Harufu ya Kifua Kikuu (TB)

Kilimota kama 5 hivi kutoka Morogoro mjini, pembezoni mwa mlima Uluguru, kuna shule moja maalumu yenye wanafunzi wenye vipaji. Wanafunzi hao, viumbe ambao jamii tunawachukia kwa udi na vumba, wanapata elimu ambayo yaweza kusaidia katika mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Viumbe gani hawa? Ni panya buku. Wanasayansi wa chuo cha Sokoine na wenzao wa Ubelgiji wameanzisha utafiti wa kuwatumia panya ili wawe na uwezo wa kuaguza (to diagnose) TB.


Nchi yetu ni moja ya nchi zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa TB. Hali hii imezidishwa hasa kutokana na tatizo la Ukimwi tunalopambana nalo, kwani wagonjwa wengi wa Ukimwi wanakuwa pia na TB. Uaguzi wa mapema wa TB ni muhimu ili kuweza kudhibiti ugonjwa kabla haujawa sugu. Kwahiyo, changamoto iliyopo ili kupunguza vifo na taabu ya ugonjwa huu ni kuutambua mapema mno.

Njia mbalimbali zinatumika sasa kuaguza TB, mfano vipimo vya kukuza vinasaba (PCR), X-ray, kupima ukohozi kwa microscopy, vipimo vya ngozi n.k. Tatizo ni kwamba, vipimo hivi ni ghali na upatikanaji wake ni wa shida katika hospitali na zahanati zilizopo vijijini, sehemu zenye waathirika wengi. Jambo lingine ni kwamba, utumiaji wa microscopy, njia ambayo inatumika kwa wingi Afrika haina usahihi wa hali ya juu (kati ya 20-40%).

Tukirudi Morogoro, watafiti wamejaribu kutumia uwezo wa panya buku kunusa harufu adimu na kuutumia katika kugundua TB. Yasemekana kuwa, bakteria wanaosababisha TB, Mycobacterium tuberculosis, wanatoa harufu ya kemikali fulani (volatile organic compounds) ambazo zina pattern fulani. Wanachofanya ni kuwapa sample ya kohozi kutoka kwa muathirika na kumfundisha panya kugundua kwa uimara harufu hizo. Uwezo wa panya hawa kugundua TB ni mkubwa (zaidi ya 85% specificity na sensitivity) na cha kufurahisha ni kwamba, panya buku wanaweza kufundishwa kukumbuka hizi harufu. Mradi huu, ulioitwa APOPO ni wa kipekee kwani unatumia rasilimali tulizonazo ili kukabiliana na matatizo yetu.

Ni changamoto kwa vijana wetu kuweza kutumia njia mbadala katika kupambana na matatizo yanayotukabili. Wanafunzi wa umeme na kompyuta wanaweza sasa kushirikiana na hawa wa Apopo ili kuweza kutengeneza vifaa portable ambavyo vitatumika hospitalini. Hii ni katika kuendeleza tafiti.

Previous ArticleNext Article
Joji was born and grew up in Dar es Salaam, Tanzania. He graduated with a B.Sc in Biochemistry in Germany, and is now pursuing a Masters degree in Microbiology & Immunology at the Swiss Federal Institute of Technology (ETH) in Zurich, Switzerland . Joji is particularly interested in matters related to global health, and basic science research that tackles public health challenges. He is engaged in mentoring Tanzanian students in higher education issues, most notably at the Kibaha High School. In this capacity, Joji blogs with Vijana FM about scientific research and development, and how youth can gain greater access to higher learning.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend