Tanzania na allergy ya Hisabati

Somo la Hisabati ni gonjwa sugu linalowasumbua wanafunzi wengi Tanzania kuanzia shule ya msingi na kuendelea. Nadharia hii ya ‘ugonjwa’ imekithiri kiasi kwamba ninadhani inabidi wakati umefika tupambane nao kwa nguvu za zaida kama gonjwa lolote linalotishia ustawi wa Taifa letu.

Mwaka jana katika mtihani wa darasa la saba, wanafunzi karibia 800,000 (kati ya 999,070) walifeli mtihani wa hisabati. Tukiendelea kwa staili hii, hao wakaguzi/wasimamizi wa hesabu, wachumi, wahandisi, wanasayansi tunaowategemea watuvushe katika karne hii watatokea wapi?

Mapungufu yaliyopo ni mengi, na sihitaji kuyaorodhesha hapa. Ila mapungufu haya yanaweza kutatuliwa, ni nia tu. Ni kwa kujumuisha mawaidha ya walimu, Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), NGO, wazazi, na wanafunzi wenyewe ndipo tutaweza kupata suluhisho zuri kuhusu mustakabali huu. Elimu ya hisabati inahitaji zaidi ya idadi ya walimu, au majengo. Tunahitaji kufahamu ni taifa gani tunataka kujenga ili tuwe washindani katika karne hii, na hivyo nia yetu hii itusaidie basi  kubadili mfumo wetu wa ufundishaji hisabati sasa.

Je, tuwafundishe vipi wanafunzi? La msingi ni kuwawezesha walimu wa somo hili, kimaslahi, na kimafunzo. Inabidi walimu wahamasishwe  ufindishaji shirikishi darasani, mfano kupitia mazoezi ya makundi, au project ndogo ndogo ambazo wanazifuatilia pamoja na kutumia nyenzo mbadala (mfano:  jiulize ustadi wa kuweza kukitumia kitabu cha log kina manufaa gani katika juhudi za mwanafunzi kutafuta maana katika shughuli za kila siku?)

Itabidi pia tuufume mtaala wa hisabati katika ngazi zote ili umuwezeshe mwanafunzi aweze kufikiri kwa kutumia hisabati au kutumia hisabati kufikiria. Kwa namna hii mwanafunzi aweze kuchanganua changamoto zozote anazokutana nazo nje ya darasa zinazohitaji uelewa wa kawaida wa hisabati ili, kwa mfano, aweze baadaye kuwa jasiri kuuliza maswali pindi anapoletewa takwimu zisizohalali (kama zile takwimu wanazotoa baadhi ya wanasiasa wakati wa uchaguzi kuhusu uchumi au ukuaji wa hiki na kile.)

Nia yetu ni baadae Tanzania iwe nchi ya kujitosheleza katika viwanda, sayansi na teknolojia na hivyo ili tufike huko, inabidi tuongeze idadi ya wanaoendelea na matumizi ya kitaaluma ya hisabati katika ngazi za juu. Aina ya mchujo tunaoendelea nao kwa sasa wa wengi kufeli mapema hautatufikisha tutakapo.

Ninadhani pia ni jambo zuri kuendeleza vipaji vya wale wanaomudu somo hili shule za msingi na sekondari, na hapa suala la mashindano linakuja. Ni kawaida kusikia makampuni makubwa nchini yakifadhili kwa mamilioni ya fedha mashindano ya urembo na vipaji vya kuimba – mfano, miss Ustaken’cheke, miss Bantu, miss Uwanja wa Fisi au yale ya kumtafuta nyota wa kuimba. Je, haitakuwa vyema basi tukiona ufadhili wa aina hii pia kwenye mashindano ya kitaifa ya Sayansi au Hisabati? Miaka ya nyuma yalikuwepo kimtindo, ila baada ya ufadhili kutoka wizarani kufutwa, mashindano ya kitaifa kwa ajili ya ushiriki wa mashindano ya Hisabati ya kimataifa yakafa.

Nchini Ghana kila mwaka kuna mashindano makubwa ya Sayansi na Hisabati kati ya shule za sekondari nchini humo. Mashindano hayo yanaonyeshwa kwenye televisheni kila Jumamosi ya wiki, na huwezi amini umaarufu wake — nchi nzima inafuatilia, wakubwa kwa watoto. Makampuni makubwa yanafadhili mashindano haya kwa kiasi kama tunazoziona kwenye mashindano Watanzania tunayoshabikia ya u’miss. Baadhi ya wanafunzi wanaoshiriki baadaye wanakuwa macelebrity dizaini ya akina Kanumba, au Aunt Ezekiel. Na ingawa wachache wanashiriki, wanafunzi walio katika shule za msingi wanapata motisha kubwa kuwaona wakubwa wao walio sekondari wakishindana ustadi katika Hisabati na Sayansi. Kwa njia hii wengi wanakuwa inspired, na kwa namna moja au nyingine maono ya mashindano yanawasukuma kujitahidi kumudu masomo hayo wanapoenda mashuleni. Ingependeza kuona kitu kama hiki Tanzania, ili nasi wanafunzi wetu wawe na ndoto nyingine zaidi ya kutaka kuwa warembo wa kitongoji fulani au mkali wa rhymes. Taifa lenye muelekeo linatakiwa kuwa na usawa wa idadi ya wanataaluma mbali mbali (akina Ole Moiyoi wakutosha, akina Shayo kadhaa, akina Magese kiasi, na akina Kanumba kadhaa).

Je, haitakuwa faraja kusikia Mtanzania akipeperusha bendera katika mashindano ya Afrika nzima ya Hisabati (PAMO), au yale ya kimataifa (International Mathematics Olympiad)? Tukijenga katika jamii yetu mila ya udadisi, na ushindani wa masuala ya kisayansi na hisabati ninadhani matokeo yake yatakuwa chanya na tutajenga taifa jasiri la watakaoleta masuluhisho ya matatizo yetu ya umasikini.

Tunapiga hatua katika elimu ndio, ila hatua za kobe ni tofauti na zile za swala. Tujenge taifa litakaloongoza.

  • Chama cha Hisabati Tanzania kinafanya mkutano wake mkuu wa 45 pale Sokoine University of Agriculture (SUA) (Solomon Mahlangu campus) Septemba 13 – 18 2010
  • Ukitaka kufahamu zaidi kuhusu Chama Cha Hisabati Tanzania bofya hapa
  • Kwa taarifa zaidi kuhusu mashindano ya Hisabati Afrika bofya hapa
Previous ArticleNext Article
Joji was born and grew up in Dar es Salaam, Tanzania. He graduated with a B.Sc in Biochemistry in Germany, and is now pursuing a Masters degree in Microbiology & Immunology at the Swiss Federal Institute of Technology (ETH) in Zurich, Switzerland . Joji is particularly interested in matters related to global health, and basic science research that tackles public health challenges. He is engaged in mentoring Tanzanian students in higher education issues, most notably at the Kibaha High School. In this capacity, Joji blogs with Vijana FM about scientific research and development, and how youth can gain greater access to higher learning.

This post has 8 Comments

8
  1. Just one quote:

    We are standing at the threshold of the 21st Century, a Century that will be characterised by competition. It is clear, therefore, that it will be a Century dominated by those with advanced technological capacity, high productivity, modern and efficient transport and communication infrastructure and, above all highly skilled manpower imbued with initiative. If we are to be active participants in the global developments of the twenty-first century we must, as a Nation, find ways of improving and strengthening ourselves in all these areas.
    B. W. Mkapa, Foreword, Tanzania Development Vision 2025

    …Ya kwangu,
    Mi bwana naona kuwa we have to really sit down, and identify our priorities and within those, move like a one way train, no turning back, to left or to the right, mpaka kieleweke!

    Hapo itakuwa rahisi hata kufanya mapinduzi ya kielimu, kisiasa n.k. But if we move on with the rhetorics on paper, we shall reap nothing!

  2. Kabla hata ya kuanza kuangalia vipaji na kuweka mashindano, naomba wadau wa browse kwenye internet kuangalia picha za madarasa ya watoto wa shule za msingi, maana baada ya hapo ndipo kama mtajua kama muhimu ni kuangalia vipaji na mashindano au kuwajengea hawa watoto madarasa, vyoo, kuwapa madawati na walimu! Ndio walimu!
    Hatuwezi kuanza kukimbia kama wenzetu walioendelea wakati badao tunatambaa!
    Sijui kwanini wabongo hatupendi ku simplify mambo yetu, watoto hawana madarasa wala walimu, halafu sie tunafikiria kutafuta hivyo vipaji! Inashangaza kweli kweli.
    Ni kama wale wanandoa, hawana nyumba wala gari, lakini io sherehe yao bwana! Sio chin ya 50m/-! Lakini watu hawajali, wao ni kuangalia vya karibu kila kukicha.
    Mifano kama hiyo iko mingi maishani kwetu wbongo, mpaka siku tutako simplify mambo yetu, kuangalia, kupanga na kuamua yapi ni maana kufanya kabla ya kukimbilia lingine, basi tutaishia kusema, bongo New York!

  3. Nionavyo, ni vyema kuwa umeliona hilo la hali duni ya madarasa na ukosefu wa walimu. Shukrani.

    Ila, jambo muhimu la kuelewa ni kwamba sikumaanisha hapa kuwa suala la vipaji liwe kipaumbele pekee. Hilo labda liwekwe bayana tena. Nimeamua kuongelea suala la vipaji, kwasababu ninadhani ni njia nzuri ya kujenga mila ya kiushindani kwa jamii yetu, na ushindani hata siku moja si jambo baya. Nimeliongelea kiundani kwasababu ushindani mwingi Tanzania ni kwenye masuala ya sanaa pekee. Sio kwamba sanaa ni jambo baya, ila nimependekeza pia tuwe na mtazamo wa kuwa na ushindani kwenye masuala ya elimu pia, despite our backwardness in that sector.

    Ninaimani kuwa vyote vipewe kipaumbele; kuongeza madawati, kuongeza walimu, mishahara yao, kubadili mtaala, kuhimiza quality ya elimu pamoja na kuendeleza vipaji vya wanaomudu somo. Sidhani kuwa eti kwa kuwa tuna ulakini kwenye jambo basic kama ukosefu wa madawati, basi tusifikirie sambamba njia zisizo simpo kama namna ipi ya kuendeleza vipaji. Inamaana kwasababu tu elimu yetu ya msingi ni duni, basi hata tusiwe na fikra kwa mfano za kuimarisha ushindani wetu kwenye utafiti kwa ‘kupampu’ pesa zaidi kwenye suala kama la research & development kwenye vyuo vyetu? Yaani, tusubiri mpaka pale tutakapokuwa na uimara wa shule ya msingi na sekondari ndipo tuanze kufikiria elimu ya juu!

    Nimeelezea vipaji ili kuweka bayana kuwa TZ kuna vipaji vya Hisabati vingi tu na hivina budi kuonekana kama vipaji vingine vile tulivyonavyo nchini. Kwahiyo vipaji sio kuwa tunavitafuta, ila vipo. Jambo ni kuweka effort kwa pamoja na sambamba kwenye matatizo tuliyoainisha na hili la vipaji ili kiujumla kuwe na progress.
    Na vipaji pekee sio suluhisho. Infact ni wachache tu watakuwa wanahusika – ila ukitokea mpango kama ule wa Ghana ni wengi watahusika na kunufaika kwa mashindano ya vipaji.

    Bongo si New York, na wala haitakuwa NY. Sidhani kuwa tunatakiwa tuwe na mtazamo wa kuiga yanayofanywa nje kila mara. Suluhisho la suala la elimu yetu (na zaidi umasikini) litabidi liwe la kitanzania. Ila sidhani kuwa ni vyema kuweka mipango kama vile dunia ya nje ya Tanzania haipo, au haina umuhimu wowote. Ghana ni masikini, Kenya, na Zimbabwe pia ila suala la vipaji wanaligusia.

    Suala la elimu lina changamoto nyingi. Na suluhisho litatokea pindi umaskini wa nchi hii utakapokufa. Na hili sio kesho, au keshokutwa. Suluhisho litakuwa multidimensional, lakini tukumbuke dunia nzima haitatusubiria.

  4. Nina mtazamo tofauti kidogo na wachangiaji waliopita. Na nitaongelea mambo kutokana na uzoefu wangu wakati nasoma shule ya msingi Chang’ombe.

    Kwanza, nina uhakika mwandishi anajua matatizo ya kutokuwa na vifaa mashuleni, walimu wa kutosha na kadhalika. Lakini hapa anazungumzia kufundisha watu na kukuza vipaji vya watu kwenye masomo kama hisabati na sayansi; na amefanya vizuri sana kutoa mifano na hata kutupa mawazo yake.

    Pili, tusijidharau au tusidharau maoni na mawazo yetu, kama vijana. Personally, I refuse to hear anything from anyone (hata Obama!) that undermines my potential — as a TZ youth. (Ingawa hii haihusiani na mjadala, kuna ‘viongozi/wabunge’ – angalau – watatu ambao wanatembelea hii tovuti.. huwezi kujua, maoni yako yanaweza kuingia kwenye fikra zao. Hakuna mtu anayejua kila kitu. Pia, kuna makala mbili kutoka hapa ambazo zimechapishwa kwenye magazeti na majarida. Kwa maneno mengine, baadhi ya maoni labda yameweza kufika kwa Watanzania zaidi ya 100,000.)

    Ukiangalia mambo yanavyoendelea kwenye siasa na uongozi kwa ujumla, utakubaliana nami kuwa kuna ‘kavita’ baridi kati ya kizazi cha wazee wetu na sisi. Bahati mbaya au nzuri, kila kijana anayetaka kuchukua hizo nafasi anatakiwa kudhihirisha kuwa anaweza kuwa kiongozi. Hilo halina mjadala.

    Lakini cha muhimu kwangu ni hiki: Ninafahamu watu wanaotembelea hii tovuti. Wengi ni wanafunzi wanaosoma Tanzania na nchi nyingine, na nina uhakika wengi tu watashikilia nafasi nyeti kwenye sekta mbalimbali hapo baadae. Kwahiyo, ni muhimu kupeana changamoto na kuwa na mijadala ya kina — Hatuwezi kuwa tunalaumu Serikali kila tukiamka ili hali tunajua fika Serikali yetu haiwezi kutekeleza kila kitu.

    Ninachojaribu kusema ni hiki: Kuwa na mawazo mazuri sio rhetoric tu (mindset ya watu haiwezi kubadilishwa na kauli moja tu kama, “Kijana amka! Wewe ndio utakuja kuwa kiongozi baadae!” Hii huchukua muda mrefu sana, hasa kwenye nchi kama yetu. Tanzania.)

    Hivi, tumefikiria labda hakuna mtu yoyote aliyeenda kwenye haya makampuni kuwaomba wadhamini mashindano kama yaliyotajwa hapo juu? Tunasubiri Serikali? Kwanini tusifikirie kitu kama hiki, tukae chini, tujipange na kuanzisha haya mashindano? Kusema ukweli, wenzangu, mimi binafsi nimelifikiria hili suala kwa kina leo asubuhi. Na naapa kuwa, kama kwenye miaka kumi ijayo hakuna mtu atakayeanzisha hii kitu, MIMI BINAFSI NITALIFANYIA KAZI.

    Haya mashindano yana faida kubwa. Fikiria, kijana akiwa anakokotoa swali la hesabu kwenye ubao huku Watanzania wote wakiangalia. Kwa mfano, unadhani ni wanafunzi wangapi watajifunza au kujikumbushia kuwa: eneo la duara = pai x nusu kipenyo x nusu kipenyo?

    Mimi nilipata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano ya taaluma (UMITASHUMTA) kwenye wilaya ya Temeke. Mashindano yalikuwa yanafanyika kwenye shule ya Wailesi. Shule shiriki kutoka Tandika Mabatini, Mgulani, Kurasini, Temeke, Mbagala… Siwezi kusema sasa hivi kuwa nilifaidika sana, ila ilinipa changamoto ambayo labda imenifanya nipende hisabati na sayansi. Kama nilifanya vizuri wakati ule (ulizia shule za Temeke zilivyo!), kwanini nisiendelee kufanya vizuri??

    Miaka lukuki baadae, “nikabahatika” kushinda zawadi ya Fizikia Dar na mkoa wa Pwani (Mock Exams)! Miaka lukuki mingine baadae, nafanya PhD ya Fizikia! Coincidence?… Amua mwenyewe. Nimesafiri na nimekutana na vichwa kutoka kila kona ya dunia kwenye hilo somo. Nawaheshimu sana, lakini sitishiki ninapokumbuka kuwa Watanzania waliniamini na kunitunuku ile tuzo ambayo ni ndogo tu. Sana.

    Vitu kama hivi vina faida kwa Watanzania? Huo ni mjadala mwingine (ila jibu langu ni NDIYO). Nafahamu Watanzania ambao wako fiti kwenye hesabu na sayansi.. Lakini wameshindwa kukuza vipaji vyao. Nina uhakika baadhi sasa hivi wangependa kuviendeleza.

    Haya, naacha rhetoric.. Kama nilivyosema, baada ya miaka kumi, kama hakuna Mtanzania atakayejitokeza na kulifanyia kazi hili, mimi binafsi nitalivalia njuga. Mashindano yataanzia mikoani, halafu kanda, na fainali zitakuwa zinafanyika kwenye miji mikubwa (Arusha, Dar na Mwanza). Hela nina uhakika zitapatikana; mpango utakuwa ni wa kujiendesha (sustainable) na faida itakuwa inaenda kusaidia shule “mahtuti.”

    Narudia tena… Nitalivalia njuga hili. Nilikuwa napanga kufanya mambo mengine baada ya kumaliza masomo. Ila nadhani hili ni muhimu zaidi — kwangu. Kwahiyo, wanaotaka kunisaidia, msisite kuniambia… Kwa hakika itabidi kwanza tuanze kwa kujadili na kuwa na mipango thabiti.

    Shukrani mwandishi; makala yako imezaa vitendo!!

  5. Sawa sawa SN.

    Kwa kweli kama kijana mwenzako, najisikia mwenye furaha wakati raia wetu, hasa waliosoma nje, halafu wakapata nasaha ya kukumbuka kusaidia jamii.

    Mie nakutakia kila la heri na ulilolisema kweli ni la maana na kama kweli utashiriki katika kutafuta vipaji vya fizikia au hisabati, basi itakua hamasa kubwa kwa wadogo zetu kama sio watoto wetu.

    Mie kama mkazi wa Bunju, hali nionayo pale ni kwamba wale vijana na watoto wanahitaji zaidi, walimu, madawati, vyoo, maji na umeme, pia syllabus books, kalamu, vifutio na vitu kama hivyo, na mie kama kijana niliesomeshwa na serikali mpaka nikaishia kupata elimu ya juu ulaya, naahidi hili ndilo litakua kipaumbele kwa upande wangu.

    Bila kusahau msisitizo wa ICT, ambao ulikua mkondo na mwelekeo wangu kabla kujiongezea elimu ya biashara.
    Kama wote sie tutaamua na kujikita kwa kile tukifikiriacho, basi ni poa tu, so long as its sustaining and sustainable!

  6. Nionavyo, nakuelewa na nimekuwa nikisoma maoni yako yote hapa…

    Hayo matatizo yapo na sio kama nayafumbia macho. Lakini kama hatutaweza kuwa na kitu endelevu, miaka 20 baadae tutakuwa tunaendelea kuwa na midahalo hii hii. Huo ndio msimamo wangu (kwasababu nimechoka kulalamikia Serikali.. naweza nikaandika kitabu kikubwa kuliko Biblia, kulaumu Serikali ya Tanzania).

    Unajua kwanini nimeliweka hili hadharani? Ili kama kuna mtu amechangamka aweze kulifanyia kazi. Kwasababu mpaka mimi nimalize masomo, nijipange n.k. itanichukua hiyo miaka 10! Wakati huo wadogo zetu wengi watakuwa wameshaachwa kwenye mataa…

    Kwahiyo, moyo wangu utasuuzika nikiona kitu kama hiki kikianzishwa — faida itapatikana, na hela zitapatikana; ninachotaka ni kitu kuwa endelevu na faida iende kwenye kusaidia hizo shule zetu ‘mahtuti’ kununua madawati, kujenga madarasa… orodha ni ndefu sana.

    Muda ukifika, nitaanika mambo…

    Ningependa kusema hivi: Sio lazima iwe sayansi au hisabati tu. Kuna mambo ambayo kusema ukweli TZ tuko nyuma. Nimeshawahi kuuliza (hapa) hivi kwanini hatuna somo la Uandishi (i.e. Creative Writing)? Labda majukwaa kama haya yatumike kuhamasisha watu kufuatilia vipaji vya uandishi, pia…?

  7. Hii mada nayo imenigusa sana. Mimi sikuwa nafaulu Hesabu. Ila cha ajabu kwenye Mtihani wa Taifa wa Kidato cha 4 nilipata ‘Msonge’ yaani A! Hivyo toka wakati huo nikawa naamini kuwa inawezekana kujifunza mwenyewe Hesabu na kufaulu!

    Kwa uelewa wangu tatizo moja ni kuwa hatuifanyi Hisabati iwe sehemu ya maisha na utamaduni wetu. Nadhani ni vyema vitabu vikaandikwa kwa lugha nyepesi na mifano iwe inatoka kwenye jamii husika – kwa mfano mnakumbuka lile swali la kutafuta eneo ambalo mbuzi aliyefungwa kamba yenye urefu fulani atakula majani? Basi vitabu vyetu vikiwa na maswali kama hayo tena yanayomchochea mwanafunzi ajisomee na kujifunza mwenyewe bila kumtegemea mwalimu basi tutafika mbali.

    Ila kama walivyonena watafiti mbalimbali, ni vigumu kwa mwanafunzi mwenye njaa kujifunza hivyo tuangalie suala la umaskini mashuleni.

  8. ni kweli suala hili ni muhimu sana kama Tanzania tunauwezo wa kushiriki tamasha mbalimbali kama ya utamaduni mipira na dini je haiwezekani kwa hili la kitaaluma , mimi na amini ya kianzishwa mashindano haya pia itakuwa kama burudani kwa watanzania wote

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend