Ukosefu wa pato, ukimya wa Vijana?

Na Michael Dalali

Hali ya ukosefu wa fursa za ajira nchini Tanzania inazidi kukua siku hadi siku. Hii inawakumba zaidi vijana ambao wanahodhi asilimia kubwa ya tegemeo katika nguvukazi ya Taifa — kwa zaidi ya asilimia 65.

Vijana hawa, ambao wanapita katika mifumo ya kuwajenga kitaaluma na fani, bado wanakuwa wahanga wakubwa wa kadhia hii ya ukosefu wa fursa za kuajiriwa wala kujiajiri. Hali ambayo ni tete; kwani, si tu kurudisha nyuma jitihada za vijana hawa kujiletea maendeleo yao binafsi, bali pia kwa kiasi kikubwa inalirudisha nyuma Taifa zima.

Takwimu za ukosefu wa ajira za vijana ni takribani asilimia 11, tofauti na matarajio ya MKUKUTA ambao ulipanga kushusha ukosefu wa ajira mpaka asilimia 6.9 mnamo mwaka jana (2010).

Kwa upande mwingine takwimu hizo hazitoi picha kamilifu ya uhalisia wa hali tete ya ukosefu wa ajira na fursa za uzalishaji pato, kwani hali ya sasa na ongezeko la wahitimu toka vyuo vya ufundi na vya elimu ya juu imeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini utete unaweza kudhihirika pia kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa nguvukazi na ajira (ILFS), zinazodhihirisha ongezeko la watu takribani 760,000 katika soko la ajira kila mwaka. Ambapo kati yao ni 40,000 tu ndio wanapata ajira kila mwaka, ikiacha zaidi ya watu 720,000 bila ajira.

Naamini utafiti wa hali ya nguvukazi na ajira (ILFS) ukifanywa mwaka huu ama ujao utatoa majibu yenye kuonesha hali kuwa mbaya zaidi tofauti na takwimu hizo zilizopatikana mnamo mwaka 2001.

Ni kweli nchi nyingi duniani zinakumbwa na kadhia hii ya ukosefu wa ajira. Lakini kila nchi inavyolishughulikia tatizo hili ndipo utofauti na upekee huonekana.

Mathalani vijana wa nchi za Misri na Tunisia hivi karibuni walivyolichukulia tatizo la ukosefu wa ajira na kukithiri kwa hali ngumu katika maisha yao inatoa upekee, kwani vijana hao wameweza kumudu kuondosha utawala ambao haukuwa ukionesha jitihada za kutosha kivitendo kulishughulikia tatizo hilo.

Fukuto la Misri. Picha kwa hisani ya "Boston Big Picture".

Nchi za Ulaya, mathalani Ujerumani, zimekuwa pia na tatizo hili, lakini jitihada zao za kuhakikisha mafunzo ya kujiajiri na kuweka mifumo ya kitaasisi na kiuwezeshaji kwa vijana hawa zinatoa tumaini na upekee wa jinsi nchi inavyojitahidi katika kupambana na hali ngumu ya vijana wanaokosa ajira ama fursa za kujiajiri.

Uwepo wa pensheni kwa wasio na ajira zinazotolewa katika nchi hizo nyingi za Ulaya unasaidia kupunguza makali ya maisha kwa vijana wasio na ajira, ama pato katika kipindi chao cha mpito, mpaka watakapopata fursa za kushiriki katika uzalishaji mali iwe kwa kuajiriwa ama kujiajiri.

Ukimya wa vijana wa Kitanzania haimaanishi wao hawaguswi na utete wa ukosefu wa ajira. La hasha!

Wala ukimya huu haumaanishi hawatafakari namna ya wao kujikwamua kutoka katika hali ya ukosefu wa fursa za kuzalisha pato lao. Ukimya huu haumaanishi hawatathmini jitihada za serikali pamoja na wadau katika kusaidia kupunguza makali ya tatizo hili.

Vijana Vocational Training @ globalallianceafrica.org

Hakika vijana wanaona na wanafikiri. Vijana hawa ambao wengi ni wasomi toka vyuo vya ufundi na elimu ya juu wana uwezo wa kuchambua baina ya kauli tupu na utendaji wa kauli hizo.

Ikumbukwe sio vijana tu huliangalia na huguswa na athari za ukosefu wa ajira na fursa za uzalishaji wa pato, bali jamii nzima inayowazunguka vijana hawa —  hasa wazazi wa vijana ambao wamegharamika katika kuwalea na kuwasomesha — inaumia kila uchao inaposhuhudia juhudi zao zinagota kwa vijana kukaa majumbani miaka kwa miaka wakisaka ajira ama fursa za kujiajiri.

Najua wapo baadhi ya viongozi au wananchi wanaweza kukimbilia kutoa majibu mepesi katika kadhia hii tete, kuwa ni ukosefu wa ari kwa vijana katika kujituma na kujiajiri. Si rahisi kama utamkaji wa matamshi hayo! Kwani hakika hata kwa wenye utashi wa kujiajiri, ama hata wale wenye utashi wa kufanya kazi kwa kujitolea, wanakumbwa na changamoto nyingi sana zinazowakwamisha.

Naamini endapo kuna utashi madhubuti wa kulishughulikia tatizo la ukosefu wa ajira na uzalishaji pato kwa vijana, basi njia na mbinu zipo nyingi tu. Njia na mbinu hizi hazikomei kwenye mafunzo ya ujasiriamali (kama wengi wanapokimbilia) ama mabadiliko ya kimitaala ya elimu tu bali zapaswa ziende zaidi. Kwa mfano, uboreshwaji wa sekta kama ya kilimo, utalii, viwanda na biashara ambazo kwa kiasi kikubwa zitazaa matunda ya kupokea vijana wengi zaidi na kusaidia wao kuzalisha pato lao na kwa Taifa.

Kwa namna nyingine, tatizo la ukosefu wa ajira limetokana na uendeshaji mbovu wa mashirika; kwa mfano, mashirika ya umma ambayo yangeweza kuzalisha ajira zaidi. Unaweza kujionea uendeshwaji goigoi wa sekta ya miundo mbinu, hususan shirika la ndege la Taifa (ATCL) au shirika la reli (TRL), ulivyo na athari hasi kwa ajira nchini. Endapo mashirika haya mawili yangeweza kuendeshwa kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu, yangeweza kuchochea ongezeko kubwa la ajira nchini na kusaidia ukuaji wa pato la mtu mmoja-mmoja — hasa vijana wetu ambao wanahitimu kutoka katika vyuo kadha wa kadha nchini na hata wengine toka nje ya nchi.

Ndio mantiki ya Hayati Mwl. Nyerere enzi za uongozi wake katika awamu ya kwanza, licha ya jitihada nyingi za kuhakikisha huduma za kijamii, kama vile upatikanaji wa elimu kwa ngazi zote tangu awali hadi ile ya watu wazima, alihakikisha anaimarisha sekta za kilimo na viwanda pasipo kusahau miundo mbinu kwa kuimarisha sekta hizi na nyingine kivitendo na si kuishia kwenye hatua ya sera na mipango mitamu-mitamu.

Naamini, endapo kweli tukiwa tunatambua nguvu, thamani na mchango wa vijana kama uliotolewa katika kipindi cha chaguzi zetu nchini, basi viongozi na watumishi wa umma walio madarakani hawana budi kukosa usingizi ama starehe kwa kuhakikisha utatuzi wa kudumu wa ukosefu wa ajira na fursa pana za kujiajiri kwa vijana unafikiwa.

Toleo mbadala: Mwananchi | Imechapishwa tarehe 23 Februari, 2011.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 13 Comments

13
  1. Makala hii ambayo ilikuwa na dhamira ya kuweka wazi tatizo la ajira kwa vijana imeshindwa kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa vithibiti.

    Utumiaji wa takwimu bila ya kuweka chanzo cha takwimu hizo kumedhoofisha hoja ya muandishi kwa kiwango kikubwa.

    Ukosefu wa maelezo ya kina kwa masuala anayotaka kutuaminisha wasomaji kunaacha masuala mengi.
    Anaposema vijana wanakutana na changamoto zinazowakwamisha wakitaka kujiajiri au kuajiriwa, anakusudia changamoto gani? Au anapozungumzia mantiki ya Mwalimu Nyerere, tungetarajia atuthibitishie kuwa sera za ajira za Nyerere zilikuwa bora na atuondolee shaka wasomaji wake kuwa sera hizo hazikufanikiwa kwa kuwa hazikuwa endelevu.

    Juu ya dosari zote hizo nimeshindwa zaidi kumuelewa mwandishi anapokiri kuwa kuna ukimya, kuwa vijana hawazungumzii suala hili la ukosefu wa ajira lakini akathubutu kusema kuwa vijana wanaona na kufikiri na kukiainisha kile wanachokifikiria.
    Penye ukimya, mwandishi amejuaje kwa uhakika kile kinachofikiriwa?

  2. Hyperkei,

    Duh, bandiko lako lenye “constructive criticism” natumai halitaonwa kama shambulizi, bali chachu ya kutaka ushahidi na umakini zaidi.

    Ni muhimu waandishi na wachangiaji kutoagua kwamba wasomaji wanaelewa vitu ambavyo havijawekwa wazi. Ni muhimu kwenda na fikra kwamba watu hawajui sana na muandishi anawaelezea kikamilifu na kupunguza maswali yanayoweza kubashiriwa kirahisi.

    Nikimpa muandishi “benevolent benefit of the doubt” -naamini Vijana FM kama sehemu ya watu makini-, nataka pia kuamini kwamba takwimu hizi hazijatoka hewani, lakini kama mdadisi wa asili, ningependa kujua vyanzo vya takwimu, maana katika dunia ya leo ya Google na hyperlinks, muandishi anaweza kunitambulisha sources muhimu ambazo nilikuwa sizijui.

    Kwa hivyo napenda kusisitiza zaidi kwamba, kutaja vyanzo vya takwimu si tu kuna manufaa kwa muandishi kwa maana ya kumuongezea uwezo wa kuaminika, bali pia kutatunufaisha wadadisi wengine kama sie ambao baada ya kumaliza kusoma habari, tutataka kwenda kudodosa zaidi kwenye vyanzo (kama muda upo).

    Naandika kutokana na uzoefu wangu binafsi, nimepanua sana wigo wa vyanzo vyangu muhimu (na “Favorites” Menu ya browser) kwa kusoma na kudonoa vyanzo kutoka maandiko ya wengine.

    Natumai ujumbe umefika na umechukuliwa uzuri.

  3. Ujumbe umefika na unachukuliwa vizuri tu, na ni vizuri mmeliona hilo. Mwandishi atapita hapa kuona kinachoendelea.

    Lakini, kwa upande mwingine ningependa kuwataarifu kuwa Michael huandaa makala kwa ajili ya gazeti la Mwananchi na kazi yake inahusika moja kwa moja na ukusanyaji wa taarifa kama hizi. Hivyo hufanya utafiti na kuandika makala fupi (kulingana na nafasi anayopewa) — kama mnavyojua baadhi ya takwimu (hasa kutoka Tanzania ambazo zimeorodheshwa hapo juu) hazipatikani kwenye mtandao kirahisi ndio maana hata mimi nimeshindwa kuongeza hyperlinks kama kwenye makala zake nyingine zilizopita.

    Jamani, hiyo tovuti ya MKUKUTA mi’ nitaipata wapi. Kwa hiyo nimeamua kumpa benefit of doubt.

    Kama ikitokea Ndugu Dalali hatapata muda na kuja hapa kutuambia ametoa wapi hizi takwimu, mimi nitachofanya ni kuongezea tu “source” chini ya makala baada ya siku kadhaa, kuwa makala hii imetoka kwenye gazeti la Mwananchi.

    Sitaki kuzama zaidi na kujibu maswali ambayo yameelekezwa kwa mwandishi, ila neno “ukimya” hapa labda linamaanisha kinyume cha yale yanayotokea Mashariki ya Kati?

  4. Nimetoka kuchimba makabrasha yangu.

    Michael aliituma hii makala tarehe 18 Februari na nikapata nafasi ya “kuihariri” Ijumaa iliyopita (25 Februari) na kuipost hapa.

    Makala hii ilichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi tarehe 23, kama inavyooneshwa kwenye “chanzo” (ilibidi niperuzi ili kuangalia kama imechapishwa tayari au la).

    Samahani kwa usumbufu wowote uliotokea; michango inakaribishwa.

  5. Hii nayo ni changamoto kwa makampuni kutofautisha namna ya uwasilishaji wa makala zao zinazochapishwa kwenye karatasi na zile za elektroniki.

    Juu ya kuwa baadhi ya vyanzo vya takwimu labda havipatikani kwenye mtandao, mwandishi bado alitakiwa kutuambia wasomaji wake vyanzo vya takwimu zake.

    Kwa upande mwengine, kwa vile hii ni makala rasmi iliyochapishwa gazetini, ningependa pia kuchangia kwenye matumizi ya lugha.

    Matumizi ya lugha kwenye makala hii yanahuzunisha kwa kweli na tungependa kuona wahariri wanafanya kazi yao ipaswavyo na kuhakikisha Kiswahili sanifu kinatumika. Nitatoa mfano wa machache niliyoyaona kama msomaji kutetea hoja yangu.

    1. Matumizi ya ngeli.

    Mwandishi ameshindwa kabisa kutumia ngeli sahihi anapowasilisha hoja zake kwenye maeneo kadhaa.
    “……..kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa nguvukazi na ajira (ILFS), unaodhihirisha…..” (takwimu zinazodhihirisha)

    “………bali jamii nzima inayowazunguka vijana hawa inaumia kila uchao wanaposhuhudia……….” (jamii inaposhuhudia)

    “Unaweza kujionea uendeshwaji goigoi wa sekta ya miundo mbinu, hususan shirika la ndege la Taifa (ATCL) au shirika la reli (TRL) lilivyo na athari hasi kwa ajira nchini” (uendeshwaji ulivyo na athari…)

    2. Matumizi ya mifumo ya sentensi.

    “…. wana uwezo wa kuchambua baina ya kauli tupu dhidi ya utendaji wa kauli hizo …“ (‘baina ya …na .’ na ‘dhidi ya ..na …’ hazipaswi kuingiliana)

    “…. licha ya jitihada nyingi za kuhakikisha huduma za kijamii, mathalani upatikanaji wa elimu. Alihakikisha anaimarisha sekta za kilimo na viwanda…” (sentensi inayoanza na licha haiwezi kuwekewa kituo kikubwa hapo ilipowekwa)

    3. Misamiati

    “…imeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni..” (matumizi ya maradufu yanatia shaka iwapo ameitumia kwa maana yake rasmi au kimakosa akimaanisha ‘kiwango kikubwa’. Kama maana rasmi tunaomba chanzo cha takwimu hiyo)

    “Licha ya takwimu hizo, bado hazitoi picha ya kutosha ya uhalisia wa hali tete…” (picha ya kutosha haileti maana)

    4. Mengineyo

    “Mathalani” Neno hilo nafikiri nimelisoma zaidi ya mara tano kwenye makala hii ndogo. Inapoteza ladha kwa msomaji kurudia neno hilo kwa hilo wakati wote.
    “kuajiriwa na kujiajiri”. Kiswahili ni lugha yenye muuondo wake kwenye sauti pia. “mla huliwa, zaa zaliwa, kujiajiri kuajiriwa”

    “Alihakikisha anaimarisha sekta za kilimo na viwanda pasipo kusahau miundo mbinu kwa kuimarisha sekta hizi na nyingine kivitendo” Mfano wa marudio ya matumizi ya maneno kama “anaimarisha kwa kuimarisha” umejitokeza sehemu nyingi. Ni vitu vidogo vidogo ambavyo vinaondoa hamu ya msomaji.

    “wanapaswa wapaswa”. Inapendeza zaidi iwapo mwandishi anadumisha aina moja ya matumizi ya maneno. Ikiwa atatumia wala, wapaswa, wafikiri afanye hivyo mwanzo hadi mwisho, na ikiwa atatumia wanakula, wanapaswa, wanafikiri afanye hivyo mwanzo hadi mwisho pia.

  6. Hyperkei, mapendekezo yako (namba 1 – 3) yamefanyiwa kazi. Shukrani kwa kunisaidia kurekebisha.

    Kama unaona kuna dosari nyingine, tafadhali, usisite kuniambia na mimi nitakutumia muswada wa hii makala ili uihariri zaidi.

    Ni matumaini yangu angalau sasa hivi inasomeka na inaeleweka kwa urahisi zaidi kulinganisha na ile iliyochapishwa kwenye gazeti la Mwananchi.

  7. SN samahani sana kwa usumbufu uliojitokeza.

    Nilipozungumzia wahariri nilikusudia wahariri wa gazeti la Mwananchi kuwa hawafanyi kazi yao ipaswavyo na kuruhusu makala yenye makosa kuchapishwa.

    Nna wasi wasi kuwa mhariri wa Mwananchi hata hakuisoma hasa kwa sababu kwa kuisoma mara moja tu angegundua hayo yote yaliyoainishwa na mengineyo.

    Kwa kuirekebisha hapa makala yao umewafanyia favor kubwa sana, walitakiwa kuaibishwa kwa yale makosa kuanishwa kwa rangi nyekundu kisha wakatumiwa link :@

    Waswahili wanasema “huruma hailei mwana”, kurekebisha makala yao bila ya kuchukua hatua ni sawa na sisi kulea ‘uozo’ kwa kuyaruhusu magazeti kuandika bila ya kusimamia viwango.

    btw: unauhakika hujavunja kanuni za hati miliki kwa kuibadilisha hiyo makala? :))

  8. Hahahaha! Bila samahani (kabisa)…

    Eneweiz, kutokana na ukiukwaji wa maadili ya tovuti hii uliojitokeza Ijumaa iliyopita nimeamua kujiuzulu. Nimetuma barua kwa wahusika na natumaini wataruhusu nifanye vile ninavyotaka, yaani niwajibike.

    Wenu mtiifu,
    — Martyr Muammar Gaddafi.

  9. Ndugu,

    Kwanza napenda kuomba radhi kwa kutoingia katika jukwaa letu hili kwa muda kidogo na hivyo kupelekea kuchelewa kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wachangiaji.

    Napenda kutanguliza shukrani zangu za dhati kwa nyote mlioisoma na pia kuchukua hatua nyingine ya kutoa maoni yenu. Nashukuru sana!

    Daima naheshimu maoni, mawazo, sahihisho na ushauri. Hivyo kwangu maoni, ushauri na masahihisho yote yaliyoainishwa nimeyachukua kama chachu ya kujifunza zaidi na zaidi katika uandishi, lugha fasaha ya Kiswahili na zaidi uwasilishaji wa hoja.

    Ni kweli makala hii imelenga zaidi kutumika katumiwa katika magazeti nchini na haswa gazeti la MWANANCHI ambalo nimekuwa nikichangia kuandikia kama mwananchi wa kawaida kutumia kile kwa sasa kinashika kasi na kuitwa; “citizen journalism”.

    Hivyo lazima nikiri, si mtaaluma kama mwanahabari lakini nina mapenzi na uandishi na baada ya kupokea maoni ya mara kwa mara ka maelekezo nimekua toka hatua moja hadi nyingine katika uandishi. Na bado naendelea kujifunza siku hata siku. Kwani elimu daima haina mwisho!

    Kwa makala nyingi, nilipokea masahihisho toka kwa wanahabari ambao wamekuwa wakihusika kuchapa kazi zangu (hapa si MWANANCHI, narejea magazeti ambayo zamani nimekuwa nikiyaandikia, na kuwa karibu na baadhi ya waandishi) kuwa makala si muhimu sana kuandika vyanzo kwa kina kama tunavyofanya katika maandiko ya kitaaluma “academic papers” na ndiyo sababu kuu ya kutoweka.

    Kwa maslahi ya wengi kupata fursa ya kusoma kwa kina, naomba niainishe vyanzo vyangu hususan vya takwimu;

    1. MKUKUTA I
    2. MKUKUTA Annual Implementation Report 2009/10
    3. ILFS, 2001
    4. Tamko la Wanaharakati Wasio Wakiserikali, Wakati na Baada ya Uchaguzi 2010: Tanzania ipi tunayoitaka?
    ( http://www.corruptiontracker.or.tz/dev/index.php?option=com_docman&task=cat_view&gid=23&Itemid=44&lang=br)

    Pia juu ya hoja ya kutoanisha changamoto, ni kweli nililenga kufanya makusudi (kwani makala zinazofata zinalenga kuainisha kwa kina). Na naomba nikiri nilifanya makusudi!

    Ni kusudio langu kuandika kwa upana na kina juu ya tatizo la ukosefu wa ajira na fursa za kuzalisha kipato. Naamini ni eneo tete na pana sana. Makala moja tu haiwezi kusanifu kwa upana tatizo hili. Makala hii ya kwanza ilikuwa ni chokozo-ambalo limezaa mjadala wenye afya. Nashukuru sana.

    Kwa namna nyingine, simaanishi vijana wa kitanzania wapo kimya!simaanishi kiuhalisia hawaguswi na tatizo endapo mtu akisoma tena na tena makala yangu anaweza kuwa shahidi wa hili. Lakini ninachotaka kukionyesha hapa kiujumla utete wa tatizo ni tofauti na namna ambavyo linashughulikiwa. Kuanzia kwa waathirika wenyewe (kutopaza sauti zao-labda makala nyingine itaangalia kwanini sauti zao hazisikiki?) hadi kwa watunga sera na viongozi kwa ujumla kama wadau wa kuu wa kutakua kero za wananchi.

    Hayo ndiyo mawazo yangu binafsi juu ya andiko langu na mchango toka kwenu.

    Nashukuru sana kwa maoni mliyotoa, maswali hakika kwangu ni faraja sana kuona wasomaji wakiwa na mitazamo mipana na kutoa maoni kwa uhuru. Daima kila siku nipo darasani-hivyo leo ninyi kwa kiasi kikubwa mmechangia kitu katika uwezo wangu.

    Wenu,

    Michael Dalali

  10. Hoja ya 3. Misamiati:
    ““…imeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni..” (matumizi ya maradufu yanatia shaka iwapo ameitumia kwa maana yake rasmi au kimakosa akimaanisha ‘kiwango kikubwa’. Kama maana rasmi tunaomba chanzo cha takwimu hiyo)

    “Licha ya takwimu hizo, bado hazitoi picha ya kutosha ya uhalisia wa hali tete…” (picha ya kutosha haileti maana)”

    Binafsi nasimamia bado katika hii hoja na kuona uzito wake. Nitafafanua;

    Ukiangalia vyanzo vya kitakwimu, hata katika ripoti ya utendaji wa MKUKUTA I iliyotolewa mnamo Novemba, 2010! Bado kuna matumizi ya takwimu za nyuma sana. Mfano: ILFS, 2001!

    Naamini toka mwaka 2001hadi 2011 kuna mengi sana yamebadilika (iwe mabadiliko “hasi” au “chanya”) ambayo sidhani kama takwimu zinazowasilishwa na kuendelea kutumika zinabeba picha halisi.

    Uzito wa tatizo, nakiri sijafanya tafiti ya kisayansi ya moja kwa moja kudhibitisha, lakini naweza kupata hali kwa kuangalia ongezeko la idadi ya watu wanao achwa katika sekta ya ajira kama nilivyotanabaisha katika aya ya tano (5).

    Pili, pia ikumbukwe hali ya vyuo vya elimu ya ufundi na juu iliyokuwa miaka ya 2001 ni tofauti kabisa na ya 2011. Kumekuwa na ongezeko la vyuo, ambavyo vinazalisha wahitimu katika fani mbalimbali. Hawa wote sensa ikifanyika kujua wangapi wapo katika ajira na wangapi bado hawapo katika ajira naamini matokeo yatakuwa tofauti na ya takwimu za ILFS ya 2001.

    Hii ni misingi ya hoja zangu katika matumizi ya misamiati kama yalivyohojiwa na mchangiaji juu ya “3.Misamiati”!

    Takwimu iliyotumika katika aya ya kwanza (1) ya asilimia 65 ya nguvukazi inapatikana pia katika; Sera ya Taifa ya Vijana, 2007!

    Kuna mchangiaji ameomba nakala ya MKUKUTA, naamini MKUKUTA II ambayo nakala yake kwa sasa imeanza kupatikana mtandaoni itakuwa ya msaada;

    MKUKUTA II: http://www.povertymonitoring.go.tz/Mkukuta/MKUKUTA%20BOOK%20II%202010.pdf

    Nashukuru!

    Michael Dalali

  11. Dalali twende taratibu,

    Neno ‘maradufu’ lina shina kwenye neno la kiarabu ‘durufu’ lenye maana ya ‘to dublicate’ na hivyo neno ‘maradufu’ lina maana ya ‘to double’ au kwa Kiswahili chepesi ni ‘ mara mbili’

    Kiuandishi huwezi kutumia tarakimu kamili (to double) kutokana na dhana tu, kwa vile takwimu zilizopo ni za mwaka 2001.
    Bila ya shaka kuna mantiki ya kusema kuna ongezeko lakini hakuna mantiki ya kusema kwa uhakika kuwa ongezeko hilo ni mara mbili, kwani hakuna ushahidi wa hilo na kuna uwezekano wa kuwa labda ni mara mbili na nusu, mara tatu au mara moja nukta nne mbili pia. 🙂

    Kwa vile hakuna mantiki ya kutumia tarakimu kamili ikiwa hakuna ushahidi uliopelekea kufikia tarakimu hiyo kamili, ndipo nilipootea kuwa umetumia neno maradufu kimakosa ukimaanisha ‘kuna ongezeko kubwa’ na kutotumia maana yake sahihi kama ilivyoanishwa kwenye kamusu- ‘mara mbili’. Nikimaanisha kuwa umetumia msamiati ‘maradufu’ bila ya kujua maana yake rasmi.

    Juu ya hivyo kutokujua Kiswahili sanifu kwa mimi, wewe, SN au mwengine yoyote yule sio kosa japokuwa inaweza kuwa ni jambo la aibu, lakini kwa gazeti kama MWANANCHI kuchapa makala yenye makosa mengi hivi ni kosa na kutuvunjia heshima wasomaji.

    Tunafurahi kusikia wananchi wanashikirishwa kutoa maoni yao, lakini tunafurahi zaidi kuona viwango vinazingatiwa. Na ikiwa hawawezi kupitia makala za hao wananchi ili kusimamia viwango, basi ni bora wasiweke hizo makala kabisa.

    China ilimahanika ilipogundua kuwa kwa kila gazeti moja linalochapishwa kuna makosa 46 ambayo ni mengi mno ukilinganisha na nchi za Ulaya na Marekani (kumbuka Kichina standard kinatumia herufi 4,000 wakati Kiingereza kinatumia herufi 26 tu) na kufikiri kubadili mfumo wa masomo mashuleni, wakati hii makala moja pekee tayari ina makosa zaidi ya kumi (yapo makosa mengine mengi ambayo sikuyaainisha kwenye post yangu ya awali) kwa kuisoma chapchap tu.

    http://www.newsgd.com/culture/culturenews/200702060004.htm

    Kwako wewe kama mwananchi, unafikiri ni halali kwa gazeti kuchapisha makala zenye makosa hivi? Unafikiri makala zenye makosa zinapochapwa kwenye gazeti zinatoa ujumbe gani kwa kijana wa sekondari?

    *Nilipata kujifunza lugha moja ya kigeni zamani, na semester ya tatu ilikuwa ni kusoma magazeti tu. Nimekumbwa na fadhaa kuona mfumo huo kumbe hauwezikani Tanzania. 🙁

  12. Nashukuru kwa ufafanuzi wa neno “maradufu” (nina subiri kurejea vyema katika kamusi yangu ya TUKI-maana kwa sasa nipo mbali nayo kidogo)!

    Kama ulivyosema, lengo haswa kuonyesha uwezekano wa ongezeko kuwa hivyo sina tatizo kwa sahihisho la neno. Naridhia kabisa sahihisho hilo na kutumia neno kama; “ongezeko kubwa”! Endapo maradufu maana haswa ni mara mbili.

    Kwa upande mwingine juu ya Mwananchi kupacha makala. Ni kweli wahariri walipaswa kuiboresha. Sidhani kuna ubaya wananchi kuchangia endapo ikisahihishwa “fine tuned” vizuri na wataalamu wa tansia hiyo yaani wanahabari.

    Naamini matumizi ya lugha fasaha na upunguzaji wa makosa ya kilugha ni changamoto ya wote, yaani wasomaji, waandishi nk. Ni jukumu letu kuhakikisha tunajifunza kila siku na tunakosoana katika lengo la kujenga.

    Nashukuru sana kwa muongozo, narudia tena katika hoja ya awali niliyoitoa kwamba maoni yenu yananipa chachu kujifunza na kujisahihisha zaidi makosa ya mara kwa mara ninayo yafanya katika lugha ya Kiswahili.

    Lugha nyingine pia zinakumbwa na haya, ndiyo maana hata lugha ya Kiingereza ina kitabu cha “Common mistakes in English”! Lengo ni kuainisha makosa ambayo huwa watumiaji wa lugha ya kiingereza huyafanya.

    Nashukuru sana, usichoke kunishauri na kusaihisha kazi. Ningependa kupata baruapepe yako. Yangu: michaeldalali (at) yahoo (dot) com

  13. Wadau, najitokeza kwamara ya kwanza kuchangia katika mtiririko huu, nawapongeza wale wote amabo wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kiswahili hakiachi asili yake, lakini kwa dhati ya pekee nimpongeze mwandishi kwa uchokozi na pia unyenyekevu wake wa kukubali makosa nikiamini ana nia ya dhati ya kukua katika marekebisho kadhaa, lakini kilichonisikitisha ni kuona jinsi tulivyotumia muda mwingi kwa kuhukumu kitabu kwa kuangalia jalada…Ningependa tundelee kuchangia kwa uchokozi wa mwenzetu kuhusu tatizo la msingi, ambalo nadhani si lugha ya kiswahili bali ajira kwa vijana wa Kitanzania..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend