Ubani wa Malenga

Ubani wa Malenga

Tuufukizie ubani,
mzimu huu wa malenga,
Mashairi tuyaghani,
Tuwaamshe hawa walengwa.

Tumfufue shabani,
Tenzi safi tumuimbie.
Tumfukuze rubani,
Kusadikika tuhamie.

Tumpigie kura domo kaya,
Anayesema bila kufikiri,
Tumuimbie na kwaya,
Nambari wani sasa ni sisi.

Tuwauzie madini, gesi na mafuta pia,
Lakini kabla ya yote, tuwape wachote bure.
Wakoloni ni wadhamini, tuwape ardhi bila udhia,
Tuwaambie wajenge lami, kutoka wami hadi upare.

Wanasiasa ni kama simba,
Na Ikulu pande la nyama;
Waitazama kwa uchu,
Madaraka kweli ni miba.

Wamewanyanyapaa walokonda, wakati vitambi ndo vina ngoma.
Tunawafunga kwa rushwa manesi, wakati wala nchi wajinafasi.
Hongo sasa ni kodi, kuna risiti hadi ya VAT,
Rushwa rafiki wa haki, kama hutaki nenda mahakamani.

Asiyefunzwa na mamaye, sasa sharti aende jeshini.
Kigogo yeye wanawe, elimu ughaibuni.
Wametupa pande la jiwe, sio mkate wenye jibini,
Mbili kumi na tano liwalo na liwe, tusikubali waturubuni.

Tumkumbuke bwana Hussein,
Hata bila tuzo, ukweli tuseme.
Sanaa tumeitupa,
Sasa jukwaa la maigizo bungeni.

Tuufukizie ubani,
mzimu huu wa malenga,
Mashairi tuyaghani,
Tuwaamshe hawa walengwa.

Related links:

Neema is a poet from Tanzania, East Africa. Her passion is entrepreneurship and writing – basically FREEDOM. Her recently published book of poetry, See Through The Complicated, can be found on Amazon.com.

0 Comments

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Human verification:

Please type the characters of this captcha image in the input box

*