“Mwendo ni kula raha – 1”

Nilikuwa nasubiri kipindi hiki kwa udi na uvumba; baada ya mtihani wangu wa mwisho wa kidato cha nne, mwendo ni kula raha tu mpaka matokeo yatakapotoka Machi au Aprili mwaka kesho. Lakini mpaka sasa hivi mambo yamekuwa kinyume kabisa na niliyotarajia. Siku mbili nilizokuwa nyumbani bila la maana la kufanya zimeniboa sana, kwasababu marafiki zangu wengi, ambao wanafanya masomo ya biashara, wanamaliza mitihani yao leo Ijumaa.

Tokea saa tisa mchana, muda ambao marafiki zangu watakuwa wanakusanya mitihani yao ya mwisho, nimekuwa nikiitolea mimacho simu yangu. Sijui masela wanapanga kufanya nini leo? Bahati nzuri wimbo mpya wa msanii chipukizi Mangwea Ghetto Langu” upo hewani na unanipa fikra tofauti kidogo. Nasikiliza mashairi yake huku macho yangu yakiranda-randa kwenye chumba changu. Kuanzia mwanzo wa wimbo hadi mwisho, nimelinganisha ghetto la Mangwea na langu na sijaona chochote kile ambacho kitampagawisha demu ye yote yule! Hata wa Uswazi!

DJ Stevie B anaonekana kaupenda sana huu wimbo na anaamua kuucheza tena. Safari hii naamua kutolinganisha chumba changu na ghetto la Mangwea; nafumba macho yangu taratibu na nayaachia kazi masikio yangu kufaidi midundo mwanana na mashairi.

Joto linalosababishwa na jua kali la Bongo linanipa uvivu kiasi, na nahisi usingizi unaanza kuninyemelea. Nilichokuwa nasubiri siku nzima kinatokea: napokea ujumbe mfupi kutoka kwa rafiki yangu Deo unaosema, “Magz! 2day ni Billz! Dingi na maza hawapo, so pick-up ni yetu. Mzuka?”

Bila kusita, namjibu haraka-haraka, “U r da man! Tunaanza na kiti moto na nyagi au?”

Ananijibu kwa kizushi, “Unaulizia makonzi kituo cha polisi? Mtu kibao zitazuka. Hadi demu wako HAHAHA!”

“Acha masihara Deo! Mi mgumu, halafu yule wa geti kali simuwezi. Poa mzee, muda ule ule.. Cine Club then BILLZZZ!”

Deo anapenda sana utani. Napokea ujumbe wake mwingine, “Neema kakuzimia Magz! Ananisumbua kinoma. Nadhani hata ukimpeleka kula mihogo na chachandu hatamaind.. only 4 u! Peace!”

Nashindwa kujizuia kuangua kicheko, ingawa mimi ndiye ninayetaniwa. Nimekuwa muoga kufuata Deo anayosema na kumtokea Neema. Sio kwamba simfagilii. Basi tu; kuingia kichwa kichwa na kupigwa kibuti halafu masela wajue ni noma. Wakati mawazo ya matokeo ya kupigwa kibuti yakijikita kwenye akili yangu, naamua kulala kwenye kitanda na kuegesha kichwa kwenye mto. Natazama kona za dari ambazo zina tando za buibui. Kila siku huwa nasema nitaziondoa kesho, lakini huwa nasahau…

*      *      *

“Ngo! Ngo! Ngo! Magirini, chakula tayari! Baba anasema leo tunakula pamoja mezani,” sauti ya binti anayetusaidia kazi za ndani, Hadija, inanizindua kutoka usingizini.

Namjibu kwa unyonge, “Haya. Ninakuja sasa hivi.” Nanyanyuka kutoka kitandani, nawasha taa na kuangalia muda kwenye simu yangu. Ni saa mbili na nusu; Deo atakuja kunichukua saa tatu hivi, kwahiyo nina dakika thelathini tu za kuongea na baba na mama na kuwaomba ruhusa ya kutoka leo usiku.

Naenda bafuni kunawa uso na kupiga mswaki haraka-haraka kisha najongea sebuleni, baba na mama walipo wakiangalia runinga. “Shikamoo baba, shikamoo mama.”

Wote wananijibu, “Marahaba.” Baba anaendelea, “Yaani tokea tumerudi kutoka kazini ulikuwa umelala? Hukusikia hata mlio wa gari?”

Namjibu kwa kifupi tu, “Hapana baba.”

Baba ananiangalia kwa jicho ambalo linaashiria amekerwa kiasi, kisha anamuangalia mama. Inaonekana walikuwa wameshajadili wanachotaka kuniambia. Anageuka na kuniangalia huku akiwa amekunja ndita, “OK, leo ndio mwisho wako kukaa nyumbani bila kufanya kitu chochote! Kuanzia kesho shughuli za bustani na vitu vingine nje ni jukumu lako. Nikiona majani yaliyokauka kwenye maua, wa kwanza kukuuliza itakuwa ni wewe.”

Natingisha kichwa kuashiria kuwa naafikiana naye.

Baba ananyanyuka kutoka alipoketi na kuelekea mezani kwa ajili ya chakula cha jioni huku akiniambia, “Halafu kitu kingine. Unajua kuendesha gari sasa hivi? Nitakutafutia leseni ili uwe unashughulikia mambo ya shamba kuanzia wiki ijayo. Mtu kama wewe inabidi uwe bize mpaka tutakapoanza zoezi la kukutafutia shule A-level.” Baada ya kuketi na kuanza kupakua chakula, baba anamwambia mama anayevuta kiti ili aketi, “Hivi vidume vikiachiwa uhuru vinaanza kuvuta bangi na kuwapa mimba binti za watu.”

Mama anamjibu, “Baba mkwe asingekuacha huru baada ya kumaliza kidato cha sita labda tusingekutana baba Magirini!”

Baba anatabasamu kisha ananiangalia na kuniambia, “Vipi, mbona hukai? Leo hutaki kula makande?”

Mazingara ya maongezi yamebadilika, na wakati huu utani ukiendelea ni muda muafaka kuomba ruhusa ya kutoka, “Unajua mitihani ilikuwa migumu sana. Nilikuwa napanga kutoka leo. Nitakuwa na Deo na marafiki zangu wengine.”

Mama anaanza kutabasamu na kumwambia baba, “Si nilikwambia? Haya, mpe hela ya taksi ya kurudia.”

Baba anaanza kunipa nasaha zake kama kawaida, “Usinywe pombe. Sitaki kusikia mambo ya wasichana! Kabisa!” Kwa shingo upande anatoa hela kwenye pochi yake na kunikabidhi, “Unajua cha kufanya, Magirini. Usirudi kwa lifti za marafiki zako walevi. Kukiwa na shida nipigie simu.”

Sitaki kutibua kitu chochote sasa hivi, kwahiyo napokea hela na kusema, “Ndiyo baba, nitafuata maelekezo yako yote.”

Kabla sijaondoka baba ananiambia, “Halafu niliona buibui kwenye chumba chako leo asubuhi. Unasubiri mimi, mama yako na Hadija tukusaidie?”

Bahati mbaya mazingara ya maongezi yanageuka ghafla, lakini mama anaokoa jahazi kwa kumkata kauli baba, “Baba Magirini, mwache.”

Bila kusita baba anamwambia mama, “Mbona unamtetea sana? Angekuwa dada yake hapa maongezi yangekuwa tofauti kabisa.”

Mama anamjibu, “Huo mjadala mwingine. Haya Magirini toka hapa kabla baba yako hajabadili mawazo.”

Nakimbia chumbani kwangu kuvaa nguo kwa ajili ya usiku kama wa leo. Kabla ya kutoka, najipulizia manukato halafu naangalia simu yangu ambayo ina ujumbe kutoka kwa Deo, “Am on my wei. Neema naye atakuwepo.. HEHEHE!”

Ile kutoka tu nje ya geti, naona Deo anawasili akiendesha gari kwa mwendo mkali huku akitimua vumbi. Nafungua mlango na kungia ndani ya gari, kisha namwambia, “Mzee una fujo! Yaani mzee mzima nimejipinda kupendeza, halafu kichaa unakuja kunitimulia vumbi?”

Tunaanza safari ya kuelekea Cine Club huku akiniambia, “Sorry mzee. Mzuka umenipanda kupita maelezo leo. Nina uhakika nitapata msonge kwenye pepa la Commerce!”

“Sio mchezo mzee! Endesha taratibu basi, Deo. Kichaa kama huoni matuta vile. Kumbuka hauna leseni, na tukipigwa mkono sasa hivi kila kitu kitaharibika. Usiku mrefu kinoma na starehe zote zinatusubiri.”

Deo anacheka huku akiniambia, “Mzee wa busara unaongea kama dingi yako siku hizi.” Bahati nzuri anapunguza mwendo. Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, anaanza utani, “Ohh! Mzee, kuhusu suala la starehe, nadhani unajua kuwa Neema atakuwa nasi. Fanyia kazi mzigo ule. Oh hooo, Magirini!”

“Acha uzushi mzee. Umenikomalia siku nzima. Umetumwa nini?”

Ananiangalia huku akitabasamu bila kusema lolote, kisha anageuka kuangalia tunapokwenda. Tunatoka Mikocheni na kuingia kwenye barabara ya Old Bagamoyo. Upepo mwanana wa bahari unaingia kwenye pick-up ya Deo. Naamua kuwasha redio na kusikiliza muziki ili kuanza starehe rasmi.

Deo ananiambia, “Hii pick-up ya shamba mzee. Redio yake haikamati hata Clouds FM!”

Sote tunaangua kicheko. Namwambia, “Haya basi, ngoja nitafute hata RTD nimsikilize Deborah Mwenda na hadithi zake za mazimwi!” Nafanikiwa kudaka mawimbi ya Clouds FM, halafu namwambia, “Nilikuwa naogopa kichizi hadithi za mazimwi. Sijui zimwi lina macho matatu.”

Deo anacheka huku akiniambia, “Nazikumbuka zile. Mi’ nilikuwa naimaind ile hadithi ya Binti Chura. Mpaka leo bado naikumbuka.”

Taratibu tunawasili karibu na kituo cha basi cha Warioba. Deo anapunguza gia, anakata kona kuingia Cine Club na  anafanikiwa kuona sehemu ya kuegesha gari.

Baada ya kuegesha gari, kuzima redio na kufunga vioo, tunaanza kuelekea sehemu ambapo marafiki zetu walipo. Mwanga ni hafifu, lakini namuona Neema akiwa amekaa kwenye meza moja na marafiki zetu. Kasi ya mapigo ya moyo inaongezeka lakini najitahidi kuficha hisia na kuvaa uso wa mbuzi…

Itaendelea wiki ijayo.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 7 Comments

7
  1. Sisi tulienda TGI tulipomaliza mitihani ya kidato cha sita. Bado najaribu kukumbuka kidato cha nne ilikuwaje. Nasubiria nione mwisho wa hii hadithi, ni nzuri inavyoelekea.

  2. Baba anasema “Nitakutafutia leseni ili….” Ingawa ni kweli inatokea kwa wingi, hali hii inasikitisha. Mtu kupewa leseni kiholela.

    Hii kweli inakamata hali halisi ya maisha ya vijana wa mjini. Nadhani dogo aliyemaliza kidato cha nne kule Kangantebe, Bukoba hatoweza kuelewa hii. Nevertheless, these narratives should persist.

  3. Hahahahaha! Priceless, yaani Magirini kadata…nimependa “Unaulizia makonzi kituo cha polisi? Mtu kibao zitazuka. Hadi demu wako HAHAHA!”…Imenikumbusha wakati nimemaliza O na A-Level…kweli kuna chaos wakati huo…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend