Ndoa ya Mkeka

Ndoa ya Mkeka

Nimesikia tetesi,
Kitanda kimeingia papasi.
Tuwaulize wazazi,
Tumtafute na Kadhi,
Eti ndoa ya mkeka, muungano au maradhi?
Nasikia kuna juzuu imeandikwa na madalali,
Ati ndoa ya hivi si kitu bali ni doa,
Bila ya hati wala mshenga, watoto wa ndoa hii sio halali,
Wanadai wajomba hawakupatiwa mahari,
Wanamtaka mtoto wao arudi kwao bado mwali,
Miaka 50, wanaitaka Zanzibari!

Kisiwa sharti kizungukwe maji,
Umoja ni nguvu, utengano ni ula mbivu,
Nyumba tatu, familia moja,
Nani atawalisha hawa wazee wa hoja?
Watoto hatuijui tofauti ya serikali na dola.
Hofu yetu sisi ni ndogo,
Ukoo wetu mpya ni upi?
Kama ndoa ya kweli ni hati,
Undugu wetu sisi upo wapi?

Labda kuna la kheri, tukijadili bila ya jazba!
Lakini wawakilishi wetu wamwaga sumu kwenye baraza.
Chuki, Hasira, Dharau, na Majivuno,
Mstakabali wa kizazi chetu, miaka mitano ndio ratiba,
Ubinafsi, uchoyo, na uroho havina tija,
Tukipanda hivi, yapi yatakua mavuno?

Ukoloni kuushinda walitamani,
Nchi moja ya Afrika waliamini,
Karume na Nyerere chambo majini.
Michanga kuichanganya, na kuitosa baharini,
Taifa moja kuzaliwa, mtoto mzuri Tanzania.
Tukaisifu kwa tenzi,
Na kuapa milele kuienzi,
Lakini leo hii pepo imejaa inzi.
Hivi watoto wa ndoa hii, ni wa mama au wa baba?

Mishale ya vita huchongwa wakati wa amani,
Na chuki hujenga kuta bila hata ya tofali.
Jana pekee ndio yetu,
Historia tusisahau.
Leo ni mbegu ya kesho, na kesho ni ya vitukuu.
Je sisi tunapanda nini kwa ajili yao? Mchicha ama mbuyu?
Maamuzi yetu ya leo yasije yakawarudisha juzi,
Miaka kumi mbeleni, utumwa usije rudi.
Tujiulize kwa kina, kama vile sitini na nne,
Bila ubani wala pete, tutazame miaka ya mbele,
Ndoa hii ya mkeka, faida au hasara,
Na tukiamua kuivunja, ujinga au busara?

Neema is a poet from Tanzania, East Africa. Her passion is entrepreneurship and writing – basically FREEDOM. Her recently published book of poetry, See Through The Complicated, can be found on Amazon.com.

0 Comments

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Human verification:

Please type the characters of this captcha image in the input box

*