Unapenda Mpira kuliko Elimu?

Jezi za timu zetu zilikuwa hazina majina ya wachezaji migongoni (na tunajua kwanini ilikuwa mwiko kwa wachezaji kubadilishana jezi baada ya mechi!). Lakini kila mtu – hasa mabeki wa vilabu Afrika Mashariki nzima – walikuwa wanajua kuandika “Edibily Jonas Lunyamila” kwa ufasaha. Ndio, jina la yule winga machachari aliyekuwa anatumia guu la m@#i! Hakika alitingisha Afrika Mashariki alipokuwa anavaa uzi wa njano.
Wengi tulikuwa tuna ndoto za kuwa kama Lunyamila, Mohammed Hussein “Mmachinga”, Thomas Kipese “Uncle Tom”, Kizota, Gagarhino…Nilishawahi kuota nawapiga ‘matobo’ mabeki kama Lunya; kupiga mashuti kama Chinga; kuteleza kwenye chaki kama Kipese; kupewa kadi nyekundu baada ya kupiga mabeki ‘vipepsi’ kama Kizota; na kuchana nyavu kama Gagarhino (hivi ni kweli jamaa alichana nyavu alipopiga penati dhidi ya timu ya Sigara?)! Tafadhali usiniulize ndoto zangu zimefinifikisha wapi – maana’ke itanibidi niandike kitabu ili kujibu hilo swali tu!

Kutokana na sababu mbalimbali baadhi ya wachezaji waliamua kusitisha masomo yao ya sekondari ili kujiingiza kwenye kabumbu ya ridhaa Tanzania. Sina uhakika, lakini kulikuwa na tetesi kuwa mmoja wa wachezaji maarufu aliingia kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga wakati yupo kidato cha tatu na kuamua kuachana na shule baada ya ‘kuhitimu’ kidato cha nne.

Ndoto za kizazi cha sasa zimebadilika. Sasa hivi Vijana wana ndoto za kucheza mpira wa kulipwa nje ya nchi, hasa Ulaya. Sipingi kuwa Bongo kuna vipaji vingi sana, lakini huwa nashtuka pale Kijana anapoamua kuweka vitabu pembeni ili kujaribu kutimiza ndoto zake. Kwa kifupi, vikwazo ni vingi sana kwenye safari ya kuwa mchezaji wa kulipwa. Ukiangalia safari za Vijana wengine kutoka nchi mbalimbali waliofanikiwa utakubaliana nami kuwa ni kama kamari. Kuna kujeruhiwa, suala la kupata timu inayokufaa na kocha ambaye atakufanya ujiamini, na muhimu zaidi kuliko vitu vingine vyote ni kuwa utahitaji bahati sana.

Siwezi kuweka wachezaji chipukizi wote kwenye kundi moja; lakini itakuwa ni jambo la busara sana kutokimbia umande hadi pale utakapokuwa na uhakika kuwa utafanikiwa kwenye mpira wa kulipwa.

Pia, mawakala, makocha na watu waliokuwa karibu na wachezaji wenye ndoto za kusakata kabumbu Ulaya hawana budi kuwapa picha halisi na mawaidha ya busara kama The Right to Dream Academy ya Ghana inavyofanya.

Tunajua wapi wachezaji wengi wa Tanzania walipoishia na wanapoishia. Lakini, unadhani labda mambo yangekuwa tofauti kidogo kama wangejaribu kujiendeleza na mambo mengine? Bila shaka wangekuwa na fani nyingine baada ya kumalizana na mpira – hasa ukizingatia mpira wa kulipwa ni kazi ya miaka kumi hadi kumi na tano tu.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend