“Mwendo ni kula raha – 3”

Sehemu ya pili ya hadithi hii inapatikana hapa

Neema ananivuta hadi nje ya ukumbi huku akiwa bado amenishika mkono. Kufika tu nje kwenye nuru, anaamua kuniachia. Naongeza ukubwa wa hatua kadhaa ili tuweze kutembea sambamba, bega kwa bega, Neema akiwa upande wangu wa kushoto. Nageuka na kumuangalia usoni kwa udadisi; ingawa nimelewa kidogo, kwa mara ya kwanza naona vizuri uzuri na urembo wa Neema. Naiambia nafsi yangu, binti kama huyu hahitaji kujipodoa. Sielewi kwanini kajipaka rangi nyeusi kwenye kope za macho.

Wakati tukiwasili kwenye kontena lililopo kama mita 20 kutoka kwenye malango ya Club Billicanas, Neema ananiambia, “Vipi, unaonekana wewe sio muongeaji sana?”

Natabasamu tu. Pamoja tunakaa kwenye ukingo wa sakafu ya saruji iliyopo mbele ya kontena mbali kidogo na sehemu madereva taksi walipo, naamua kumuuliza, “Mitihani yako ilikuwaje?”

Neema anaangua kicheko, ananimbia, “Deo was right! Wewe Magirini kweli mzee wa busara. Kila wakati unaongelea mambo serious! Huwezi kuongelea vitu vingine? Lakini… Bahati yako unajua kucheza muziki.”

Nacheka tu bila kusema chochote. Naangalia chini, kisha nanyanyua uso wangu polepole na kutazama sketi nyekundu aliyovaa, na saa yake ya kiganjani: ni saa nane na nusu usiku. Naendelea kunyanyua uso wangu, nguo aliyovaa inanipa mwanya wa kuona ngozi kwenye mabega yake; inaonekana anasikia baridi. “Vipi, unasikia baridi?” Namuuliza huku nikivua shati langu haraka-haraka na kubakia na fulana. Kwa moyo mkunjufu namkabidhi shati langu, “Jifunike mabega na hili shati. Najua unasikia baridi.”

Bila kusita Neema anachukua shati langu na kujifunika. “Asante Magz. You are so kind.” Ananimbia huku akitabasamu.

Kabla ya kufungua kinywa changu, nasikia mtu akituita kwa sauti, “Magiriniiiii, Magiriiiniiiii! Neeema, Neeeema!”

Naitikia, “Naaam! Niko hapa!” Nanyanyuka, naangalia sehemu sauti inapotoka na kumuona Deo akija sehemu mimi na Neema tulipo huku akipepesuka.

“Mzee Magirini, I am gonna miss you, man! Neema, this is my real friend right here! Msikilize sana!” Nadhani Deo amekunywa pombe ndio maana anaropoka. “Magirini, najua utaenda shule nyingine. Ninavyomjua dingi yako, he will send you to some stupid nerdy boarding school. Mimi mzee wa Commerce nitabaki Dar. Itaboa kinoma mchizi wangu.”

Ni kawaida ya Deo kuchanganya lugha akiwa amekunywa. “Deo, tulia kwanza. Kaa chini hapa.” Baada ya kukaa na kutulia, namuuliza, “Mzee, umekunywa ngapi?”

“Acha hizo mzee. Moja tu.” Sisemi chochote, baadae anasema, “Nimekunywa mbili tu. Niamini.”

Neema anaingilia, “Vipi Magirini, mbona anaonekana yuko alright tu. Mwache.”

Namuangalia Neema kwa jicho kali bila kufungua kinywa kwa sekunde kadhaa. Kisha nageuka na kumuambia Deo, “Nipe funguo za pick-up!”

Deo ananijibu, “Tuliza boli mtoto wa mama. I am OK. I can drive mzee. Unanijua mimi mzee. Bia nne hazinipelekeshi.”

Tunaendelea kuzozana kwa dakika kama tano hivi, lakini Deo anagoma kabisa kunipa funguo za gari. Neema anaondoka na kutuacha mimi na Deo tukiendelea kutupiana maneno. Usiku umebadilika ghafla; dakika chache zilizopita kila mtu alikuwa anatabasamu, sasa hivi nyuso zetu zimejaa ndita.

Punde kundi zima, likiongozwa na Dullah na Neema, linakuja tulipo. Dullah anauliza, “Wazee, vipi tena?”

Namjibu, “Huyu Binti Chura nadhani kanywa pombe. Sitaki aendeshe gari.”

Nawaangalia na bahati mbaya hakuna yeyote anayeniunga mkono. Kingo ananiambia, “Achana na Deo. Mi’ nilikuwa nae. Hajalewa wala nini. Au wewe ndio umelewa?” Wote wanaangua kicheko.

Najihisi kama popo; walimwengu wananitaa ndege ingawa nazaa. Lakini sina jinsi, nainamisha kichwa changu na kuzama kwenye ziwa la fedheha.

Deo ananiambia, “Ndio maana wazazi wako wakakupa jina Magirini.”

*      *      *

Kwa mbali nasikia sauti ya baba, “Magirini, amka. Amka!”

Inaniwia vigumu kuamka haraka-haraka kutokana na kaubaridi ka asubuhi. Kwahiyo nageukia upande wa pili dirisha la chumba changu lilipo, nalivuta shuka na kujifunika kichwa. Nilitegemea kusikia tena sauti ya baba akinisihi niamke. Lakini kimya. Nasikia kishindo kidogo cha miguu yake akielekea kwenye dirisha na kufungua pazia. Ingawa mwanga wa jua la asubuhi ni hafifu, unapenya kwenye shuka langu na kutua usoni. Usingizi unatokomea kwa kasi.

“Magirini, amka, kapige mswaki. Nahitaji kuongea na wewe.”

Nakumbuka kuwa sijamsalimia. “Shikamoo baba!”

“Marahaba,” ananijibu huku akingalia nje ya dirisha. “Haya nenda kapige mswaki.”

Sio kawaida ya baba kuniamsha Jumamosi asubuhi, hasa kama anajua nilikuwa nimetoka usiku uliopita. Wakati napiga mswaki, nashindwa kujizuia kujiuliza maswali lukuki. Vipi, baba anajua kama jana nilikunywa pombe? Au amesikia kelele za marafiki zangu wakati Deo aliponirudisha kwa gari ya wazazi wake? Labda amekasirika kwasababu sikurudi nyumbani kwa taksi kama alivyoniagiza?

Baada ya kunawa uso na kupiga mswaki, narudi chumbani na kumkuta baba akimalizia kuondoa tando za buibui kwenye dari. Kuna kitu hakiko sawa; ameamua hadi kutandika kitanda changu! Nashikwa na bumbuwazi na kubaki nimesimama mlangoni. Baba anaketi kwenye kitanda na kuniambia, “Njoo hapa ukae,” huku akinyoosha mkono kuniamuru nikae kitandani karibu naye.

“Niambie, jana ilikuwaje? Ulirudi kwa usafiri gani?”

“Samahani baba, niliamua kurudi na gari ya Deo. Sitarudia tena.”

Nilitegemea ataanza kupaza sauti kunigombeza, lakini anaendelea kuhoji kwa upole, “Deo nd’o alikuwa anaendesha gari? Alikuwa kwenye hali gani? Usijaribu kunilaghai mwanangu.”

Moyo wangu unaanza kuwa mzito, lakini mapigo yanaongeza kasi. Sielewi kinachoendelea. “Alikunywa kidogo tu nadhani… Kwani vipi?”

Baba anainamisha kichwa chini kuangalia sakafu huku akitingisha kichwa, ananiuliza, “Yeye nd’o alikurudisha hapa na wenzako wengine?”

“Ndio… Kwani vipi?”

Ananyanyua uso wake na kuniangalia usoni. Na mimi namuangalia usoni. Nadhani leo ndio mara ya kwanza kumuona baba yangu akilengwa na machozi. Ananiambia, “Baba Deo kanipigia simu kutoka Moshi… ” Ananyamaza kwa muda mfupi na kumeza mate. “Baba Deo alinipigia simu kunitaarifu rafiki yako Deo aligonga nguzo ya nyaya za simu iliyoko karibu na nyumbani kwao. Alikuwa mwenyewe kwenye gari.”

Siamini ninayosikia kutoka kwenye kinywa cha baba. Namuuliza, “Haiwezekani. Nadhani aliwarudisha marafiki zangu… Kesha’pelekwa hospitali?”

“Pole sana mwanangu. Baba Deo anadhani alifariki pale pale alipopata ajali. Pole sana Magirini.”

Naanza kutokwa na machozi, huku baba akijaribu kunifariji, “Pole sana mwanangu. Ndio maisha haya. Mimi na mama yako tuko hapa kukufariji kwenye kipindi hiki kigumu.”

“Baba, siamini unachoniambia. Niache mwenyewe kwa muda. Nitakuja sebuleni…”

Anabaki akiniangalia kwa dakika kadhaa, mkono wake wa kuume ukiwa juu ya bega langu la kushoto. “Sawa. Mama yako yuko sebuleni. Mimi itanibidi niende Muhimbili kumsaidia mjomba’ake Deo na mipango ya mazishi na vitu vingine mpaka baba Deo atakaporudi kutoka Moshi jioni.”  Ananyanyuka, anatoka chumbani na kufunga mlango polepole.

Nashindwa kujizuia kububujikwa na machozi na kupiga mayowe. Maisha ya ujana ni kama kishada kinachopepea kwenye anga karibu na ufukwe wa bahari. Mara nyingi upepo huonekana ni mwanana kwenye macho ya wengi. Lakini, mara chache, kamba ya kishada ikikatika, sote tunaona jinsi kishada kinavyobebwa na upepo na kutoweka. Kibaya zaidi, najihisi kama mimi ndiye nilikuwa nimeshika kamba ya kishada. Lakini nitafanya nini sasa. Nitabaki na kuishi na majuto…

*      *      * MWISHO *      *      *

Ingawa mtiririko na matukio mwanzoni mwa hadithi hii ni ya kutunga, kisa hiki ni cha kweli; hasa jinsi kinavyoishia. Nilisimuliwa na rafiki yangu mwishoni mwa mwaka 2002.

(c) SN 2010

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 6 Comments

6
  1. Magirini kumbe romantic bway. Anavuta pointi kwa kugawa shati kwa manzi. Btw, inakuwa vipi anaitwa na msela na kuitikia “Naaam”?

    Aise, tumepoteza wengi kwa hii drink driving. Kwanini Magirini hakutumia nguvu kumkataza mwenzake na kuchukua funguo? Kwanini alikubali kupanda gari la dereva aliyelewa? Maswali mazito, ila ujana mara nyingine haya huyafikirii. Mentality ya “what could go wrong?”

  2. Nimependa jinsi baba Magirini alivyokuwa mpole, baada ya kumfuatilia kwenye hadithi zilizopita, dah!!..ni kama kumwona Simba anakula nyasi..hah

    Joji hata mimi nilishtuka nilivyoona Magirini anaitika Naam, kweli mtoto wa mama kama Marehemu Deo alivyokuwa akimwita..

    R.I.P akina Deo wote

  3. Wazee, sio kama hatujui tunayoyafanya, au hatujui kabisa madhara yake. Wakati mwingine ni ile “peer pressure” tu. Kama ulivyosoma hapo juu, Magirini ni kama popo — marafiki zake wanamuaita ndege; ingawa anajua dhati kuwa yeye ni mamalia, bado anakubali kuitwa ndege, na kukubali kupakia kwenye gari linaloendeshwa na rafiki yake ambaye amelewa.

    Mara ngapi tumekosea au kufanya uovu kwa kufuata mkumbo, kwasababu tu tunaogopa kutaniwa na marafiki zetu? Mara ngapi tumepoteza marafiki zetu kwenye ajali za kizembe (baada ya kulewa)?

    Mi’ mshkaji wangu mmoja alifariki kwenye ajali ya gari akienda Kurasini kununua “kuberi”…

  4. Aise Deo mbishi kinoma, ila hii story iko familiar, tukisha pata uchachu busara yote inayeyuka, kwa kweli inasikitisha kwa Magirini kupoteza swahiba wa karibu namna hio, ka story kazuri ila kafupi, mkuu ungeendelea kutufunga kamba tu, wenzako tulishanogewa!

    Safi sana SN!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend