Wawepo, wasiwepo, mambo safi!

Na Michael Dalali

Kikao cha nne cha Bunge la Kumi kinachoendelea mjini Dodoma kinaibua maswali mengi, hasa kuhusu ufinyu wa ushiriki.  Ni miezi takribani tisa toka wabunge hawa watangazwe washindi baada ya mikiki mikiki ya kampeni, ambapo walijinadi kuhitaji kutumwa kwenda kuwakilisha wananchi katika chombo cha kutunga sheria za kuongoza nchi.

Hivi karibuni, naamini wengi wa wananchi ambao wamekuwa wakifuatilia vikao vya Bunge ni mashahidi wa ufinyu wa ushiriki wa wawakilishi wetu. Hali hii inaibua maswali mengi sana miongoni mwa wananchi wanaojali maslahi ya nchi.

“Hivi, Bunge hili linaendeleza tabia kama ya Bunge lililopita (Bunge la Tisa)?” “Kuna sababu gani hasa zinazowafanya wabunge kutomudu kushiriki vikao vya Bunge wakati hiyo ni sehemu yao ya kazi?” Haya ni baadhi ya maswali ambayo huwa nakumbana nayo toka kwa wananchi wakati wakifuatilia Bunge na kuoneshwa — kupitia televisheni — viti vilivyo vitupu.

Hakika inaibua ‘sintofahamu’ ambayo nadhani wabunge wenyewe ndio wanaweza kuichambua kwa kina.

Lakini, mawazo yanayoweza kuja akilini haraka haraka ni pengine; mosi, kikao cha Bunge kimekuwa kirefu sana kuliko vile vya awali ambavyo wabunge wanaweza kuhimili kutulia na kukishiriki kikamilifu. Hii inaweza kupimwa kwa kulinganisha vikao vitatu vya mwanzo, ambavyo havikuzidi mwezi, na kikao cha nne cha bajeti, ambacho ni takribani miezi mitatu.

Kwa upande mwingine, inawezekana wabunge wa Bunge la Kumi tayari wameshazoea mwenendo na utendaji kazi, na imewafanya kujua namna ya kuishi Bungeni ‘kiujanja-ujanja’. Ni miongoni mwa tabia inayotokana na kuanza kuzoea kitu fulani — baadaye mazoea yanapitiliza na kumfanya mtu kujisahau kabisa.

Hii inaendana na kujua namna ya kukwepa rungu la sheria na kanuni kumwangukia. Mathalani, kanuni za kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2007, ibara ya 71(1) (c) — Mbunge atakoma kuwa Mbunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika.

Pia, kanuni ya 143(1) inaweka wazi kwamba kuhudhuria vikao vya Bunge ni jukumu la kwanza la mbunge.

Kanuni hiyo hiyo ina kanuni ndogo ya pili inayonukuu ibara ya 71(1) (c) ya Katiba, kuwa, ikiwa mbunge atashindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake.

Na ikiwa mbunge atashindwa kuhudhuria nusu ya vikao vya Bunge bila sababu ya msingi, atapewa onyo.

Ikiwa mbunge atashindwa kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake kwa sababu maalumu, atatakiwa kupata kibali cha Spika.

Hapa tunaona kanuni za Bunge zinampa mamlaka makubwa mno Spika kumruhusu mbunge kutohudhuria vikao. Kwani yeye ndiye kisheria anayeidhinisha kutokuwepo kwa mbunge wakati kikao kinaendelea.

Swali la msingi: Je, wabunge wote tunaoona hawahudhurii vikao, wameidhinishwa na Spika?

Hata hivyo, inasemekana kuna baadhi ya wabunge, tena wa kuchaguliwa, wanaocheza na tafsiri za kanuni; kwa  mfano, ‘mikutano mitatu mfululizo’.

Wengine inasemekana hukwepa kanuni kwa kusaini mwanzo wa mkutano, kisha wanaendelea na shughuli zao binafsi na kuacha kuhudhuria vikao vingine wanavyopaswa kushiriki.

Hali hiyo inayoendelea inatoa picha ya uwepo wa haja ya kuangalia upya kanuni; kama baadhi ya wananchi wanavyoshauri, kuwepo na kanuni inayowabana katika mahudhurio ya “vikao” na sio “mikutano” kama ilivyo sasa.

Kupungua kwa mwamko na hamasa ya ushiriki inaweza pia kuwa miongoni mwa sababu inayoendana na kuzoea Bunge. Kwani inawezekana katika vikao vya awali wengi wa wawakilishi wetu walikuwa na upya ambao ulikuwa chachu ya wao kushiriki kikamilifu.

Richard Mushi, mtaalamu wa teknohama, akichangia juu ya mahudhurio hafifu ya wabunge, alitumia lugha ya taswira kuwasilisha hoja yake, “House girl wangu mara aje mara asije, tofauti na alivyoanza kazi, ni mazoea sasa yanafanya asiheshimu ofisi.” Ndivyo niwaonavyo wabunge wetu jinsi wanavyoenenda. Wameshazoea, sasa janja-janja kibao, hakika inaudhi.

Nachelea kuamini kuwa kupungua kwa mwamko na hamasa kumeanza kwa wawakilishi wetu na kuwafanya wasihudhurie vikao. Kama ni hivyo, basi ile hali ya business as usual (mambo kama kawaida) itakuwa tayari imetamalaki; ambayo inachagiza ufanywaji wa mambo bora liende kukamilisha muda na si kuzingatia ufanisi, tija na viwango kwa maslahi ya wananchi waliowatuma kuwawakilisha na taifa zima kwa ujumla.

Katika kujaribu kuendeleza tafakuri juu ya nini hasa ambacho kinaweza kuwa kinawasibu wawakilishi wetu, nafahamu Spika na waratibu hawawezi kugonganisha ratiba za Bunge na kazi za kamati au majukumu mengine, kiasi cha kufanya ukosefu wa ushiriki kuwa mkubwa kiasi kile, hasa hiki kikao cha bajeti kinachoendelea. Inawezekana kule kuchanganya siasa na biashara kukawa pia moja ya sababu ambazo zinawafanya wabunge wetu kutotulia Bungeni, kwani kwa baadhi ya wafanyabiashara, ambao wao ndio wahusika wakuu katika utendaji, inaweza kuathiri sana ushiriki madhubuti.

Kama ni shughuli ya jimbo husika, naamini wananchi wanafahamu na kuelewa kuwa wamemtuma mwakilishi wao Bungeni. Hivyo, wananchi makini wenye kujua haki zao za kiraia wanapaswa kumuhoji wanapomuona akiwa jimboni wakati shughuli za vikao vya Bunge zikiendelea.

Umuhimu wa kuwepo makatibu na watendaji wengine wa ofisi za wabunge unajitokeza, hususan katika vipindi vya vikao; endapo mbunge atakuwa makini kuhakikisha ana wasaidizi. Hawa ni watumishi imara kuweza kuendelea kuwahudumia wananchi katika kipindi ambacho mbunge anakuwa Bungeni.

Hakika, kama wananchi ambao tunawakilishwa na wabunge wetu, ni muhimu kuhoji nini hasa kinachowafanya kutokuhudhuria vikao vya Bunge kama moja ya majukumu na kazi ambazo waliomba tuwapatie.

Achilia mbali wale wabunge ambao tayari tumeanza kuoneshwa kupitia vyombo vya habari, kuwa licha ya kuhudhuria vikao, wanakuwa kama hawapo kwani wamekuwa wakiishia kuchapa usingizi wa pono au wakipiga soga wakati mijadala inaendelea.

Na hivi tunashukuru sana wananchi kupata fursa ya kufuatilia vikao vya Bunge kupitia vyombo vya habari kama televisheni. Je, visingekuwapo, hali ingekuwaje?

Michael Dalali anapatikana kwa njia ya barua pepe:  michael (at) michaeldalali (dot) com.

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend