Tunahitaji watoto wanasiasa?

Kuna jambo limekuwa likinigusa kwa muda sasa, na jambo hili ni kuchipukia kwa kasi hivi karibuni mchakato wa kuwa na watoto wadogo wanaoitwa chipukizi wa chama. Watoto hawa huwa na wa umri wa miaka kumi (10) na kuendelea husajiliwa na chama cha kisiasa ili kujifunza fikra za chama, uongozi, utiifu, pamoja na kupigania haki na maslahi ya msingi kwa watoto. Chipukizi hawa pia huwasilisha mawazo endelevu wapatapo nafasi, kwa mfano wito wao hivi karibuni wa kuanzisha mpango wa mabasi maalum ya wanafunzi.

Picha kwa hisani ya www.othmanmichuzi.blogspot.com

Utamaduni huu wa kuwa na chipukizi wa chama cha kisiasa chimbuko lake ni enzi zile za chama kimoja nchini Tanzania. Vijana wa zamani watatuelezea zaidi kuhusu haya; kuhusu kauli mbiu za chama, kuhusu “zidumu fikra za kiongozi” au kuhusu nyimbo za uhamasishaji za chama kimoja. Ingawa nia yao enzi hizo ilikuwa ni kujenga taifa la vijana wazalendo, kuna ishara ya kuwa badala yake tume(tuta)-kuja kujenga taifa la wanaofikiria zaidi utiifu kwa chama cha siasa kwanza huku maslahi ya taifa yakifuata baadaye; wananchi na viongozi wao. Tumevuna siasa ya kiushabiki zaidi na sio siasa zinazolenga sera na uwajibikaji, yaani siasa za kimazoea; anayependa upinzani atakuwa mpinzani mpaka kufa, na anayeshabikia ‘washika’ nchi ni hayo hayo.

Swali langu, je, kuna haja ya kuwa na makundi ya watoto wa vyama vya kisiasa katika karne hii ya demokrasia na yenye siasa za vyama vingi?

Kwanini tunaendelea kupanda mbegu za kutenganisha vijana wetu kwa fikra za kisiasa wangali na umri mdogo? Ninapouliza hili, tumboni ninapata baridi nikitaka kufananisha na wale chipukizi wa Ujerumani wa 1930. Ni wazi mipango ya kuwa na chipukizi yamepitwa na wakati.

Mwenyekiti mpya wa Chipukizi wa CCM taifa Gabriel Amos Makalla alipotangazwa ushindi wa uchaguzi. Picha na Latifa Ganzel

Ninaamini ni jambo jema kama tukihamisha nguvu zetu kwenye elimu ya uraia na kusitisha uwepo wa chipukizi wa vyama vya siasa. Elimu safi ya uraia itavuna vijana wazalendo, wenye mapenzi kwa nchi yao kwanza na wenye kutaka kuona taifa lao linaelekea mahala pema bila kujali tofauti za kivyama. Na sio kutayarisha vijana waliopandikizwa mafundisho ya kisiasa tokea utotoni wenye hatari ya wao kuwa na fikra za chama kwanza kabla ya maslahi ya taifa.

Kwanini tusiwe na mpango wa kuwa na chipukizi wa kitaifa, na sio wa kivyama vya siasa?

Uskauti je?

Maskauti ni vijana kati ya umri miaka nane na kuendelea ambao hupitia mafunzo mbalimbali ya kidarasa pamoja na ya nje yanayolenga kujenga elimu ya kitabia, uraia, jiografia, mapishi, na kuendeleza sifa mbalimbali chanya kwa mtoto zitakazomsaidia hapo mbeleni kama mwananchi. Vijana hawa katika mafunzo hushiriki michezo inayojenga ushirikiano, hujifunza huduma ya kwanza, uongozi, uwajibikaji katika kikundi au uongozi, uraia wema, na umuhimu wa mazingira. Kila stadi anayoimudu mwanachama anapewa nishani, pamoja na motisha ili ajiendeleze zaidi.

Kama kweli tunataka kuendeleza mchakato wa chipukizi, uskauti ni modeli tosha kwa ajili ya hili. Chipukizi wetu wa kitaifa wawe maskauti au kama maskauti.

Ushiriki wa mapema wa watoto katika siasa ya vyama haumjengi mtoto wa KITANZANIA. Kwenye kivuli cha siasa za vyama tunamjengea mtoto sifa za kupenda utofauti zaidi unaozingatia uanachama wa kisiasa na sio umoja au utaifa. Tuache kuhimiza watoto kupenda kuvaa sare zenye rangi ya chama cha siasa na sio zenye rangi ya bendera ya Taifa.

Tudhamirie kuwa na chipukizi wa kitaifa ambao elimu yao ya nje ya darasa iwajenge kuwa na fikra za kiubunifu, wawe wadadisi na wenye mtazamo wa kufikiria nje ya box. Jeshi la vijana hawa litatusaidia hapo baadaye katika kuleta mapinduzi yatakayotuvusha katika bahari hii ya umasikini.

TATIZO la rushwa katika chaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), linaonekana kuzidi kukua baada ya uchaguzi wa viongozi wa chipukizi taifa kukumbwa na matukio ya utoaji takrima kwa wajumbe wa mkutano huo.

Habari zilizopatikana kutoka katika mkutano huo uliofanyika mjini Morogoro, Desemba 29 mwaka jana, zinaeleza baadhi ya wapambe wa wagombea waligawa pesa hadharani na wengine kukutana nao usiku wa manane.

Utoaji wa rushwa kwa wajumbe ulianza siku moja kabla ya uchaguzi huo ambapo wapambe wa wagombea hao watoto wadogo wa miaka kumi, walipita kwa wajumbe wakiomba kura na kutoa takrima mbalimbali zikiwamo pesa.

Katika uchaguzi huo ambao watoto wa vigogo ndani ya chama hicho waliibuka washindi, unaelezwa kuwa ni ishara mbaya kwa CCM kwa vile sasa hata watoto wadogo wa miaka 10, wanafundishwa kutoa na kupokea rushwa.

Wajumbe wa mkutano huo ni wenyeviti wote wa Chipukizi wilaya ambao ni watoto wa miaka 10 hadi 13, na makatibu wa Chipukizi na uhamasishaji wa wilaya ambao huwa ni vijana wakubwa.

Pia uchunguzi huo umebaini kuwa makatibu wa mikoa wa UVCCM ndio waliotumiwa na vigogo ndani ya CCM kupanga mkakati wa kuwawezesha watoto wao, kushinda katika uchaguzi huo.

“Hilo si siri kweli tuliitwa na baadhi ya watu ambao walijitambulisha walitumwa na kigogo na kupewa msimamo wa kuhakikisha kijana anashinda, tusimwangushe,” alisema mjumbe mmoja wa mkutano huo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Morogoro, Jonas Nkya alikanusha hayo akisema uchaguzi ulifanyika vizuri na yeye binafsi alishuhudia hakukuwepo vitendo vyovyote vya rushwa. Kigezo kingine ambacho Nkya alikichukulia kama sehemu ya uchaguzi kwenda vizuri ni kutokuwepo na malalamiko.

“Hadi sasa hakuna kiongozi wala mgombea ambaye amewasilisha malalamiko kuulalamikia,” alisema Nkya huku akitoa wito wa yeyote ambaye hakuridhika na uchaguzi huo kutosita kuwasilisha malalamiko yake.

Baadhi ya wajumbe wengine wa mkutano huo, waliiambia Mwananchi Jumapili kwa masharti ya kutotajwa majina kuwa uchaguzi huo uligubikwa na rushwa kuchafuana majina miongoni mwa kambi hali iliyosababisha watoto wa vigogo kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.

Walisema pamoja na kuweka msimamo wao mwanzo wa kuhakikisha hawawachagui watoto wa vigogo, msimamo huo ulishindikana kutokana na shinikizo la viongozi wa juu na kulainishwa kwa rushwa.

“Kwa kweli sisi wajumbe tulishaweka msimamo wetu baada ya kuona nafasi nyeti zote katika umoja wetu zinachukuliwa na watoto wa wakubwa na hivyo, kupendekeza tuwachague walalahoi wenzetu,” alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Kanda ya Ziwa.

Baadhi ya wajumbe hao walidai msimamo huo uliwashtua baadhi ya viongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa waliokuwepo mkoani hapa na kuamua kumshauri mmoja wa wagombea wa uchaguzi huo, Halfan Kikwete asitokee katika uchaguzi huo kwa kukwepa aibu ya kushindwa.

Waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Gabriel Makala ambaye ni mtoto wa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Taifa, Amos Makala kuwa Mwenyekiti mpya wa chipukizi taifa baada ya kupata kura 300 kati ya kura 357 zilizopigwa na hivyo kuwashinda wagombea wenzake saba waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mbali na Makala pia mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Halfan Kikwete alichaguliwa kuwa mjumbe wa baraza kuu kutoka Tanzania bara kwa kura 301 bila kuwako ukumbini hali mbayo iliwashangaza wafuatiliaji wengi wa uchaguzi huo.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika uchaguzi huo, uliohudhuriwa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emanuel Nchimbi, mshauri wa rais January Makamba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM taifa, Amos Makala pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya ulibaini kulikuwepo na mazingira ya rushwa.

Mwandishi wa habari hii aliyekuwepo katika chuo cha ualimu Kigurunyembe siku moja kabla ya uchaguzi huo saa 7:00 usiku, alishuhudia vigogo mbalimbali wakiwaamsha wajumbe katika vyumba vyao na kugawa fedha kuwashawishi wawapigie kura wagombea wao.

Hata hivyo, habari zingine zimedai kuwa makatibu wa Chipukizi na Uhamasishaji waliitisha mgomo siku moja kabla ya uchaguzi huo wakidai posho waliyopewa ni ndogo na hivyo hata wakipiga kura hawatawachagua watoto wa vigogo.

Hatua hiyo ilimfanya kiongozi mmoja wa CCM kunusuru jahazi kwa kuwapa sh 30,000 kila mmoja na hivyo uchaguzi ukafanyika.

Previous ArticleNext Article
Joji was born and grew up in Dar es Salaam, Tanzania. He graduated with a B.Sc in Biochemistry in Germany, and is now pursuing a Masters degree in Microbiology & Immunology at the Swiss Federal Institute of Technology (ETH) in Zurich, Switzerland . Joji is particularly interested in matters related to global health, and basic science research that tackles public health challenges. He is engaged in mentoring Tanzanian students in higher education issues, most notably at the Kibaha High School. In this capacity, Joji blogs with Vijana FM about scientific research and development, and how youth can gain greater access to higher learning.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend