Hivi punde tu nimemaliza kukisoma kitabu cha Malcolm Gladwell kiitwacho Outliers: the story of success. Nimeona ni vyema kuwasilisha hapa machache kuhusu kitabu hiki ili nawe ukinunue na kukisoma. Kabla sijaendelea, ningependa kuweka bayana kuwa kitabu hiki sio ‘self help book’ – yaani vile tabu vinavyotoa listi ya ni yepi ya kufanya ili ufanikiwe kimaisha.
Katika makala iliyopita, SN alitupatia maswali na hoja muhimu kuhusu suala la motisha na mafanikio kiujumla kimaisha. Ndani ya Outliers, Gladwell anatupatia mwanga kuhusu sifa zinazowaunganisha watu kadhaa wenye ‘mafanikio’ katika nyanja mbali mbali. Anaeleza kuwa ‘mafanikio’ hayatokani na kipaji pekee yaani talent au genius, bali ni mjumuiko wa sifa ambazo mara nyingi hatuzifikirii kama bahati, malezi, mila, historia ya familia/uzawa n.k. Ni muhimu pia kuweka bayana kuwa hapa haongelei ile bahati kama ya kushinda bahati nasibu, bali aina ya bahati ya kuwa ‘at the right place at the right time’ na kuwa na uwezo wa kuitumia nafasi hiyo kwa manufaa yako kiufanisi.
Ndani ya Outliers, Gladwell anaeleza mifano ya umuhimu wa uzawa katika mafanikio, anatoa maelezo kwanini wayahudi wengi wanaendesha uchumi wa miji kama New York. Ohh, na pia hujawahi kujiuliza kwanini Wachina/Wakorea/Wajapani wengi ni wakali katika hisabati? Hasa hasa Wachina tunaokumbana nao vyuoni huku ulaya na marekani? Gladwell anaelezea kuwa chimbuko ni kutokana na lugha zao kuwapa advantage fulani katika kuhesabu, yaani zipo very concise kuzidi lugha kama kiingereza au nyingine nyingi. Sijui kiswahili kikoje katika fikra hii, ila hii ni mada nyingine ukizingatia kuwa nchini TZ hisabati bado ni gonjwa sugu.
Waweza kukinunua Outliers hapa: http://www.amazon.com/dp/0316017922
Soma kazi zake nyingine hapa: http://www.gladwell.com/


