Penye Kufuka Moshi

Wanasema, la mgambo likilia ujue kuna jambo, na mimi leo nauliza kulikoni wasanii wa muziki huu wa bongo flava?. Majuzi niliandika shairi na mwisho wa shairi nilisema kwa utani, heshimu sanaa, kwani imeajiri vijana wengi zaidi ya wizara ya Kapwaya. Pamoja nilisema kiutani, lakini nilitaka watu waelewe umuhimu wa sanaa hii katika maisha ya vijana. Kuporomoka kwa muziki huu, kutaadhiri maisha ya vijana wengi waliojiajiri kupitia muziki huu, hivyo ni vyema kuutetea na kuulinda kwa kila hali na mali.

Gumzo la mjini ni juu ya vita kati ya ma-Dj na wasanii, pia vita kati ya wakongwe wa muziki wa bongo flava na wasanii chipukizi kwenye muziki huu. Afande Sele ameshutumu ma-Dj kwa kuchangia kudhofisha bongo flava. Shutuma hizi zimekuwa za siku nyingi lakini kwa muda mrefu zimekuwa ni minong’ono tu, lakini leo O-ten na Dudubaya nao wamejitoa mhanga na kuwasema Ma-Dj. Hivyo nimeachwa nikiamini, panapofuka moshi ujue pana moto.

Shutuma za ma-Dj kubeba wasanii na kulazimisha wasanii wawalipe fedha ili kucheza nyimbo zao redioni, ni ukiukwaji wa maadili ya kazi zao. Pili, kwa tabia hii basi ni kweli muziki wa bongo flava utakuwa unatawaliwa na fedha badala ya ubora wa kazi na ubunifu. Kwa mfano, mimi kama msanii mwenye kutengeneza kazi mbovu, najua nitasikika tu kwani ma-Dj watafanya kila wawezalo nisikike na hatimaye kupendwa, kisa fedha nilizowahonga. Hii inahatarisha fani na pia inahatarisha maendeleo ya sanaa hii.

Afande Sele kama mmoja wa wasanii wakongwe pia amewasema wasanii wapya katika nyongeza ya shutuma zake dhidi ya ma-Dj. Afande Sele amedai kwamba wasanii wapya hawana ubunifu wala mashairi yenye kubeba ujumbe wenye msingi. Hivyo nyimbo zao nyingi zinakosa maudhui ya kina lakini zinatamba kwani zimekuwa zikibebwa na ma-Dj. Hapa Afande amekuwa na hoja sawa na ile ya msanii Nas kipindi kile aliposema Hip Hop Is Dead.

Pamoja na baadhi kukubaliana na Afande, lakini wapo baadhi wameuliza maswali ya msingi, kama, kwanini wasanii wakongwe hawawashirikishi wasanii chipukizi kwenye nyimbo zao. Hapo hapo wengine wamedai, kulalamika kwa wasanii wakongwe ni kutokana na style zao kupitwa na wakati hivyo kukosa airplay. Mimi nimekuja kuona pande zote mbili wana hoja za msingi, kivipi?

Wasanii wakongwe wangejaribu kushirikiana na wasanii wapya, hilo linaweza kuwasaidia na kuwakuza wasanii wapya kisanii. Hili litaongeza ushirikiano baina ya wasanii na katika ushiriano huu, itawasaidia katika kutetea haki na maslahi yao pamoja, kwani kutengana ni udhaifu. Pili, ni kweli baadhi ya styles za zamani leo hii haziwezi kuvuma na mfano mzuri ni huyu msanii Sugu au Mr. II. Leo hii ninadiriki kusema moja kati ya sababu kuu ya kushuka kisanii kwa Sugu ni kung’ang’ania kwake na kuendelea kurap na style yake ile ile ya miaka ya tisini. Albamu yake ya Veto ilinisikitisha mimi kama mpenzi wa bongo flava, kwani ilikosa ubunifu na upya.

Hivyo basi, badala ya kusukumana kati ya pande hizi mbili, mimi nadhani la msingi ni ushirikiano kati ya wasanii wakongwe na wapya, ili kuongeza chachu ya ubunifu kwenye sanaa. Muziki wa bongo flava hauwezi kuachwa ukafa hivi hivi baada ya safari ndefu ya kuufikisha hapa ulipofikia leo.

Maudhui ya fasihi za kina katika muziki wa bongo flava lazima udumishwe kwani heshima ya muziki lazima ilindwe, kwasababu hatutaki kurudi kwenye zama zile ambapo muziki huu ulionekana ni muziku wa kihuni tu. Tulinde heshima na tudumishe mshikamano. Ujumbe kwa wasanii wakongwe, mwalimu bora na mwenye mafanikio ni yule ambaye huwa mwanafunzi kwa kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wanafunzi wake pia. Hivyo basi, tuhakikishe tunauzima moshi huu kabla ya moto kuanza kuwaka, kwani bado tunaishi kwenye nyumba ya nyasi. Kidumu chama cha bongo flava.

Previous ArticleNext Article
Bahati was born and raised in Tanzania, and then moved to California to pursue his college education. He graduated in 2008 with a Bachelor’s Degree in Political Science and a minor in Sociology. Bahati expects to be doing his Masters in African Studies in the near future. He is currently working on starting a t-shirt business and a possible publication of some of his writings. One thing that Bahati cannot live without is music, specifically Hip Hop & Bongoflava which he argues are both the voice of the youth today, and is excited to look into how Bongoflava can be a source of further entrepreneurship among the youth in Tanzania. Bahati believes that Bongoflava can help to reduce poverty in Tanzania, as can a more collective effort among key players.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend