Nyumba Moja, Katiba Moja

Na Michael Dalali

Kadri kila kaya inavyojitahidi kuwa na kitabu kitakatifu kwa mujibu wa imani yao — yaani Msahafu kwa Waislamu au Biblia kwa Wakristo — hii inafungua mlango wa kuwa na kitabu cha mamlaka ya nchi. Katiba!

Kadri kila wakati kaya ikiketi chini na kusoma kitabu kitakatifu kwa minajili ya kujiimarisha kiimani na kupanua maarifa ya “elimu ahera”, ndivyo hivyo pia inapaswa kaya zikae mara kwa mara na kusoma kitabu cha mamlaka ya nchi. Katiba!

Licha ya uwepo wa maduka ya vitabu vya aina mbalimbali katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kitabu cha katiba, bado wananchi wachache wanamudu kuwa na nakala ya kitabu hicho muhimu ambacho kinaweza kuwasaidia kuhakikisha haki na maslahi ya kila mmoja yanalindwa. Kuhakikisha maslahi ya nchi kwa ujumla yanasimamiwa.

Bado upatikanaji wa katiba katika maduka nayo ni suala la mjadala mpana, maana licha ya kutokupatikana kirahisi katika maduka mengine, hata lile duka la serikali nakala zinapatikana kwa nadra na kwa uchache.

Hata kwenye shule za msingi na sekondari, iwe za kata ama zisizo za kata, bado kwa sehemu kubwa upatikanaji wa kitabu cha katiba ni ndoto. Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambapo hata katiba moja ya mfano hakuna!

Mabadiliko ya 14 na ya mwisho katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchini Ujerumani, kila mwanafunzi ambaye anafuzu mafunzo yake hupatiwa cheti sambamba na katiba ya nchi yao. Je, wao walitafakari nini kuona umuhimu wa kuwagawia wahitimu wao katiba ya nchi yao? Je, wanafunzi na wahitimu wangapi nchini wana katiba — iwe wamenunua kwa fedha zao ama wamepewa?

Tatizo la ukosefu wa katiba linakuwa kubwa zaidi hasa pale ambapo viongozi wetu wa ngazi za chini, mwenyekiti wa kijiji ama mtendaji wa kijiji, nao pia katiba kwao ndoto. Hata ofisi ya serikali za mitaa hakuna. Mwe!

Kutokana na ukweli huu, ni wazi kuwa wananchi wengi wa nchi hii, kama inavyoeleweka kuwa idadi kubwa wanaishi vijijini, watakuwa hawana uelewa wa kutosha juu ya suala zima la katiba na miongozo yake katika maisha yao ya kila siku. Si nia ya makala hii kutafuta wa kumtupia lawama kutokana na hali hii. La hasha! Nia ni kuamsha ari kwa kila Mtanzania kuona kuwa anapungukiwa na kitu kwa kutokuwa na katiba, achilia mbali kuifahamu vyema.

Kila Mtanzania ajue kuwa, matatizo yote yanayomkabili katika eneo lake, ya kukosa huduma bora za afya, maji na elimu, kuonewa na kudhulumiwa haki zake, matatizo ya miundo mbinu, ya kiusalama na haki ya kupatiwa maendeleo, vyote hivi vipo katika katiba na katiba inaeleza vyema, nini kifanyike, wapi na kwa wakati gani; ukiachilia mbali dosari mbalimbali za kupitwa na wakati na mapungufu mengine yanayozaa uhalali wa kutaka kuiandika upya.

Sina shaka kuwa, kila mmoja wetu anatambua kuwa, maudhui ndani ya katiba ni kwa maslahi ya kila mwananchi. Hivyo maudhui hayo yanapaswa kuhubiriwa na kujadiliwa miongoni mwa kila raia. Cha kujiuliza hapa ni kwamba, ziwapi jitihada za dhati za kuwafikishia wananchi ujumbe uliomo ndani ya kitabu hicho cha kimamlaka na utawala?

Haki ya Uhuru wa Mawazo.

Imeshapata kusemwa, haki haiombwi! Haki haipewi katika sahani kama pishi la mchele. Kila mwananchi, kila mwalimu, kila mtendaji wa serikali za mitaa ama kijiji anapaswa aweke juhudi ya dhati kuhakikisha anakuwa na nakala ya katiba.

Kila shule ihakikishe inakuwa na nakala za kutosha za katiba. Kila mwanafunzi ahakikishe anapata wasaa wa kusoma kwa mfumo wa makundi ama mmoja mmoja.

Kila kaya nchini ihakikishe ina nakala ya katiba na iwe inatenga muda wa kusoma aidha kama kaya nzima au kila mwanakaya kwa nafasi yake.

Kama vile tunavyojitahidi kujifunza masuala ya kiimani, ndivyo hivyo pia tujitahidi kuwekeza katika kujifunza masuala ya kidunia hususan utendaji wa tawala, katiba na mantiki yake.

Kama tunavyopeana zawadi za vitabu ndivyo pia tuanze tamaduni ya kupeana zawadi ya kitabu cha sheria na taratibu za nchi: “Katiba”. Tujitahidi pia hata kupeleka zawadi za katiba kwa ndugu na marafiki zetu jijini na vijijini pia, na kwa wale Watanzania waliopo nje ya mipaka ya nchi yetu.

Katiba ya Tanzania na makala nyingine za Dalali:

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 1 Comment

1

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend