Ukiwezeshwa unaweza; usipowezeshwa je?

Na Sakura

Kwetu Tanzania nako kumekuwa na ‘siasa’ nyingi za kumnyanyua mwanamke, au kama wasemavyo wenyewe “kumkomboa”. Na wimbo huu wa ‘haki za wanawake’ umeimbwa sana kwenye ngazi zote za kijamii.

Harakati hizi zinazokwenda kwa kauli mbiu ya “mwanamke akiwezeshwa anaweza” zimegubikwa na hali ya utata. Hiyo kauli mbiu yenyewe tu tayari ina mushkeli. Wanaposema mwanamke akiwezeshwa anaweza, wanamaanisha kuwa mwanamke hawezi kama hajawezeshwa? Na huyu wa kumuwezesha mwanamke ni nani? Mwanaume? Na ikiwa ni hivyo, kauli mbiu hiyo inamlenga mwanaume ambaye hatima ya mwanamke imo mikononi mwake au mwanamke mwenyewe?

Binafsi kauli hiyo siioni kuwa na mantiki katika kumsaidia mwanamke. Zaidi naiona  kama ni miongoni mwa yale yanayomdumaza mwanamke na kumfanya asichakarike; asubiri kuletewa riziki kwenye kiganja cha mkono kama si kutiliwa kinywani kabisa.

Philip Marmo na ujumbe kutoka SADC.

Lakini mie si mwakilishi katika SADC na tafakuri yangu inaweza kuwa na walakini. Maana wao waliafikiana kuwa nchi zote, kwenye umoja huo, ziwe na uwakilishi wa wanawake wa asilimia 50 kwa sekta zote kufikia mwaka 2015. Philip Marmo alikuja na kutueleza hadithi hiyo. Hatujui kilichopita baada ya hapo, lakini serikali iliamua kutenga asilimia 40 ya viti vya Bunge, maalum kwa wanawake.

Mwanamke huhitaji kuzunguka kupiga kampeni, wala kutayarisha sera na mikakati ya maendeleo jimboni. Kwanza, huna jimbo, utaanzia wapi hata ukitaka! Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unachaguliwa ndani ya chama chako tu!

Hili nalo likazua kadhia mpya. Mifumo ya kuwapata wanawake hao ndani ya vyama ikaacha kitahanani mitaani. Chama ‘kikubwa’ kikazua gumzo kuwa kimegawa ubunge wa ‘lipustiki’ hasa kwa vijana. Anaeijua kuipaka ikapakika, anaingia orodhani. ‘Ucheshi’ hasa kwa viongozi waandamizi wanaume ukatajwa kuamua nafasi ya jina lako kwenye orodha hiyo.

Upande wa pili nao ukaibuka na lake. Ukaja na ubunge wa ‘wastaa’, au ‘kujuana’ ukipenda. Mtoto, mkwe, mama watoto, karani wa muda mrefu, wote hawakuachwa nyuma; wakaingia Bungeni. “Shida gani, nasaba si ipo bwana na sisi si ndo wenye chama!” Yakazungumzwa. Viongozi wanawake chamani wakalalama kupigwa pute kwa ukosefu wa vinasaba husika. Viti maalum vyenye lengo la kumuinua mwanamke vikaingia doa, vikabadilishwa jina mitaani, vikaitwa ‘viti vya fadhila’.

Hukumu ikapita, wanawake 96 wakatangazwa kuingia ‘mjengoni’ kwa mlango wa nyuma. Kwa ajili ya majadiliano tuseme hili ni jambo jema. Tumemnyanyua mwanamke huyu, akafika Bungeni, tukamtarajia asikike. Aonekane ili wanawake wengine wapate ujasiri kutoka kwake. Miaka mitano ikaisha. Hansad zikapitiwa, wanawake wa viti maalum hawakujumuika katika kuchangia hoja wala kuuliza masuali Bungeni, isipokuwa wachache wa kuhesabu kiganjani.

Ikiwa lengo lilikuwa ni kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kwa kutumia mfumo huo, naweza sema lengo hilo halikutimia na hakuna tathmini iliyofanywa inayoonesha vyenginevyo. Mwanamke mwenyewe aliyewezeshwa kumbe hakuwezesheka seuze mafanikio kutiririka kwa mwanamke wa chini! Ndio kwanza anawaza kurudi tena Bungeni kwa nafasi ile ile ya viti maalum. Na vyama vya wanawake vikimpigia debe kuwa uwekaji wa kikomo kwa muhula miwili Bungeni ni kuzuwia maendeleo yake!

Mshahara wa milioni 12 usiotozwa kodi kila mwezi (kwa kila Bbunge) ungeweza kulipa ada ya mwaka ya masomo kwa takriban wanafunzi watatu. Hivyo, kwa mwaka mmoja ungeweza kusomesha wanafunzi watano digrii kamili ya miaka minne pamoja na fedha zao za kujikimu. Ukiongeza na posho na marupurupu mengine pamoja na kiinua mgongo kipindi cha Ubunge kinapokwisha, kila Mbunge angeweza kusomesha digrii kamili wanafunzi 50, ambayo ingekaribia wanafunzi 5,000 kwa kipindi cha miaka mitano kwa Wabunge wote. Makadirio yangu ni mepesi sana utanambia, basi toa elfu moja. Kwa miaka mitano tungeweza kusomesha wanafunzi wa kike 4,000!

H. Mdee

Ukiniuliza mimi kipi kati ya hayo mawili ni kumkomboa mwanamke, bila ya kujiuliza masuala mengi, nitaingia kwenye elimu kwani naamini ni rahisi kwa mwanamke mwenye elimu kujiamini, na hivyo kumuwezesha kuingia kwenye kinyang’anyiro cha nafasi za uongozi bila ya kuhitaji upendeleo maalum.

Si tumeona kuwa wapo wanawake waliogombea majimboni na wakashinda! Na tena wala hawakuanza leo wala jana. Huko makazini wanawake walioweza bila ya kuwezeshwa kwa namna hii mbona wamejaa tele!

Lakini mimi si mwakilishi kwenye SADC…

Juu ya hayo yote, nashauri usisubiri kuwezeshwa; jiwezeshe kwani mwenyewe unaweza!

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

This post has 9 Comments

9
  1. Ukiwezeshwa huwezi, ukiwezeshwa umewezeshwa. Huwezi kuwa umewezeshwa halafu hapo hapo ukawa umeweza, ama umeweza, ama umewezeshwa. Viwili hivi havichanganyiki kama maji na mafuta.

    Ukielewa msingi wa kanuni hii utagundua mzizi wa tatizo la dhana nzima ya “kuwezesha”. Not to say that it is not relevant when tailored towards some paradigm shift, with attention to the details of the matter.

    But one can argue that that is hardly what is transpiring in the current halls of power, academe and the respected rungs of civil society.

  2. Mmhhh hapo sijakuelewa vizuri ndugu Msangi. Manake naona hapo ulichofanya ni word play zaidi kuliko kingine. Maana yangu ni kama ifuatavyo. Unaweza kuwezeshwa na kushindwa, hivyo inaleta maana mtu akisema kuwezeshwa na kuweza.

    Kwani mtu akisema, jamaa kasaidiwa lakini hasaidiki, maana yake ni nini?, kuna tofauti kati ya hili la hili suala la kuwezeshwa?.

    Labda mfano mwingine uwe huu wa, dont give a man a fish, but teach him how to fish, hili je ukilinganisha na hilo la kuwezeshwa, linaleta maana au hivi ni vitu viwili tofauti kabisa?

  3. @Bahati

    Msangi anakusudia anaewezeshwa hawezi, hata akipata mafanikio basi inakuwa ‘kawezesheka’ na sio ‘kaweza’. Kuweza kunakwenda na juhudi binafi.

    Na ndio maana mwandishi akasema

    “Mwanamke mwenyewe aliyewezeshwa kumbe hakuwezesheka seuze mafanikio kutiririka kwa mwanamke wa chini!” ( na sio hakuweza kwa sababu huwezi kuwezeshwa ukaweza)

    Suala hili la ubunge wa viti maalum haliingii kwenye “dont give a man a fish, but teach him how to fish” kwa sababu hatuoni wanachofundishwa ili kuweza kujitegemea.

    Tuangalie target iko wapi. Kama target ni kutaka kuwafanya wanawake wawe na nguvu sawa na wanaume kwenye masuala ya siasa na uongozi, basi kumuwezesha huku kunakoendelea hakuna mantiki kwa sababu hawawezeshwi kushindana na wanaume kwenye majimbo na badala yake wanachaguliwa kwa vigezo ambavyo havitapelekea mwanamke kusimama mwenyewe jimbonii ili kuchaguliwa.

    Labda unaweza kusema wameliwezesha bunge kuwa na wanawake asilimia 40. Lakini kwa wanawake wa kawaida hakuna cha kujifunza kutoka kwa wabunge wa viti maalum zaidi ya kuwa kujipamba na kujipodoa kunaweza ‘kukufikisha mbali’, na sidhani kama hayo ndio mafunzo tunayotaka kutoa.

    @SN

    Hakuna neno ‘mushkeri’, neno sahihi ni ‘mushkeli’ ambalo hutamkwa mushkel’ au mushkeil’ kwa lafudhi ya kiarabu.

  4. Bila ya kuondoa taadhima yangu kuhusu suala zima la kusaidiana, suala ambalo ni muhimu bila shaka, nataka pia niseme kwamba suala zima la “kuwezesha” kinamama limekaa ki-mfumodume na pia Waingereza wanasema “condescending”.

    Naelewa kazi inaenda sio tu na mshahara, bali pia na ujira wa kijamii katika mambo kama wenzetu wanachokiita “credit”. Lakini popte unapoona watu wanagombea credit na kujitwisha ulimbwende wa kuokoa wanawake kwa sana huku wakitangazia dunia kwa sana, kazi halisi inakuwa haifanyiki. Kwa hiyo sishangai kusikia kwamba kuna watu wanapigia kelele “kuwezesha wanawake” kama hilo litafanya gurudumu la NGO kuwa na grisi ya kutosha (katika karama hii hata vyama vya siasa navyo ni NGO tu). Na zaidi, hapa sioni “kumfundisha mwanamke kuvua samaki” naona zaidi “kuwapa wanawake fulani samaki”. Huku wengine wakishangilia kwamba idadi ya wanawake bungeni imepanda, bila kuangalia matokeo.

    Tushaongea sana kuhusu idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shuleni kupanda, na kuhoji kuhusu matokeo. Sioni kama hili la kuongeza wanawake bungeni bila kuongeza matokeo lina tofauti yoyote nzuri. Tunaweza kupata tofauti mbaya tu ya kuridhika kwamba tunawanawake wengi bungeni, bila kuchanganua zaidi kwamba wanawake wenyewe hawajui katiba inasema je kuhusu nguvu za rais kwa mfano, na wana maoni gani kuhusu kubadilisha katiba. Nafikiri hili ni tatizo kwa wabunge wengi, hata wanaume, lakini tunapoongelea wanawake kwa nia ya “kuwawezesha”. How condescending, kama hakuna mtu anayeweza mwenyewe bila kusaidiwa, kuna umuhimu gani kujitukuza kwa “kuwawezesha” wanawake? Kwa upande mwingine, mbona hao wabunge wanaume nao wanawezeshwa kwa michango ya hali na mali na hatusemai kwamba “wamewezeshwa” ?

  5. @Msangi – “Kwa upande mwingine, mbona hao wabunge wanaume nao wanawezeshwa kwa michango ya hali na mali na hatusemai kwamba “wamewezeshwa” ?” Huu ni mfano mzuri wa kitu tunachoita double standard. Jamii yetu na nyingi za Kiafrika, hata katika nchi zilizoendelea bado zina mfumo dume. Kwanini mwanamke asiweze kutongoza mwanaume n.k, ndio hayo hayo, kwani akifanya hivyo ni malaya, pamoja hakuna ukweli uliodhitishwa na hilo, lakini huo ndio mtazamo wa jamii.

    Suala la kuezeshwa linaweza kuwa katika namna nyingi na tafsiri tofauti. Wao kupewa nafasi ya viti maalumu sio ni vipi linaweza kutolewa katika kuezeshwa, kwani hapa wanawezeshwa kisiasa, hasa ukizingatia bado ni ngumu mwanamke kuingia katika siasa. Lakini tatizo limekuja hapa, kama ulivyogusia wewe mwenyewe. Pamoja wengi wao wamewezeshwa lakini hakuna wanalolifanya. Walio wengi wao ndio hao ambao nilisema, hata wakiwezeshwa hawawezesheki.

    Nadhani Hyperkei alitoa mfano wa wao huishia kujipodoa tu. Wengi wao wangekuwa wako serious, wangetumia uwezeshwaji huo kupitia viti maalumu kuanza kujijenga kisiasa/ ku-spread political influence yao ili taratibu watu waanze kuona kuwa hata wanawake wanaweza. Tatizo lipo kwa hao wanaowezeshwa kwani wameshindwa/ wanashindwa kutumia nafasi zao vizuri kujijenga.

    Mimi bado sijaona tatizo la kuwezeshwa, bali suala ni je, unatumiaje nafasi hiyo wewe binafsi, ndio issue inakuja hapo. Lakini ulichosema kuhusu wanaume ni kweli hata wao huwezeshwa lakini mwanaume haolewi hata kama mwanamke ndiye aliyegharamia kila kitu, thats just the way things are, although hakuna tatizo kwenye kuwezeshwa regardless ya jinsia yako.

  6. @Bahati

    Tatizo halipo kwa hao wanaowezeshwa. Tatizo lipo kwa wawezeshaji na mfumo wa uwezeshaji. Ikiwa unamchagua mtu kwa vigezo vya urembo au nasaba unatarajia nini?
    Sisi wananchi pesa yetu ya kodi inakatwa kulipa mishahara ya wabunge wa viti maalum lakini hatima ya uchaguzi wao inaachwa wazi bila ya masharti kwa vyama ambavyo vinaweka vigezo tusivyovitaka.

    Kwa nini sisi wananchi tulipie uwezeshaji wa aina hii? Value for money iko wapi kama tutalipa watu mishahara minono kisha hatuoni faida yake?

    Jee uwezeshaji huu uliokwisha endelea kwa miaka mingi, umeleta faida gani kwa jamii yetu? Kuna tathmini zozote zilizofanywa zikaonyesha kuwa kuna faida yoyote?

    Suala lengine la kuangalia ni jee wanawake wana interest na hamu ya kuingia kwenye siasa?
    (sio suala la kuweza, ni suala la kutaka. Sawa na wanawake wengi kuwa na uwezo wa kuwa mechanical engineers lakini hawawi kwa sababu hawataki.)

    Kama hatujaibua interest kwa wanawake ya kuingia kwenye siasa, huu uwezeshaji unaoendelea una mantiki yoyote? Hivi mbunge aliechaguliwa kwa lipstick au nasaba anaweza kuamsha interest hiyo kwa wanawake wenye uwezo?

    Wengi huchukulia mfano wa nchi za Scandinavia ambazo uwakilishi wa wanawake bungeni unaridhisha lakini jee tumeangalia mifumo yao ya kijamii ikoje? Mgawanyiko wa kazi na majukumu katika ngazi zote za kijamii ukoje?

  7. @Hyperkei

    hapo nimekubaliana na wewe moja kwa moja, hivyo suala ni mfumo wa uwezeshwaji. Mimi suala langu lilikuwa kwenye hoja ya mwanzo ya Msangi, kuhusu kuwezeshwa na kuweza, kwani nina amini unaweza kuwezeshwa na kuweza, hivyo viwili vinauwiano.

    Hoja yako kuwa mfumo huu wa viti maalumu umekuwepo kwa muda sasa na hakuna matunda yeyote tuliyovuna nakubaliana na wewe. Nadhani kuna haja ya kuuangalia mfumo huo na kurekebisha mambo fulani fulani. Lakini tukisema tutoe kabisa utaratibu huu wa viti maalumu, huoni kuwa wanawake watakosa wawakilishi bungeni? Sasa sijui hilo litakuwa na madhara makubwa kiasi gani kwa wanawake au itakuwa tu business as usual.

    Nadhani kuna umuhimu wakutafuta balance kati ya kuwezesha wanawake kwa njia ya viti maalumu na kuhakikisha wanaweza na kufanikisha wanachotarajiwa kukifanikisha.

    Labda swali langu liwe hili, wanawake Tanzania hawana interest na siasa au mfumo dume ndio unawakatisha tamaa?..nini chanzo, nini tatizo hapo. Na je, unadhani nini kifanyike kuongeza interest ya siasa miongoni mwa wanawake wa Kitanzania?

    Swali la mwisho, unadhani wake za viongozi, kama wake za marais wanaweza kusaidia kwenye hili au? Na akina Mary Nagu je?

  8. Mimi sielewi hii dhana ya kuwa lazima kuwe na uwiano sawa bungeni. Inafaida gani? Manake nikitizama nchi kama Japan, Marekani, Uingereza, India, China, sioni wamepungua nini kwa kukosa uwakilishi wa kulazimishia wa wanawake.

    Kama wanawake hawana uwezo au hawana interest ya kuingia bungeni basi hakuna mantiki ya kulazimisha kuingiza wanawake wowote tu mradi wawe wa jinsia hiyo.

    Tunataka wanawake wenye kujitambua kuwa wao ni wanawake sio wanawake ambao wanaona sawa kuchaguliwa kwa vigezo ovyoovyo kama ngono au mtoto wa mdhamini wa chama.

    Naamini mwanawake wakiamua kuingia bungeni hakuna mfumo dume unaoweza kumzuwia, kwa sababu tumewaona wanawake walioweza huko na walioweza mengine magumu kuliko hayo hapo hapo Tanzania.

    Wengi wanahitaji msaada katika level za chini za kijamii na sio kwenye ngazi za juu. Ni bora hata basi wangeamua ku-fund kampeni majimboni kwa wagombea wanawake watakaojitokeza. Akishinda hapo tutajua kuwa wananchi wamemchagua na anaweza kuwa na manufaa.

    Pia hiyo ingesaidia vyama kuhakikisha vinaweka wagombea wanawake wenye vigezo vinavyokubalika kwa wananchi.

    Hao wake wa marais mimi naona wanatumika kukampenia waume zao tu wala hawawezi kuwa role model kwa wanawake wengine kwa sababu hawana qualities walizozipata kwa juhudi binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend