Umri

Na Shaaban bin Robert

Nilikuwa na umri wa miaka ishirini na saba. Maisha yalikuwa bado mapya na matumaini yake yalikuwa mengi sana. Katika afya nilikuwa nimejaa utomvu wa uzima na katika moyo furaha. Kichwa kilikuwa bado kuota mvi na ugonjwa ulikuwa mbali na mwili. Uchovu ulikuwa kitu kigeni kukiona mwilini. Nilikuwa katika mwanzo tu wa maisha; bado sijafika katikati wala mwisho wake. Kurasa za maisha yangu yaliyopita zilikuwa chache na matendo haba yaliyoandikwa juu yake katika wakati wa nyuma yalikuwa hayawezi kuwatamanisha wengine kuyanakili wala kuniridhisha mimi mwenyewe.

Wakati mmoja nilifikiri kuwa yote yaliyo azizi au bora kwa mtu ni matendo yake aliyotenda zamani; na kwa kuwa mimi sikupata kutenda tendo lolote la maana nilijiona sawa kabisa na maskini. Wazo hili lilibatilishwa na fikira kuwa pengine ubora wa mtu huwezekana kuwa katika wakati ujao. Kwa kujifariji hivi nilijiandaa kusaburi kwa uangalifu sana nishike bahati yangu wakati wowote itokeapo. Kwa desturi bahati ina miujiza mingi sana. Haina ahadi na mtu yeyote na mara nyingi huchelewa kwenda kwa mtu. Kwa hivi wakati mwingi ulipita katika kungoja. Baadaye bahati ilitokea lakini mara kwa mara niliposimama wima kuiendea niliteleza nikaanguka chini. Nilipotaka kunyosha mkono kuishika yalitokea mazuio ambayo sikuyatazamia au nilifungiwa milango ya mbele nisionane nayo.

Milango ya nyuma ya kuifikia bahati ilikuwa mingi lakini haikunishawishi hata kidogo. Nilitaka ikiwezekana niweze kuwajihiana na bahati uso kwa uso mbele ya hadhara siyo mafichoni. Yamkini mtauliza. Ulingoja bahati gani? Bahati niliyokuwa nikingoja ilikuwa ni ya kutenda jambo lisilo aibu mbele ya macho ya watu katika maisha yangu yote. Ikiwa kabla ya umri wangu wa sasa nilipata kutenda aibu ambayo mimi mwenyewe sifahamu lakini inayokumbukwa na wengine nilitaka nisitende tena aibu hiyo katika wakati wangu ujao.

Labda utashangaa sababu mimi nilitaka sana bahati ya namna hii badala ya bahati ya vitu kama vile utajiri au mamlaka ya juu ya watu vinavyotafutwa na wengi kwa sababu ya fahari yake. Nasadiki kuwa utajiri ni kitu cha tamaa na mamlaka yana fahari lakini nilivihofu vitu hivi sababu pengine wenye vitu hivi kwa wingi na kufurika aibu iliwatia alama mbaya sana. Niliona mamia ya waliouza roho zao kwa vitu hivi lakini pato lao lote lilikuwa ni uharibifu wa majina yao. Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa duniani. Jambo hili sikulipenda. Nilitaka niwe na jina lililo mbali na madoa katika umaskini na unyonge wakati wote wa maisha yangu.

Jambo hili likiwa jepesi au gumu, kumpa moyo mtu au uchovu, mimi nilikusudia kulipata kwa hali yoyote. Kama nikishindwa kufaulu kupata lote nilitaka nipate nusu au robo yake. Kidogo bora kuliko kukosa kabisa; na jaribu dogo la wema bora kuliko kubwa la ubaya. Maisha ya mtu ni msingi wa maendeleo ya nchi. Doa lolote liwezekanao kuzuiwa kuyaaibisha ni wajibu kushindwa kabisa.

Mwisho wa kunukuu.

Tujadili

Previous ArticleNext Article
Joji was born and grew up in Dar es Salaam, Tanzania. He graduated with a B.Sc in Biochemistry in Germany, and is now pursuing a Masters degree in Microbiology & Immunology at the Swiss Federal Institute of Technology (ETH) in Zurich, Switzerland . Joji is particularly interested in matters related to global health, and basic science research that tackles public health challenges. He is engaged in mentoring Tanzanian students in higher education issues, most notably at the Kibaha High School. In this capacity, Joji blogs with Vijana FM about scientific research and development, and how youth can gain greater access to higher learning.

This post has 8 Comments

8
  1. Kwa kweli Mzee Shabaan Robert hapa kaonesha kwa ufundi wa hali ya juu jinsi kijana mwenye kiu na maendeleo anatakiwa afikiri hasa pale anapokuwa yupo katika kilele cha ujana wake. Muda ambao unapokuwa unakaribia kumaliza elimu rasmi au ndio umesha ihitimu na unaelekea katika njia ya kuanza kuandika historia yako. Njia panda kati ya ujana na utu uzima.

  2. hapa anatupa mfano hai sisi vijana wa sasa tuache kujawa na fikra za ufisadi ufisadi tu. wengi wetu tunajisahau na kutaka kujilimbikiza mali ambayo binafsi ninadhani sio chanzo cha furaha maishani hapa.

  3. Yaani Shaaban ameonesha kiu ya ujana na hasa nia ya kutaka mafanikio haraka. Maisha yamebadilika ghafla kutokana na kukua kwa teknolojia, ubepari na biashara huria. Wengi twajifikiria wenyewe kwahiyo maisha yamekuwa na ushindani mkubwa mno. Nadhani hii ni ngazi mojawapo katika hatua za ubinadamu, ila muda utafika ambapo tutaweza kuishi pamoja kwa kujaliana zaidi. Labda yangu ni mawazo nadharia.

  4. Naona aibu hata kuandika hapa kwasababu sijakisoma hiki kitabu (msako umeanza rasmi jana!).

    Mliotangulia m’meshasema ya kutosha kuhusu maudhui ya hii insha. Jamani, lugha iliyotumiwa ni.. sijui nisemaje..imekaa kishairi-shairi hivi hivi. Yaani, ukisoma unakuwa kama unateleza hivi kutokana na mtiririko mzuri sana.

    Kitu kingine, ambacho hata mimi huwa napenda sana, ni mwandishi kumpa msomaji fursa ya kuingia kwenye akili au ubongo wa mhusika. Msomaji anakuwa kama anaogelea kwenye mawazo ya mhusika; kama mhusika anazama, msomaji pia anazama nae.

  5. dah. nyie acheni tu. Nilipokuwa sekondari Shaaban Robert aliniumiza kichwa sana, na nilikuwa mvivu kumsoma. Ila sahivi ndio ninaona umuhimu wa huyu gwiji. Kitabu hiki kiko out-of-print kwa sasa, ila nimeweza kukisaka kupitia inter-library loan ya chuo kwani hakikuwepo katika maktaba ya hapa. Kwahiyo kama kuna maktaba kubwa karibu yako nenda uulizie kitabu hiki, au waulize kama wana huduma ya ‘inter-library loan’ yaani uwezekano wa kukiazima kupitia maktaba pacha nyingine kokote duniani. Si kirefu sana, ila ndani yake kumejaa simulizi za ndani kuhusu maisha yake. Ndani yake utaona ukarimu, ucheshi, alivyo romantic, genius na hekima tele alizokuwa nao.

    Mfano, akiandika kuhusu marehemu mkewe:
    “Sura yake ilikuwa jamali kwa kimo cha kadiri. Uso ulikuwa mviringo wa yai, nywele nyeusi za kushuka, paji pana, nyusi za upindi, macho mazuri yaliyokuwa na tazamo juu ya kila kitu, kope za kitana, masikio ya kingo yasiyopitwa na sauti ndogo, meno ya mwanya yaliyojipanga vizuri mithili ya lulu katika chaza, ulimi wa fasaha na maneno ya kiada yaliyotawaliwa kila wakati, midomo ya imara isiyokwisha tabasamu, sauti pole na tamko kama wimbo, kidevu cha mfuto katikati yake palikuwa na kidimbwi kidogo, shingo kama mnara ambayo juu yake paliota kichwa cha mawazo mengi, chini ya shingo mabega yalikuwa kama matawi ya maua, kifua cha madaha, mikono ya mbinu, tumbo jembamba, miundi ya kunyoka na miguu ya mvungu…..” pp 4

    Ingawa hisia zake kwenye sura ya ‘Umri’ ni za wakati wa kale. Kwa kweli ni mengi unaweza kupokea kama wosia au hekima sisi vijana wa sasa.

  6. Fasihi iliyoimarika (ambayo inaakisi yanayotokea kwenye jamii) kamwe haiwezi kufa.

    Shaaban angezaliwa kwenye nchi za Magharibi, wangejenga sanamu ya kumuenzi. Lakini kama unavyotujua Watanzania…; hata picha yake kuipata kwenye mtandao ni kazi.

    Hiyo aya kuhusu marehemu mke wake ni kali sana. Ukiacha utaalamu na umahiri wake wa kucheza na maneno, ukifikiria kila kiungo anachoongelea utakubaliana nami kuwa alikuwa anamjua mke wake kwa undani. Kuna vitu vidogo vidogo ambavyo watu wengi hawatilii maanani au hawavioni. Lakini kama kukiwa na ukaribu kama unavyooneshwa na Shaaban hapo juu… mambo ya mapenzi hayo. Tuwaachie wakubwa.

    Mimi nadhani kile kitabu cha Kusadikika nilikimaindi kuliko maelezo. Sijui kwanini. Lakini kuna sehemu ya akili yangu inayojuta kwanini sikutafuta vitabu vingine vya huyu msela.

    Ebanae, ukipata muda uwe una-post aya mbili tatu kila baada ya siku mbili hivi… Natanguliza shukrani za dhati.

  7. Vipi kijana Joji, una mpango wa kumpiga neno mtoto wa pwani ya Afrika Mashariki nini? Naona unasoma vitu kwa undani kuhusu romance inavyoelezewa kwa Kiswahili sanifu.

  8. LOL. Kumbeeee! Dogo anachukua “utirio” na maujanja kutoka kwa Shabaan ili somo lieleweke. Kila la kheri, Joji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend