Maswali matano na Elineema L. Mauki

Elineema L Mauki ni mhandisi na mbunifu/mwanzilishi wa Najali Reusable Sanitary Pads. Tulipata nafasi ya kusikia kutoka kwake kuhusu ubunifu na sapoti anayopata, lakini pia changamoto anazopitia kwa kutengeneza bidhaa inayosuluhisha matatio ya jamii.

1. Wazo la kutengeneza bidhaa hizi ulilitoa wapi na tuambie kidogo kuhusu kampuni yako?

Kwa majina naitwa Elineema L Mauki, ni Mhandisi Msanifu wa Sayansi na Teknolojia ya Nguo na Viwanda.

Wazo la kutengeneza bidhaa hizi za taulo ya kike za kufuliwa za ”Najali Reusable Sanitary Pads TZ” nilikua nalo tangu kipindi nasoma Chuo kikuu, UDSM – 2017 ambapo, mwaka wangu wa mwisho wa masomo 2017/2018, nilipendekeza na kuandika andiko langu la kufanyia tafiti ”Design and Fabrication of Re-usable Sanitary Pad Incorporated with Aloevera Fibres” kama sehemu mojawapo ya somo na matakwa ya kutunukiwa Shahada yangu ya awali ya Uhandisi Usanifu wa Sayansi na Teknolojia ya Nguo-2018.

Hii ni kutokana na changamoto ambazo nilikua naziona kwenye jamii yangu, kwa mfano: Changamoto ya kwanza ni ya uchafuzi wa mazingira, mfano katika kupanga kwangu nyumba za kupanga kuna wakati mwingine mara kwa mara sisi wapangaji tulikua tunachangishwa kiasi cha pesa kwa ajili ya usafi wa maliwato na jambo la kustajabisha zaidi na kushangaza ni kuona uchafu uliokuwa ukitolewa kwenye sinki la choo ni bidhaa za kike zilizokuwa zikitupwa mule baada ya matumizi, hivyo kufanya kuziba kwa choo.

Na changamoto ya pili ni gharama na upatikanaji wa shida wa taulo za kike za kufua nchini. Nakumbuka Juni 2018, nikiwa naendelea pia kufanya tafiti zangu ambazo nilizianza Octoba 2017, kikao cha Bunge Tukufu la Tanzania, kilibaini uwepo wa gharama kubwa isiyo rafiki kwa wanunuaji/watumiaji wa bidhaa za usafi wa hedhi. Hivyo Bunge liliamua na kuona haja ya kuzifutia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa viwanda vinavyojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa bidhaa hizi za taulo za kike nchini, japo kitendo hiki hakikuweza kufanikisha uwepo wa bei nafuu wa bidhaa hizi kwenye masoko, ivyo kufanya Bunge la Tanzania kufuta tena msamaha na kurudisha upya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za taulo za kike kwa mwaka wa fedha uliofata, 2019 mpaka sasa.

Kutokana na hizo changamoto mnamo mwaka 2020, nilianzisha ”Magnetic’s Fe Enterprises Limited” ambayo ni moja ya miongoni mwa biashara bunifu ya kijamii iliyokuja na inayojihusisha hasa kwenye maeneo ya usafi kwa lengo la kuboresha upatikanaji kwa urahisi wa elimu kwa wanafunzi wa kike kuweza na kumudu mizunguko yao ya hedhi salama kwa kupitia uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa taulo za Najali na pia kwa wanawake wakazi wa vijijini upatikanaji wa taulo hizo kwa gharama nafuu.

2. Ni matatizo gani kwenye jamii unaona bidhaa yako inasuluhisha?

Bidhaa yetu ya ”NAJALIpad” inasuluhisha matatizo yafuatayo kwa mtoto wa kike na mwanamke:

  1. Changamoto ya magonjwa: Bidhaa hii ni njia mbadala ya kupunguza magonjwa shambulizi kwa mtoto wa kike na mwanamke kama TSS (Toxic Shock Syndrome), UTI (Urinary Tract Infections) na Saratani ya kizazi yasababishwayo na kutumia mara kwa mara bidhaa zilizotengenezwa na uji wa kemikali kwa muda mrefu.
  2. Changamoto ya uchafuzi wa mazingira: Bidhaa hii Inatunza mazingira kwa kuwa ina uwezo wa kutumika zaidi ya mara moja, kufukiwa na kuoza ardhini bila kusababisha madhara yoyote na kurudisha nidhamu ya usafi kwa watoto wa kike.
  3. Changamoto ya kukosa masomo: Bidhaa hii inaongeza maudhurio kwenye vipindi vya masomo darasani kwa wanafunzi wa kutwa na bweni kipindi chote cha hedhi.
  4. Changamoto ya gharama: Bidhaa hii Inapunguza gharama ukilinganisha na uwezo wake wa kutumika zaidi ya mara moja takribani 12+ na kudumu kwa muda mrefu bila madhara yoyote.

3. Unapata msaada gani kutoka kwa Serikali na unahisi wabunifu kama nyie mnaweza kusapotiwa vipi na Serikali au jamii mnayoisuluhisha matatizo yao?

Msaada kutoka Serikalini ni kwa sasa kampuni na mradi upo kwenye programu ya kiatamizi chini ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO).

Ningependa kuona wabunifu tunapewa kipaumbele kutoka serikalini na kutiwa moyo wa kuendelea kuleta bunifu zenye tija kwenye jamii kwa kuanzisha viwanda, kama tulivyo na sera yetu ya ”Tanzania ya viwanda” bila kufanya hivi wabunifu wengi wanakata tamaa kwa kukosa mwanga wa kuendeleza bunifu zao zenye tija kwenye jamii yetu.

Ningeomba pia serikali iweze kutenga ruzuku kwa ajili ya kuwalea na kuwaendeleza wabunifu, hii itasaidia sana kuwakuza vyema na kufanya bunifu zao kufika mahali pazuri ikiwa ni pamoja na uanzishwaji mwingi wa viwanda vya ndani. Ningependa pia jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanajihusisha na maswala ya mtoto wa kike na haki za wanawake nchini/duniani yaweze kushirikiana nasi na kutoa support kwenye ubunifu huu ili iwe tija ya kukuza na kuendeleza bidhaa hizi zenye suluhisho endelevu kwenye usafi wa hedhi.

4. Ni changamoto gani unaipata kwenye uzalishaji mpaka kupata bidhaa kamili na unazishindaje changamoto hizo?

Changamoto kubwa hasa ninayoipata kwenye uzalishaji ni upatikanaji wa shida wa baadhi ya malighafi stahiki za kufanyia ubunifu huu. Hii ni kwa sababu nchini hatuna viwanda vyenye teknolojia ya kuandaa au kuchakata malighafi za nguo ambazo zinaendana na ”specifications” zangu ambazo nakuwa nahitaji ili ubunifu wangu uweze kukidhi mahitaji husika ya bidhaa.

Hivyo inanilazimu kuendelea kutumia sehemu yangu ya taaluma ya teknolojia ya nguo kufanya tafiti endelevu kwenye malighafi zinazopatikana nchini na kuweza kuandaa viwango mbadala ambavyo vinakidhi matakwa ya bidhaa za usafi wa hedhi na kwa kufata kiwango na muongozo kutoka Shirika la Viwango Nchini (TBS).

5. Unahisi je Watanzania wanakubali kazi za kibunifu za Kitanzania? Na ni vipi Watanzania wanaweza kuwa na motisha ya kupenda vitu kutoka kwao/vya kwao?

Ni kweli Watanzania walio wengi hawakubali kazi za kibunifu za Kitanzania, hii pia iakatisha morali kwa wabunifu wetu.

Hii wazi ni kasumba ambayo sisi Watanzania tunayo, kwa mfano sio tu hata kwenye maswala ya bidhaa za viwandani, bali hii ipo hata kwenye tasnia zingine, unakuta mtanzania anapenda burudani kwa mfano na anapenda muimba mziki kutoka mataifa ya nje na anapoteza upendo wa kizalendo kwa kuto support kazi za wasanii wetu amabao ni wazawa wa ndani. Hii pia ipo kwa kutokukubali na kuamini kazi zetu wenyewe, hivyo nipende tu kutoa motisha kwa Watanzania kujivunia kazi zetu ambazo ni mazao yetu wenyewe  na zinazofanywa na wabunifu wetu wa ndani ya nchi, hii itakua chachu ya kuongeza wigo wa kukua kwa uchumi na kuongeza ujenzi wa viwanda vingi nchini. Na kwa upande wa serikali inaweza kuongeza jitihada kwa kuandaa na kuboresha maonesho mfano Saba Saba nk, yenye tija ya kuzitangaza bidhaa zetu za ndani ili Watanzania wapate kuziona na kuviinua viwanda vyetu vya ndani kutengeneza bidhaa zenye ubora.


Unaweza kuwasiliana na Elineema na NAJALIpads kwa:

Previous ArticleNext Article
Eunice is a multi-niche freelance writer with experience in writing health, lifestyle, finance, interviews, tech, travel, entrepreneurship, automotive, and mental health articles.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Send this to a friend