Msekwa ameajiri wahuni wa kutosha

Na Jenerali Ulimwengu

KATIKA hali tuliyoishuhudia wakati wa kura za maoni ndani ya chama – tawala si rahisi kwa ye yote anayefuatilia masuala ya siasa za nchi hii kupuuza masuala yaliyojitokeza. Masuala haya ni mengi, na bila shaka tutaendelea kuyajadili kwa muda mrefu, lakini wiki tunaweza kuyagusia baadhi yake kabla hayajapoa.

Kwanza, kama nilivyosema wiki jana, siasa za chama-tawala kunyata. Mambo tuliyoyashuhudia katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM yanakifu, yanachusha, yanatia kinyaa.

Lakini ni zaidi ya hayo. Kuchusha pekee, ama kutia kinyaa, si jambo jema na wala si hali ya kupendeza. Mtu anaposema anaona kinyaa, labda athari kubwa inayoweza kumtokea ni kupata kichefuchefu na hatimaye  kutapika. Kwa yale tuliyoyaona mwaka huu, si uongo kusema kwamba kama kuna watu miongoni mwetu ambao bado wana chembe za uungwana, wamepata kichefuchefu, na wengine labda walijisikia kutapika.

Lakini kichefuchefu si sawa na kifo, na hutokea mtu aliyekolewa na kichefuchefu akafikia hata hatua ya kutapika na bado asife iwapo kutapika kwake hakutokani na maradhi yaliyo mwilini mwake bali ni kutokana na kichefuchefu kinachotokana na hali ya kuudhiwa na kuwa na kinyaa. Binadamu wanao uwezo mkubwa wa kushuhudia mambo ya kuudhi na bado wasife kutokana nayo.

Hata hivyo, mambo hayo yanaudhi, yanakera. Isitoshe, baadhi ya yale tuliyoyashuhudia siyo tu yanaudhi, ila pia yanatisha. Yanatishia usalama wetu kama Taifa kwa sababu yanao uwezo wa kutupeleka mahali ambako hatukutarajia kwenda, mahali pa kutuhilikisha.

Niliwahi kueleza kwamba tumeanza kutumia lugha nyepesi kuelezea dhana nzito. Nimekuwa nikijaribu kueleza kwamba kile tunachokiita ‘kero’ mara nyingi si kero bali ni janga, ni hatari, ni saratani, ni ukoma. Rushwa, kama rushwa, ndani ya jamii haiwezi kuwa kero; ni janga kwa sababu inao uwezo wa kuua jamii nzima.

Lakini, pia, rushwa ni kielelezo kimojawapo cha uoza, na vielelezo vipo vingi. Katika michakato ya uchaguzi, ni kweli, tumeshuhudia vitendo vya rushwa, kwa maana ya watu kugawa fedha na wengine kupokea fedha hizo kwa madhumuni ya kuathiri matokeo ya uchaguzi. Hiyo ni rushwa kama ile anayotoa mtu mwenye shauri mahakamani kumpa hakimu, au mtu mwenye tatizo la kiusalama kumpa askari polisi.

Uoza wa aina hiyo umetokea sana katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama-tawala, na ni vyema kuukemea kwa nguvu zetu zote, na ni lazima kukataa na kutupilia mbali kauli za kipuuzi za watu kama wasemaji wa chama-tawala niliowasikia. Upuuzi ukisikika, tujifunze kuutaja kama upuuzi, na huu ni upuuzi.

Sasa, ndani ya chama-tawala wametokea wahuni waliohamia huko na kisha wakapewa kibarua cha kutoa matamko ya kipuuzi mara kwa mara, maneno yenye mantiki iliyopinda na isiyoweza kumshawishi hata mgonjwa wa Mirembe. Hawa wanajulikana, asili yao inaeleweka, na kwa maana hiyo hawashangazi wanapotoa matamko yasiyokuwa na mantiki yo yote ila tu kujaza nafasi katika vyombo vya habari kwa sababu ni muhimu kwa wanajamii kujua kwamba chama-tawala kimejibu shutuma hii au ile.

Lakini kwa kuwaendekeza wapuuzi kama hawa, na kuwazoea kama wasemaji wa mara kwa mara wa chama-tawala, ipo hatari kwamba hata watu wasiotarajiwa kutamka maneno ya kihuni kuingia katika mkumbo huo na kujisemea tu, alimradi wamesema. Mazoea huzaa hulka, na hulka huzaa utamaduni.

Ndivyo ninavyomwangalia Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa chama-tawala, na jinsi anavyozungumzia janga kubwa la uoza ndani ya chama chake. Msekwa anasema kwamba, na anataka tuamini kwamba tatizo la rushwa haliwezi kuwekwa mlangoni kwa chama chake, kwa sababu ni tatizo la Taifa zima.

Hapa kama kuna mtu amemwelea Msekwa, naomba anisaidie. Ni kweli tatizo la rushwa ni la Taifa zima, lakini kwa nini liseelekezwe kwa chama-tawala, chama ambacho, kama wanavyotamba wasemaji wake, ndicho kilichopewa dhamana ya kuongoza Taifa letu? Ni chama hicho kilichoomba, tena kwa nguvu za fedha na jeuri za aina nyingine, kipewe madaraka ya kuongoza nchi yetu, na hiyo dhamama kikapewa.

Sasa, kama nchi nzima imejaa rushwa, kama alivyoeleza Msekwa kwa ufasaha mkubwa, sisi tumwulize nani kama si chama hicho? Lakini labda Msekwa, kwa kuathirika kutokana na ule upuuzi ulioingizwa ndani ya chama chake na wale wahuni niliowataja mapema, alisahau kwamba alikuwa anaulizwa swali kuhusu chama chake.

Endelea kusoma hapa…

Previous ArticleNext Article
Steven was born and raised in Dar es Salaam, and moved to Germany for his studies. He graduated with a BSc. in Physics (Jacobs University Bremen), and then a MSc. in Engineering Physics (Technische Universität München). Steven is currently pursuing a PhD in Physics (growth of coatings/multilayers for next generation lithography reflective optics) in the Netherlands. He’s thinking about starting his own business in a few years; something high-tech related. At Vijana FM, Steven discusses issues critical to youths in Tanzania, music, sport and a host of other angles. He’s also helping Vijana FM with a Swahili translation project.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend