwa ananiita mimi, na nilimwitikia kwasababu Eric ni rafiki yangu wa karibu na ni mwanafunzi mwenzangu toka Ghana. Nilijua bila shaka mzee huyu amenifananisha na rafiki yangu. Nikamsogelea, tukasalimia na mara hii anaonesha heshima sana kwangu japo haikuwa desturi yake. Kumbe ana shida, jana yake alilala nje kwa sababu shirila la nyumba limemfukuza. Na baridi hii, nilimwonea huruma sana.

Cha msingi nataka kusikiliza anasemaje. Ananiuliza kama naweza kumsitiri au namjua mtu yeyote mwenye chumba cha ziada, maana mtu aliyekuwa anaishi naye na ambaye alikuwa mpangaji halali amefariki, na hivyo kisheria hapa Uswidi lazima aondoke maana kimkataba hatambuliwi. Jawabu ninalompa ni kwamba sina sehemu ya kumsitiri kwa muda huu maana na mimi naishi na mtu na sina taarifa juu ya mtu mwenye chumba cha ziada.

Kumsaidi tu, nampa majina ya makampuni mbalimbali yanayohusiana na shughuli za kupangisha vyumba. Kisha namtakia kila la kheri, naondoka zangu nikimuacha na masikitiko kwa kuwa labda alidhani tatizo limeisha. Ukweli maisha hapa ni magumu hasa ukiwa huna mahala pa kuishi na kazi.

Kipindi hiki cha baridi kali kimekuwa hatari Ulaya. Ulaya Mashariki zaidi ya watu mia nne wamepoteza maisha, wengi wao wakiwa wazee na wale wasio na makazi (maalumu). Baridi hili kama hauna kipoozeo (heater) basi ujue utakufa maana ikiambatana na theluji au barafu mara nyingi hupelekea damu kuganda, na hivyo hupelekea maumivu katika sehemu mbalimbali nyingi za mwili hasa kwenye vidole na kwenye paji la uso.

Mzee huyu kwa jinsi ninavyomuona atakuwa amepata taabu kweli usiku uliopita. Mzee huyu si mzungu. Ni mtu mweusi kama mimi, yeye anatoka Kameruni, nchi yenye mchezaji soka maarufu wa kimataifa Samuel Eto’o, aliyewahi kufika Tanzania na wasakata kambumbu wenzake.

Huku Uswidi kila katika mji utakaoenda hautakosa Mkameruni, ni wengi sana mithili ya Wachagga ambao wametapakaa kila mkoa Tanzania wakifanya biashara. Ila Wakameruni hawa hawafanyi biashara, wengi wao wapo huku kwa sababu za ‘kimaisha’. Kameruni maisha ni magumu sana na hivyo wengi wanazamia huku na nchi nyingine za Ulaya. Uzuri wa Wakameruni ni uwezo wao katika lugha, wanaweza kuzungumza lugha ya Kiingereza na Kifaransa kwa ufasaha sana. Pia ni wa watu wanaojituma sana katika kazi.

Si kwa mazuri hayo tu, bali nao wana mabaya wao. Kwa mtazamo wangu, wachache niliokutana nao ni watu ambao wana ubaguzi, wabinafsi, lakini cha kushangaza sana ni kuwa wanadharau watu kutoka Afrika ya Mashariki. Wanaona uchache wetu hapa Uswidi na sehemu nyingine za Ulaya na wanadhani sisi si watu wa kujituma, ni waoga, na hatujui lugha.

Tuendelee na mzee wetu; basi mzee huyu ni mmoja kati wa ya watu wanaodharau sana vijana, hasa wa kiume. Mara nyingi huongea vizuri na vijana wa kike hasa wanaotoka bara la Afrika. Huwadharau hata Wakameruni wenzake, bila shaka ndio sababu ya kutopata msaada kutoka kwao kwa maana wanafahamu hulka yake.

Kwa sababu ni wa makamo, alidhani yeye ni bora kuliko vijana wadogo. Hiyo si sababu kwa maana inawezekana kijana mdogo akawa na hekima kuliko mtu mzima. Nikakumbuka msemo wa Kiswahili, “Mtu mzima hovyo.” Si watu wote wazima wana hekima, wengine ni hovyo kweli kweli! Cha msingi na muhimu ni heshima; mdogo aheshimu mkubwa na mkubwa afanye vivyo hivyo kwa wadogo, hapo maisha yakutakuwa na amani. Vinginevyo vijana watacharuka. Hawana simile vijana wa siku hizi.

Heshima ni alama ya upendo pia, kama hauna heshima kwa mtu mwingine inamaanisha upendo kwa mtu yule umepotea. Ni muhimu kujenga heshima kama kweli tunapenda upendo uwe kati yetu. Jamii ya Tanzania kwa sasa inatazamwa kama jamii yenye maadili yaliyoporomoka kupita kiasi. Vijana wadogo wanatukana wazazi wao, wanabaka walimu, wengine wamepotelea katika matumizi ya madawa ya kulevya, vitendo vya uwizi na ujambazi na wengine kwenye biashara ya ngono.

Heshima ni jambo la muhimu sana, na haijalishi wewe ni nani na umri gani. Kwa sisi Waafrika, utamaduni wetu unatufunza kuwa watu wenye heshima mara zote kwa watu wazima na wadogo. Tunahitaji kuwasaidia walimu kuanzia shule za awali, msingi, sekondari mpaka vyuo kuimarisha na kusisitiza heshima, upendo na kujitoa kwa ajili ya manufaa ya jamii. Hivi vyote vikipotea basi hata uzalendo hautakuwepo kamwe!

Tusibaki kuwa watu wa kulalamikia rushwa, uongozi uliodorora na maendeleo duni. Hivyo vyote huanzia nyumbani kwa wazazi na watoto. Lazima kaya zetu zijengwe na upendo, uzalendo na heshima ili taifa liwe na watu wa aina hiyo. Bila shaka wale walio viongozi bora leo hii hapa Tanzania na sehemu nyingine duniani wana historia nzuri toka huko walikotoka wangali watoto, na hatimaye baba au mama wa familia. Tubadilike na heshima tusisitize kwa rika zote!

Kajuna ni mwanafunzi wa uzamili nchini Uswidi katika fani ya Sosholojia. Barua pepe: kajunat08 (at) yahoo (dot) com

Previous ArticleNext Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend