Laana ya Binadamu, Sio Mungu: Mapigano Ya Ardhi zenye Gesi Tanzania

Makala ya Kiingereza imeandikwa na Zachariah Mampilly na kutafsiriwa na Kathleen Bomani na Bahati

Gesi haitoki! Gesi haitoki!” Wasichana kumi waliovaa sare za bluu za shule, walipiga kelele kwa shauku wakati Toyota FunCargo ya kukodi ilipowapita kwenye barabara ya vumbi nikielekea mpakani na Msumbiji. Nipo kusini mwa Tanzania karibu na kijiji kinachoitwa Msimbati. Kipo mbele kidogo ya moja kati ya baadhi ya miradi mingi ya uchimbaji mafuta na gesi inayofanywa na moja kati ya makampuni ya kimataifa. Hatima ya gesi ni kusafirishwa mpaka Dar es Salaam, makao makuu ya uchumi wa nchi, kilomita 500 magharibi. Mabomba ya kusafirishia gesi hiyo yanatarijiwa kujengwa na kampuni ya Kichina kwa mkopo kutoka kwa Serikali ya China.

Tangazo kuhusu mabomba ya gesi ulipokelewa kwa upinzani, watu elfu kumi na tano wakiandamana katika mitaa ya mji mkuu, Mtwara (jina ambalo ni la mji huo na mkoa pia). Kufuatia kutokea upinzani zaidi ya mmoja mwanzoni mwa mwaka, serikali ilipeleka jeshi kudhibiti waandamanaji. Vijiji na miji katika mkoa vilijaa wanajeshi; maduka na biashara nyingine vilichomwa moto,; wakazi kuteswa na kuuwawa; na shutuma za unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa polisi ulikuwa mkubwa.

Nilifika Mtwara kutoka Dar es Salaam (ambako ndiko ninapoishi) kama wiki moja baada ya udhibiti wa serikali, na chini ya wiki mbili kabla ujio wa raisi wa Marekani, Mh. Barack Obama. Dar ipo katika kampeni ya usafi. Barabara karibu na ubalozi wa Marekani zinapigwa deki, kuta zinapigwa rangi, bustani zikishughulikiwa, yote zikiidhirisha kuwasili kwa Tanzania katika jukwaa la kimataifa. Hata ujio wa raisi wa China Xi Jinping mwezi wa tatu haukuvuta shauku hiyo, pamoja na China inafanya biashara na Tanzania mara kumi zaidi ya Marekani.

no-gas

project-descript_1

Kusini mwa Tanzania hutembelewa na watalii mara chache. Mbali na vivutio kama Serengeti na Kilimanjaro vilivyo kaskazini pamoja na uzuri wa miji ya kihistoria iliyopo pwani kama Dar es Salaam, Bagamoyo au Stone Town, Mtwara imeendelea kutengwa, bila kuendelezwa, kulinganisha na sehemu nyingine za nchi. Pamoja na mandhari yakuvutia, hakuna cha kupendekeza kuwa Mtwara imenufaika  na ukuaji wa uchumi wa nchi katika mwongo uliopita. Sasa na ugunduzi wa nishati ya gesi katika nchi yenye upungufu wa nishati, hatimaye wananchi wa Mtwara wanategemea kufaidika na uchumi wa nchi.

Maandamano, ambayo yalianza mwezi wa kwanza kwa idhini na kuungwa mkono kimya kimya na viongozi wa serikali za kijiji, sasa umekuwa wa hatari. Kilichokuwa chanzo cha matumaini, sasa hali imeguka na kuwa tete, na wa kutilia shaka watu kutoka nje, mimi nikiwa mmoja wapo.

*          *          *

Mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watu elfu kumi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa, walikusanyika “Mashujaa Park” kuonyesha kutoridhishwa kwao na ujenzi wa mabomba ya gesi na kupanga nini cha kufanya. Uwanja wa Mashujaa ulijengwa kuadhimisha msaada wa Tanzania kwa Usumbiji katika kupigania uhuru. Pamoja mkusanyiko kwa sehemu kubwa ulikuwa wa amani, baadhi ya waandamanaji waliharibu ofisi za Serikali, na kupelekea udhibiti wa polisi. Angalau waandamanaji wanne waliuwawa. Hiyo haikivunja nguvu ya waandamanaji, upinzani ulibaki kuwa wa kichini chini. Utulivu ulirejea, labda kutokana na imani ya waandamanaji kuwa maandamano yao yatakuwa yameshawishi Serikali kubadili mipango yake.

statue

Tarehe 22 mwezi wa tano, waziri wa nishati na madini aliwasilisha bajeti yake bungeni. Bajeti hiyo ilidhibitisha ujenzi wa kilomita 500 za mabomba ya gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Gesi itasindikwa katika kiwanda kipya kinachojengwa Dar, hivyo kuleta gharama ya mpango nzima kufikia Bilioni 1.2 za Kimarekani.

Wananchi wa Mtwara walikuwa wakisubiri kwa hamu kusomwa kwa bajeti. Ujumbe mifupi ya simu ilisambaa siku kabla, ikitangaza mgomo mkubwa kama ujenzi wa mabomba ukiidhinishwa. Mabango yasiyo na majina yalionya wananchi kutoenda popote. Dakika chache kabla waziri hajasoma bajeti yake, mawasiliano ya radio na luninga yalikatika. Lakini jaribio la Serikali kuzuia habari kuhusu ujenzi wa mabomba ulikwama. Wananchi wenye madishi hawakuadhiriwa, haraka habari zikasambaa kupitia ujumbe mfupi wa simu. Ghasia zikalipuka. Zaidi ya watu tisini waliwekwa ndani, Mtwara mjini peke yake. Mabomu ya machozi yalitumika kuvunja maandamano na jeshi lilipelekwa kwenda kurudisha hali ya utulivu. Katika hotuba kali ya raisi bungeni, Kikwete aliwashutumu waandamanaji. “Maliasili ni mali ya Watanzania wote, bila kujali sehemu zilipopatikana” alifafanua.

Lakini kwa wananchi wa Mtwara, ujenzi wa mabomba ya gesi, uliamsha maswali makubwa zaidi yaliokuwa bado kupatiwa ufumbuzi. Nani wa kufaidika na rasiliamali zilizopatikana katika mkoa ulionyuma kimaendeleo? Kuna uwezekano kiasi gani kwa watu waliotengwa kudhibiti upepo wa utandawazi mara mkoa wao uliotelekezwa unapogundulika kuwa na ardhi iliyo na utajiri wa rasilimali? Ukuaji wa uchumi wa nchi una thamani kiasi gani kwa mkoa ulioachwa nyuma na mafanikio ya nchi? Lakini kali zaidi, ni nini wajibu wa raia, Serikali inapokushutumu kuhatarisha maendeleo ya nchi?

*          *          *

Ili kuweza kuelewa upinzani wa ujenzi wa mabomba, inahitaji kuelewa historia ya Tanzania. Kipindi cha 1960 kilikuwa kipindi cha shauku na tabu kwa mkoa wa Mtwara. Wimbi la upiganiaji uhuru lilikuwa likivuma barani kote Afrika. Mwaka 1957, Ghana ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kupata uhuru. Tanzania (kipinchi hicho Tanganyika) ilipata uhuru mwaka 1961, ikifuatiwa na Kenya mwaka 1963.

Lakini huko Kusini, Ureno iliweka wazi kuhusu azma yake ya kutokufuata mifano ya Uingereza na Ufaransa, hivyo kuendelea kuzitawala koloni zake, Angola na Msumbiji. Baadhi ya nchi nyingine huko kusini zilijikuta zikitawaliwa na wazungu wachache. Mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji, ukawa sehemu ya kutenganisha Africa inayobadilika na ile iliyobaki vile vile. Tanzania ilikuwa ikiongozwa na mwana Pan –Africanist Julius Nyerere, ambaye aliongoza msukumo wa mwisho wa kulikomboa bara la Afrika.

Uongozi wa Kireno, uliokuwa wa kibabe na bila huruma, ulipinga wito wa koloni zake kupewa uhuru, wakidai kuwa koloni zake ni sehemu muhimu ya nchi mama (Ureno). Msumbiji ikibaki kuwa miliki yao ya thamani. Moja kati ya maeneo yaliyochukuliwa na koloni za Ulaya, Msumbiji ilichukuliwa na Wareno mwaka 1505. Msumbiji ilikuwa kusini mwa pwani iliyokuwa ikimilikiwa na Waarabu, hivyo kufanya Msumbiji kuwa sehemu muhimu kwa Ureno katika harakati zake za kutaka kumiliki biashara iliyo bahari ya Hindi. Hivyo, kuwasukuma Waarabu, Wairani na wafanyabiashara wa Kiswahili nje ya biashara hiyo. Ureno ilienda kumiliki biashara hiyo kwa karne nne zijazo.

Mwezi wa sita, mwaka 1962, wana harakati wa uhuru kutoka Msumbiji walikutana Dar es Salaam kuunda (FRELIMO). Eduardo Mondlane, mhadhiri wa Anthropology kutoka chuo cha Syracuse, aliacha nyadhifa yake ya heshima baada ya miaka kumi na mbili na kurudi Dar mwaka 1963 kuongoza mapambano. Mondlane, aliyekuwa mtanashati na mcheshi, anabaki kuwa moja kati ya viongozi wasio sheherekewa pamoja waliwahi kupigania uhuru pia. Haraka baada ya mondlane kufahamu ukubwa wa msimamo wa Ureno, Mondlane aliamua vita ya msituni ndio njia pekee ya kushinda jeshi la kikoloni lenye nguvu zaidi yao. Nyerere aliahidi Tanzania itakuwa makao makuu ya harakati hizo. Ofisi za viongozi wa FRELIMO zilijengwa na mafunzo yalitolewa kwa wapiganaji wake. Kambi kuu ya mafunzo ilikuwa Kongwa, kusini mwa Tanzania. Wanafunzi kutoka Msumbiji na wengine kutoka mkoani, walienda kuongeza juhudi za vita, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikija kuwa sehemu kuu ya kupanga mipango. FRELIMO ilipata misaada kutoka kwa baadhi ya nchi za Scandinavian, Urusi, China, na nyingine za Afrika.

Lakini pamoja na shauku ya mwanzo na misaada ya kimataifa, vita haikuisha haraka. Uongozi wa Kireno ulidhibiti mashambulizi ya mwanzo ya wapigania uhuru wa Msumbiji, wakituma maelfu ya wanajeshi kuimarisha juhudi vitani. Baada ya muda, FRELIMO ilichukua sehemu kubwa ya vijijini kusini mwa Msumbiji. Lakini serikali ya kikoloni iliendelea kushikilia kwa  nguvu miji mikubwa. Vita iliendelea kwa muongo bila pande yeyote kumzidi nguvu mwenzie.

Vita ilizidi kuwa mbaya, kutokana  na mauaji ya halaiki na viongozi. Wareno wakishirikiana na vikosi maalumu vya Rhodesia (Zimbabwe), ambavyo vilipewa nafasi ya kuendesha shughuli zao wenyewe ndani ya Msumbiji. Jeshi la Wareno lilikubaliana na mpango wa kupanua mapambano hadi kuvuka mstari wa mbele wa waasi. Mapambano ya Jeshi la Wareno hayakuishia Msumbiji peke yake, bali walitaka kuingia hadi Tanzania kwa kuvuka mto Ruvuma uliopo mpakani.  Ushindi mkubwa ulikuwa mauaji ya Mondlane mwaka 1969 kwa kutumia mlipuko uliowekwa ndani ya mfuko ambao ulitumwa katika ofisi za FRELIMO Dar.

Lakini mikakati ya Wareno ilikuwa zaidi ya kuwalenga viongozi wa mapambano. Kama Tanzania wangetaka kuonyesha mshikamano kwa kuwasaidia ndugu zao wa Msumbiji, basi Tanzania nayo ingelipa kwa kumwaga damu. Wanajeshi wa Kireno walivamia na kuchoma vijiji kusini mwa Tanzania na kumlazimisha Nyerere kutuma majeshi yake kwenda kulinda mpaka.

Mwishoni mwa miaka ya 1960, vita ya uhuru wa Msumbiji ilikuja kuwa vita ngumu kati ya Tanzania na Ureno, ikifikia kilele mwaka 1970 na operesheni ya Gordon Knot, kampeni ya miezi saba ambayo Ureno ilituma wanajeshi 35,000 kaskani mwa Msumbiji kuziba njia zote za FRELIMO kutoka kusini mwa Tanzania.

Mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru wake kupitia kupinduliwa kwa utawala wa kimabavu huko Ureno. Nyerere alishangiliwa kidogo kutokana na mshikamano wake. Lakini uharibifu uliotokana na uvamizi wa majeshi ya Kireno ulikuwa mkubwa sana kwa wananchi wa Mtwara. Ukiacha idadi ya watu waliopoteza maisha, miundombinu kidogo iliyokuwepo iliharibiwa kabisa. Miaka arobaini baadae, mkoa wa Mtwara bado unaonyesha athari hizo.

Katika mtaa wa Toure Dar es Salaam, ambao haupo mbali sana na Ubalozi wa Mrekani, jengo la kioo na zege lililojengwa kwa kasi linatokezea. Linatazama upande wa Bahari ya Hindi, likiwa na neno HALLIBURTON nje.

Nikiwa njiani kuelekea Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, nilipita makao makuu ya Halliburton Tanzania. Mafuta na Gesi yaligunduliwa kusini mwa Tanzania kama muongo mmoja uliopita. Lakini maendeleo yanayotokana na nishati hiyo ndio kwanza yameanza kwenda kwa kasi hivi karibuni. Angalau makampuni kutoka nchi kumi tofauti yameshachukua sehemu yake. Naelekea kupanda ndege ya Precision Airways asubuhi kuelekea Mtwara. Ndege imejaa wafanyakazi kutoka Ulaya, Kaskazini na Kusini ya Amerika, na Asia. Ni ngumu kuamini wanaelekea katika mji wa pwani uliosahaulika, wenye barabara chache zenye lami na huduma ambazo kawaida huvutia watalii kuja upande huu wa Afrika.

Wafanyakazi na wananchi wa hoteli niliyofikia wana hasira na wasiwasi. Ni wiki tu imepita tangia jeshi lilipokua vijijini kwao, bila wao kutarajia, hivyo kuwashtua. Jeshi lilitumwa baada ya jeshi la polisi kuanza kuchoma biashara, pamoja na zahanati. Angalau ni watu watatu tu walipoteza maisha. Wafanya ghasia nao waliharibu ofisi ya kijiji. Ni kipindi gani hiki kitendo kilitokea, bado ni mjadala. Lakini hata kama ilitokea kabla au baada ya ujio wa polisi haina umuhimu ukizingatia ukubwa wa uharibifu uliofanyika. Uumizwaji wa watu na uharibifu wa mali zao unaonekana kila mahali na wanakijiji wapo tayari kuhakikisha hasira zao zinajulikana. Watu wengi wananiambia kuwa wamerudisha kadi zao za uwanachama wa CCM kwa hasira. Wengine wanazungumzia kupanua (maandamano) na kuwa mapambano makubwa zaidi.

Nakutana na mkulima mwenye miaka sabini na tano anayenisalimia kwa “A salaam alaikum”. Ndevu zake ni nyekundu kutokana na hina na macho yanayong’ara juani. “Watu wamepoteza imani na serikali” ananiambia. Vijana waliovaa jezi za mpira wanakusanyika kusikiliza mazungumzo yetu. Nilipouliza ni nani aliyepanga maandamano, haraka anakataa madai ya kuwa ilikuwa ni vyama vya upinzani au ni watu kutoka nje ndio wa kupewa sifa. Wananchi ndio waliofanya, anasema, huku akiungwa mkono na vijana wanaotingisha vichwa vyao. “Kama Serikali itaridhia gesi kusafirishwa, watu wapo tayari kwenda vitani”. Vijana wanatingisha vichwa zaidi huku nikienda zangu, nikiwa na wasiwasi na kilichoanzishwa na maswali yangu.

*          *          *

Mwaka 1967, Nyerere alitangaza Azimio la Arusha lililoashiria mwanzo wa Tanzania kuelekea kwenye sera ya ujamaa, sera iliyokuwa ya kipekee Afrika. Ilani ya kipekee ya ujamaa wa Tanzania ilikuwa ni mpango mkubwa wa vijiji vya kijamaa. Nyerere alitaka kuwahamishia watu wa vijijini (zaidi ya asilimia 80) katika vijiji vilivyopangwa na serikali (vilivyojulikana kama vijiji vya ujamaa) ambavyo vingewezesha huduma kuwafikia wananchi kirahisi hivyo kuboresha maisha ya vijijini. Lakini mara baada ya utekelezaji kuanza, mpango ulianza kupata changamoto. Ubunifu wa vijiji vingi ulikuwa hafifu na ahadi ya kuboresha uletwaji wa hudumu haukufanikiwa. Wakati mwingine vijiji vilikuwa vimewekwa mbali na vyanzo vya maji na shule na hospitali zilikuwa hazijajengwa kwa ubora huku zikihangaika kutoa huduma. Hapo hapo, serikali haikujiandaa vilivyo kuandaa wananchi kwa mabadiliko ambayo ilipanga kuleta. Matokeo yake, wanavijiji wengi walikuwa hawana hamu ya kuhama, huku wakipuuzia mara kwa mara amri zilizotolewa kwa hasira na watendaji ambao walikuwa hawajui wanalolifanya.

Badala ya kurudi nyuma, Serikali ilianza kutumia nguvu kulazimisha wakulima kuhamia kwenye vijiji hivyo. Ulazimishaji haukuwa muhimu sana sehemu ya kusini, sehemu ambayo vita na Wareno ilirahisisha uhamishwaji wa wananchi kwenye mpaka na kuwapeleka kuishi katika vijiji vya kijamaa vilivyokuwa vimedhibitiwa na salama. Kulinganisha na sehemu nyingine za nchi, wananchi wa sehemu ya kusini walikuwa hawana kipingamizi na kuhamishwa, ikiwa na mfano wa kujitolea kwa hiari yao kufanyiwa majaribio kwajili ya maendeleo ya nchi.  Kipindi cha 1970, kampeni ya ujamaa ilikuwa imetekelezwa zaidi sehemu ya kusini kuliko sehemu nyingine za nchi. Asilimia 38 ya vijiji vya ujamaa na asimilia 46 ya wanavijiji waliohamishiwa kwenye vijiji hivyo walikuwa huko sehemu ya kusini, pamoja wao walikuwa chini ya asilimia tano ya wananchi wote. Hata leo hakuna hasira dhidi ya mpango huo pamoja na kushindwa kwa Nyerere na jaribio lake la ujamaa.

Mwisho wa miaka ya 1970, mpango wa ujamaa ulitelekezwa na nchi kuingia katika kipindi kirefu cha ugumu ya kiuchumi. Vijiji vya ujamaa vilikimbiwa na kuachwa katika hali mbaya isiyoweza kurekebishika. Lakini wakati nchi ikikabiliwa na janga la kiuchumi lililosababishwa na utaifishwaji wa viwanda, kulikuwa na nia kidogo sana ya kubuni mpango utakaofaa kuchukua nafasi ya ujamaa. Badala yake Mtwara iliachwa kuzorota.

*          *          *

Sehemu ya kwanza niliyosimama Mtwara, mji mkuu uliolala wenye vumbi, ilikuwa ni kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa. Kananali Simbakali, veterani wa muda mrefu katika jeshi la Tanzania, aliniangalia kwa jicho la uchovu nilipoingia ofisini kwake. Bila kutaka kuanzisha kasheshe yeyote katika safari yangu, nilikuwa nimekuja kupata baraka zake kuweza kutembelea vijiji vilivyokumbwa na ghasia.

seaside

Mara moja Simbakalia alisema, watu wa nje ndio wanaochochea vurugu mkoani hapo. Akipendekeza kuwa maandamano hayakuwa yakisukumwa na wakazi wa hapo. Badala yake, ni kazi ya watu wa nje wanaotaka kulinda maslahi yao ya kisiasa au kiuchumi. Msumbiji, ananiambi, ina gesi mara kumi ya Tanzania lakini Tanzania bado inabaki kuwa chaguo la wawekezaji kutoka nje. Makampuni binafsi ya nishati ambayo yametajirika kutokana na utegemezi wa Tanzania na nishati ya kuagiza kutoka nje, hawana nia ya kuona mabomba ya gesi yakiendelezwa. Ni rahisi kuiona mantiki hiyo. Hakuna harakati, ananiambia.

Ananiashiria kuelekea mlangoni. Nakusanya vitu vyangu tayari kwa kuondoka, lakini kwanza ananiuliza kwanini nimekuja na ni nini nataka mkoani hapo? Ninamweleza ukweli. Mimi ni mhadhiri ninayeishi Tanzania kwa ufadhili wa Fulbright, niliyesikia matatizo yaliyotokea na nikataka kujionea mwenyewe ni nini kinachoendelea. Anatulia kidogo. Ananiambia nchi yeyote inayogundua rasiliamali kama nishati hupitia matatizo. Urusi, Venezuela, Saudi Arabi, hata Canada. Ni laana ya mafuta, anasema. Hajakosea. Lakini mafuta ni laana ya binadamu, sio Mungu. Na Serikali yeyote yenye busara, huweza kufanya mengi kupunguza athari hizo.

Ninamwomba anipe ruhusa kwa maandishi, ili niweze kutembelea vijiji hivyo na kuwaepushia kunyanyaswa watu watakaonekana wakiongea na mimi. Aliridhia safari yangu kwa maneno. “Hii ni nchi huru na wewe unakaribishwa kuongea na yeyote unayetaka”, alisema nilipokua nikiamka tayari kwa kuondoka, “lakini sipendekezi hivyo”.

*          *          *

Naamua kuelekea Msimbati, kijiji kilicho katikati ya vurugu hizo za mabomba hayo ya gesi. Ni safari ya masaa mawaili kuelekea upande wa kusini kutoka mji mkuu wa mkoa, ingawa ni kilomita ishirini na saba tu, huku kunguru wakiwa wanapaa angani. Nje ya Msimbati kuna hifadhi ya bahari (marine reserve) na mbele yake kuna barabara mpya ya mchanga inayoelekea kwenye “installation” kubwa ya gesi. Gesi ya Mnazi Bay iligunduliwa na kampuni ya Italia, Agip mwaka 1982, lakini ni mwaka 2004  ndipo serikali ilisaini mkataba na shirika la Kikanada, Artumas kuendeleza sehemu hiyo ilipopatikana gesi. Inakadiriwa kuwa na trilioni tatu hadi nne za “cubic feet” za gesi, inayotosha kuendesha kiwanda huko Dar es Salaam na pia kuzalisha “methanol” na mbolea ya kusafirisha huko Asia.

mtwara2

broken-house2

Kwa waangalizi wengi kutoka nje, maamuzi ya Serikali ni sahihi. Kabla ya kuondoka Dar es Salaam, nilizungumza na mwajiliwa wa Benki ya Dunia aliyeniuliza ni nini watu wa Mtwara wanachoandamania. Kwake yeye, ilikuwa ni dhahiri kutoa gesi kutoka kijijini na kuipeleka sehemu ya viwanda kuwa ni manufa kwa wote. Ufafanuzi pekee wa maamuzi ya waandamaji itakuwa lazima ni hisia na sio mantiki.

Hii ilikuwa ni fikra iliyojitokeza mara kwa mara kutoka kwa watu wengi niliyokutana nao katika nchi hii ya Afrika Mashariki iliyo sasa na nguvu kiuchumi. Mara nyingi kwa nia nzuri, walisisitiza kuwa mara wananchi wa Mtwara watakapoelewa mantiki ya kiuchumi, hawataona haja tena ya kuendelea kupinga ujenzi huo wa mabomba. Hata hivyo, watu wa kusini ni wajinga na wapo nyuma wasiojua nini ni bora, wengi waliongezea.

Mtazamo huu umechangiwa na chombo cha habari cha taifa, ambacho wengi wanakiona kama ni adui wa harakati zao. Waandishi wa habari wamevamiwa kwa kudhaniwa kuunga mkono Serikali, dhana yenye tatizo lakini yenye mantiki ukizingatia Serikali ndiyo inayoendesha chombo hicho cha habari. Habari nyini huongeza chumvi. Kabla ya kufika kwangu, nilisoma kuwa, jeshi lilipelekwa Msimbati baada ya waandamaji kuharibu jengo lililopo kwenye hifadhi ya bahari (marine reserve). Nilitembelea jengo hilo lililopo pembezoni mwa kijiji. Ni kweli kulikuwa na dirisha lililovunjwa pamoja na lango. Lakini nasumbuka kuelewa ni vipi uharibufu mdogo kama huo unaweza kusukuma Serikali kupeleka jeshi katika kijiji na kukaa hapo kwa siku tatu.

Wanakijiji wananihadithia jinsi walivyokimbia na kuishi vichakani wakisubiri usalama urejee waweze kurudi majumbani mwao. Kumbukumbu zao bado ni nzuri. Wananisimulia ahadi za uwongo za ajira, umeme, na maendeleo, ahadi zote zilizotolewa na viongozi wa juu kama wakitoa ushirikiano. Wana hasira, lakini zaidi ya hapo wamekata tamaa. Wamevunjwa moyo na Serikali ambayo mara kwa mara imewaambia wajitolee kwajili ya maendeleo ya nchi, na bara la Afrika. Wamevunjika moyo kusikia viongozi wao wenyewe wakiwaita wabinafsi, wasio na uzalendo na zaidi, wapinzani wa maendeleo. Maendeleo ndio wanayoyataka kupita kitu chochote, wananiambia. Ajira kwajili ya watoto wao, na umeme wa kuaminika kwajili ya nyumba zao. Hivi ndivyo maendeleo yalivyo punguzwa katika sehemu ambayo watu wanakidogo sana. Wananiuliza ni nini ninatarajia kufanya na kama Raisi Obama ataimarisha hali wakati wa ujio wake?

Nikiwa naondoka kijijini hapo, FunCargo iliharibika njiani kwenye barabara ya mchanga iliyojengwa na kampuni ya gesi. Magari ni machache, lakini hatimaye gari jeupe aina ya Toyota pickup lenye nembo ya “M&P” lilitokea. M&P ni kampuni ya mafuta ya Kifaransa inayoitwa Maurel & Prom. Dereva wake, aliyekuwa ni mkazi wa mkoa huo, alikuja na kutaka kutusaidia. Alikuwa na uhakika kuwa ni battery ya gari iliyokuwa ikihitaji kushtuliwa, lakini sisi sote tulikuwa hatuna vifaa vya kushtulia. Aliahidi kuturudia. Sikuwa na imani, lakini mwenyeji wangu ambaye na yeye alikuwa mtu wa hapo, alinihakikishia kuwa angerudi. Tulisubiri masaa mawili bila gari lolote kupita. Lakini alirudi na haraka tulikuwa njiani tena.

car-fixing_0

Tulisimama katika kijiji jirani na kuongea na Imam wa hapo aliyekuwa akijipumzisha kibarazani kwake. Jua lilikuwa limeanza kutua na watoto walikuwa wakifurahia likizo kwenye joto la vumbi. Wanaangalia mara kwa mara, kwa udadisi wakitaka kujua ni nini kimemvuta mgeni mwingine sehemu hiyo. Namuuliza kuhusu tetesi zinazodai kuwa maandamano yalipangwa na wapinzani wa Kiislamu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015. Dini inapenya katika nyanja zote za jamii katika nchi hii. Waislamu kwa muda mrefu wamekuwa hawana uwakilishi wa kutosha Serikalini na kwenye uchumi, pamoja na Raisi kuwa ni mtu wa dini yao. Chama tawala, CCM ambacho kimetawala Tanzania tangia uhuru, kimekuwa kikijisifia kwa kushirikisha makabila na dini zote katika uongozi. Chini ya Nyerere, Tanzania ilikuwa na sera kali iliyopinga mashirika ya kisiasa yaliyoanzishwa katika misingi ya ukabila au udini. Ilikuwa ni sera nzuri ya kisiasa na ambayo ilijenga uzalendo mkubwa ukilinganisha na nchi nyingine za jirani. Lakini kilichokuwa muhimu, kuzuia mifarakano ya ukabila au udini, sasa hivi inaonekana kama ni mbinu ya kudhoofisha harakati za Waislamu. Hata sensa hairekodi uhusiano wa dini za watu, hivyo kufanya iwe ngumu kujua jamii imesahaulika kiasi gani.

Nje ya Zanzibar, kusini mwa Tanzania ndiokwenye Waislamu wengi nchini. Kuna udokezaji wa mara kwa mara kuwa, kutoka hapa na Dar es Salaam kuwa kusahaulika kwa Mtwara kumetokana na Uislamu. CUF, chama cha siasa chenye idadi kubwa ya Waislamu, kimekuwa kikitumia hoja hii kuishambulia CCM. Imam hapingi uhusikaji wake (CUF). Lakini anapinga dhana ya kuwa waandamaji wanatumiwa tu na wanasiasa wenye uchu wa madaraka. Anatoa mfano wa Kenya na Zambia, nchi mbili za jirani ambazo hatimaye ziliongozwa na vyama vya upinzani, kujenga hoja yake. “Je mabadiliko ya chama tawala yaliboresha maisha ya wale waliosahaulika katika nchi hizo?, ” anauliza. Anatabasamu huku macho yangu yakiangalia watoto wanaondoka, baada ya koboreka na mazungumzo yetu.

*          *          *

Pamoja na athari za vita ya Msumbiji na kulazimishwa kuhamia kwenye vijiji vya ujamaa, watu wa Mtwara hawajawahi kutelekeza wazo la umoja kama nchi ya Tanzania. Chini ya Nyerere, watu wengi walikubali mantiki ya maadili ya kujitolea kwajili ya nchi ingawa wao ndio walioathirika. Uzalendo wao bado unabaki kuwa mkubwa ukilinganisha na ule wa watu wanaoishi Dar es Salaam. Lakini mjadala kuhusu mabomba ya gesi unahatarisha mfumo wa nchi.

Tanzania imesifiwa kimataifa kutokana na uongozi wake bora. Tanzania hivi karibuni imeingia kwenye nchi kumi bora za Afrika zenye uongozi bora, kwa mujibu wa Mo Ibram, Tanzania ikiwa nchi ya kwanza kutoka ukanda wa Mashariki na Kati kupata sifa hiyo. Licha ya sifa zote, nchi imejikuta ikiwa na mfarakano katika kipindi hiki kuliko kipindi chochote katika historia tangia uhuru. Mtazamo wan chi za nje juu ya Tanzania na mtazamo wa wananchi wenywe juu ya Tanzania haujawahi kuwa tofauti kiasi hiki. Rasimu ya katiba mpya inayoandaliwa inahatarisha muungano uliotete na Zanzibar. Mapigano kati ya wakulima na wafugaji waliohamishwa yameanza kuwa ni vita. Na uchaguzi mkuu upo njiani ambao utamaliza kipindi cha uongozi wa Raisi Jakaya Kikwete, na tayari kumeanza kuwa na vurugu zinazotokana na vuguvugu la uchaguzi mkuu.

Lakini nchi bado inabaki kuwa mfano wa mabadiliko yanayoendelea kutokea barani Afrika. Wakati nchi za Asia zikiendelea kwa nguvu kuingia Afrika na imani yao juu ya nafasi ya Afrika katika utandawazi wa kibepari wa mfumo wa kimataifa. Mataifa ya Magharibi yanatafuta kuimarisha utawala wake. Viongozi wa Afrika, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakitumikia taasisi za kifedha za kimataifa, sasa wanafurahia uhuru wao mpya kwa kushirikiana kwa kuingia mikataba na wawekezaji wanaotokea sehemu zote.

Kwa waandamaji, kuzidi kupanda kwa Tanzania kiuchumi inawapa nafasi ndogo. Ahadi za maendeleo zimekuwa zisizoaminika. Wanaelewa ukuaji wa uchumi, humaanisha ajira, lakini ukuaji wa uchumi unamanufaa gani kama kazi hazitapatikani kwenye kijiji chako, kwenye mji wako. Mtu anageukia wapi wakati kila mtu anataka kipande cha ardhi yako, lakini hana uchungu na amani kwa ajili ya watu wako?

[Original English content and photos courtesy © Zachariah Mampilly]

Previous ArticleNext Article
Bahati was born and raised in Tanzania, and then moved to California to pursue his college education. He graduated in 2008 with a Bachelor’s Degree in Political Science and a minor in Sociology. Bahati expects to be doing his Masters in African Studies in the near future. He is currently working on starting a t-shirt business and a possible publication of some of his writings. One thing that Bahati cannot live without is music, specifically Hip Hop & Bongoflava which he argues are both the voice of the youth today, and is excited to look into how Bongoflava can be a source of further entrepreneurship among the youth in Tanzania. Bahati believes that Bongoflava can help to reduce poverty in Tanzania, as can a more collective effort among key players.

This post has 1 Comment

1
  1. Pingback: Harakati

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend