Hatuna Kiongozi…

…pale maji yanapotufika shingoni Vijana wa Tanzania.
Kuna mambo ambayo hujiri na yataendelea kujiri kwenye jamii yetu kila kukicha. Baadhi ya mambo huhitaji hatua muhimu kuchukuliwa; kuanzia mijadala, mipangalio hadi maamuzi ya nini kifanyike kuweka mambo sawa kufuatana na matakwa ya wengi. Mengi sana yametokea nyumbani kwenye mlongo uliopita lakini inaonekana Vijana wengi tumesahau nini Shaaban Robert alichotuasa. (Kama ulikimbia umande, naongelea suala la viongozi na wananchi kujitoa mhanga lilojadiliwa kwa kina kwenye kitabu cha “Kusadikika”.) Inaonekana wengi wetu tulisoma na kukariri sentensi kadhaa tu ili tusifeli mitihani ya Kiswahili.

Ukijaribu kujikumbusha mambo kadhaa yaliyotokea – hasa rushwa na ubadhirifu – utaona kuna kama mtiririko fulani unaotabirika: Tunaanza kwa kupiga kelele, kuendelea kupiga kelele, kupiga kelele zaidi, kuwalaumu viongozi wetu, halafu mwishowe ‘tunasahau’ kabisa. Sasa jaribu kujiweka kwenye nafasi ya madaraka halafu upenyo wa kujilundikia mali unajitokeza. Naamini fika kuwa wengi wetu tutaishia kuwa mafisadi! Hii hutokana na kutokuwa na mkwara tosha; mafisadi wengi wanajua Watanzania ni watu wenye hulka ya upole na tusiojua kupigania haki zetu.

Ukiangalia kwenye vyombo vyetu vya habari na kufuatilia mijadala inayoendelea kwenye forums na blogs mbalimbali utaona kuwa hatuna viongozi. Hakuna watu wanaoweza kuwasihi na kuwapa motisha watu kupigania haki zao (hata zile za msingi). Na cha kusikitisha zaidi hatujadili kabisa “nini kifanyike” na kubaki kutapatapa kwenye maji ya kina kirefu! Lakini kuna dalili kuwa Vijana wanaanza kuamka, ila kwa mwendo wa kinyonga.

Wengi bado wanaendelea kumlaumu Mwalimu na Siasa ya Ujamaa. Lakini, angalau alikuwa ana ndoto zake ambazo aliamua kuzipigania. Alijitoa mhanga na juhudi zake na uwezo wa kutuunganisha zimetufikisha hapa tulipo na kutupa misingi ya Taifa letu kwa ujumla. Hata kama hukubaliani na Siasa za Ujamaa na Kujitegemea, nitashaanga sana usipoafiki kuwa alikuwa ana hulka ya kiongozi – kuwakutanisha watu na kuwapanga ili kufikia lengo fulani. Natamani sana tungekuwa na watu kadhaa kama Mwalimu waliokuwa na mitazamo tofauti.

Angalia kushoto, kisha kulia, halafu niambie ni nani ambaye anapaswa kupewa heshima na kuangaliwa kama kiongozi wa Vijana. Bila shaka majina kama Kabwe na Slaa yatakuwa kwenye vinywa vya watu. Lakini sidhani kama kuna mtu ambaye tunaweza kumchukulia kama taswira ya Vijana wa Tanzania.

Binafsi naamini kuna watu ambao wanaweza kuwa viongozi na kutusaidia Vijana pale tunapokumbana na vizingiti. Lakini labda imani yao kwa Taifa, hasa Serikali, ni ndogo kuliko punje ya mbegu ya mchicha kutokana na sababu mbalimbali.

Nakusihi Kijana kutojificha kama unadhani una uwezo wa kuwa kiongozi kwani Tanzania inakuhitaji (sio lazima iwe kwenye Siasa).

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend