Nchi yetu Tanzania

Pata mishkaki...

Nilikuwa napanga kuandika makala kama tatu hivi kujadili masuala kadhaa yaliyotokea kwenye hizi wiki tatu zilizopita. Ila kwa kuwa niko bize (utu uzima unanipiga chenga ya mwili), nimeamua kuzibana mada zote hapa pamoja kama mishkaki!

Usipoteze muda wako kabisa kunishauri niongelee kitu kimoja kwa wakati mmoja, kwasababu hicho kilishatokea tayari. Bahati mbaya kwa kuwa kila mtu yuko bize akijaribu kukidhi ile kitu roho inapenda — kwa mfano, kutafuta “ukweli” kama Dr. Slaa alimpora mke yule msela — mambo muhimu yanaonekana yametupita hivi hivi tu. Namaanisha: hatukuyajadili kwa kina, na labda kutafuta suluhisho au njia mbadala za kutatua matatizo yanayoikumba nchi yetu Tanzania.

Ili tuelewane vizuri, tafadhali funga hizo kurasa za tovuti za ajabu-ajabu. Usisahau kufunga na hii pia!

Wachache wanaosoma makala kwenye hii tovuti ni vijana ambao wamebahatika kusoma ughaibuni. Kinachonisikitisha ni kwamba wengi tumeridhika na mchango kiduuuuuchu wa kuwatumia ndugu zetu vijisenti Tanzania. Hivi hatutambui kuwa, labda tukifungua macho na kutumia mitandao ya kitaaluma tuliyonayo, tunaweza kuletea Taifa letu faida au maendeleo endelevu yatakayoweza kufaidisha vizazi vijavyo?

Nimeshuhudia mijadala mingi ambapo watu wanapoteza muda kubishana na kujaribu kubatilisha takwimu zinazoonesha Wakenya ndio wanaoongoza kwa kutuma hela ‘nyumbani’ kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Jamani, tufikirie mbali zaidi ya kutuma hela Tanzania.

Mi’ nawaambia hivi, “Hebu tuweke upuuzi pembeni na tufikirie zaidi ya kutuma hela nyumbani!” Usichukulie hii kauli kama matusi ya nguoni; badala yake ichukulie kama changamoto fulani itakayokufanya ufikirie mbali zaidi.

Sylvisorex howelli: Alidakwa kwenye milima ya Uluguru!

Kwa mfano, nawauliza wanasayansi: kwanini mnashindwa kuanzisha taasisi za utafiti ambazo zitakuwa zinashirikiana na za nje ya nchi? Hivi, bado wale vyura wa Mbeya wanatumwa Marekani? Kila mwezi nasikia species wapya ‘wanagunduliwa’ kule Usambara. Hivi tunashindwa kukamata panya-buku na viumbe wengine wenyewe? Tunasubiri wa Ulaya waje? Wakati tuna Watanzania kibao tu kila kona?

Badala ya kufikiria jinsi ya kujibu hayo maswali, haiba yetu itatusukuma kufikiria visingizio na kutoa mifano ambayo itavunja moyo watu wengi. Nakushauri usifuate mkumbo. Jifunze kufikiria mwenyewe na jiulize wewe binafsi unaweza kufanya nini kuleta maendeleo Tanzania. Kumbuka, nchi zinazofanya vizuri kiuchumi zinaendeshwa na ujuzi!

Hapo kuna mtihani mwingine, kwasababu taarifa zilizotolewa wiki mbili zilizopita zinasema kuna wadogo zetu ambao wanahitimu shule ya msingi huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika! Hapo hujawauliza kama wanajua kufanya hesabu za kuzidisha na kugawanya.

Mi’ binafsi machozi yalinilenga-lenga; fikiria mtoto wa miaka kumi na nne hawezi kusoma hata hii makala na kuielewa. Sasa, atapataje ujuzi wa kuweza kuyakabili maisha akianza kujitegemea? Ile ripoti ingetolewa kwenye nchi nyingine za Afrika nina uhakika kungekuwa na migomo na maandamano. Lakini Watanzania tukaisoma, tukatikisa vichwa tu na kuendelea na shughuli zetu kama kawaida.

Nadhani wengi tunadhani labda haya matatizo sio yetu; hayatuhusu. Fikiria kwa makini na jiulize, watu kila siku wanachoma vijana moto, kwanini vibaka wanaendelea kuongezeka kila kukicha?

Nitakupa mfano mwingine ili utambue kuwa hili sio tatizo la ndugu zetu wanaotoka vijijini tu. Nina marafiki wengi ambao wamesoma hadi vyuo vikuu, lakini kuandika aya mbili tatu kwa ufasaha ni mbinde. Kuna wakati napokea barua (pepe) zenye mtiririko kama huu… Yaani inanibidi nizipitie na kujaribu kuotea sehemu za kuweka vituo ili nizielewe vizuri. Umeshawahi kujiuliza kwanini hata wasomi wetu sio waandishi wazuri, hata kwa Kiswahili?

Kuna wakati najiuliza, hivi tunafanya nini hapa? Mijadala inafungua watu macho au basi tu bora liende? Naelewa kubadilisha fikra za watu huchukua muda mrefu sana, lakini, mnajua tuanzie wapi ipi kufukua mizizi ya fikra potofu, uzembe, uvivu, uchawi na ushirikina na mifumo mibovu ya elimu inayozalisha watu mbumbumbu?

Vijana wachache wamejitolea kutengeneza chombo cha Ushahidi ambacho, kama kikitumiwa ipasavyo, kinaweza kupunguza mizengwe wakati wa Uchaguzi Mkuu na kutuwezesha kuchagua viongozi tunaowataka. Lakini ushirikiano tuliopewa mpaka sasa hivi unavunja moyo sana.

Wakati watu Tanzania wamegoma kutangaza na kuelimisha umma juu ya TZelect: Chombo cha Ushahidi, watu wa ughaibuni wanatusaidia!

Na hapa siongelei zile blogs ‘kubwa’ tu zilizogoma kutusaidia kutangaza na kuelemisha umma juu ya hiki chombo. Pia, wewe msomaji ungetakiwa kutuma taarifa zile muhimu kwa rafiki zako wote! Mbona kila siku napokea barua pepe za kijinga tu? Eti nikituma ujumbe fulani kwa watu 15, nitafanikiwa kwenye shughuli zangu. Kuna tofauti gani kati ujumbe kama huo na utabiri wa Sheikh Yahya? Na hata waganga wanaowaambia watu wawaletee viungo vya walemavu wa ngozi?

Tusidanganyane kwenye mitandao kwa kunadi sera zetu bila vitendo vyovyote vya maana. Mabadiliko na maendeleo kwenye jamii yanaletwa na fikra na mawazo mazuri, mipango madhubuti na ushirikiano wa watu. Hakuna njia ya mkato;  kila mtu anapaswa kutoa mchango wake kwa namna moja au nyingine.

Baada ya Uchaguzi utasikia watu wakilalamika, “Ooh, fulani kacheza faulo kwenye jimbo fulani!” Mimi nitawacheka na kuwaambia, “Chombo cha kupunguza huo upuuzi mlikuwa nacho, ila mlikuwa hamtaki kuwajibika.”

Eneweiz, labda hizi juhudi zote za kuwaamsha vijana wa Tanzania ni kama kujaribu kuwasha sigara katikati ya kimbunga.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 4 Comments

4
  1. Yanayokukera SN tumeyasikia, wengine tunayafanyia kazi, tena kama mipango ikienda salama na uzima ukawepo, basi tutaingia katikati ya dimbwi la matatizo hasa la elimu nakutoa mchango wetu.
    Ila nashangaa na kusikitishwa kwa kutokupata msaada kutoka kwenye “blog kubwa”, maana inadhihirisha wabongo vipaumbele vyetu viko wapi hasa.
    Nakuomba usikate tamaa, na pia nawe uingie katika mchakato wa kusaidia jamii yetu, hasa ukiwa bongo.
    Kila kitu kinawezekana, ni kuwa na nia na ari tu, kukumbuka kuwa tuna majukumu na Tanzania yetu, na mchango wowote hata uwe kiduchu vipi, utasaidia mno maendeleo ya nchi yetu.
    Tuko pamoja SN.

  2. Nionavyo, nadhani suala la elimu na kuamsha watu kufuatilia mambo yanayoathiri maendeleo ya nchi ni jambo nyeti mno, kama ulivyosema. Na mimi nitalivalia njuga hilo (tutataarifiana); kinachotakiwa ni kushirikiana, kwasababu kuingia mwenyewe kichwa-kichwa, aisee vikwazo ni vingi na inakatisha tamaa.

    Sisi tutaendelea kufanya tunachoweza kadri ya uwezo wetu, ila ushirikiano na uwajibikaji wa watu ukiwa mdogo, mafanikio itakuwa kama ndoto za Alinacha.

    Hata hivyo, wahenga walisema, “Haba na haba hujaza kibaba.”

  3. Suala la watu walioko nje kusaidia nyumbani ni suala tete. Watu wengi wanafikiri msaada ni fedha tu. Wanasahau kuwa mawazo au ushauri wa kitaalamu unaweza kuwa mchango mkubwa vile vile.

    (Tatizo hili lipo kwa pande zote mbili, walioko diaspora na walioko nyumbani.)

    Wengi wako tayari kupokea michango ya fedha kwa ajili ya maendeleo yao, lakini hawako tayari kupokea mawazo ambayo yatawataka wao pia kuchangia walau kidogo ili kujisaidia. Niliwahi kukutana na mfumo huu wa uchangishaji pesa kwa raia wa kawaida.

    http://www.youtube.com/watch?v=bCjQ_6VJ-qU&feature=related

    Unaponunua healthy meal kwenye mgawaha, gharama zaidi kidogo inaongezwa (yen 20 approx. 300 TZS), na kukusanywa na kupelekwa kwenye shule za nchi masikini Afrika kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.

    Nilipojaribu ku-introduce wazo hili kwa hoteli zetu Tanzania (ili pesa kusaidia kutoa huduma kwa maeneo ya karibu), zile hoteli zinazomilikiwa na Wazungu zilikubali moja kwa moja lakini zenye wamiliki wa Kitanzania takriban zote zilikataa na kudai kuwa wateja wao wasingependa kununua vyakula kwa gharama zaidi wakirejelea wateja wao raia wa Tanzania.

    Zoezi zima lilikuwa na lengo la kuwaamsha raia wasaidie katika maendeleo yao wenyewe, lakini kwa bahati mbaya lilifeli moja kwa moja 🙁

    Wengi tuko tayari kumsifu mzungu (raia wa kawaida) anaejitolea na kuanzisha shule nchini mwetu bila ya kujiuliza amejitolea na kujinyima kiasi gani. Labda wengi wangelijua, huenda asaa, mambo yangebadilika.

    http://en.wikipedia.org/wiki/Three_Cups_of_Tea

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend