Vazi la Taifa kwa kamati, imla iso tamati

Na Kiranga

Nimekuwa nikifuatilia habari ya vazi la taifa kwa zaidi ya mwaka sasa. Mwanzoni kabisa nilifikiri ni habari ya waandishi kuongeza chumvi kwa kutaka kuuza magazeti, maana haikuniingia akilini kwamba kwa muda huu na matatizo yote yanayotukabili kweli kuna “kiongozi” anayeweza kuweka vitu katika mizani atataka kujishusha kwa kudakia kisicho kipaumbele. Nikajiuliza, lakini tangu lini viongozi wetu wa sasa wakategemewa kuweka vitu katika mizani? Nikataka uhakika zaidi.

Kukaja kauli, kamati, vikao vyenye ushahidi wa picha zilizosherehekewa, na mpaka vitisho vya ki-Augustine Mrema vilivyotoka kutoka kwa Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr. Emmanuel Nchimbi, kuhusu umuhimu wa kumaliza mchakato huu wa “kutafuta” vazi la taifa. Nikaona hakuna sababu ya kuendelea kunyamaza, hata kama ni kwa kuonesha dunia na Watanzania wenzangu tu kwamba kazi tunaijua na kanyaboya tunaijua tukiiona hata maili elfu kumi.

Kwa nini naliita zoezi hili kanyaboya? Ni zoezi lililojikita zaidi katika kuonesha serikali inafanya kazi, kuliko katika kufanya kazi yenyewe. Halina uhalisi. Ni hadaa ya wazi ikimbiliayo kututusi. Napata tabu kuelewa kijana anayejitambulisha na usomi kama Dr. Nchimbi, ambaye tungetegemea apeleke nguvu mpya serikalini kwa kutetea ushirikishwaji moja kwa moja wa wananchi, bila mazingaombwe ya kamati za kiimla ziso tamati, anakuwa mshabiki wa kuiongezea serikali kazi ya kupaka rangi nyumba bila kurekebisha msingi wa nyumba unaodidimia kwa nyufa.

22.12. 2011. Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dr. Emmanuel Nchimbi akizundua kamati maalum ya kutafuta Vazi la Taifa. Picha na Francis Dande; issamichuzi.blogspot.com

Waziri anahamanika na vazi la taifa wakati wananchi hawana hata mavazi? Seuze la taifa! Swala zima la “Vazi la taifa kwa kamati ya kiserikali” linanuka utawala wa kiimla unaokusudia kutuma ujumbe kipropaganda kwamba “wananchi hamuwezi kupata vazi mkalienzi wenyewe mpaka msaidiwe na serikali”. Ni tusi kwa mtu anayefikiri. Mi’ si mpinga serikali kwamba niseme serikali haitakikani. Kuna masuala makubwa, magumu, yanahitaji kusimamiwa na serikali.

Mathalani, hususan kwetu huku, hatujafikia kiwango cha uchumi wa kusema watu binafsi watasimamia mtandao wa barabara. Inabidi serikali ilipwe kodi, nayo itumie kodi kuimarisha miundombinu kama barabara. Ingawa hata hili nalo kuna mabepari wa soko huria wanaweza kutaka liachwe kwenye nguvu za soko, lakini hata nchi zilizoendelea tunaona serikali zinasimamia hili. Kwa hiyo, yapo mambo haya. Sipingi serikali kufanya kazi yake pale inapotakiwa. Lakini vazi la taifa? Baada ya hilo tutataka serikali itupangie nini tena? Chakula? Maana waziri wa afya anaweza kusema Watanzania tunahitaji kula mboga fulani kila Alhamisi ili kudumisha afya.

Nani ni mtoto hivyo kuhitaji kuvishwa? Vazi gani la taifa ambalo halihusiki na propaganda za kisiasa litatoka katika kamati ya kiserikali? Tayari kwa kufanya vazi la taifa jambo la kamati ya kiserikali, wamelitia doa la siasa jambo la kiutamaduni. Watu wengine wataanza kuangalia “kamati yenyewe yumo nani?” Mmiliki wa redio inayokuwa karibu sana na chama tawala? Mambo ya kutuzuga tu na kutengeneza ukondoo kwa wananchi na mianya ya rushwa. Sina nia ya kupanda mbegu ya kugawanya watu, lakini kuna matatizo mengine tunaweza kuyaona hivi hivi watu wanayapalilia bila sababu.

Kama leo wakisema “vazi la taifa hili hapa”, kesho nini kitawazuia kusema “na duka mtakalonunulia hili hapa”, na keshokutwa tunarudishwa enzi za Mfalme Jean-Bédel Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kuambiwa “wanafunzi wote mtabadili sare zenu na shurti mnunue duka la bwana mkubwa mmoja”. Au enzi za kamanda Thomas Sankara aliyekuwa akifanya ukaguzi mwenyewe ofisi za serikali kuhakikisha wafanyakazi wa serikali wanavaa “vazi la taifa”. Lakini angalau Sankara alikuwa mchuuzi wa “nchi ya kufikirika” aliyekuwa na mada ya kutaka viwanda vya kwao vishone nguo zaidi, sio watu washabikie mitumba ya California tu. Nchimbi wetu anahubiri vazi la taifa bila kufufua viwanda, sijui tutaliagiza kutoka Pakistani?

Najua unaweza kusema napeleka mambo mbali, lakini dhima hii ya kupumbaza wananchi kwa umangimeza uliojaa imla ni ile ile ya Bokassa tu, wafanye watu wajione wanyonge na hawawezi hata kile kidogo ambacho wanaweza, kisha badala ya kufanya kazi muhimu kama kushughulikia ubora wa pamba yetu, na kufufua viwanda vya nguo pamoja na kuhuisha vikundi vya mafundi washoni kwa kuwezesha mazingira ya mikopo nafuu (kazi nzito ya serikali), tafuta mazingaombwe yasiyo mwanzo wala mwisho kama kamati ya “Vazi la Taifa”.

Tunashuhudia ukoloni ukirudi upya. Ukoloni ambao ni mgumu sana kuung’amua kwa sababu mkoloni sasa si Muingereza, ni mweusi mwenzetu. Badala ya kutuambia “kibwaya chako ni vazi la kishenzi, vaa suti”, mkoloni huyu wa leo anatuambia “wewe huwezi kuchagua vazi zuri, tuachie sie watawala wako tukupangie”. Hiyo habari nzima ya kwamba kamati itatafuta vazi halafu litapelekwa kwa wananchi ni kutafuta mzozo tu, na kwa kweli inanikumbusha hukumu za sinema za “cowboys” wa zamani Magharibi ya Marekani ambapo watu wanakubaliana kumnyonga “mhalifu” kwanza, halafu kabla ya kumnyonga wanajidai kumpa tia nafasi ya hukumu ya haki.

Watu wakikaa kimya si kama hawaoni viongozi wanavyotapatapa kwa kushindwa kufanya la maana katikati ya utajiri wa umasikini. Hasha, pengine wanawavutia pumzi mlitangaze hilo vazi la taifa walichomelee moto mbali. Mtu hana chakula, dawa, elimu, mavazi wala matumaini yoyote katika maisha, unamwambia habari za vazi la taifa? Si ataona unamtukana? Na ukisema sio lazima wote wawe nalo hilo vazi, je litakuwa “vazi la taifa” kweli? Au tunataka kurudishana kwenye propaganda za kuuma na kupuliza kama Mobutu Sese Seko na sera zake za danganya toto kwa kisingizio cha “Uafrika”?

Nchimbi na kamati ya mazingaombwe, wingu la “vita baridi” lishaisha, ukungu umetoka machoni pa watu. Mnapofanya kazi kweli tunaona, mnapotapatapa kujionyesha mnafanya kazi kama mtu anayechafua meza kwa makaratasi bila kufanya la maana tunaona. Kama mna nia ya kweli kupata vazi la taifa vunjeni kamati, rudini kusuka mpango wa kufufua viwanda vya nguo na kuweka mazingira ya mafundi ushoni wadogo wadogo pamoja na wanamitindo wetu kuweza kufaidika kwa kushona nguo nchini. Wananchi wanaweza kuchagua wenyewe. Hawakuhitaji kamati wala kikao kuvaa khanga na vitenge, vikoi na migolole. Hizi habari za “vazi la taifa kwa kamati” zinaleta maswali mengi kuliko majibu, mwishowe mtaona aibu bure kwa kutaka kuturudisha mwaka 1984 wakati jini la muamko wa kisiasa lishatoka katika chupa ya “chama chashika hatamu”. Wengine tushajua viongozi wamegeuka watawala, watawala wakageuka wa-twawala, na “chama chashika hatamu” kimegeuka “chama chashika patamu”.

Kama Mwalimu Nyerere, aliyekuwa na kazi ya kulijenga taifa hili, kipenzi cha wengi, aliyetawala bila televisheni ya kuonesha watu vibikini vya Hollywood bali RTD iliyojaa “Mazungumzo Baada ya Habari” ya Abdul Ngalawa, MWATEX bila mitumba, magazeti ya Uhuru na Mzalendo bila tovuti za ukosoaji na TANU/CCM bila chama cha upinzani, alishindwa au hakutaka kuwepo vazi la taifa, nini kinafanya viongozi wa Tanzania ya leo waamini kwamba vazi la taifa la kuamuliwa na serikali ni jambo jema na linawezekana? Au Waziri wa Vijana , Michezo na Utamaduni hajui methali ya Kiswahili isemayo, “Samaki mkunje bado mbichi, akishakauka hakunjiki”? Je kasikia “Fupa lilomshinda fisi mbwa hataliweza”?

*    *    *

Ndugu msomaji, una maoni gani? Je, Watanzania tunahitaji Vazi la Taifa? La kuchaguliwa na kamati maalumu ya serikali?

Makala zaidi kutoka kwa Kiranga:

Previous ArticleNext Article
Joji was born and grew up in Dar es Salaam, Tanzania. He graduated with a B.Sc in Biochemistry in Germany, and is now pursuing a Masters degree in Microbiology & Immunology at the Swiss Federal Institute of Technology (ETH) in Zurich, Switzerland . Joji is particularly interested in matters related to global health, and basic science research that tackles public health challenges. He is engaged in mentoring Tanzanian students in higher education issues, most notably at the Kibaha High School. In this capacity, Joji blogs with Vijana FM about scientific research and development, and how youth can gain greater access to higher learning.

This post has 27 Comments

27
  1. Nipo nje ya mzunguko wa habari hivi sasa kwa hiyo nashindwa kujua background ya uamuzi wa serikali.

    Hivi serikali imeeleza sababu zozote za kwa nini inadhani sasa ni wakati muafaka wa kutafuta vazi la taifa? Vazi hilo wanatarajia tulitumie wapi, kwa faida gani? Ukosefu wa vazi la taifa unatuathiri kwa kiwango gani?

    Anaejua chochote kwenye hilo, naomba anifafanulie

  2. Nimefurahishwa na makala yako nzuri! Una hoja za msingi sana, hasa kwa mtu anayeweza kusoma kati ya mistari au nyuma ya maneno. Kama tungeondoa ladha ya hasira (ambayo ni halali kabisa!) katika makala yako, kwa ufupi ingeweza kusomeka hivi:
    Vazi la taifa litakuwa na maana tu kama
    -Sera za serikali zinazohusu biashara ya nguo na mavazi zingehakkikisha mazingira rafiki kwa viwanda vya ndani na maisha ya kijasiriamali ya watanzania wanaojihusisha na usanifu na usanii wa vitambaa na nguo (cultural industry yetu) ili mchakato wa vazi la taifa ulete maana ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
    -Vazi litakuwa milki ya Watanzania kwa kutengenezwa nao wenyewe
    -Litazalishwa kwa viwango na gharama ambazo watanzania watamudu kulinunua
    Baada ya kuyasema hayo, inabidi tujiulize kama tukikosa timu ya taifa, Tanzania itaathirika vipi! Kwani kushughulikia masuala ya timu ya taifa ni ‘kucheza’ wakati tuna mambo mengine muhimu?
    Mavazi si kitu muhimu?? Dhana ya vazi la Taifa ni upuuzi tu?? Kama ni upuuzi, umeibukia wapi? Ili kama ni upuuzi basi tuukomeshe. Na tukishaukomesha wale vijana wetu ambao wanaifanya fani ya mavazi kama kipaji, kazi na njia yao ya kipato watakuwa katika nafasi gani?
    Nadhani tuchukue muda, tuvute pumzi, tuliangalie upya na tushauri pale inapowezekana.

  3. Mjumbe Merinyo,

    Vazi la taifa si upuuzi, ni muhimu. Ila kutaka kupata vazi la taifa kwa kamati ni kama kutaka kupata utamaduni kwa sheria. You can’t legislate culture. Utaleta ukandamizaji tu. Sasa leo ukiwaambia Wamasai vazi la taifa hili, na wao tayari wana vazi lao la kimila itakuwaje? Wasipolivaa la taifa watapungua uzalendo? Hata ukiupata utamaduni huu unaolazimishwa kwa kamati/ sheria, hautakuwa wa watu kweli, utakuwa artificial.

    Hata tukipata vazi la taifa kwa kamati, litakuwa vazi lililopangwa kuwa la taifa, si la taifa kikweli lililotokea kwa watu. Mti hukua kutoka chini kwenda juu, kamwe haukui kutoka juu kuja chini. Vivyo hivyo mambo ya utamaduni yaachwe yatoke kwa watu wenyewe, ama sivyo tutageuza utamaduni uwe siasa ndipo hapo wengine wanaona propaganda.

  4. Halafu kuna swala zima limetajwa la kupata vazi la taifa ili “tuitangaze nchi”. Kuna wengine kama mambo ya utamaduni tunapenda kwa utamaduni tu, hizi habari za “commoditization, politization and commercialization of culture” hatupendi. Kwa nini mie nivae batiki ili kujionyesha Mtanzania, niwe kama nyani katika zoo ili tu kuzidisha utalii Tanzania wakati sina hata hakika kwamba hizo fedha za utalii zinatumika vizuri?

    Hivi nchi kama Marekani wana vazi la taifa? Mbona wanaitangaza nchi yao vizuri sana?

    Unawaambia watu wavae vazi la taifa ili kuitangaza Tanzania wakati hata hiyo website ya Tanzania Tourism Board imekaa kama ya mtoto wa miaka kumi na tano anayejifunza web design na static cobwebsites?

    Serikali haiko serious bado.

  5. Ninaelewa kuwa tuna shida kubwa SANA hapa Tanzania sasa hivi. Tuna mkwamo wa uongozi na mmomonyoko wa maadili kiasi kwamba sisi wananchi tumejaa hasira na chuki (halali) juu ya hali hii. Kiasi kwamba hakuna chochote tena kitakachofanywa ambacho tuko tayari kukikubali kama si jambo la kujaribu kurekebisha udhaifu na maovu yaliyopo. Na wananchi wako radhi na wangefurahi endapo wangesikia kuwa kiongozi fulani anayetuhumiwa kwa ufisadi amekamatwa, amefikishwa mahakamani, kesi yake imeharakishwa na amefungwa! Hilo litapokelewa kwa shangwe bila kujali kama haki ilitendeka katika mwenendo mzima wa kumshughulikia fisadi huyo.
    Ninasema haya kwa kutambua ni kwanini wenzangu hawako tayari kuangalia upande chanya au wa msingi wa dhana ya vazi la taifa, kujaribu kushauri kwa utulivu, na hapo hapo kupata fursa ya kuonyesha upande dhaifu au usiofaa katika dhana nzima au mfumo wa mchakato wa suala zima la vazi la taifa.
    Nayasema haya kwa sababu suala la vazi la taifa halikuibuliwa na serikali. Tuliliibua sisi (wasanii na wajasiriamali wazawa) kipindi cha mwanzoni cha uongozi wa awamu ya tatu ya mzee Mkapa. Tuliliibua kwa sababu ya umuhimu wake (si rahisi kuujadili hapa, na maelezo marefu) na kwa vile lilitamkwa katika sera ya utamaduni ya 1997. Tukaanza na mama Mkapa kulijadili na baadae akatupa changamoto ya kuliandalia mchakato. Tulikuwa timu ya watu kama dazani hivi.
    Baadaye ikawa historia kwa sababu ambazo si lazima kuzielezea hapa. Kwa hiyo serikali ilipolianza tena mwaka 2003/2004 tulifirahi lakini baadhi yetu (mimi binafsi nikiwemo) hatukufurahishwa na jinsi lilivyoendeshwa. Hakuna atakayethubutu kujitokeza na kukana hili. Mimi niliandika mfululizo wa makala kama 6 hivi katika gazeti la Rai wakati ule kujaribu kutetea hoja zetu na kukosoa mwenendo mzima uliotumika.
    Kwa kuwa nimeteuliwa katika kamati ya sasa, mimi binafsi nina nia ya kuliangalia hili suala katika mwanga chanya na kushiriki na wenzangu na wananchi kuhakikisha kuwa safari hii tutafanikiwa. Muhimu ni kuiangalia dhana nzima ya vazi la taifa, umuhimu wake kwa jamii yoyote kama taifa na namna bora kabisa ya kuweza kuitimiza azma hiyo.
    Siamini kwamba litakuwa jambo la busara kulioanisha na ufisadi (kwa kuwa si mradi wa kifisadi kwa kiasi ninachojua!), ugumu wa maisha, bei ya umeme au nyama dukani, ajali za barabarani n.k. Tutazame historia, utamaduni, sera, utaifa, umuhimu na mambo kama hayo. Tuhojiane na kutafuta majibu, tukosoe na kutoa pendekezo mbadala, si kubeza, kulaani na kukatisha tamaa.
    Maoni zaidi yanaweza kutolewa kwa namba ya bure (toll-free) 15046.
    Karibuni ndugu zangu.

  6. Kiranga ulipotelea wapi kaka yangu? Ila umerudi kwa ari na kasi mpya, na nadhani hii makala itazalisha “Viranga” wengine.

    Kuna mtu hapo ameuliza swali la msingi — ambalo ningependa lijibiwe na Merinyo — sasa, hilo vazi, kwanza, madhumuni yake ni nini hasa? Kwa mtazamo wa wana kamati, watu 12 wanaweza kuja na vazi la taifa lenye makabila zaidi ya 120? Na historia, tamaduni za hizo jamii zipelekwe wapi?

    Kwa mtazamo wangu tu, Tanzania ipo kwenye kipindi chenye changamoto nyingi sana; za kiuchumi, kijamii, n.k. Lakini, cha kustaajabisha, hili la vazi la taifa linapigiwa kelele kuliko mambo mengine muhimu na nyeti ambayo yanaathiri mwelekeo wa nchi yetu moja kwa moja. Serikali, ambayo inategemea misaada na mikopo, inawezaje kutumia hela (hata iwe senti 10 tu) kwenye mambo kama mavazi? Mbona hatukusikia kamati zikiundwa mwaka jana baada ya matokeo ya kushangaza ya kitado cha nne? Taasisi mbalimbali zimefanya tafiti zinazoonesha kuwa kuna watu wanamaliza shule ya msingi bila kujua kusoma wala kuandika, je serikali iliunda kamati hapo?

    Kama ni utambulisho wa Tanzania nchi za nje, basi serikali ianze kuwekeza kwanza kwenye mambo ya desturi na mila, na vivutio vya watalii ambavyo havitumiwi ipasavyo.

    Tafadhali, anzeni na tovuti yenu ya utalii Tanzania… hata mje na vazi la bure la Taifa, sitatupa lubega yangu!

  7. Tatizo lingine nchi (serikali) haieleweki inaelekea wapi. Mara inajitoa katika shughuli za biashara kiasi hata cha kuza nyumba zake na mashirika ya umma, hapo hapo inajichanganya na kina Hasanali na Kusaga ambao ni wafanyabiashara as far as I am concerned.

    Caesar’s wife must always remain above suspicion. Leo wanamitindo wanaoshindana na Hasanali na wenye redio wanaoshindana na Kusaga wakisema serikali imewapa upendeleo hawa kwa sababu let’s say zilizo less than noble, serikali itajitetea vipi?

    Ndiyo maana pointi ya serikali kujitoa katika mambo kama haya inakuwa muhimu. Waacheni kina Hasanali na Kusaga waandae mashindano ya kutafuta vazi la taifa, likiwavutia watu kiasi cha kukubalika ndio vazi la taifa tena hilo, itafikia wakati kila mtu kuanzia mmachinga mpaka rais watalivaa litakubalika.

    Ila hizi habari za kamati kamati, kila kitu kamati zinatudumaza tu. Mwisho tutapenga kamasi kwa kamasi, na hata mkono wa kuchambia tutataka serikali iunde kamati. Ashakum si matusi.

  8. Mniwie radhi nimekuwa nje kidogo ya mzunguko huu kutokana na majukumu binafsi (si ya kamati :-))!
    Basi na tuendelee na mjadala wetu mintaarafu dhana ya vazi la taifa. Ni vigimu kutaja kwa usahihi kabisa dhana hii ilizuka lini duniani, lakini bila shaka ni baada ya nchi za kisasa kujitambua kama ‘mataifa’ na mawasiliano kuruhusu mwingiliano na mbadilishano wa kiutamaduni.
    Mjadala wa dhana hii hapa Tanzania umemea na kushamiri kutokana na matukio kwa watu binafsi na makundi ya wananchi wetu kujihoji na kuhojiana imekuwaje sisi hatuna vazi letu la taifa? Hii ni kutokana na kukumbana na mbabaiko pale ambapo katika mikusanyiko ya makundi mbali mbali ya kimataifa, inapotajwa kuwa “leo ni siku ya kiutamaduni, kila mtu na avae vazi lake la kitaifa”. Mimi binafsi nilikutana na kadhia hii nyuma huko 1993 nilipokuwa ziarani Marekani na vijana wenzangu (wakati huo) kutoka nchi zingine 19 za kiafrika. Waama niling’ara wakati ule kwani kutokana na fani yangu nilikuwa nimeenda na mavazi mawili: moja la asili la ndugu zangu Wamasai na lingine la ubunifu tunaloliita ‘serengeti’ – ambalo hadi sasa ni maarufusana kwa wateja katika duka letu la mavazi Afrika Sana pale Sinza. Hii ‘serengeti’ ni shati ambalo ushonaji wake umetohoa uvaaji wa waafrika wengi au makabila mengi ya Tanzania (hii ilikuja kuboreshwa zaidi kutokana na utafiti wetu wa uvaaji wa makabila 9 ya Tanzania mwaka 2001 – 2002 na likaja kushika naffasi ya kwanza vazi la kiume katika mashindano ya 2004 mkoani Kilimanjaro). Anyway, naweza kusema kuwa nilitumia tu ubunifu wangu kujinasua katika shida hiyo, jambo ambalo Watanzania wengine bila shaka imekuwa ikiwapa shida.
    Kutokana na ‘shida’ hii waliyokuwa wanaipata, Watanzania wakaanza kudodosa na kuihoji dhana ya vazi la taifa.
    Sasa: Vazi la Taifa ni nini? Huwa ninapenda kutoa jibu fupi la kiufundi: ni vazi ambalo hutambulisha utaifa wa mvaaji wake. Kwa maelezo ya kidhana zaidi, hili laweza kuwa vazi la asili au la kiutamaduni la jamii ya taifa fulani. Vazi hili katika mazingira ya kawaida (pale ambapo mchakato wa tasnia ya kiutamaduni na mwenendo wa shughuli za kiuchumi wa jamii husika umeweza kuibua mavazi hayo) halitafutwi. Kwa Tanzania, jamii zetu pale tulipokuja kujiwa na wageni waliotuletea bidhaa zao za nguo na za kimavazi hatukuwa tumefikia hatua ya kiteknolojia ya useketaji wa vitambaa na utengenezaji wa mavazi kufikia kiwango cha teknolojia waliyokuwa wamefikia wageni hao – wazungu kutoka ulaya na waarabu.
    Kutokana na hili, mwenendo wa kupokea vya wageni (kipya kinyemi) ukaanza katika suala la mavazi na masuala mengine (imani, teknolojia, lugha nk).Kama mkosi, basi twaweeza kusema kuwa huu ulikuwa mkosi wa kihistoria!
    Na mwenendo huu wa kujisaili na kusailiana kuhusiana na mavazi yetu (si la taifa pekee!) umekuwepo miongoni mwa Watanzania wengi wenye urazini na raghba na ‘vyao’ na ‘kwetu’. Suala la vazi la taifa kuingizwa katika sera ya utamaduni, kwa hiyo, haikuwa tu kutokana na mbinu za wanasiasa za kujitafutia sifa au kupandikizia watu mambo yasiyo na umuhimu, bali mwitikio wa haja ya wananchi ya kuwa na vazi lao.
    Vazi hili kwa ajili ya nani? Kama ni utambulisho wa kitaifa, basi vazi hili ni mali ya Watanzania wote na litavaliwa na yeyote mwenye kutaka kuionea fahari nchi yake. Najua kuna wanaosema sasa hivi: “fahari kwa lipi?”. Inabidi tutambue kuwa nchi yetu, taifa letu ni SISI. Sidhani kama mmoja wa nduguzo akiwa na tabia mbaya na chafu, basi utaamua kulaani na kuichukia familia yako, bali utailinda na kuitetea popote, ikibidi wewe ujenge tabia na mwenendo ambao utakuwa unatoa taswira nzuri kwa wengine juu ya familia yenu. Au utakuwa kazi yako ni kuiponda tu familia yenu na kubeza jambo lolote ambalo litakuwa linapangwa kutekelezwa hapo nyumbani kwenu?
    Vazi la taifa litavaliwa kwa taratibu mbalimbali zitakazokubaliwa na makundi mbalimbali nchini. Haliwezi kuwa sare ya kulazimishwa kuvaa. Litakuwa ni vazi zuri ambalo matumaini yangu ni kwamba watu binafsi wataweza wakalivaa kwa mtindo wanaopenda na mahali watakapoamua. Wabunge wataweza kupanga utaratibu wao na namna yao ya kulitengeneza, wafanyakazi katika wizara na ofisi mbalimbali wataweza kupanga utaratibu na namna ya ushonaji wao. Mapendekezo ya litashonwaje na kuvaliwa kwa utaratibu gani yatatokana na maoni na matakwa ya wananchi. Ndio maana maoni na mawazo ya wananchi ni muhimu sana (toll-free 15046).
    Kwanini sasa? Mimi sidhani kumewahi kuwa na wakati maalum wa kushughulikia hili jambo tangia lianzishwe 2003/2004. Nadhani waziri Nchimbi ameendelea tu kutekeleza wajibu wake kama waziri kwa masuala yaliyoko ofisini kwake.
    Naamini mawaziri wengine nao wanaendelea kushughulikia yao. Nisilojua, na ambalo mawaziri wanaoshughulikia viwanda, biashara na uwezeshaji wanapaswa kutoa majibu ni kuhusu uwekaji wa sera wezeshaji kwa wananchi na rafiki kwa uchumi wetu wa ndani katika tasnia ya nguo na mavazi ili watanzania waweze kutengeneza na kuvaa nguo ‘zao’, jambo ambalo litastawisha sana dhana yetu ya vazi la taifa.
    Asanteni!

  9. Asante Merinyo kwa maelezo yako lakini bado nna machache ya kukuuliza

    1. Kutokana na maelezo yako ni kuwa serikali unatumia fedha na rasilimali zake nyengine ili kukidhi hitaji la Watanzania wanaokwenda nchi za nje, na kushindwa kujitambulidha kwa vazi la taifa? Hivi mlishakaa mkaangalia idadi ( percentage) ya raia wenye hitaji hilo?
    * hiyo ndio faida pekee ya vazi hilo uliyoianisha

    2. Bajeti ya zoezi zima la kutafuta vazi hilo ni kiasi gani? Kwa sababu Kama raia nna haki ya kujua, kodi yangu inatumiwa wapi kwa mbadala wa kitu gani.

  10. Mjumbe Merinyo shukurani kwa maelezo yako ya kina. Hakika uwepo wako hapa tu unatudhihirishia kwamba unajali maoni ya watu – hata kama ni tofauti na yako- na unaenda na wakati. Sitaki kuamini kwamba sababu moja inayokufanya uweze kuwepo kirahisi hapa ni kwamba wewe si mtu wa serikali “per se” na hujaambukizwa ugonjwa wa “kufunga vioo” ambao sasa hivi unaonekana kama ni moja ya sifa zinazotakiwa ili kuwa serikalini.

    Baada ya hayo, swala la msingi naweza kusema halijajibiwa. Nalo ni hili la kuuliza kwamba kuna umuhimu gani wa kuliundia hili jambo kamati ya serikali? Unatueleza kwamba kuna mashindano yalifanyika na kuna nguo za aina ya “Serengeti” zishashonwa, kwa nini kusiwe na juhudi za watu binafsi kulitangaza hili vazi, na mengine ya aina hiyo, hata tukiwa na “mavazi ya taifa” (badala ya vazi la taifa) haitakuwa mbaya.

    Moja ya mambo yanayotajwa kukera watu hapa ni huu utegemezi wetu kwa serikali hata kwa vitu ambavyo wananchi wenyewe wanaweza kuvifanya.

    Kuna ulazima gani wa jambo hili kufanywa na serikali? Wananchi wenyewe hawawezi kuji organize katika hili? Au ni kujilemaza na kupenda kusukuma watu oka juu kwenda chini tu?

    Maana matatizo yetu mengi yanatokana na “attitude”. Mtu anaweza kuwa na mtaro wa majitaka nje ya nyumba yake unafurika na kutoa harufu kwa sababu takataka za barabarani zimeingia mtaroni na kuziba njia ya ma, lakini hanyai hata kidole kwani hiyo ni “kazi ya serikali”. Je, hizi kamati nazo ni aina fulani ya kulegeza wananchi kiasi hata kile wananchoweza waendelee kufikiri ni kazi ya serikali?

    Kikubwa hasa ambacho serikali inaweza kukifanya ambacho nyie wanakamati mngekutana wenyewe bila serikali kuwakutanisha, na mgeweza kukifanya ni nini? Tayari mna redio (Clouds) mna wabunifu na wengine wenye uzoefu mkubwa tu na fani hii kama wewe Mjumbe Merinyo na mwenzako Hasanali, na hata sina uhakika wajumbe wengine wanazo, lakini wameteuliwa na kwa kuangalia mfano wako, Hasanali na Kusaga, inaonekana kuna uzoefu mkubwa.

    Sasa kwa nini mnaihitaji serikali? Wengine wakisema mnataka kutengeneza some sort of cabal, a monopoly of sorts reeking of TANESCO like might, mtaweza kukataa?

  11. Jamani, nadhani mtakuwa mnaniwia radhi kila ninapoonekana kuingia mitini kwa kipindi. Si kusudio langu kukuacheni mkiwa na kiu ya jibu kwa kipindi kirefu, natamani ningekuwa na ka-blackberry na mimi nikawa na tweet kila saa! Lkn unajua tena, wazee na bb wapi na wapi!!!
    Haya, twende sasa! Hyperkei, nadhani kama nilijieleza sivyo na kuonekana kusema kuwa faida pekee ni hiyo, samahani. Nadhani kuna faida, sababu, haja na hata hoja ya kuwa na kitu. Vazi la taifa kama dhana ni kitu kilichoenea takriban maeneo yote duniani. Kutoka Bhutan, Japan, China, Uingereza, Urusi na kwengineko. Kwa hiyo kama dhana, ni jambo ambalo ndani yake linabeba fahari ya utaifa, imani ya utambulisho wa kiutamaduni, n.k. Labda ndiyo sababu mabalozi wetu wa kiutamaduni kupitia fani ya ulimbwende wanapokutanishwa kwenye fainali za dunia kunakuwa na kipengele cha kushindanisha vazi la taifa. Kama nitakuwa ninakosea, waendeshaji wa mashindano hayo kina Lundenga, Chipungahelo na Maria Sarungi watanihukumu. Kuhusu asilimia ya raia wenye hitaji hilo, naomba niseme ukweli kuwa mimi binafsi sijafanya utafiti na kuwa na takwimu kuhusu hilo. Na kama engekuwepo mtu ambaye ameshafanya hilo, hajaleta matokeo. Wala serikali sidhani kama imeshafanya hilo.
    Kuhusu, bajeti ya vazi la taifa au kamati yake, naomba niseme kuwa mimi ni mtu wa sekta binafsi PER SE na sina mamlaka )hata kama ningekuwa na fununu) ya kueleza lolote kuhusu hilo. Nadhani unajua kidogo kuhusu kanuni na mipaka.
    Sasa kwa kaka Alphonse: swali la msingi ni kuhusu haja ya kuliundia suala la vazi la taifa kamati ya kiserikali. Nionavyo mimi (MAONI BINAFSI, SI YA KAMATI!), imeonekana kuwa ili vazi hili liwe na uhalali wa kisharia (kwani limetajwa katika sera ya utamaduni kama moja ya mambo ambayo serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, watahakikisha linakuwepo), basi kuna haja ya serikali kulisukuma na kulipa nguvu. Sidhani kuwa uundaji wa kamati ndiyo namna pekee ya kulifanya, lakini siamini kama kuna mwiko wa kutotumia kamati katika suala hili (ati kwa sababu tu kwamba mambo yote yaliyowahi kuundiwa kamati yameonekana kutozaa matunda tarajiwa, au yamekuwa yakibeba harufu ya ulaji!).
    Ila naomba nikupe dole kwa ushauri wa kuacha watu wafanye mambo wenyewe, bila kutia mkono wa serikali. Hili linazungumzika na ni wazo valid sana, tujaribu kuangalia jumlisha na toa zake katika hili. Bado uwanja mpana, mpira huoooooo!!!!!!!

  12. Mimi nadhani tulipe muda tuone, manake linaweza kuja kutoka vazi zuri sana, wote tukalipenda, lakini na sisi wasiwasi wetu tumeshaweka hadharani, tusije kuonekana wabaya baadae.

    Mimi kinachonitatiza ni hiki. Viongozi wenyewe hawavai hata batiki wakienda kwenye mikutano ya kimataifa. Siajwahi kuona Mh. Rais amevaa vazi la huko kwao, bali naonaga suti tu, na hayuko peke yake kwenye hili. Sasa hii demand ghafla imetoka wapi, manake sioni hata chembe ya hamu ya uvaaji wa nguo za kiasili kwa viongozi, manake hata huyo nchimbi sijawahi kuona amevaa kuo za kabila lake, au hata batika na mavazi mengine ya kitanzania, kama anavaaga basi I will take that back.

    Kama moja ya nia ya vazi hili ni kuongeza mshikamano na uzalendo, basi mchakato huu ungefanya mambo mengine, manake uzalendo hauletwi na vazi bali hutoka moyoni kwa mapenzi ya nchi yako, kitu ambacho viongozi wenyewe (sio wote) siamini wana mapenzi hayo na nchi kutokana na vitendo vyao.

    Lakini kama nilivyosema awali, linaweza kuja kupatikana vazi zuri sana, wenyewe tukafurahia. Hivyo basi, mimi binafsi siliungi sana suala hili, lakini nitaacha kulirushia mawe, na kusubiri kuona ni nini kitafuatia.

    Kila la kheri jamani, lakini hapo hapo, naombeni msome ile makala iliyokuwa raiamwema http://www.raiamwema.co.tz/vazi-la-taifa-kwa-nchi-ya-wavaa-mitumba sijui wana kamati mna mawazo gani juu ya hoja hii.

  13. Vazi la Taifa linatakiwa liwe la kiasili sio kitu kinachotolewa akilini mwa mtu/watu mwaka 2012.

    http://udadisi.blogspot.com/2012/01/vazi-la-taifa-alilobuni-lucy-lameck.html

    Vazi litakalobuniwa leo litakua “out of style” ndani ya miaka michache, sasa tutatengeneza kamati nyingine na kubuni jipya? Hii serikali ya CCM imeishiwa ideas.

    Je, hili ni tatizo kubwa la serikali kulishikia bango katika matatizo yote tuliyo nayo? Nani aliyemtuma mbunge wake kuomba serikali iangalie suala la vazi la taifa kwa sababu hawawezi kujisitiri nje au ndani ya mipaka.

    Mtu yoyote aliye kwenye hii kamati ni part of the problem ya hii nchi just kwa vile kuna chakula watu wanatetea hadi ujinga. Kila kikao kinapo kaa wakina mama kibao wanakufa katika uzazi hela inapukutika watu kudiscuss fashion, kama huna hasira i question your patriotism whatever the f*** you are wearing.

  14. Mimi nalia na transparency ya matumizi ya huu mchakato mzima. Iwapo daraja la Kigamboni na barabara nyengine tunapewa makadirio ya gharama itakayoingia serikali, ni lazima kwa projects nyengine kama hizi tupiganie tupewe makadirio. Hatuwezi tu tukatafuta vazi la taifa kwa gharama zozote kwa mfano, wakati kuna mambo mengine yenye pressing need ya kutatuliwa mapema zaidi. Ni haki yetu Watanzania kujua tuna”nunua” vazi la taifa kwa pesa ngapi, ili kupima value for money ya mchakato huo.
    Ajira ngapi zitazalishwa kwa mradi huo? Kuwepo kwa vazi la taifa kutasaidia nchi kwa value gani kwa kulinganisha na kutokuwepo kwake?

    Tofauti na Tanzania, katika nchi tulizotajiwa, tayari kulikuwa na vazi lililozoeleka kwa asilimia kubwa ya jamii kabla ya vazi hilo kutangazwa kuwa vazi la taifa, hivyo mchakato wa kulitangaza haukuchukuwa nguvu wala gharama kubwa, na consequences zake tayari zilikuwa zinaonekana kuwa limekubalika (lilishakubalika kabla ya mshakato wa kulitambulisha)

    Kwetu hali haipo hivyo, tunaweza kubuni hilo vazi, kisha watu wasilipende, wasilitumie, likabakia kwenye makabrasha ya kamati tu, au kugeuka kuwa vazi la taifa linalojuulikana nje ya nchi pekee. Kuna risk analysis ilifanywa kwenye hili? Kuna uwezekano wa kiasi gani wa hili vazi kukubalika? Na lisipokubalika pesa yetu inakuwaje?

    Kwenye nchi ya wavaa mitumba, vazi hili linanafasi gani ya kukubalika?

  15. Hivi, lazima Tanzania tufuate wanayofanya nchi nyingine?, kwa maana ya lazima na sisi tuwe na azi moja la taifa, badala ya kusema sisi tutasheherekea our diversity. Tukaboresha nguo hizo hizo ambazo zipo za makabila mbali mbali.

    Nadhani Tanzania inahitaji fikra za kibunifu, kwani ninaanza kuwa na wasiwasi, intellectuality continues to fail us. Kweli wingi wa Masters degrees si wingi wa maarifa. Hili ni kwa Tanzania kwa ujumla. Tuwe tofauti, we dont have to be like Nigerians. Ghana wao wana Kente, je sisi Tanzania tuna kitu kama Kente?, kama Khanga ni Kente yetu, basi we good then, whats the hassle.

  16. Nimerudi tena uwandani jamani, nilisafiri kijijini kidogo!
    Nashukuru kuwa wenzangu mmeendelea kutoa maoni yenu. Nimeona pia wengine wameanza kutukana!!! (mfano: kama huna hasira i question your patriotism whatever the f*** you are wearing.) A patriot has to be angry???? Kwa hiyo kuweza kutamka f*** ni uzalendo?? Ajabu!!!!! Mimi hushiriki nyanja zenye ustaarabu ambazo hata waratibu wake wanapenda na kuheshimu ustaarabu. Kwani hata hili suala la vazi la taifa ni suala tu la kusailiana na kukubaliana au kutofautiana kistaarabu katika masuala ya kitaifa au ya utaifa. Na kama tukitumia ustaarabu katika kuulizana na kuelezana, naamini tutafika pahali tuelewane hata kama si kukubaliana. Suala hili linategemea sana mawazo na maoni ya kila mmoja wetu, ndio maana nilitoa ile anuani-pepe ya maoni info@vazilataifa.com na toll-free number kwa ajili ya sms 15046 ili maoni ya yeyote yawe rasmi. Lakini si maoni yenye matukano, yawe ya kistaarabu na yenye kujenga kwa maana ya kutoa hoja, maelezo yenye lumbi, mantiki na ushawishi wa hoja.
    Naamini nimejitahidi kutoa maoni yangu, hata kama hayakuwa ya maana sana lakini huenda yamesaidia kuweka urari kwa kiasi fulani. Kwaherini kwa sasa!!!
    Kuanzia wiki ijayo tutakuwa tunapata maoni ya wananchi kwenye kanda mbalimbali nchini (Kaskazini – Arusha, Kanda ya Ziwa – Mwanza, Kati – Dodoma, Nyanda za juu Kusini – Mbeya na Mashariki na Pwani – Mtwara) kwa mtindo kama town hall meetings. Tutaendelea kuangalia maoni ya wanamitandao na kuyazingatia; lakini nivema yawe rasmi kwa njia niliyoeleza.

  17. Merinyo ukianza ku-lecture ustaarabu ni nini utaanza kuchemsha. Watu wataanza kuchukua etimology ya “utsaarabu” na kukuta root ni “arab” na kusema dhana nzima ni ya kigeni, kwa mtu aliye katika kamati ya kutafuta vazi la taifa kutokujua kwamba ustaarabu wako ni ushenzi kwa mwingine kunaleta maswali mengi sana.

    Kati ya anayetukana ushenzi na anayekataa kutukana ushenzi kwa sababu kutukana si “ustaarabu” nani mstaarabu?

    Mimi naona anayetukana ushenzi mstaarabu. Tatizo si kutukana, tatizo unatukana nini na wapi. Na yeyote anatetukana kamati hii kwa hasira mimi nampa maksi za uanamapinduzi na utaifa kwa sababu hataki habari za ukoloni mamboleo za wachache kuwaamulia wengi. Anachomelea mbali habari za ustaarabu wa kijinga uliopelekea leo miaka 50 baada ya uhuru bado tuko ombaomba sawa na nchi zenye vita wakati nchi yetu si tu ina amani, bali ia na maziwa (ya kijiografia na ya wanyama) na asali.

    Natumaini hizo ziara zenu za “Town Hall meeting” style ziataweza ku accommodate out of scope issues, kwa maana huko mnakoenda watu hawana maji na umeme, sasa mtu ambaye hana maji na umeme uklianza kumuuliza msawali ya vazi gani la taifa anataka kuvaa wakati hata hana uhakika wa kulifua na kulipiga pasi kileo, naona kama mtakuwa mnacheza Makida Makida na kutafuta kutupiwa mawe na wananchi wenye hasira ambayo haijatulizwa na ulimbwende wa elimu ndogo kama sie wengine tunaoweza kuwa entertain humu mitandaoni.

    Wewe mwenyewe ushahalalisha hasira ya wananchi katika response yako ya kwanza kwamba kwa kusema “nio halali kabisa”. Vipi sasa unataka kuleta censorship on self censors?

  18. Asante Kaguta kwa mchango wako murua sana!
    Ili kuepusha mgongano wa utamaduni na ustaafrika wetu, basi nadhani ni busara nimalizie kwa kusema tu kwamba sisi kama kamati tuliteuliwa kwa suala la vazi la taifa, si umeme (una wizara na waziri wake, akitaka anaweza pia kuteua kamati!), wala maji, wala ufisadi, wala kilimo nk nk.
    Sasa sisi tuko kwenye masuala ya mavazi kama wadau tu, serikali imetuteua kuweza kuchukua maoni YENU na kuyafikisha kwake. Hayo mengine tuibane serikali kwa mahali na nafasi yake. Mie binafsi nina masuala kadhaa ambayo pia huwa natafuta mahali na nafasi yake kuibana serikali, na si kawaida yangu kuchanganya mambo na kuchomeka pasipostahili.
    Lakini pia nitajitahidi nisichanganye hasira na matusi au lugha isiyokubalika katika ustaafrika wangu.
    Asante, na kila la heri katika harakati hizi za kuiweka jamii yetu sawa (Inshaalah pale itakapowezekana!!)

  19. Nashukuru kwa kupata blog hii kwani nimetafuta muda mrefu ni wapi nipitishe maoni yangu ili yawafikie watu wa kamati maalum ya vazi la taifa.

    Kwanza kabisa, nachukua nafasi hii kuipongeza wizara husika kuendeleza wazo hili la vazi la taifa.

    Mapendekezo yangu (namwomba Mungu awasukume wajumbe wayakubali na yapitishwe) kuhusu vazi la taifa ni kama ifuatavyo:

    1. Vazi la taifa linapaswa kutokana na utamaduni wa makabila ya Tanzania. Isiwe ubunifu wa wanamitindo ya mavazi. Kama litatokana na ubunifu wa wanamitindo wa mavazi halitakuwa na ladha ya taifa bali ladha ya kisiasa tu.

    2. Kamati ya vazi la taifa ikusanye sampuli ya mavazi kutoka makabila angalau 10 ya Tanzania ambayo yamedumisha mila ya mavazi yao kisha watanzania wapige kura kulipigia vazi mojawapo ya kabila zetu. Vazi litakalopata kura nyingi ndilo lipitishwe kuwa vazi la taifa. Wabunifu wa mitindo hapo ndipo waweze kubuni aina mbalimbali za ushonaji bila kupoteza hadhi na ladha ya vazi la kabila hilo litakalokuwa limepigiwa kura nyingi. Upigaji kura waweza kufanywa kwa kupitia Vyuo Vikuu, Shule za Sekondari na baadhi ya Mikoa ya bara na visiwani ili kupata uwakilishi mzuri kitaifa.

    Kama ilivyo kwa lugha ya kiswahili kwamba iliteuliwa lahaja ya Unguja na ikapitishwa kuwa lugha ya taifa, hata vazi la taifa ifanyike hivyo ili kuhalalisha mchakato uwe wa wananchi wote badala ya wanasiasa tu na kamati yao. Itakumbukwa kwamba kulikuwa na hoja ya kufanya kisukuma kiwe lugha ya taifa, lakini kiswahili kilipitishwa na leo hii ndiyo lugha ya taifa.

    3. Vazi la taifa kama wazo la hapo juu litakataliwa, napendekeza kwamba liwe na mtawanyiko wa vionjo na tuwe na aina tatu au nne za vazi la taifa.

    Aina ya kwanza iwe vazi lenye vionjo na nakshi za rangi ya bendera ya taifa. (Wabunifu wanaweza kubuni zaidi mtawanyiko na mpangilio wa rangi) ili kuepuka kuwa na sare za taifa badala ya vazi la taifa.

    Aina ya pili iwe vazi lenye vionjo vya wanyama maarufu tanzania kama twiga au tembo.(Wabunifu wanaweza zaidi zoezi hilo).

    Aina ya tatu, vazi liwe na vionjo vya mavazi ya baadhi ya makabila wanaoendeleza mila za mavazi yao hadi leo.(Wabunifu wanaweza kushiriki hilo zoezi).

    Aina ya nne ya vazi la taifa, iwe vazi ambalo linakubaliwa na madhehebu ya dini zote kubwa hapa Tanzania (Ukristo na Uislam wote wanasisitiza mavazi ya heshima na kustiri mwili vyema).

    Ninaamini kama mawazo yangu haya yakifanyiwa kazi tutapata vazi la taifa lenye hadhi kitaifa na kimataifa, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.

    Wazo langu la kuteua vazi moja au mawili kutokana na mavazi ya makabila ya hapa nchini, na vazi la kabila hilo lisiwe linavaliwa na makabila mengine ya nchi jirani au mataifa mengine, ndilo wazo ninalotamani lipitishwe na kamati ya vazi la taifa kama Nyerere alivyofanya wakati anatafuta lugha ipi iwe ya taifa.

    Nasubiri kupata comments kutoka kwa wajumbe wa kamati ya vazi la taifa hasa mjumbe huyu ambaye amewajibu baadhi ya washiriki wa blog hii.

    Nashukuru sana.

    Juma Milinga
    KIGOMA- UJIJI

  20. Nashukuru sana Juma, na nawashukuru tena sana wana vijanafm kwa kunivumilia kukosekana kwangu uwandani. Ndo tulikuwa kule mikoani: kaskazini,kanda ya ziwa,kati,nyanda za juu kusini,na wiki ijayo tutaenda Mtwara.
    Kabla ya kwenda Dodoma kwa kanda ya katitulikuwa pale BASATA kwenye jukwaa la sanaa ambapo tulipata mawazo kedekede, kama ambavyo imekuwa pia mikoani. Jana nilikutana na wana Rotary wa Dar es salaam Mzizima, na kesho natarajia kukutana na TGNP kama watanipa fursa.
    Naomba nimwambie Juma wa Kigoma kuwa nayachukua mawazo yake kama yalivyo na yataingia kwenye taarifa yetu kama yalivyo,yakijumuishwa na ya aina yake.
    Kutoa majibu kwa hoja kwa sasa kwangu itakuwa vigumu jamani,kichwa kimejaa, na hapa nilipo naendelea na homework yangu niliyopewa na mkuu kwenye kamati.
    Nikuhakikishieni tu kwamba pamoja na magumu yaliyopo,mtapata matokeo ya kazi yetu.
    Usiku mwema!

  21. Leotumekuwa na wadau wa TGNP kama nilivyokuambieni jana.
    Mawazo yalikuwa mazuri; pia kulikuwa na kongamano lakila wiki linalowakutanisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar. Ilikuwa changamot kubwa sana kwetu kamati kwa sababu pale ndio kisima cha vuguvugu la urazini juu ya haki na usawa wa kijinsia na matumizi bora na ya haki ya rasilimali za taifa. Tumeyachukua mawazo yao na yanaingia pia katika taarifa zetu. Hoja kuu zilizoibuka ni maana ya kushughulikia vazi wakati jamii zetu za Tanzania zimegubikwa na matatizo kibao, vipi vazi litaleta mabadiliko katika taifa letu, tafsiri ya utafutaji wa vazi katika dhana nzima ya uchumi na ajira ya watanzania, vazi hili hasa ni la nani (kwa ajili ya nani?)……
    Kwa kweli tumefurahishwa sana na changamoto hizo zilizoakisi urazini wa hali ya juu,lakini tulifurahishwa na jinsi changamoto hizo zinavyoweza kutafsiriwa kama mapendekezo na maangalizo mema na ya kujenga katika dhana nzima ya vazi la taifa.
    Usiku mwema!

  22. Samahani kwa kutumia kiingereza.
    According to my perception the national dressing design should have some pigments from the Masai dressing

  23. I like the helpful info you provide in your articles. I’ll bookmark your blog and check again here frequently. I’m quite sure I’ll learn many new stuff right here! Best of luck for the next!

  24. Hello There. I found your blog using msn. This is an extremely well written article.
    I’ll make sure to bookmark it and return to read more of your useful info.

    Thanks for the post. I’ll certainly comeback.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend