Viongozi wetu wanataka wakumbukwaje?

Na Ramadhani Msoma

Kila mara niangaliapo jinsi mambo yanavyoendeshwa na walio kwenye madaraka ya umma, na hasa katika serikali za hivi karibuni, kuna jambo ninaloliona haliko sawa. Nafahamu kuwa ili uweze kufanya kazi yako vizuri iwe katika ofisi za umma au binafsi lazima uwe na ari na hamasa ya kuifanya hiyo kazi ili iwe na matokeo mazuri na mwisho wa siku tuwe na hayo maendeleo tunayoyataka.

Historia inatufundisha jinsi baadhi ya watu waliopata kuwa viongozi kwenye nchi nyingine  walivyoweza kufanya makubwa na kuacha majina yao mioyoni mwa watu waliokuwa wakiwaongoza — legacy. Kwangu mimi kiongozi lazima uhamasishwe na kuiacha hiyo legacy ili watu wakukumbuke hata baada ya kutoka uongozini na hata baada ya kutangulia mbele za haki (kufa).

Kwa bahati mbaya watu wetu katika uongozi suala hilo haliwapi motisha. Watu wanapenda vyeo ‘ubwana mkubwa’, na vitu vingine viendanavyo na ubwana mkubwa mathalan magari mazuri. Pia nyakati zingine kupata fursa za kusukuma masuala yao ya kujinufaisha binafsi (biashara halali na zisizo halali)  kwa kutumia hizo nafasi kupata hili au lile kinyume na utaratibu. Ukisoma historia za nchi za wenzetu na hata ya kwetu kwa wakati fulani kulikuwa na watu wenye hamasa hiyo, mfano Mwalimu Nyerere, kina Bibi Titi au Edward Sokoine ambao bado wanaishi kwenye mioyo ya Watanzania.

Kwa nchi za wenzetu zinazopiga hatua kubwa za kimaendeleo, viongozi wao walikuwa na ari ya kufanya makubwa kwenye nchi na kuacha majina mazuri kwenye utendaji wao kwa mataifa na serikali wanazoziongoza. Watu kama Mahathir Mohamed (Waziri Mkuu wa zamani wa Malaysia), Lee Kuan Yew (ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Singapore) bado wanaishi kwenye mioyo ya watu waliokuwa wakiwaongoza  kwa michango yao katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi.  Watawala wetu wanajua haya lakini hawana hamu hiyo ya kukumbukwa na kuingia kwenye historia ya nchi hii! Na kama huna hamasa hiyo bali tu ya kujitajirisha wewe na familia yako kwa kweli huna haja ya kuumiza akili yako kutafuta uongozi wa umma. Wananchi wanapaswa kuwaogopa viongozi wa namna hii. Wanapaswa kuwakataa na kutokuwapa ridhaa.

Tatizo kubwa linalosababisha ukosefu wa hamasa, ikiwemo ya mambo ya msingi kama kupiga vita umaskini au kupambana na rushwa ambayo ni matatizo yanayoikwamisha nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo, ni kutokuwa na mipango na fikra za kutizama masuala kwa muda mrefu. Wengi wa watawala wetu kutokana na matendo yao yanasanifu zaidi fikra zao kuwa katika vipindi vifupi vifupi kwa uwepo wao madarakani (kadiri ya vipindi vya kiuchaguzi). Hawataki kufikiria na kutizama taifa katika muda mrefu hata baada ya wao kuondoka madarakani muda mrefu baadaye kwa hiyo hawana haja na kuacha majina yao yatajwe kwa sababu nzuri.

Kuondoa umaskini na kupiga vita rushwa kwa vitendo badala ya maneno matupu ya kwenye majukwaa ya kisiasa tu ndiyo ingekuwa msukumo hasa unaowapa hamasa watawala wetu kutaka nafasi serikalini. Kwa kweli Tanzania isingewasahau kwa mchango huo lakini hamna juhudi zinazotia matumaini, yaani juhudi hazilingani na ukubwa wa matatizo. Bado kuna upungufu hasa wa kiutendaji kama tukipima kwa matokeo.

Nchini Brazili rais wao wa zamani, Lula da Silva,  atakumbukwa sana katika kujenga uchumi wa kisasa nchini mwake na hasa kupunguza umaskini wa kutupwa kwa kuwaondoka Wabrazili milioni 30 kutoka kwenye umaskini wa kutupwa. Je, viongozi hujiuliza wanataka kuwaondoa Watanzania wangapi kwenye umaskini wa kutupwa labda ndani ya miaka mitano?

Brazili ni mbali lakini tuangalie Waethiopia watamkumbukaje Waziri Mkuu wao Meles Zenawi  aliyefariki mwaka jana (2012)  ambaye alisimamia ukuaji wa uchumi wa Ethiopia kwa wastani wa asilimia 11 kwa miaka saba toka mwaka 2004 mpaka 2011 (kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)? Mwandishi na mchumi aliyebobea, Joseph E. Stiglitz, aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa Globalization and Its Discontents  juu ya Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Ethiopia: “Meles showed that, with the right policies in place, even a poor African country could experience sustained economic growth. (Meles ameonyesha kwamba, kukiwa na sera nzuri, hata nchi masikini ya Afrika inaweza ikapata maendeleo endelevu ya kiuchumi.)

Nawapongeza baadhi ya watendaji na mawaziri katika awamu hii hasa baada ya mabadiliko yaliyofanyika kwa kujitahidi kubadilisha hali ya wizara wanazoziongoza na taasisi zake. Tunapaswa kutambua bado kuna kazi kubwa mbeleni. Nilipata fursa kumsikiliza waziri wa uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati wa uzinduzi wa safari za treni katika mji wa Dar es Salaam, kutoka Ubungo kwenda Stesheni, akasema kuhusu hatua hiyo kuwa ni “kiburi tu cha mtu masikini”. Naamini tunahitaji kiburi hicho cha kujaribu pia kwenye maeneo mengine ya kupunguza kero hapana nchini.

Kwa ujumla uongozi ni dhamana na sio kazi tu kama kazi nyingine kwamba mwisho wa siku ili mradi mkono uende kinywani. Kiongozi kwa kweli inabidi awe mtu anayeweza kujinasibisha na watu masikini ambao ni wengi katika nchi hii. Mara nyingi naona kama wapiga kura hatufahamu ni nini viongozi wetu tunataka watufanyie na namna gani wasipoenenda tuwawajibishe ndio maana tunavumilia tu utendaji mbovu.

Ili mtu awe kiongozi lazima awe na hamasa ya kuleta mabadiliko na awe na hamasa ya kuacha jina zuri nyuma yake. Lazima awe mtu mwenye maono ya mbali, uelewa wa kutosha wa jamii hii ya Watanzania, anayefahamu matatizo ya Watanzania na kama aliwahi kuwa kwenye uongozi basi angalau tujue aliwahi kufanya nini kwenye uongozi wake kabla hatujamchagua kuwa mbunge au rais.

Kinachosikitisha hamasa ninayoijadili haionekani katika nyuso na juhudi za wataka uraisi mwaka 2015, naona uroho wa madaraka. Wataka uongozi wengi  hawatuonyeshi uongozi sasa! Watuonyeshe uongozi kabla ya kuanza hizo mbio zao. Haiwezekani watu watumie muda mwingi kutafuta uongozi kana kwamba hiyo ni shughuli ya kudumu, na wako kwenye uongozi wa aina fulani tayari, badala ya kutumia muda huo kuonyesha uongozi. Tumeshashuhudia baadhi ya viongozi walioenda na njia ya kutumia nguvu na mikakati mingi kupata madaraka na namna walivyoshindwa kuibadilisha nchi. Hivyo hatupaswi kuingia katika mtego ule ule.

Barua pepe ya mwandishi: ramamsoma (at) gmail (dot) com

Previous ArticleNext Article

This post has 2 Comments

2
  1. Asante sana kwa maoni yako na ufafanuzi kuhusu uongozi ma viongozi ,umejikita kataika Tanzania lakini.Mambo ni yale yale kuengineko Afrika.Viongozi wengi wanaochaguliwa wanaweka bele masilahi yao tu.Hushindwa kusaidia raia kutoka umaskini wa kutupwa ingawa hudai kupitia vyombo vya habari kwamba wanafanya kazi nzuri ya kuhudumia wananchi.Inabidi wapiga kura wawe makini wakati wa uchaguzi pia wakatae rushwa.ili mataifa ya Afrika apige hatua kimaendeleo.

  2. Jean kweli unavyosema matatizo ya uongozi yapo Afrika nzima.Ni muhimu sana kwa sisi watu wakawaida kudai kutendewa vema na viongozi wetu ambao kiukweli wamekuwa watawala zaidi kuliko kuwa viongozi.Asante kwa kuchangia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend