Jinsi ya kuokoa biashara yako isife kipindi hiki cha COVID-19


Katika kipindi hiki cha COVID-19, mambo mengi yamebadilika sana. Dunia haipo sawa tena kama zamani. Kila kitu kimekuwa tofauti, mienendo ya binadamu imebadilika. Nayo biashara imebadilika, haipo sawa kama zamani.

Mizigo toka China haifiki kwa ukubwa ule wa kawaida, watu hawakusanyiki na kukutana tena sehemu za biashara. Kila mtu anajiweka mbali na mazingira ya kawaida. Hii yote ni sababu ya virusi vya Corona.

Ni katika kipindi hiki ambacho unatakiwa kujiongeza ili uweze kwenda na wakati. Ndio, ni wakati huu wa COVID-19. Unahitaji mbinu na ubunifu mpya ili uweze kuishi katika kipindi hiki cha mpito, ndio maana leo nimekulete njia tano za kujiongeza ili biashara yako isife katika kipindi hiki kigumu.

Ni katika kipindi hiki ambacho unatakiwa kujiongeza ili uweze kwenda na wakati.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia katika biashara yako kipindi hiki cha COVID-19:

1. Punguza matumizi

Chunguza biashara yako pale inapopoteza pesa nyingi, kama kwenye kodi, na fikiria kuuza vitu mtandaoni. Kama kwenye matumizi ya kawaida basi hakikisha unapunguza vile kadri inavyowezekana.

Katika kupunguza matumizi ni sio pesa tu, hata kwenye vitu. Hakikisha kila unachouza unakitoa kwa kiwango kinachotakiwa na watumiaji. Kama ni Mama wa mgahawani hakikisha haupiki tena kilo 10 kama zamani, ila pika kutokana na mahitaji ya wateja wako. Kama ulikuwa unanunua mzigo mkubwa wa nguo, basi chukua kiasi kile ambacho hakitakuwa shida kuchukuliwa na wateja wako.

Tumia kile unachokiingiza, na weka akiba pale inapowezekana. Punguza matumizi na huduma unayotoa kulingana na wateja wako. Hiyo itasaidia kupatikana kwa hela ya akiba ambayo itakuwa msaada kukuinua kama mtaji pale unapokwama.

Tumia kile unachokiingiza, na weka akiba pale inapowezekana.

2. Soma alama za nyakati

Mambo hayapo kama zamani tena, hivyo inabidi uyaelewe mazingira ya sasa. Kama biashara yako inahusisha mikusanyiko ya watu, basi soma alama za nyakati. Kama biashara yako inahusisha matembezi, basi jua kipindi hiki sio nyakati zake.

Hivyo ni vema kuelewa aina ya biashara yako na nyakati za sasa za COVID-19. Tafuta njia za kisasa ambazo zitakufanya uweze kuwafikia wateja wako bila hatari kwako na kwa wateja wako. Ni katika nyakati hizi ambazo unatakiwa kufuata taratibu za afya kuliko nyakati zote.

Tafuta njia za kisasa ambazo zitakufanya uweze kuwafikia wateja wako

Weka maji ya kunawa nje ya saluni yako. Hand sanitizer iwe kama maji ya baraka dukani kwako. Na barakoa iwe ile nguo uipendayo pale unapohudumia watu. Na huko ndio kusoma alama za nyakati ili kuendeana na mazingira ya sasa. Kamwe usimpe wasi wasi wala hofu mteja wako, bali ifanye biashara yako sehemu salama kwake, hakika na kesho atarudi tena.

3. Fanya kitu kipya na jifunze kutoka kwa wengine

Angalia wengine wenye biashara zinazofanya vizuri wanafanyaje. Iga pale unapoweza na boresha yako pia. Kujifunza hakuna mwisho, katika kipindi hiki ndio unatakiwa kujifunza vitu vipya ili uende sawa na mazingira ya sasa. Panga mkakati mpya wa biashara yako, usiuze kwa mazoea ya zamani.

Ni katika kipindi hiki unachotakiwa kujifunza kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wako. Kama inawezekana kuwafikishia wateja wako huduma yako, ongeza njia salama “Home Delivery”. Kwa biashara ya vyakula angalia vile unaweza fanya package nzuri na “take away”.

Ni katika kipindi hiki unachotakiwa kujifunza kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wako

Hakikisha unajifunza kitu kipya kitakachookoa biashara yako katika kipindi hiki, hata kama itabidi kumuiga mtu, Iga kama hauvunji sheria kufanya hivyo. Lazima mipango yako iwe tofauti kama siku zote, mipango mipya ndio itakuhakikishia biashara yako inaenda sawa.

4. Vaa viatu vya wateja wako

Jiulize ni nini hofu ya wateja katika kipindi hiki? Na ufanye kitu gani ili kuwaondolea hofu hiyo ili waendelee kununua bidhaa yako. Usikose kufanya biashara kama ulivyokuwa unafanya siku za nyuma.

Usikose kufanya biashara kama ulivyokuwa unafanya siku za nyuma.

Ingia mawazoni mwao na waza ni nini kitawafanya waamini usalama wa bidhaa zako, na fanyia kazi eneo hilo. Hakikisha unavaa barakoa, maji tiririka yapo katika biashara yako. Ipo nafasi ya kutosha kwa ajili yao ili kuepuka misongamano.

Kwa wale wateja wanaogopa kutoka nje, wapelekee mpaka nyumbani. Kama wanaogopa mkusanyiko, basi chukua oda zao hata kwa WhatsApp. Hakikisha unaishi nao kama kawaida, ila kwa kufuata taratibu zote za afya. Usimpoteze mteja wako hata mmoja katika kipindi hiki.

Jiulize, wewe ungekuwa wao ungetaka nini kiboreshwe? Na anzia hapo kuboresha biashara yako.

5. Kuwa na mawazo chanya

Kila asubuhi amka na mawazo chanya. Amini kuwa itakuwa siku njema kwako huku tukivumilia yale tunayoyapitia kipindi hiki. Usinyongeke na biashara yako, maana ipo siku huu ugonjwa hautakuapo tena. Na biashara zitaendelea kama kawaida.

Muhimu ni kujua kuishi vizuri na biashara zetu katika kipindi hiki, fanya tathimini ya hasara na vile unavyoweza kuamka tena pale mambo yatakapo kaa sawa. Usiache kufanya unachokifanya, ila kuwa mbunifu. Kuacha kufanya sio dalili njema ila jitahidi kutafuta sababu na njia za kuendelea kufanya.

Usiache kufanya unachokifanya, ila kuwa mbunifu.

Kitu kikubwa cha kuzingatia katika kipindi hiki, ni vile unapanga mambo yako na maamuzi unayoyachukua katika biashara. Jitahidi kupanga vizuri ramani yako ya ubunifu na mauzo, huku ukichukua maamuzi yaliyosahihi katika ustawi wa biashara. Hata katika nyakati ngumu kama hizi, bado kuna fursa, cha msingi ni kusimama katika mkakati kazi ulio makini na unaoendana na mazingira ya sasa. 

Wakati tunapambana na mishe zetu tusisahau kuchukua tahadhali ya COVID-19. Hilo ndio la muhimu zaidi, maana mtaji wa kwanza ni afya.

Previous ArticleNext Article
Leonce Godfrey has been in the field of Digital media and digital marketing with more than 3 years experience working in various capacities with highly reputable companies and organizations. He is writer, storyteller, content creator, photographer and journalist by professional. He simply amazing.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend