Five Questions with Grace Matata

Ukitafakari maana ya majina yake mawili basi unapata uwiano wa kipekee. Nitakupa mfano mdogo; kuna wale wenzangu na mimi ambao wanapenda kusikiliza Hip Hop. Lakini hii huleta “Matata” sana hasa kukiwa na watu wengi kwasababu sio wote wanapenda aina hiyo ya muziki. Njia pekee ya kutatua hilo tatizo ni kuleta “Neema” au “Grace” kwa kucheza nyimbo ambazo kila mtu anazipenda.

Nyimbo za Grace Matata hutuletea neema fulani hivi kwenye vichwa vyetu ambavyo husongwa na mawazo yenye matata lukuki. Sauti yake na vitu anavyoimba sio vitu vya kawaida kwenye masikio ya Watanzania wengi; na ukitulia na kumsikiliza kwa makini bila shaka unaweza ukasuuza fikra zako. Moja ya nyimbo zake maarufu ni ‘Free Soul’:

 

[audio:http://vijana.fm/wp-content/uploads/2011/06/Free_soul_Grace-matata.mp3|titles=Grace Matata – Free soul]

 

Pia ana wimbo mwingine unaoitwa “Nyakati”:

 

[audio:http://vijana.fm/wp-content/uploads/2011/06/Grace-Matata-Nyakati.mp3|titles=Grace Matata – Nyakati]

 

Ukiacha hayo, amekuwa akishirikishwa kwenye nyimbo za wasanii wengine wanaofanya aina tofauti ya muziki. Mfano mzuri ni wimbo “Rafiki”  wa Stereo:

 

[audio:http://vijana.fm/wp-content/uploads/2011/06/Rafiki-feat.-Goapele-Grace-Matata.mp3|titles=Stereo ft Goapele & Grace Matata – Rafiki ]

 

Baada ya msako wa muda mrefu sana, tulifanikiwa kumpata Grace na hakusita kutupa mwenendo wa shughuli zake…

 

1. Kati ya vipaji ambavyo vimezaliwa Bongo, nadhani wewe una “upekee” wa aina fulani. Sauti yako ni [kama] ya waimbaji wa “soul”, kitu ambacho ni adimu sana Tanzania. Wewe binafsi unajichukuliaje? Na uligunduaje kuwa unaweza kuimba kwa mtindo huu?

Blessed!! Hivyo ndivyo ninavyojichukulia inapokuja kwenye suala zima la sanaa na muziki, na tofauti niliyonayo kwenye music scene ya hapa nyumbani. Ni baraka. Nilibarikiwa kupata exposure ya muziki ambao ni tofauti kidogo tokea nikiwa mdogo. Kwa hiyo, huwa najichukulia kuwa niko blessed tu…

Kuhusu jinsi nilivyojua kwamba nina uwezo wa kufanya aina hii ya muziki; siku zote nimekuwa navutiwa na waimbaji wa kike wenye “deep, strong, soulful voices”, ambao wanapiga au hutumia ala zozote za muziki. Nakumbuka makabrasha yangu ya mwanzo kabisa yalikuwa na nyimbo za Tracy Chapman, na baadae Chris Pureka n.k. Hivyo nimekua huku nikiamini kwamba hiyo ndio aina maridhawa kabisa ya uimbaji na uandishi. Simple, rich soulful tunes na melodies na mashairi mazuri. Nikaja kugundua uwezo wangu wa kufanya aina hii ya muziki kipindi hicho na nimekuwa naimba hivi ever since I can remember!

2. Kama msanii yoyote nchini, nina uhakika umepitia changamoto nyingi mno. Unawashauri nini vijana watakaopenda kufuata nyayo zako (ingawa safari yako bado ni ndefu)? Kuna kitu chochote ambacho ungependa kuwashauri wadogo zetu wa kike?

Ndiyo, safari bado ni ndefu kwa kweli. Najifunza vitu vipya kila siku, na kadri ninavyojifunza zaidi ndio natambua kwamba huu ni mwanzo tu. Na mwanzo ni mgumu. Ila kupata ule ujasiri tu wa kuanza kufanya kitu unachokipenda ndio wasanii wapya wanatakiwa kufanya. Kuwa jasiri, kujua nini wanataka kufanya, kuwa makini, kujiamini na wanachokifanya, na kujipa changamoto kila wakati na kuelewa kwamba sio rahisi hata kidogo kufikia ndoto zako, lakini mwishoni unaweza kuja kuvuna ulichopanda.

Nimekuwa msichana na sasa naweza kujiita mwanamke; na kwa kweli, hizo hatua mbili au hivyo vipindi viwili sio rahisi. Kuwa mtoto wa kike kwenye zama hizi ni jambo gumu sana; ni changamoto. Mimi binafsi nilibahatika — naweza kusema — kukua kwenye miaka ambayo maisha hayakuwa as complicated kama sasa. Lakini bado ilikuwa ni changamoto. Kwa hiyo sasa hivi kitu ninachoweza kufanya ni kufikiria tu changamoto zinazowakuta kina dada sasa hivi.

Ushauri wangu mkubwa kwa wadogo zetu wa kike (wawe wasanii au la) ni kujaribu kujijua mwenyewe. Jitambue. Jua nafasi yako, thamani yako na uwezo wako. Kila kukicha naona watoto wengi wakifanya maamuzi mabaya sababu tu bado hawajajitambua. Kuna rafiki yangu anapenda sana kusema, “Utoto sio Ujinga”. Kwa sababu tu wewe ni mdogo haimaanishi una kibali cha kuwa mjinga. Take control.

3. “Free Soul” ni wimbo ambao nadhani sitakosea nikiuchukulia kama classic. Nani aliandika yale mashairi? Nani alibuni mpangilio wa ala n.k.? Unaweza kutupa mtiririko mzima kuanzia utunzi hadi wimbo kusikika kwenye vituo vya redio?

Nadhani ndoto ya kila msanii ni kufanya kazi ambayo inawagusa watu wengi sana kwa muda mrefu. Na kwa watu kusema ‘Free Soul’  ni classic hiyo ni heshima kubwa kwangu; asante!

Grace Matata ni muimbaji na mtunzi (singer/songwriter) na kama nyimbo zangu zote, mashairi ya ‘Free Soul’ niliandika mimi. Mpangilio mzima wa ala ulifanywa na Duke akishirikiana na Willie HD, ambaye ni producer wangu na amefanya mpangilio wa nyimbo zangu zote tatu: Wimbo, Nyakati na Free Soul. Naweza kusema Willie HD is ‘my premo’, anajua nini nataka na tuna chemistry nzuri ndani ya studio.

Nadhani mtiririko mzima wa utunzi mpaka kazi kufika redio unategemea na msanii mwenyewe. Kwangu mara nyingine unapewa beat/instrumental, unaandika mashairi kisha unarekodi, halafu mwishowe unapeleka kazi yako kwenye vituo vya radio. Au unapata wazo ambalo unampelekea producer wako kisha wote mnakaa kuangalia mnaweza kufanya nini. It sounds so simple, ila I know better.. Haha!

4. Unadhani utakuwa wapi baada ya miaka mitatu au mitano? Una mipango gani ya kutumiza ndoto zako?

Niko chuoni kwa sasa. Nasomea digrii yangu ya kwanza ya mambo ya ushuru IFM, mwaka wa pili. Baada ya mwaka hivi ninategemea nitakuwa nimemaliza chuo… Ndani ya miaka mitano najiona nikiwa “mkubwa” na “bora zaidi” kama mtunzi, muandishi na muimbaji. I dream to be the biggest female recording na performing artist from Tanzania. Uongozi au management yangu ni changa na haina uzoefu sana ila iko makini sana na inakua pamoja na mimi. Wanaelewa aina ya sauti tunayoitaka na wako tayari kuilea na wanaamini ninachokifanya.

Mpango wangu ni keep doing what I do the best way I know how to.

5. Najua kwamba unasuka albamu sasa hivi; ambayo tunaisubiri kwa hamu! Unatuahidi nini? Na umejipangaje kujitangaza nje ya nchi (kwasababu una ‘potential’ kubwa sana ya kufanya vizuri nje ya Tanzania)?

Ndio! Najua album imekuwa inasubiriwa sana. Katika mwaka uliopita au zaidi mambo mengi yamekuwa yanaingiliana, na kikubwa zaidi ni shule… Album itaitwa “Nyakati”. Ninachoweza kusema ni itakuwa ni Grace Matata, at a personal level. It is so honest and raw. Kila wimbo una hadithi yake, na mpaka sasa nyimbo zote nimeziandika mwenyewe. Itakuwa ni vitu nilivyopitia ndani ya hii miaka miwili. The good, the bad, the lessons etc.

Kuhusu huipromete nje, hilo ndio suala hasa tunalo jaribu kulitafutia njia. Mpaka sasa internet ndio imekuwa rafiki yetu mkubwa. Social networks zimekua zaidi ya sehemu ya kukutana na kubadilishana mawazo na mashabiki. Mtandao wetu sio m kubwa sana, ila tunaamini support tuliyo nayo kutoka kwa media, kama Vijana FM na watu wengine tunaoendelea kuongea nao, itasababisha mafanikio katika suala zima la promotion.

Timu nzima ya Vijana FM inapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Grace kwa kukubali kuhojiwa nasi. Tunamtakia kila la heri kwenye shughuli zake na tutakuwepo kumsaidia kufikisha muziki wake mbali zaidi.

Kama unaishi ughaibuni tunakuomba uwakalishe kitako marafiki zako na uwasikilizishe nyimbo za Grace!

Makala nyingine:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 4 Comments

4
  1. nyimbo ya “nyakati” ni kitu kingine. Nilikuwa ninamwangalia Ms. Matata kwa mabli, lakini baada ya hii interview na kusikia “nyakati”, duh!..hongera zako Grace.

    Nimefurahi kuwa kuna vipaji vinaongezeka, kwani wengine tulianza kuchoka kusikia wanamuziki hao hao wa kike kila siku, na aina hiyo hiyo na muziki. This is a breath of fresh air….

  2. nimefurahishwa na Grace kwa kujipatia ‘niche’ yake mwenyewe Tanzania. Nadhani kwa sasa unaongoza njia kwenye muziki wa soul nchini. jitahidi kucheza na mtandao, hasa youtube.com na facebook, aina hii ya muziki ni rahisi sana kupendwa nchi za nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend